Tanzania na Misri Kushirikiana Katika Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Barabara

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,897
942

TANZANIA NA MISRI KUSHIRIKIANA KATIKA UJENZI NA UKARABATI MIUNDOMBINU YA BARABARA.

Tanzania na Misri zimekubaliana kushirikiana katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Barabara na Madaraja yatakayochochea maendeleo na ukuaji wa Uchumi katika mataifa hayo mawili.

Msimamo huo umetolewa katika kikao kazi cha kimkakati kati ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa Pamoja na Waziri wa Uchukuzi wa Misri, L.G Kamel Alwazeer kilichofanyika tarehe 20 Februari 2024 Dar es salaam katika Kituo cha Mikutano (JNICC)

Akizungumza katika Kikao hicho, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Tanzania na Misri wamekubaliana kushirikiana kimkakati katika ujenzi wa miundombinu ikiwa ni Pamoja na ujenzi na ukarabari wa Barabara kutoka Cairo nchini Misri kupita Tanzani hadi Cape town nchini Afrika kusini.

“Tumekubaliana kukaa kwa Pamoja kuona namna ya kushirikiana kukarabati kwa viwango vya hali ya juu mtandao wa Barabara ambao unaunganisha Afrika kutoka Misri mpaka Afrika Kusini ambapo nchini kwetu, sehemu ya Barabara hiyo inaanzia Mkoa Songwe kutokea Zambia kupita Mbeya – Dodoma – Arusha kuelekea Namanga mpakani mwa Kenya na Tanzania” amesema Bashungwa

Bashungwa ameweka msisitizo wa mchakato huo kufanyika kwa haraka ili barabara hiyo iweze kuchochea ukuaji wa Uchumi katika Mataifa inapopita barabara hiyo.

Aidha, Mawaziri hao wamekubaliana kushirikiana katika kubadilisha uzoefu wa kitaalam kwa Wanafunzi wanaohitimu taaluma ya Uhandisi na Ukandarasi katika vyuo mbalimbali kupitia mpango wa mafunzo kwa vitendo (SEAP) katika mataifa hayo mawili.

Kadhalika, Waziri Bashungwa ameuelekeza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuhakikisha miradi ya barabara ambayo itatekelezwa, kupitia mikataba kuwe na vipengele vya kumlazimisha Mkandarasi kuwachukua wahitimu wa Ukandarasi na Uhandisi katika kusimamia miradi na kupata uzoefu wa kitaalam.

"Nimewapa jukumu TANROADS kuweka vigezo katika mikataba ya utekelezaji wa miradi vya kuhakikisha vijana wahitimu wa Ukandarasi na Uhandisi wanapewa nafasi ili kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuwawezesha Watanzania kujijengea uchumi wao wenyewe” amesisitiza Bashungwa

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi wa Misri, L.G Kamel Alwazeer amesema Serikali ya Misri na Tanzania itaendelea kushirikiana katika kukuza uchumi wa mataifa hayo ikiwemo kuunganisha Tanzania na Misri kwa njia kuu ya Cape Town - Egypt inayopita zaidi ya nchi kumi.

Amesema watasaidia kutoa mafunzo ya utaalam katika sekta ya Ujenzi na Uchukuzi na kusaidia Ujenzi wa Barabara na Madaraja ya Kisasa ambapo miradi hiyo itaunganishwa kwa pamoja.

Mawaziri wamekutana ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano kati ya Serikali Tanzania na Misri katika kubadilishana uzoefu wa kiutendaji na kudumisha urafiki ulioasisiwa baina ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Julius K. Nyerere na Rais wa Kwanza wa Misri Ali Muhammad Nagib.
 

Attachments

  • GG2n4OVXYAAdhTP.jpg
    GG2n4OVXYAAdhTP.jpg
    144.9 KB · Views: 2
  • GG2n5DoWAAAS7rP.jpg
    GG2n5DoWAAAS7rP.jpg
    251.4 KB · Views: 2
  • GG2n5DgWgAAnIE7.jpg
    GG2n5DgWgAAnIE7.jpg
    283.6 KB · Views: 2
  • GG2n65GWsAAL1Gi.jpg
    GG2n65GWsAAL1Gi.jpg
    288.9 KB · Views: 2
  • GG2n65HXcAAMTPk.jpg
    GG2n65HXcAAMTPk.jpg
    257 KB · Views: 2
  • GG2n65EXwAAfAKW.jpg
    GG2n65EXwAAfAKW.jpg
    285.6 KB · Views: 2
Back
Top Bottom