Tanapa itatumia satelaiti kufuatilia ujangili wa tembo

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA) limezindua rasmi programu maalumu ya kufuatilia mienendo ya makundi ya tembo kupitia teknolijia ya kisasa ya satalaiti kama njia mojawapo ya kuwalinda kutokana na biashara haramu ya meno.

Programu hiyo inafadhiliwa na taasisi za Global Environment Facility kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) ambapo tembo 30 wanaoongoza makundi 30 katika mfumo wa Ikolojia wa Ruaha -Rungwa watavalishwa kola maalumu shingoni zenye vifaa vinavyorekodi mienendo yao kwa kutumia satalaiti. Kola hizo zina uwezo wa kufanya kazi kwa miaka mitatu mfululizo bila kubadili betri zake.

Teknolojia hiyo ya kisasa kabisa inawezesha kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya makundi ya tembo ndani na nje ya hifadhi, kujua walipo, wanapopita, kasi yao ya kutembea, sehemu wanazojificha, wanazokunywa maji na wanazopumzika. Pia kuweza kujua maeneo wanayokaa wanyama hao kwa muda mrefu, iwapo wamekufa, wamejeruhiwa, wamehama hifadhi moja hadi nyingie na taarifa nyingine nyingi zinazowahusu hivyo kuwa rahisi kwa askari wa wanyamapori kufuatilia usalama wao wa kila siku.

Ufungaji wa kola kwa wanyamapori ambao wako katika hatari ya kutoweka umefanywa na Taasisi ya World Elephant Centre (WEC) kupitia Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa Allan Kijazi anasema madhumuni makubwa ya programu hiyo ni kupata taarifa za kina za mienendo ya tembo katika mfumo wa ikolojia wa Ruaha-Rungwa ambazo zitasaidia sana kubainisha maeneo ya shoroba na mitawanyiko kwa ajili ya ulinzi wao.

Shirika la Kimataifa la UNDP kupitia ushirika wake na TANAPA na SPANEST limeshalizawadia zabuni ya kutekeleza kazi hiyo Taasisi ya World Elephant Centre ya nchini Tanzania ili kuongeza hali ya usalama wa tembo hifadhini. Akizungumzia mafanikio ya programu hiyo , Kijazi anasema kuwa eneo la mfumo wa ikolojia ya Ruaha ni kubwa na lina tembo wengi kuliko eneo jingine nchini hivyo halina budi kuangaliwa kwa ukaribu zaidi.

“Tunafurahi kwamba kola hizo zitaunganishwa na mifumo ya mawasiliano kwa njia ya satalaiti na kuliwezesha shirika kufanya kazi ya ulinzi kwa ufanisi zaidi kwa kuhakikisha kila wanapokuwepo wanyama hao, askari wanakuwepo pia,”anaeleza Kijazi na kuongeza kuwa programu hiyo ya kuwafunga kola tembo itafanyika pia katika hifadhi zote za taifa nchini. Mtafiti Mwandamizi wa WEC, Dk Alfred Kikoti anasema kola hizo zinatumia teknolojia ya hali ya juu ya kisasa ya mawasiliano ya satalaiti ya utambuzi wa jiografia ya maeneo (GPS) na kompyuta.

Dk Kikoti anasema kupitia teknolojia hiyo ya kisasa kabisa ambapo taarifa za mienendo ya wanyama pori hao zitaripotiwa moja kwa moja kwenye satalaiti na kurushwa mara moja katika chumba maalumu cha ulinzi. Anasisitiza kuwa kwa kuzingatia kwamba tembo wana tabia ya kutembea katika makundi makubwa, kola hizo zenye uwezo wa kufanya kazi kwa miaka mitatu bila kubadili betri zake zinafungwa kwa tembo 30 wanaoongoza makundi 30.

Alisema baada ya kukamilika kwa zoezi hilo linalogharimu dola za Kimarekani 15,000 sawa na Sh milioni 30 za Kitanzania kwa tembo mmoja, askari wa doria wataweza kufanya doria kwa kuongozwa na taarifa zitakazotolewa na kola tofauti na sasa ambapo hufanywa siku zote kwa kukisia tu. “Huchukua wastani wa dakika 30 kumfunga kola tembo……. Zoezi ambalo pia linahusisha matumizi ya helkopta ili kuyabaini makundi ya tembo yalipo pia uchomaji wa dawa ya usingizi kwa tembo anayefungwa kola,” anasema Dk Kikoti.

