Tanzania na Elimu ya Kutokujitegemea

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Na Sammy Makilla
MAKALA haya yameandaliwa baada ya msomaji kupitia utafiti wa Rebecca Maarsland (2006) na chapisho lake maalum juu ya hili lililoitwa: Dhana Kurubani au Mapambano ya Nani Awe na Uwezo Zaidi?

Muasisi wa dhana ya Elimu ya Kujitegemea ni Mwalimu J.K. Nyerere. Baada ya kutoa chapisho lake la Ujamaa na Kujitegemea alikwenda hatua moja mbele zaidi na kuoanisha umuhimu wa kumuandaa mtoto anapokuwa shuleni ili aanze kujitegemea kwa kiasi fulani huko huko shuleni.

Mwalimu kama ilivyo kwa mambo mengi aliona mbali sana zaidi ya wengi wetu tunavyoona. Alijua fika kuwa Tanzania haina fedha, wakati ambapo maendeleo ya aina yoyote yanahitaji fedha. Hata hivyo, akagundua kwamba Watanzania sio tu wana rasilimali nguvu-kazi bali pia kuna msururu wa vitu wanavyoweza kuvifanya wao wenyewe kwa kutumia nguvu na akili zao za kuzaliwa. Haya yalikuwa ni mawazo ya kimaendeleo na kimapinduzi. Laiti yangelifanyika kwa moyo safi kama Nyerere alivyotumaini yangelichangia si haba kutuweka katika daraja ya juu zaidi kuliko daraja tuliyomo hivi sasa.

Kwa bahati mbaya viongozi na walimu wakorofi wachache walipoichakachua dhana ya Elimu ya Kujitegemea, uongozi wa baadaye wa Tanzania bila fikra wala tafakuri ukaamua kumtupa mwana na maji machafu yaliyomwogeshea. Wakaturudisha nyuma kwa zaidi ya miongo miwili kimaendeleo.

Ni muhimu tujiulize hivi leo, je, kuna mzazi anayempenda mwanawe kikweli kweli atakayekataa mtoto wake asifundishwe upishi na kazi za nyumbani (domestic science); au kilimo au ufugaji au uvuvi au biashara au ufundi wa kutengeneza kitu fulani wakati akiwa shuleni ? Kama wapo, basi nchi hii itakuwa imeingia katika awamu mbaya kimaisha, kiroho na kimaendeleo ya kuanza kukubali elimu ya kutokujitegemea.

Ila, hofu ya wazazi ni pale wenye shule, viongozi na walimu wanapogeuza miradi ya kujitegemea kuwa maeneo ya wao kujinufaisha na kujilimbikizia mali kibinafsi.

Elimu ya Kujitegemea ina faida mbalimbali. Katika kilimo na ufugaji, mathalani, ikiendeshwa vyema inaweza kuwapatia wanafunzi chakula cha kutosha na pengine kupunguza matatizo yanayosababishwa na upatikanaji wa chakula mashuleni. Kadhalika, wanafunzi wanapata chakula bora na chenye lishe zaidi kuliko kile cha kununua. Ndivyo ilivyo katika ufugaji samaki au uvuvi na ufugaji wa kuku na ndege wengine pia.

Katika masuala ya ufundi, wanafunzi wanaweza wakajitengenezea vitu mbalimbali wenyewe bila kutegemea fundi fulani. Ni kichekecho leo, kuwa tuna watoto wasiojua kushonea kifungo achilia mbali kushona nguo iliyofumuka.

Hili linatokea wakati watoto wa shule za msingi kwingineko ( India ) katika eneo hili la ufundi wanaweza kufanya mradi wa kutumia kompyuta unaoingizia shule kipato kikubwa kuliko ada wanayolipa na hivyo wao kusamehewa sehemu kubwa ya ada.

Maeneo ya ufundi yako mengi. Kuna kushona, kusuka au kufuma vitu na vichwa vya watu mbalimbali; kuna kurepea vifaa vilivyoharibika; kuna kutumia kompyuta na teknohama; kuna kuchonga, kuumba na kufinyanga vitu mbalimbali; na kuna kubuni vifaa mbalimbali vinavyorahisisha maisha ya kila siku ya watu wetu. Kwa kupata mabingwa wa shughuli hizi ndani au nje ya nchi shule inaweza ikafanya maajabu katika kuwaandaa wanafunzi wake kupambana na dunia ya utandawazi wangali wapo shuleni na hivyo kurahisisha mapambano yao pale wanapomaliza shule.

Ingawa shule nyingi hivi leo zina kitu kinachoitwa mabaraza ya walimu na wazazi au PTA (Parents Teachers Association) wizara ya elimu inatia mashaka kama ina baraza la wataalamu, wazazi na wanafunzi la kuishauri ili maamuzi yake yawe yanayowafunga watu wote kwa pamoja na siyo ya mtu mmoja au ya kidiktena. Mathalani, uamuzi wa kufuta michezo mashuleni na kuondoa masomo ya biashara. Maamuzi yote haya yalifanyika kwa namna ambayo yalionesha zaidi kuwa ni ya mtu anayeamua mambo ya shamba lake na mifugo yake binafsi. Maamuzi yanayohusu sehemu yoyote kubwa ya jamii ya Kitanzania hayafai kufanywa kiimla.

