BabuK
JF-Expert Member
- Jul 30, 2008
- 1,845
- 329
RAIS wa Somalia, Shehe Sharif Ahmed amesema nchi yake itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha uharamia unakwisha katika Ukanda wa Bahari ya Hindi. Amesema yeye na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete wamekubaliana kuhakikisha ushirikiano wa kiulinzi na usalama unakuwepo wakati wote katika ukanda huo. Rais Ahmed ameyasema hayo leo asubuhi alipozungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam muda mfupi kabla ya kurejea nchini kwake. Pamoja na kuathiri eneo la ukanda wa Bahari ya Hindi na Tanzania kwa ujumla, maharamia wanatishia maisha ya watu na shughuli za maendeleo katika sehemu kubwa ulimwenguni. Nchi yangu itajitahidi kushirikiana na Tanzania kwa kiasi kikubwa katika masuala ya ulinzi na usalama wa ukanda huo na kuukomesha. Hayo ndiyo pia tuliyokubaliana na Rais mwenzangu Kikwete tulipozungumza jana (juzi) na nadhani yatafanikiwa, alisema Rais Ahmed. Kuhusu hali ya ukame nchini kwake alisema; wananchi wangu wapatao milioni 3.5 wanateseka kwa njaa kali lakini ninamshukuru Rais Kikwete na Watanzania wote kwa kutupatia msaada utakaowawezesha kuishi. Kuhusu namna ya kufikisha msaada huo na mingine ya kimataifa wakati kukiwa na zuio la kundi la kigaidi la Alshaabab, alisema; Hatuna budi kuyakomboa maeneo hayo na kuhakikisha watu wake wanafikiwa na kusaidiwa. Nia yetu ni kuhakikisha kundi hilo linatoweka kabisa katika nchi hii (Somalia) ndio maana tumekubaliana na Rais Kikwete kushirikiana kuhakikisha linaondoshwa hata kama itakuwa kwa njia ya mazungumzo, alisema Rais Ahmed. Kwa maelezo yake, Serikali ya Somalia ipo tayari kufanya mazungumzo na kundi hilo la Alshaabab ingawa anahisi litakataa kukaa mezani. |