Tamko la Baraza la Habari Tanzania kuhusu madai ya CCM juu ya ushiriki wake katika midahalo ya Urais

Informer

JF-Expert Member
Jul 29, 2006
1,582
6,627
nn.png

TAMKO LA BARAZA LA HABARI TANZANIA (MCT) KUHUSU MADAI YA CCM JUU YA USHIRIKI WAKE KATIKA MIDAHALO YA URAIS

Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesikitishwa na taarifa iliyotolewa Jumatano tarehe 23 Septemba 2015 na Chama cha Mapinduzi (CCM) ikipotosha ukweli na kulenga kulionyesha Baraza kama chombo kinachopendelea upande mmoja katika midahalo iliyokusudiwa ya wagombea urais na wagombea wenza wao. Baraza lisingependa kabisa kuingia katika malumbano yasiyo na tija na vyama vya siasa, lakini linapenda Watanzania waelewe kuwa kama taasisi, haliegemei chama chochote kwa kuwa jukumu lake ni kuhudumia Watanzania wote bila kujali vyama vyao vya siasa au hata kama hawana vyama. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana wadau mbali mbali walilitaka Baraza kuratibu midahalo hiyo. Baraza linatoa maelezo yafuatayo iii kurekebisha upotoshaji uliofanywa.


USULI

Mnamo Mwezi Aprili 2015, Baraza lilipigiwa simu na mwakilishi wa Nation Media Group akitaka kujua kama lingeweza kuandaa midahalo ya wagombea urais wa Tanzania mwaka huu. Katibu Mtendaji alieleza kuwa midahalo ni jambo zuri lakini haikuwa katika mpango kazi wa Baraza na hivyo pia haikuwa na bajeti. Katibu aliombwa na akakubali kuedelea kutafakari jambo hilo. Mwakilishi wa Nation Media Group aliahidi kusaidia kutafuta fedha kwa ajili ya jambo hilo ikiwa MCT wangekubali kuandaa.

Mei 20, 2015 mwakilishi wa Ford Foundation (FF) East Africa, taasisi ambayo pamoja na mambo mengine hutoa misaada kwa ajili ya kuendeleza uhuru wa maoni na vyombo vya habari alikuja Dar es Salaam na kukutana na Katibu wa MCT. Alieleza utayari wa FF kufadhili midahalo hiyo ikiwa MCT ingekubali kuiandaa. Alisema uchunguzi waliofanya ulionyesha kuwa MCT ndiyo chombo ambacho kingeweza kuvileta pamoja vyombo vya habari kushirikiana kufanya jambo hilo muhimu. Kwa maoni ya FF, MCT ilikubalika kwa wanataaluma ya habari na vyombo vyao lakini pia ni chombo ambacho kinaonekana kuwa hakifungamani (neutral) na hivyo kingeweza kufanya washiriki na vyama vyao kuwa na imani kuwa midahalo haitatumika kusaidia baadhi au kukandamiza wengine.

Tarehe 15 Julai kiliitishwa kikao cha wadau Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam chini ya uratibu wa Mwananchi Communications Ltd. Ford Foundation pia walihudhuria. Kikao hicho kiliunda kamati ya Maandalizi ya watu 10, na kikaamua kwa sauti moja kuwa mratibu wa midahalo hiyo atakuwa MCT na mwenyekiti wa Kamati atakuwa Katibu Mtendaji wa MCT akisaidiwa na Dr. Ayub Rioba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ieleweke kwamba wajumbe wa Kamati walioteuliwa walikuwa ama viongozi wa juu kabisa wa taasisi zao, ama maafisa waandamizi. Kikao kiliamua pia kwamba lengo liwe kuandaa midahalo miwili, mmoja wa wagombea wenza na mwingine wa wagombea urais. Tangu hapo mchakato wa kuandaa midahalo ukaanza.

