Tanzania na Korea Kusini Zakubaliana Kuboresha Mandhari ya Jiji la Dodoma

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,898
942

Tanzania na Korea Kusini Zakubaliana Kuboresha Mandhari ya Jiji la Dodoma

Imeelezwa kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Korea Kusini umechochea kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini ikiwemo mradi wa kimkakati wa daraja la Tanzanite lililojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Korea Kusini kupitia mfuko wa ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi (Economic Development Cooperation Fund -EDCF).

Hayo yamebainishwa tarehe 26 Januari, 2024 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano yaliyohusisha Ofisi ya Waziri Mkuu na National Agency for Adminstrative City Constraction and Heerim Architects and Planners ya Nchini Korea Kusini ambapo pamoja na mambo mengine amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo kunaweka msingi imara wa Biashara na Uwekezaji baina ya Nchi hizo mbili huku miradi mingi zaidi ikitarajiwa kurekelezwa Nchini hususani Jijini Dodoma ambako ni Makao makuu ya Tanzania.

Amesema kupitia kusainiwa kwa hati hizo Tanzania itanufaika na teknolojia ya kisasa ya usanifu na ujenzi wa majengo na miundombinu mingine itayopendezesha mji mkuu Dodoma, sambamba na kupatikana kwa fursa mpya za ushirikiano na makampuni ambayo yana uzoefu mkubwa wa usanifu na ujenzi hususani wa majengo katika miji na majiji makubwa ;

Waziri Jenista amesisitiza kuwa maendeleo ya Jiji la Dodoma yanahitaji uwekezaji mkubwa katika majengo, maeneo ya mapumziko, mazingira, miundombinu ya mawasiliano na maeneo mengine ya kuvutia hivyo ili kufikia lengo hilo Serikali inapaswa kushirikiana kikamilifu na sekta binafsi ili kufikia maendeleo hayo

Aidha amesema kuwa uhusiano huo umedhihirishwa pia na ziara za Viongozi wa ngazi ya juu katika Mataifa yetu haya mawili. Moja ya ziara hizo maalum ilifanywa Oktoba 2022 na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alifanya ziara ya kikazi nchini Korea Kusini.

"Akiwa Korea Kusini Mheshimiwa Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) aliitembelea National Agency for Administrative City Construction, taasisi hii ni wakala wa kitaifa nchini Korea Kusini inayosimamia na kuendeleza ujenzi wa jiji la Sejong nchini humo, kimsingi jiji la Sejong limejengwa kwa mandhari nzuri na ya kuvutia sana, muonekano wake wa kuvutia ulimfanya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kumkaribisha Mtendaji Mkuu wa taasisi hii Nchini Tanzania ili kubadilishana uzoefu na viongozi wa taasisi zinazofanana na hizi hapa kwetu Tanzania,” alisema Waziri Jenista

Waziri Mhagama alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza na kuwekeza nchini kwa kuzingatia uboreshwaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini hususani kwenye Makao Makuu ya nchi Dodoma.

"Lengo hili litafikiwa kwa ufanisi endapo Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta binafsi ili kufikia maendeleo haya. Kwa kuzingatia hilo, nitoe wito kwa Wawekezaji katika nyanja zote, wanaume kwa wanawake kuwekeza Jijini Dodoma ili kuuendeleza na kuupendezesha Mji wetu Mkuu". Ameeleza Waziri Mhagama.

=MWISHO=
 

Attachments

  • GE5waFyXMAAEEW3.jpg
    GE5waFyXMAAEEW3.jpg
    116 KB · Views: 5
  • GE5wYZ2XoAAgUWD.jpg
    GE5wYZ2XoAAgUWD.jpg
    165.3 KB · Views: 7
  • 37b7d6a7f52aa5f759725788b4cd75be.jpg
    37b7d6a7f52aa5f759725788b4cd75be.jpg
    158.8 KB · Views: 6
Back
Top Bottom