SoC04 Tanzania yenye kiwango kidogo cha Usugu wa Vimelea vya Magonjwa Dhidi ya Dawa (UVIMADA) ifikapo Mwaka 2035

Tanzania Tuitakayo competition threads

Nimechoka Sana

New Member
May 4, 2024
3
2
Utangulizi
Akizungumza kwenye Kongamano la Usugu wa Vimelea vya Magonjwa Dhidi ya dawa (UVIMADA), Novemba 17, 2023, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alinukuliwa akisema takwimu za mwaka 2019 zinaonesha watu 12,500 nchini walifariki kutokana na athari za UVIMADA. Aidha, takwimu zingine zilizotolewa kwenye kongamano hilo zilionesha kuwa takriban watu 54,000 walifariki kutokana na changamoto zinazohusiana kwa ukaribu na UVIMADA na kwamba janga hili nchini ni kubwa mara 8 zaidi kuliko ugonjwa wa Malaria.

Kwa mujibu wa tafiti, vifo vitokanavyo na UVIMADA vitafikia Milioni 10 duniani kwa mwaka ifikapo mwaka 2050, pia ni mojawapo ya majanga yanayotabiriwa kutokea duniani siku za usoni.

Makala haya yanapendekeza mikakati ya kinga dhidi ya Janga hili Pamoja na kupunguza ¾ ya idadi ya vifo vilivyopo sasa ifikapo mwaka 2035.

UVIMADA ni nini hasa? Kwa tafsiri isiyo rasmi sana, ni hali inayotokea baada ya vimelea vya Magonjwa ikiwemo Bakteria, Virusi, Fangasi na Parasite vinapopitia mabadiliko yanayoviwezesha kushindwa kuitikia dawa za Antibayotiki anazotumia Mgonjwa kwenye Ugonjwa husika hivyo kuvifanya viendelee kuishi pasipo mgonjwa kupona au kupata ahueni ya afya yake.

Pamoja na mambo mengine, hali hii inaweza kusababishwa na kutumia dawa za Antibayotiki pasipo kupata ushauri wa wataalamu, kutokumeza dozi sahihi ya dawa (Overdose na Underdose), kutokufuata muda sahihi wa kumeza dawa pamoja na matumizi ya biadhaa za nyama, maziwa na mayai zenye masalia ya Antibayotiki.

Tanzania ifanye nini kuikabili hali hii?
Kwa mujibu wa Makala ya gazeti la Mwananchi la Novemba 9, 2023, takwimu zinaonesha matumizi ya dawa dhidi ya vimelea nchini yanakadiriwa kufikia asilimia 62.3, sambamba na makadirio ya usugu kwa asilimia 59.8. Kwa lugha rahisi, katika kundi la watu 100, watu 60 wana vimelea sugu visivyotibika kirahisi.

photo_2024-05-04_17-28-18.jpg

Majibu ya Maabara yakionesha usugu wa vimelea: Chanzo (Majibu binafsi)
UVIMADA itakuwa janga kubwa zaidi ifikapo mwaka 2035 kwani Tanzania imo kwenye orodha ya nchi 14 za kusini mwa Jangwa la Sahara zenye kiwango kikubwa cha UVIMADA, hivyo napendekeza mambo yafuatayo;

Mipango ya Muda mfupi (Mwaka 2028)
  • Serikali isambaze maji safi na salama kila kijiji, ihuishe kampeni yake ya kutakasa mikono iliyofanyika wakati wa janga la UVIKO 19 katika ngazi ya kaya pia sehemu zinazohusisha mkusanyiko wa watu wengi ziwekewe vitakasa mikono na maji tiririka ili kudumisha usafi wa mikono
  • Ianzishwe kampeni kubwa ya kudumu ya elimu ya Matumizi ya njia sahihi za kujikinga na Magonjwa ya zinaa kwani magonjwa haya (au dalili zake) huchangia kwa kiasi kikubwa matumizi holela ya dawa za Antibayotiki
  • Hadi kufikia robo ya kwanza ya 2024, laini za simu Milioni 73.42 zimesajiliwa nchini. Tutumie TEHAMA kufikia watu kupitia jumbe elimishi ambazo zitajikita kwenye dhima ya UVIMADA.
  • Yawekwe mabango yenye jumbe za UVIMADA kwenye Barabara, miji na maeneo yote ya umma yanayotumika kwenye mikusanyiko ya watu wengi. Aidha, viandaliwe vipindi/jumbe kwenye redio, luninga na mitandao ya Kijamii vitakavyotoa elimu ya kutosha kuhusu UVIMADA
  • Vongozi wa dini wana ushawishi mkubwa, wapewe semina na elimu kuhusu UVIMADA ili wawahubirie wafuasi wao wanapokuwa kwenye ibada zao za kila siku
  • Tafiti zinaonesha uelewa wa dhana ya UVIMADA ni mdogo hata kwa wanafunzi wa kada za afya Pamoja na watumishi wa kada hiyo. Msisitizo wa elimu ya mafunzo kwa wanafunzi ujikite katika kufafanua dhana hii kwa vitendo, lakini watumishi wapewe mara kwa mara elimu pamoja na kuweka miongozi mipya kwenye masharti ya kuhuisha leseni zao ambapo watapaswa kuhudhuria Continuing Professional Development (CPD course) zenye elimu ya UVIMADA
  • Serikali isimamie kwa ukali Sheria ya kutotoa Antibayotiki bila cheti cha daktari, kwa wanaokiuka wachukuliwe hatua pia uanzishwe mfumo maalumu (Online Portal) wa kuripoti vituo na watoa huduma wasiozingatia miongozo hii
  • Mashamba ya ufugaji mkubwa wa kuku yasajiliwe, yawekewe Mwongozo wa matumizi ya dawa za Antibayotiki Pamoja na kufuatiliwa mara kwa mara kama yanafuata miongozo hiyo
Mipango ya Muda mrefu (Mwaka 2032)
Idara zote za Hospitali/Polyclinic ziwe na timu ya watu wataohusika na kuthibitisha kwenye mifumo matumizi ya Antibayotiki kwa wagonjwa wao (Antibiotics Approval Team). Timu hii itadhibiti ubora na kupunguza makosa yanayoweza kufanywa na daktari kwa makusudi au kwa bahati mbaya.

