Tanganyika yaibuka CECAFA bila rais wa nchi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tanganyika yaibuka CECAFA bila rais wa nchi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Isango, Dec 1, 2011.

Thread Status:
Not open for further replies.
 1. I

  Isango R I P

  #1
  Dec 1, 2011
  Joined: Jul 23, 2008
  Messages: 295
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 35
  [TABLE]
  [TR]
  [TD]
  Tanganyika yaibuka CECAFA bila Rais.

  Michuano ya Chalenji mwaka 2011 imeibua jambo kubwa sana katika akili yangu, na huenda ikaibua mambo mazito sana kwa watanzania wanaofikiri. Michuano hii ya Chalenji, (CECAFA), ni Michuano ya pamoja ya Shirikisho la mpira wa miguu unaohusisha nchi za Afrika Mashariki na Kati. Nchi zinazotajwa moja kwa moja katika shirikisho hilo ni pamoja na Kenya , Uganda , Tanzania , Sudan , Ethiopia , Eritrea , Zanzibar , Somalia , Rwanda , Burundi na Djibouti .

  Huenda sio suala la msingi sana kujihusisha na idadi ya nchi wanachama, lakini angalau kila mshiriki katika mashindano haya ni nchi huru inayojitegemea. Nimejisikia mkiwa sana , na huenda ilikuwa ni bahati mbaya kwangu kuhudhuria uwanja wa Taifa siku hiyo.

  Tarehe 25 Novemba nilishuhudia Shindano kati ya timu ya Zanzibar na Uganda . Lakini pia tarehe 26 Novemba niliangalia mchuano mkali kati ya timu ya Kilimanjaro Stars ambayo ni timu ya Tanganyika , dhidi ya Timu ya Amavumbi ambayo ni timu ya taifa ya Rwanda .

  Kilichonishangaza sana na kunisababisha niandike makala haya, ni ukweli kuwa timu ya Tanganyika haikutumia gari lililotolewa na Benk ya NMB kwa ajili ya Timu inayoitwa Taifa Stars. Hii ni kwa sababu Taifa Stars ina wachezaji toka Bara na Zanzibar, hivyo ni Timu ya Muungano, na Rais wa Jamhuri hiyo ni ndugu Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri wake Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ni Mizengo Pinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Anna Makinda. Hiyo ni kwa upande wa serikali ya jamhuri ya Muungano, yenye katiba moja iliyotungwa na kufanyiwa marekebisho siku hadi siku.

  Timu ya Kilimanjaro Stars ilikosa vitu vingi sana vya msingi, kuliko zilivyokuwa nazo timu zingine kutoka nchi zinazoshiriki mashindano hayo. Tuchukulie kwa mfano Timu ya Taifa ya Zanzibar . Kwanza ni Timu inayojitegemea kutoka kwenye Taifa linalojitegema,( Zanzibar ) hapa vile vile Kilimanjaro Stars ni Timu inayotoka katika Taifa linalojitegemea. Zanzibar Rais wake ni Dr. Alli Mohamedi Shein, je Rais wa Tanganyika ni nani? Timu ya Kilimanjaro Stars haina Rais. Rais anayetajwa, hata Waziri Mkuu aliyekuwa mgeni rasmi siku hiyo ni wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania .

  Wakati Zanzibar wanacheza uwanjani, Wimbo wao huu ulichezwa na kikundi maalumu cha bendi cha jeshi………………………………………
  Kama hiyo haitoshi walikuwa na Bendera yao yenye rangi nne. Bendera ya Zanzibar ina rangi ya bluu bahari, ina rangi nyeusi, ina rangi ya Kijani na Njano. Sikupata ufafanuzi haraka kujua kila rangi ina maana gain, lakini ninachojuani kuwa Zanzibar walikuja na Bendera yao.

  Baadaye katika kujiuliza hayo nilifikia kujiuliza mengi zaidi. Kilimanjaro Stars kwanini haikuwa na wimbo wa Tanganyika mpaka ikatumia wimbo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Maana ilitumia wimbo ulioimbwa siku hiyo uliimbwa kuiombea Afrika na utenzi wa pili wa wimbo huo ndio wa kuiombea Tanzania.Wimbo wa Tanganyika uko wapi? Kwanini Kilimanjaro Stars wamekatazwa kutumia gari la Timu ya Taifa (Taifa Stars) lakini wakaruhusiwa kuutumia wimbo wa Muungano?.Kilimanjaro Stars inatoka nchi gani ambayo haina Wimbo, haina Rais, lakini pia haina bendera?

  Ilikuwaje Timu hii ya Kilimanjaro Stars wakakatazwa kutumia gari la Timu ya Taifa wakaruhusiwa kutumia bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Nchi yao haina Bendera? Kama haina Bendera imeshiriki mashindano hayo kama nchi wakati haina Rais, haina wimbo wake, haina bendera yake, Ni timu ambayo nchi yake haina jeshi, nchi yake haina Bunge.Imekuwaje nchi mwanachama wa kuruhusiwa kucheza CECAFA?

