Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema mpaka dakika ya sasa.
Pili nipende kuwapongeza sana vijana wote wa mkoa wa Arusha na nchi nzima kwa ujumla kwa jinsi walivyojitokeza kwa nguvu zao zote kufanya maandalizi ya umoja wa kupinga udikteta Tanzania yaani UKUTA ambayo yalikuwa yafanyike Sept 1. Hongereni sana.
Agizo la kuaandaa na kutekeleza UKUTA lilitoka ndani ya chombo cha juu sana cha chama chetu yaani kamati kuu. Na tokea limetolewa kwa ngazi za kitaifa, kikanda, kimkoa, kiwilaya, kimajimbo, kikata, na mpaka kwenye misingi hakuna kijana yoyote wa CHADEMA mkoa wa Arusha aliyepinga kwa namna yoyote ile. Maandalizi yalifanyika kwa kiwango cha juu sana mpaka hapo busara za viongozi wetu wa juu zilipotumika kusitisha kwa muda wa mwezi mmoja.
Sisi vijana wa CHADEMA mkoa wa Arusha tumepokea kwa mikono miwili agizo la kusitisha kufanyika kwa UKUTA tarehe 1 Sept kwa lengo la kuwapa muda wa mwezi mmoja viongozi wetu wa kidini kukutana na mtukufu Rais Mh John Magufuli.
Tunazipongeza sana busara hizi walizozionyesha viongozi wetu wa kitaifa akiwemo Mh. Freeman Mbowe na mzalendo wa kweli mzee wetu Mh Edward Lowassa.
Sisi vijana wa CHADEMA mkoa wa Arusha tutaendelea kufanya maandalizi ya UKUTA mpaka tarehe 1 Oct kwa ngazi zote za chini kama viongozi wetu walivyotuagiza huku tukisubiri majibu ya viongozi wetu wa dini baada ya kukutana na Mh mtukufu Rais. Niwahakikishie tumejipanga vizuri na tunaendelea kujipanga zaidi.
Tumeona kiandiko kinachosambazwa na bwana mmoja anayejiita John Ole Kapara wanaojiita CHADEMA-Asili. Kinachozungumzia kutoridhishwa na hekima na busara za Mh. Mbowe na Mh. Lowassa kwa kupokea ombi la viongozi wetu wa kiimani na kuendelea kusema amewasiliana na viongozi hao wa kidini na familia ya baba wa Taifa mwalimu Julius Nyerere na kuambiwa hawajawahi kuwasiliana na viongozi wa kitaifa wa CHADEMA.
Kwanza vijana wenzangu wa CHADEMA nawaomba mlipuuze andiko hilo kwa kuwa halina mashiko kabisa hata kiuandishi na huyo bwana John Ole Kapara hafahamiki anaishi sehemu gani hapa mkoani Arusha.
Hii ni mbinu na mikakati ya CCM pamoja na vyombo vya serikali vinavyokisaidia CCM kujaribu kupunguza nguvu za vijana wa CHADEMA mkoa wa Arusha ambao wameitingisha CCM na serikali yake kwa kipindi cha mwezi mmoja na tumeshuhudia vyombo hivi jinsi vilivyopaniki ikiwemo jeshi la Polisi, Mwanasheria mkuu wa serikali, msajili wa vyama vya siasa na hata mawaziri wenye dhamana ya vyombo vya habari na jeshi la polisi. Tunawahakikishia vijana wa CHADEMA mkoa wa Arusha tuko imara na kwa hii awamu ya pili tutakuja na mikakati ya tofauti kabisa.
Baada ya kuyasema hayo kwa mara nyingine nichukue tena fursa hii kuwashukuru sana vijana wa CHADEMA mkoa wa Arusha kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiuonyesha na niwahakikishie kama kiongozi wao tuko pamoja katika kipindi hiki cha kutafuta demokrasia ya kweli katika Taifa letu.
Mungu wabariki na wazidishie HEKIMA na BUSARA viongozi wetu wa kitaifa akiwemo Mh Lowassa, Mungu ibariki CHADEMA, Mungu ibariki Tanzania.
Wasalaam
Exad Mamuya
Mwenyekiti BAVICHA mkoa wa Arusha.