Serikali ianzishe ‘Tume (Idara) ya kudhibiti UVIMADA’ itakayokuwa chini ya Wizara ya Afya ambayo itahusisha wadau wa viwanda vya madawa na vyakula, wataalamu wa Afya, watafiti Pamoja na wataalamu kutoka kada za Kilimo na Mifugo. Bodi hii itapaswa kushughulikia masuala yote yanayohusu UVIMADA ndani ya nchi ikishirikiana na Serikali Pamoja na taasisi zingine za Kimataifa

Pia, uanzishwe mfumo maalumu wa kukusanya taarifa (Kanzi Data) za kimaabara za wagonjwa wenye UVIMADA utakaoratibiwa kwenye ngazi ya kanda kutoka hospitali zote za chini yake. Kwa muktadha huu, ziwepo kanda 5, Kanda ya Ziwa (Bugando), Kanda ya Kaskazini (KCMC), Kanda ya Kati (Benjamin Mkapa Dodoma), Kanda ya Kusini (Mbeya ZRH) na Kanda ya Pwani (Muhimbili). Vituo hivi vitachakata taarifa na kuziwasilisha makao makuu ya Tume/Idara ya Kudhibiti UVIMADA yatakayokuwa na Ofisi zake maalumu kwenye eneo litakaloonekana linafaa.

Pamoja na mambo mengine, taarifa hizi zitatumika katika kufuatilia ukubwa wa Janga hili, kupanga mipango kisera na kibajeti, kuratibu tafiti pamoja na kutoa miongozo mbalimbali kwa niaba ya Serikali.

Hitimisho
Mwaka 1945, Alexander Fleming, Mgunduzi wa Antibayotiki ya kwanza (Penicillin) alionesha wasiwasi wake na kuonya kuwa ipo siku dawa hizi zitauzwa kama njugu madukani hali itakayopelekea kutokea kwa UVIMADA. Fleming hayupo duniani, lakini maneno yake yanaishi.

Mipango hii imejikita kwenye sura kubwa ya kuwezesha wananchi kuwa na uelewa mpana wa masuala anuai yanayohusu UVIMADA huku ikiwapa nafasi watumishi wa afya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

photo_2024-05-04_17-39-26.jpg

Ujumbe ukionesha matumizi mabaya ya Azithromycin: Chanzo, Mtandao wa X

Ikiwa Serikali itapokea na kutekeleza mipango hii ikishirikiana na wananchi, kama ilivyokuwa Mei 8, 1980 kwenye Mkutano wa 33 wa Baraza la Afya Duniani uliotangaza kutokomezwa kwa ugonjwa wa Ndui Duniani, mwaka 2035 itaitangazia dunia imefanikiwa kupunguza ¾ ya idadi ya sasa ya watu wanaopoteza Maisha kutokana na UVIMADA, na wakati huo nchi zingine zikiwa kwenye kilele cha athari zake, Shirika la Afya Duniani Pamoja na taasisi zingine za Masuala ya Afya zitakuja kujifunza na kututumia kama mfano katika kusaidia nchi zingine kukabiliana na janga hili.
 
Akizungumza kwenye Kongamano la Usugu wa Vimelea vya Magonjwa Dhidi ya dawa (UVIMADA),
Uvimada, sounds funny 😅

Anyway turudi kwenye mada ya UVIMADA:
Pointi ulizoelezea zafaa haswaaa zikifuatiliwa. Na kwa kuongezea tu.

Inabidi kuangalia mfumo wa kuteketeza ipasavyo dawa zilizoharibika au kuisha muda wake. Maana huwa ninauliza swali? Mfano mtoto mdogo akapeaa antibayotiki ya chupa labda Flucamox syrup na ikabaki huwa wanaitupa wapi? Je haiwezi kuoelekea usugu????
 
Uvimada, sounds funny 😅

Anyway turudi kwenye mada ya UVIMADA:
Pointi ulizoelezea zafaa haswaaa zikifuatiliwa. Na kwa kuongezea tu.

Inabidi kuangalia mfumo wa kuteketeza ipasavyo dawa zilizoharibika au kuisha muda wake. Maana huwa ninauliza swali? Mfano mtoto mdogo akapeaa antibayotiki ya chupa labda Flucamox syrup na ikabaki huwa wanaitupa wapi? Je haiwezi kuoelekea usugu????
Ni kweli mkuu, hii pia ni changamoto kubwa. Inaweza kusababisha usugu pia. Nadhani kuna haja ya Serikali kuangalia suala hili kwa upana
 
Back
Top Bottom