Tanzania ya Viwanda na Miongozo ya kuvuliwa baraghashia na ujenzi wa uwanja wa kumbukumbu ya Push-up

ZILLAHENDER MPEMA

JF-Expert Member
Apr 4, 2015
2,055
4,243
Wakati wataalamu wa Historia na mambo ya kale Duniani wakiyaorodhesha mambo saba na kuyaita"maajabu saba" ya ulimwengu,Taifa la Tanzania kila uchwao linapiga hatua kwa kasi inayosadikiwa kufikia mwendokasi wa ukillaza wa division 4.30km/saa kujitafutia nafasi ya kuwa nchi ya kwanza Duniani kutajwa kama "nchi ya ajabu".Zimebaki hatua kadhaa ili serikali yetu tukufu ya ccm ifikie azma yake ya siku nyingi ya kulifanya Taifa letu litambulike kama " Taifa la ajabu Duniani"

Chini ya utawala wa awamu ya Tano,tayari tumeshashuhidia juhudi za makusudi za serikali na vyombo vyake vikililazimisha Taifa kurejea kwa kasi katika "Zama za giza"ambazo Taifa letu lilipitia miaka zaidi ya 50 iliyopita.

Ni katika awamu hii,wasomi wetu kwa makusudi wameweka chini taaluma zao na kukubali " kutii bila shuruti" kuitikia pambio ya kuisifu serikali kwa kuwa wabunifu wa maigizo mapya mithiri ya bongo movies.

Ili Taifa liweze kuifikia ndoto ya kuwa Taifa la viwanda na uchumi wa kati,lilipaswa kuwatumia wataalamu wetu wa ndani na wale wa nje ya nchi kufanya mijadala huru ya kitaaluma itakayoweza kuwajengea uwezo na kutoa hamasa za kiuwajibikaji ili watu wetu watambue thamani ya mchango wao katika kuifikia Tanzania tunayoitaka.Kinyume chake badala ya kuzitumia akili za wasomi wetu,tumeamua kuziruhusu akili ndogo zenye muono wa kiitikadi na zisizo na chembe ya kimaendeleo zitamalaki nchini.

Bunge ambalo lilipaswa kuwa dira ya Taifa katika kuisimamia Mipango ya Maendeleo ya serikali,sasa limeacha wajibu wake wa msingi wa kuisimamia na kuishauri serikali na sasa limejikita katika siasa za maji taka za kujadili mambo ya kipuuzi yasiyo na tija kwa Taifa.Sasa tunaushuhudia mhimili huu muhimu katika uendeshaji wa serikali ukijibadili toka chombo huru,na sasa bunge limegeuka kamati kuu ya chama,badala ya kuisimamia serikali,sasa limegeuka kuwa mtetezi wa serikali katika mambo ya hovyo yasiyo na tija kwa Taifa letu.Ni katika kipindi hiki ili lifikie malengo ya kuwa"kitengo cha propaganda"cha serikali,bunge letu limewatoa nje ya bunge wabunge wote makini walioonekana kujipanga ili kuisimamia serikali,badala yake ndani ya ukumbi wa bunge kumesheheni wabunge villaza wenye uwezo wa kujadili miongozo ya ujenzi wa viwanja vya kumbukumbu ya push-ups na kuvuana baraghashia.

Uko wapi "utukufu na ukuu wa bunge?Wakati mabunge ya mataifa mengine yakijikita katika kujadili hoja za kimaendeleo kama vile ujenzi wa viwanda vidogo,viwanda vya kati na vikubwa,huku kwetu tunalitumia bunge kulipumbaza Taifa kwa kujadili vitu vya kipumbavu kabisa ambavyo jamii haikuvitarajia kama vinaweza kutumia kodi zetu kuvijadili bungeni.Hii ni aibu kwa chombo hiki chenye dhamana ya kuisimamia serikali,lakini kimejigeuza na kuwa kitengo cha propaganda cha serikali.

