TAMWA-ZNZ yataka kasi mpya zaidi Usimamizi kesi za Udhalilishaji

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
157
99
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.. JAN 22,2023.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kinaishauri Serikali kuongeza juhudi katika kusimamia matukio ya udhalilishaji wa kijinsia (GBV) ili haki iweze kutendeka na kwa wakati muafaka.

Pamoja na kupigwa vita kwa vitendo vya GBV na vya watoto (VAC) bado vitendo hivyo vinaendelea na kiwango cha upatikanaji wa haki bado ni mdogo.

Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hivi karibuni imetoa taarifa ya mwaka 2022 ambapo imetaja kuripotiwa kwa matukio 1360 katika vituo vya polisi.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa ni matukio 181 tu sawa na asilimia 13 ndiyo yaliyotiwa hatiani, wakati makosa mengi bado yapo katika hatua za polisi na mahakama na matukio mengine watuhumiwa wameachwa huru na mengine hakuna hatua iliyochukuliwa wakati mengine watuhumiwa hawakupatikana.

Hivyo, kuna umuhimu mkubwa wa kuzidisha nguvu katika kusimamia matukio haya katika hatua zote ili hali ya utafutaji wa haki kwa waaathirika iweze kuleta maana zaidi.

Tunashauri taasisi husika pamoja na wananchi kutokufuta kesi kwa sababu zozote zile kwani kesi GBV na VAC ni kesi dhidi ya nchi na siyo dhidi ya mtu ama familia.

Ili kurahisisha upatikanaji wa hukumu, Serikali inahitaji kuimarisha mifumo ya mkono kwa mkono ili kesi isikilizwe sehemu moja na kupatikana kwa hukumu ambapo sheria namba 9 ya ushahidi ya mwaka 2016 katika kifungu cha 66 kimetoa nafasi ya kusikiliza kesi kwa njia ya kielectroniki.

Kama taarifa ilivyoeleza watoto wengi ndio walioathirika hivyo, sambamba na kupatikana kwa haki ni vyema waathirika kupatiwa kiwango cha kutosha cha msaada wa kisaikolojia ili ule msemo wa kutokuachwa nyuma mtu yeyote uweze kufikiwa Zanzibar.

TAMWA, ZNZ inapenda kuzipongeza taasisi husika hata hivyo kwa maendeleo haya hasa Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kwa kutoa taarifa hizi ambazo zitakuwa ni chachu ya kuchukua hatua nyengine.

Dkt.Mzuri Issa,
Mkurugenzi TAMWA ZNZ.
 
Back
Top Bottom