Kwa usuli huo ni wazi basi kwamba madai yoyote ya kuwa MCT ina ajenda ya kubeba baadhi ya vyama ni upuuzi wa kusikitisha, maana MCT imetakiwa kuratibu na kuongoza kamati ya wadau ya watu huru na ajenda ya midahalo hiyo iko wazi. Wadau waliokuwa pamoja katika jambo hilo ni kutoka vyombo vya habari, jumuia ya kiraia (civil society) na sekta binafsi (private sector). Taasisi washirika ni Mwananchi Communication Ltd (MCL), ITV/Radio One, Azam TV, The Guardian Ltd, na Tanzania Media Foundation (TMF).

Nyingine ni CEO Roundtable, Internews, TAMWA, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC), Tanzania Standard Newspapers, na MCT. Kwa mantiki hiyo, madai ya kwamba MCT inahodhi jambo hilo ni vigumu kuyaelewa.


KAZI YA KAMATI NA MAANDALIZI

Kamati imefanya mikutano sita, ukiwamo mmoja na Makamu wa Rais wa Ford Foundation toka makao makuu Marekani. Kazi ya kamati, pamoja na mambo mengine, ilikuwa kuandaa na kupitisha bajeti, kutafuta fedha, kuwasiliana na vyama vya siasa, kuandaa vigezo na masharti ya ushiriki, kuandaa kanuni za mdahalo, kuandaa waendesha midahalo na kwa ujumla kuhakikisha kuwa midahalo inaendeshwa kwa kiwango cha juu kabisa cha weledi.

Kati ya mambo yaliyoamuliwa ni kwamba vyama vitakiwe kuthibitisha ushiriki kwa maandishi. Jambo hili, ambalo sasa linaonekana kuwasumbua CCM, halikukilenga chama chochote kimojawapo. Lilionekana muhimu kwa sababu zifuatazo: kwanza, uzoefu wa mshirika mmojawapo, CEO Roundtable, ulithibitisha kuwa vyama na wanasiasa wetu wana tabia ya kutotabirika. Hapo nyuma CEO Roundtable waliandaa mdahalo kwa ajili ya watangaza nia wa CCM ambapo watangaza nia watano walikubali kushiriki.

Hata hivyo, siku ya mdahalo alitokea Balozi Amina Salum Ali peke yake! Kati ya watu waliokubali kushiriki na wakaacha kutokea ni Bw. January Makamba (kwa hiyo anapashwa kuelewa kwa nini wadau walitaka uthibitisho wa maandishi). Wadau wanaichukulia midahalo ya wagombea kwa uzito mkubwa na wanategemea umakini toka kwa wahusika wote maana haya sio majadiliano ya kawaida ya kila siku katika vipindi vya redio na luninga.

Pili, wadhamini na wahisani nao pia walipenda kuona uthibitisho wa maandishi. Hii pia inatokana na ukweli kwamba huko nyuma chama kimoja kikubwa kilikuwa na mazoea ya kuzuia wagombea wake, wa ngazi mbali mbali, kushiriki midahalo. CCM wanapaswa kuwa watu wa mwisho kutolielewa jambo hili.


UKWELI KUHUSU UTHIBITISHO WA CCM KUSHIRIKI MDAHALO

Baraza la Habari, kama sekretariati ya Kamati ya Maandalizi, liliviandikia vyama vyote barua kuvialika kushiriki. Baada ya hapo, ufuatiliaji ulifanywa kwa simu na maandishi pia. Ni kweli kuwa timu ya watu wawili ilitumwa kuonana na Katibu Mkuu wa CCM kumshawishi akubali mgombea wa CCM ashiriki. Hatua hii mahsusi kwa CCM ilichukuliwa kwa sababu mbili: kwanza, CCM ni chama kikubwa na ndicho kilichoko madarakani. Mdahalo bila CCM hauwezi kupewa uzito na Watanzania; lakini pili, CCM ina historia ya kukwepa midahalo, hivyo ilionekana jitihada za ziada zifanyike.