Kwa upande wake, Mratibu wa SPANEST, Godwel ole Meing’ataki anasema zoezi la kuwafunga kola tembo ni moja ya jitihada za programu hiyo kuhakikisha tembo wanalinda pia kuimarisha mapambano dhidi ya ujangili hifadhini. “Kupitia kifaa hicho askari wa wanyamapori watakabiliana kirahisi na majangili wa meno ya tembo katika azma ile ile ya kuwanusuru wanyama hao ambao wanaliingizia Taifa letu fedha nyingi za kigeni kupitia utalii,” anasema Meing’ataki.

Licha ya tembo hao kufungwa kifaa hicho pia wadau wa uhifadhi hawana budi kuendelea kukabiliana na ujangili kwa pamoja kwa ustawi wa taifa letu, “Meing’ataki anasisitiza. Tanzania ina historia ya uhifadhi wa wanyamapori tangu ilipojipatia Uhuru wake mwaka 1961 na ina uwezo wa kukabiliana na vita dhidi ya ujangili katika hifadhi.

Anaeleza kuwa Serikali ya Tanzania ililazimika kuwatumia askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika mapambano hayo dhidi ya ujangili katika jitihada za kuokoa wanyamapori hususani tembo ambao wapo katika hatari ya kutoweka kutokana na kushamiri kwa biashara haramu ya meno ya tembo. Wakati Tanzania ilipopata Uhuru miaka 52 iliyopita “ilikuwa na tembo wapatao 150,000 lakini miaka ya 1980 idadi ya tembo ilipungua na kufikia 50,000 kutokana na ongezeko na mauaji ya tembo yanayosababishwa na biashara haramu.

Anasema jitihada zimeendelea kufanyika kukabiliana na biashara hiyo ya meno ya tembo lakini tatizo kubwa limebakia katika maeneo ya mfumo wa ikolojia ya Selous – Ruaha.“Katika maeneo hayo yenye mfumo wa ikolojia ya Selous – Ruaha jitihada zinaendelea kufanyika ikiwemo kutokomeza kabisa magenge yanayojihusiha na ujangili, “ anasema “Meing’ataki .

Jitihada za kutokomeza ujangili zinaunga mkono jamii ya kimataifa ambapo Julai mwaka jana, Rais wa Marekani , Barak Obama, alitangaza rasmi marufuku mpya ya biashara haramu ya meno ya tembo nchini Marekani jambo lililowezesha kufungwa kwa soko kubwa la meno ya tembo duniani.

Mkurugenzi wa Shirika la kimataifa la World Wide Fund (WWF), Carlos Drews anasema kutoweka kwa idadi kubwa ya tembo katika maeneo yenye mfumo wa ikolojia ya Ruaha – Ruangwa kunaweza kuhusishwa na magenge ya kimataifa yanayojihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo. “Uuaji wa maelfu ya tembo katika ikolojia ya Ruaha –Ruangwa ni kielelezo tosha cha kwamba magenge ya kihalifu ya kimataifa yanajihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo ambapo jitihada za makusudi shurti zifanyike katika kukabiliana na ujangili huo kabla wanyamapori hao hawajatokweka hifadhini, “ anasema Drews .

Matokeo ya Sensa ya Tembo ya mwaka 2014 yaliyotolewa Juni mwaka jana yamebainisha kuwa nchi nzima ya Tanzania ina idadi ya tembo wapatao 43,500 katika mbuga na hifadhi zake kadhaa. Idadi hiyo ya tembo hao ni pungufu kwa asilimia 60 kutoka ile ya tembo wapatao 110,000 waliokisiwa kuwepo nchini miaka mitano iliyopita .

Sensa hiyo imefanyika nchini kote kwa kipindi cha miezi sita , kuanzia mwezi Mei 2014 hadi Novemba mwaka huu na baadaye majumuisho kufanyika mwezi Desemba 2014 hadi Aprili 2015 iliyofanywa na Taasisi ya Wanyamapori (TAWIRI) wakishirikiana na Shirika la Uhifadhi la Frankfurt (FZS) la nchini Ujerumani. Programu maalumu ya kufuatilia mienendo ya makundi ya tembo kupitia teknolojia ya kisasa ya satalaiti utaleta ufanisi katika kuimarisha ulinzi wa wanyamapori hususan tembo.

habari Leo
 
Back
Top Bottom