Tanzania tumekuwa Taifa la Ombaomba

Kiwi

JF-Expert Member
Sep 30, 2009
1,054
990
Habari za kazi wakuu,

Miaka ya karibuni kumekuwa na wimbi la kuomba kiasi ambacho kinaleta kichefuchefu. Kuanzia mkuu wa nchi kutamka hadharani wakati wa kampeni yake kuwa 'nisingesafiri sana nje ya nchi wote mngekufa njaa' nimeona kumekuwa na kuhalalisha dhana hii potofu kuwa bila kuomba msaada/misaada hakuna linaloweza kufanyika.

Suala la kuomba misaada limekithiri sana. Karibu kila siku kwenye TV zetu kuna matangazo kuhusu mtu/watu fulani wanahitaji msaada kwa jambo moja au lingine, iwe ni msaada wa pesa za matibabu, msaada wa pesa za kusomesha watoto, mpaka msaada wa malezi ya watoto.

Ni ukweli usiopingika kuwa utamaduni wetu wa kiafrika siku zote watu husaidiana kwa hali na mali kwenye shoida ama raha. Lakini pia ni ukweli usiopingika ya kuwa utamaduni wetu wa kiafrika unathamini sana heshima ya mtu/watu. Kuomba ni kudhalilika/kudhalilishwa/kujidhalilisha. Kwa kumbukumbu zangu ilikuwa ni aibu kubwa sana kuomba! Siku za nyuma tulikuwa tunapiga hodi kwa jirani kuomba endapo mtu umepungukiwa. Tulikuwa tunaombana hata chumvi na sukari. Lakini hiyo haikuwa tabia, na kila mtu alikuwa anafahamu hivyo. Inapokuwa tabia, basi hukemewa na kila mtu. Ilikuwa aibu kila kukicha mtu kuonekana unaomba leo chumvi, kesho sukari, keshokutwa moto n.k. Jamii yetu ilikuwa haikubaliani na tabia hii. Cha kusikitisha ni kwamba leo hii kuanzia viongozi wa serikali, asasi zisizo za serikali taasisi mbalimbali mpaka ngazi za familia, kuomba tumehalalisha. Unakuta mradi mzuri sana umetayarishwa, na ukiuliza pesa za kufanikisha mradi huo zitatoka wapi? Jibu liko tayari, tutaomba pesa kwa wafadhili! Hii kasumba ya kupanga maisha yako halafu mtu/watu wengine wagharimie ufanikishaji wa azma hiyo siyo tabia nzuri. Na ole wako mtu/watu wakuombe msaada ushindwe kuwapatia.

Maswala ya michango ya arusi imekuwa kero kwenye jamii yetu, na inakuwa vigumu sana kuwaelimisha watu ya kuwa sio lazima uombe mchango ili kufanikisha arusi. Ukisema hivyo unakuwa hueleweki, kama kwamba unapotosha utamaduni wa kitanzania wa kusaidiana kwa hali na mali.

Mtazamo wangu binafsi ni kuwa hii tabia ikemewe kuanzia ngazi za chini (familia) ili tuweze kujenga taifa la watu wanaojisikia sifa na fahari ya kufanikisha azma za maisha yao bila kutegemea misaada! Serikali ione aibu kujidhalilisha mbele ya uso wa dunia kwa kuwa taifa tegemezi, na hata taasisi zingine zote ziandae mipango kabambe ya kujisimamia wenyewe. Haikatazwi unapokwama kuomba msaada wa nguvu ya ziada, lakini isiwe mipango yote inaanza na kumalizika kwa kutegemea misaada. Inatosha!
 
Back
Top Bottom