  Zanzibar ilikuwa ni nchi kamili. Ina Rais, anaitwa Mohamedi Alli Shein, Ina bendera yake,ina rangi nne. Ina wimbo wake, Timu ya Zanzibar ina kocha wa Timu ya Taifa,hapa kwa bahati nzuri timu yetu ya Kilimanjaro nayo ilikuwa na Kocha wa Timu ya Tanganyika, yaani Charles Boniface Mkwasa akisaidiwa na Jamhuri Kiwelu. Zanzibar ni nchi yenye jeshi, ambayo kwa mujibu wa Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inasema "kutakuwa na Idara maalumu inayohusisha Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM) , Chuo cha Mafunzo (magereza)" na Rais wa Zanzibar anaweza kuamua jambo lolote kuhusu Idara hiyo maalumu. Tafsiri fupi ni kuwa Rais wa Zanzibar anaweza kutumia jeshi lake la KMKM kulipeleka kwenye mapigano Somalia bila kumshirikisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Hii inanipa tafsiri kuwa Zanzibar ina jeshi lake nainajitegemea. Je Jeshi la Tanganyika ambapo Timu ya Kilimanjaro Stars ndo inatoka jeshi lake liko wapi? Mbona Jeshi la huko linaitwa Jeshi la wananchi wa Tanzania? Jeshi la Tanganyika lipo wapi?

  Nilirejea maelezo kuwa Katika kitabu chake Pan Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika – Zanzibar Union, Profesa Issa Shivji, mwanazuoni mashuhuri wa kikatiba na mwanafunzi wa historia ya Muungano huu alikuwa amemnukuu aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati wa utawala wa hayati Sheikh Abedi Amani Karume, Bw. Wolfgang Dourado akimnukuu Sheikh Karume juu ya nafasi ya Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano: “‘Msiwe na wasi wasi, sisi tuna haki ya kuwakilishwa katika Bunge lao lakini wao hawana haki ya kuwakilishwa katika Baraza letu la Mapinduzi’”. Mbunge gani anatoka bara yupo katika Baraza la wawakilishi?.Hii ina maana kweli Wazanzibar wanafurahi kwa kuwa wao wanawakilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini sisi watanganyika hatuna uwakilishi katika Baraza lao la wawakilishi? NIkashindwa kuelewa.

  Nikajiuliza tena Kumbe Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliposema haiwezi kuwa sehemu ya maamuzi makubwa kama yanayopendekezwa na Muswada wa katiba bila kwanza wananchi wa Tanzania na Wabunge wenyewe kupata muda wa kutosha wa kuyatafakari masuala haya yote kwa uzito unaoyastahili na kuyafanyia maamuzi ya busara ilikuwa sahihi? Kwanini tulilazimishwa kukubali mawazo ya CCM yanayoonyesha kupingana katika Uhalisia?

  Kumbe yanawezekana tu endapo Muungano huu utawekwa mbele ya wananchi ili waamue – kwa kura ya maoni - kama wanataka kuendelea nao au la; na kama wanataka kuendelea nao ni muundo gani wa Muungano wanaoutaka, lingekuwa ni jambo la busara kuliko kulaani vitu tunavyoviishi? Tunaishi Serikali Tatu lakini tunahubiri Serikali Mbili? Kwanini?  Kumbe tuna wajibu mbele ya historia na kwa vizazi vya sasa na vijavyo, kuhakikisha kwamba tunapata muafaka wa kitaifa juu ya Tanzania tunayoitaka. Hukumu ya historia, endapo sisi tutaendekeza ushabiki wa kisiasa na kufanya maamuzi ya mambo makubwa kama haya kwa kupiga kelele au kwa kuzomea wengine tunaendelea kujipalia Mkaa.

  Kwa mtazamo huo Kikwete hana uhalali wa kutusaidia kutuamulia ni katiba gani tuwe nayo,Katika Matatizo mengi ambayo hayana majibu ya Haraka Kikwete anajitwalia kwa nguvu kutuamulia hayo, eti anaaminiwa na kundi kubwa. Kikwete huyu huyu huyu ambaye Viongozi wawili wa serikali yake walisema kuwa hakuna haja ya Katiba mpya, wakiwemo mwanasheria Mkuu na Waziri wa sheria na katiba, leo huyu tumwamini. Tuna lipi la kumwamini Kikwete? Tuna lipi la kumwamini afikiri kwa niaba ya kila kundi? Kikwete anaaminiwa na kundi lipi hasa? Kundi la Wazee wa Dar es salaam aliloongea nao pale TPA, Kikwete anayesema kuwa foleni za magari Dar es salaam ni ishara ya kuwa nchi imeendelea, anaweza kweli kufikiri tofauti atuondolee kero hii, Kikwete ambaye anapingana na wananchi wengi wanaotaka wezi wa EPA wakamatwe, wahusika wa Richmond wasghulikiwe, wa meremeta watajwe. Yeye anayafanya hayo kuwa siri, je Kikwete atafikiriaje kwa niaba yetu? Kikwete anayesema dada zetu wanapata mamba kwa kiherehere leo akiamua kuweka maoni katika Katiba tutapelekwa wapi? Kikwete anayesema hahitaji kura za wafanyakazi leo anataka kutengeneza katiba kwa niaba yao . Ujasiri gani huu?
  Kikwete anajua alivyoingia madarakani kwa kuchakachua, Kikwete anajua kuwa yeye ni kigeugeu, ameshindwa kuwatimua Lowasa na Chenge japo kila siku anatamba, leo huu ujasiri atapata wapi? Uhalali huu utatokana na nini?. Atatuteuliaje tume kwa ajili ya katiba yetu. Kikwete ajitokeze atuambie Rais wetu TAngayika ni nani? Bendera yetu iko wapi? Wimbo wetu uko wapi? Jeshi letu liko wapi?. 0786-426414
  [/TD]
  [/TR]
  [/TABLE]
   
 2. Cha Moto

  Cha Moto JF-Expert Member

  #2
  Dec 1, 2011
  Joined: Jul 2, 2011
  Messages: 945
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  Makala nzuri, wataisoma
   
Thread Status:
Not open for further replies.
Loading...