Hayati Baba wa Taifa(R.I.P) katika harakati za kuliletea Maendeleo" Taifa changa la Tanzania",aliyaorodhesha mambo makuu matatu kama kikwazo cha kuyafikia Maendeleo aliyoyatamani.Mambo hayo aliyataja kuwa ni UJINGA,UMASIKINI NA MARADHI.Mwalimu Nyerere aliamini toka moyoni kuwa ili Taifa liweze kupiga hatua kwa kasi kuyafikia Maendeleo,ni lazima lijikite katika kutatua changamoto za Ujinga,umasikini wa fikra na kipato pamoja na maradhi na alielekeza nguvu zake katika kuwapiga vita maadui hawa.

Dunia inaenda kwa kasi sana,leo hii katikati ya kushamili na kuwepo kwa wasomi waliojaa katika idara na Taasisi za serikali,serikali ya awamu ya Tano imekuja na "adui mpya"wa Maendeleo ya nchi yetu.Sasa kwa mujibu wa Mheshimiwa Rais wa JMT,adui mkubwa wa Maendeleo ya Taifa letu ni hoja kinzani zinazojaribu kuikosoa na kuisimamia serikali.Kwamba katika awamu hii,ukiwa na hoja kinzani wewe ni adui mpya wa Maendeleo ya Taifa letu na Rais amejiapiza kutokuwa mvumilivu kwa yeyote atakayemchelewesha kuwaletea wananchi Maendeleo.

Katika awamu hii kila mtu atakayethubutu kuhoji jambo lolote iwe bungeni au mahali pengine popote,kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu alipoutangaza Ujinga,umaskini na maladhi kuwa maadui wa Maendeleo,sasa wapinzani na wakosoaji wa utawala wa awamu ya Tano wametangazwa rasmi kuwa ndiyo maadui wapya na vikwazo vinavyomzuia Rais kuliletea Taifa Maendeleo.Maadui hawa ili wasitimize azma yao ya kumzuia Rais kutuletea Maendeleo,sasa serikali ya ccm imeanza kuwasaka na kuwafurusha popote walipo wasiwe vikwazo vya Maendeleo.

Wapinzani hawa wa Maendeleo kwa mujibu wa Rais sasa wanafukuzwa bungeni,wanazuiwa kufanya siasa na sasa wanazingirwa popote walipo kwa hofu kwamba wanaweza kuzunguanza na wananchi jambo ambalo serikali inahisi kuwa ni kikwazo cha maendeleo.Kupitia adui huyu mpya,bunge linepoteza weledi,hakuna mijadala fikirishi bungeni yenye kuibua fikra za mapinduzi ya kiuchumi,sasa ni mwendo wa "ndiyoooooo" hata kwenye mambo ya kipuuzi.

Tanzania si Mali ya ccm na serikali yake,serikali za vyama zitapita lakini Taifa la Tanzania litasimama,kuwaruhusu watu wachache wajione kuwa ndiyo wenye mamlaka ya kufikiri kwa niaba ya Watanzania ni jambo llisilokubalika na linafaa kupuuzwa kuliko upuuzi wenyewe.

Ili tuendelee Taifa letu linapaswa kutoa nafasi ya mijadala huru,liruhusu wazalendo wa Taifa hili waitafakari kwa pamoja hatima ya Taifa hili,wabishane na kupingana kizalendo na ikibidi hata "wachapane makonde" lakini mwisho wa siku waje na suruhisho la matatizo yetu.

Kuwageuza washindani wa serikali kuwa maadui wa maendeleo na kuamua kutumia vyombo vya dola kuwadhibiti wapinzani wako kwa kisingizio chepesi cha kuwaletea watu Maendeleo ni jambo lisilokubalika,serikali inapaswa iache ubabe,iwe sikivu na iyaruhusu makundi ya kijamii vikiwemo vyama vya siasa kutoa michango yenye tija ili tuweze kupiga kasi kuyafikia maendeleo tunayoyaota,kuwageuza wapinzani wako kuwa "adui mpya"wa maendeleo ni hatua ya mwisho ya Uthibitisho wa Taifa letu kukidhi vigezo vyote vya kuwa Taifa la Maajabu ulimwenguni.

Karibu tujadili.
 
Back
Top Bottom