Tuangalie mfano huu mdogo wa kweli: Meneja mmojakatika shirika la serikali mkoani Tabora, hakuamini pale mtoto wake aliyekuwa akisoma shule ya Siha, Hai, Mkoani Kilimanjaro miaka hiyo, baada ya kujifunzakatika somo la ufugaji ng'ombe aliporudi nyumbani na kumuomba fedha ajenge banda la ng'ombe na kumnunuia angalau ng'ombe mmoja wa maziwa. Alifanya hivyo shingo upande akihofia nyumba yake kuwa chafu na harufu mbaya ya mifugo.

Kilichotokea, kijana wake aliweza kufuga na bado kuweka mazingira masafi na baadaye kumshawishi baba yake kujenga jiko linalotumia biogas kupunguza gharama za mkaa. Yule kijana alipochaguliwa kwenda kidato cha tano, baba alishikwa na mchecheto nani ataangalia ng'ombe wawili wa mwanawe. Lakini mtoto ambaye pia alijifunza misingi ya biashara na utunzaji vitabu shule ya sekondari alimwambia baba yake amwajiri mtumishi wa kuangalia mifugo hiyo na mshahara wake utatokana na maziwa yatakayouzwa bila kumgharimu baba chochote. Baba alifanya hivyo. Sio tu baadaye kijana alijisomesha mwenyewe bali pia akajenga nyumba yake ya kwanza kwa kutumia fedha yake ya maziwa.

Kosa la kimsingi limekwishafanyika. Je, tunajifunza nini kutokana na kosa hilo ? Nadhani ni kuweka mikakati inayofaa ili kukinusuru kizazi kijacho na balaa la kuwa kizazi kisichojitegemea kwa lolote lile duniani. Ajali ya kuwa taifa la watumiaji na walaji na sio wazalishaji.

Hili linakuwa gumu mno pale ambapo viongozi waliopo madarakani hata kama hawasemi kwa maneno, lakini tabia na mtazamo waliokwishaujenga ni ule wa kuwa na taifa la wanunuzi wa takribani vitu vyote wananchi wake wanavyohitaji katika maisha yao .

Ili elimu ya kujitegemea iwe na maana mashuleni ni shurti viongozi wetu waoneshe kwa maneno na vitendo, mtazamo na mwelekeo mpya wa kutaka taifa linalojitegemea na kujitosheleza angalau kwa yale mahitaji yetu ya msingi.

Tunawapa watoto wetu picha gani tunapoagiza sindano na viberiti toka nje ? Elimu ya Kujitegemea haitovutia wananfunzi toka nje pia? Katika kila nyumba kikombe, sahani, bakuli, pasi, jiko, jokofu na kadhalika vyote vinatoka nje.

Lazima tufike mahala tupeane muda wa kubadilisha mitazamo na misimamo hii hatua kwa hatua. Hili linaweza kutokea baada ya kuainisha kwa makini nini kinachoweza kuzalishwa kwa asilimia ngapi, hadi lini, na kuliwa humu nchini na kikatosha hata kuuza nje; na kile ambacho kwa hali ilivyo sasa ni lazima kinunuliwe nje. Hili litawapa changamoto vijana wetu mashuleni kwamba wana kazi ya kufanya ili tujitosheleze kwa vile tunavyoweza kujitosheleza.

katika medani ya juu zaidi lazima tuwaze juu ya kuwa na matrekta madogo (power tiller) yanayotengenezwa Tanzania kama ilivyo kwa pampu za maji, kompresa, malori, majiko, friji, taa, feni, kompyuta na vitu kama hivyo.

Turudi katika mawazo ya awali ya muasisi wa Taifa hili,Mwalimu J.K. Nyerere. Sisi kama Watanzania hatuna fedha. Hata hivyo, tuna rasilimali watu na tuna mali asili nyingi. Viongozi wakizithamini rasilimali hizi muhimu na wanasiasa wakiacha uoga kuwa wananchi wakineemeka wao watakuwa mashakani, na kutafuta mbinu ya kuoanisha kile kidogo tulichonacho na nguvu ya wananchi ya kuanzisha miradi wanayoimiliki wao wenyewe na kunufaika nayo vilivyo, na sio vinginevyo, nchi hii inaweza kufanza maajabu katika muda mfupi kuliko tunavyotarajia.

Ushiriki wa Tanzania katika programu ya Benki ya Dunia kwenye 'Community Foundations Initiative' nadhani unatakiwa uone mbali zaidi tu ya wananchi kushirikishwa katika miradi ya shule na afya. Wakati umefika sasa wa wananchi kushirikishwa na kuwezeshwa kwa ukamilifu katika kuanzisha, kumiliki na kuendesha miradi mbalimbali ya kijamii, kibiashara na kiuchumi kwa faida yao na maeneo wanamoishi. TASAF itaacha jina zuri na bora nyuma kwa kuwapatia Watanzania hisa za aina mbalimbali katika miradi na biashara endelevu zinazokuwepo kutatua matatizo yaliyopo na yajayo ili jamii yetu iwe jamii bora na isiyo na umaskini wa kutisha.
Nchi isiyochangia kutengeneza au kuunda kitu chochote cha maana katika vitu inavyovitumia kila siku ikiwemo barabara, reli, magari, miferjei ya maji, matrekta, baiskeli, vifaa vya ujenzi na ufundi na kadhalika sio nchi inayoweza kusema ina nia ya kweli ya kuondokana na umaskini.
 
Back
Top Bottom