Bahati nzuri timu iliweza kukutana na CCM na wakakubali, kwa mdomo, kuwa wangeshiriki, na kuahidi kutuma barua "kesho yake". Ieleweke kwamba ahadi za mdomo zilitolewa na vyama vyote. Na vyote vilitakiwa kuthibitisha kwa maandishi. Pamoja na kukumbushana, ni vyama vya CHAUMMA na TLP to vilivyofanya hivyo mapema. ACT Wazalendo kilithibitisha tarehe 21 Septemba. Mpaka Kamati ya Maandalizi inaitisha mkutano wa wanahabari Jumanne 22 Septemba asubuhi, CCM haikuwa imeleta uthibitisho huo. Baada ya mkutano na waandishi, CCM wakaleta barua mchana huo iliyokuwa na tarehe ya nyuma (backdated) ikisoma tarehe 13 Septemba!

Siku hiyo hiyo, Katibu Mkuu wa CCM Bw. Abdulrahman Kinana alimpigia simu Katibu Mtendaji wa MCT kulalamikia kitendo cha kamati kuwaambia wanahabari kuwa CCM ilikuwa kati ya vyama ambavyo vilikuwa havijathibitisha kwa maandishi. Alishikilia kwamba CCM ilileta barua MCT tarehe 13 Septemba, na kwamba ilipokelewa na uthibitisho uko katika dispatch book ya CCM. Katibu Mtendaji alimwomba Bw. Kinana ampelekee kivuli (photocopy) cha ukurasa wa dispatch book unaohusika iii Baraza liweze kuchukua hatua stahili dhidi ya mfanyakazi aliyepokea barua na kutoiwasilisha. Badala ya kufanya hivyo, CCM waliamua kuwaita waandishi na kung'ang'ania kuwa MCT walipelekewa barua mapema na kuwa MCT wana ajenda ya kusaidia "wale wasiotaka mdahalo".

Madai haya nayo ni vigumu kuyaelewa kwa sababu kadhaa: kwanza, MCT imetumia raslimali zake, ikiwamo muda wa maofisa wake wa ngazi ya juu, kuratibu mchakato huu ambao haukuwa katika mpango kazi wa mwaka. Kitu gani kingelizuia Baraza kukataa kuandaa mdahalo tangu mwanzo? Pili, siku ambayo Bw. Kinana alimwambia Katibu Mtendaji kuwa barua ilipelekwa na kupokelewa MCT ni Septemba 13, 2015. Lakini Septemba 13 ilikuwa Jumapili, na MCT haifungui ofisi zake Jumapili! Ni wazi basi kuwa madai haya hayawezi kuwa kweli, na bila shaka ndiyo maana CCM hawakuweza kutuletea uthibitisho wa dispatch book ili tumchukulie hatua mfanyakazi "aliyepokea" barua hiyo. Lakini pia ieleweke kwamba awali ilikusudiwa mdahalo wa kwanza ufanyike Septemba 10, 2015. Hivyo hata kama kweli CCM wangekuwa wameleta uthibitisho wao Septemba 13, bila shaka bado kungekuwa na tatizo.

HITIMISHO

Baraza la Habari Tanzania na washirika wake wanaamini kuwa midahalo ya wagombea ni jambo zuri na muhimu katika kuimarisha demokrasia ya ushindani wa kiungwana na wa uwazi. Baraza lingependa kuona utamaduni huo ukijengeka nchini kwetu. Ifike pahala midahalo hii izoeleke na kukubalika kuwa ni sehemu muhimu ya mchakato wa kampeni. Midahalo hii isitazamwe na vyama kama kete ya "kumfunga bao" mshindani wao, bali itazamwe kuwa ni uwajibikaji kwa umma. Mafikirio ya "kufunga bao" ndiyo yanayofanya vyama vinaamua leo vishiriki na kesho visishiriki, kulingana na vinavyouona uwanja wa mapambano. Sio lengo la MCT na washirika wake kutumia midahalo kumsaidia huyu au kumwangusha yule. Vyama na washirika waone kuwa ni wajibu wao kushiriki midahalo kwa ajili ya kuwapa Watanzania haki ya kuwaelewa zaidi wagombea na maono yao.

Tunajua kwamba uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mgumu. Tunaona kwamba michuano ni mikali. Kuna taharuki na misongo ya mawazo. Lakini kwa hakika, MCT haihusiki na masaibu yoyote yanayowakumba washindani wa kisiasa katika kipindi hiki.

Tunawatakia Watanzania maandalizi bora ya uchaguzi na uchaguzi wa haki na amani.

Kajubi D. Mukajanga
Katibu Mtendaji
25 Septemba, 2015
 
Simu yangu hainiruhusu kulisoma. Bila shaka wame respond tuhuma za kukaa na Kinana kujadili namna mdahalo inavyo takiwa kufanya, kama ilivyo daiwa na Makamba.
 
ccm watamtuma polepole kuwaponda mct wakidai wamenunuliwa na ukawa
 
Simu yangu hainiruhusu kulisoma. Bila shaka wame respond tuhuma za kukaa na Kinana kujadili namna mdahalo inavyo takiwa kufanya, kama ilivyo daiwa na Makamba.
Mkuu sasa unaweza kusoma.Nimerekebisha.
 
Unataka kutufanya tuamini Ccm ndio pekeewanaotakiwa kwenye mdahalo?? Ukimaanisha hamkuona haja ya kuongeaau kukutanisha vyama vyote mjadili kwa pamoja?? Kwa misingi hiyo tukiswma mliwatafuta Ccm ili muwe na mikakati ya pamoja ya kuwakandamiza wapinzani utakataa?? Kwenye uchaguzi hakuna chama kikubwa na kidogo wote wanafursa swa. Tunaamini huo ni utetezi wa kawaida kama manazi wa Ccm mlivyo zowea kutudhaeau sisi malofa. Hivyo endeleeni na midahalo sisi tunaongea na malofa wenzwtu.
 
mmmmh ni aibu kwa nchi hii kuona watu wazima wanadanganya,hata hivyo hii tayari ccm wameshatia doa na hamna haja ya mdahalo pia
 
hhahahahhah hivi hawa CCM wanaugonjwa gan? Eti wake back date waonekane walituma ushiriki wao tar 13..
 
Pole yao MCT-Lumumba siyo mchezo -uchakachuaji kwa kwenda mbele na mbaya wanakuwa wasahaulivu.
Na pengine pia walikosa Mfanyakazi wa kujilipua hapo MCT kuwa ondolea magarasha waliyoyafanya.



Madai haya nayo ni vigumu kuyaelewa kwa sababu kadhaa: kwanza, MCT imetumia raslimali zake, ikiwamo muda wa maofisa wake wa ngazi ya juu, kuratibu mchakato huu ambao haukuwa katika mpango kazi wa mwaka. Kitu gani kingelizuia Baraza kukataa kuandaa mdahalo tangu mwanzo? Pili, siku ambayo Bw. Kinana alimwambia Katibu Mtendaji kuwa barua ilipelekwa na kupokelewa MCT ni Septemba 13, 2015. Lakini Septemba 13 ilikuwa Jumapili, na MCT haifungui ofisi zake Jumapili! Ni wazi basi kuwa madai haya hayawezi kuwa kweli, na bila shaka ndiyo maana CCM hawakuweza kutuletea uthibitisho wa dispatch book ili tumchukulie hatua mfanyakazi "aliyepokea" barua hiyo. Lakini pia ieleweke kwamba awali ilikusudiwa mdahalo wa kwanza ufanyike Septemba 10, 2015. Hivyo hata kama kweli CCM wangekuwa wameleta uthibitisho wao Septemba 13, bila shaka bado kungekuwa na tatizo.
 
..waandishi wa habari wana kumbukumbu fupi kidogo.

..Mzee Yussufu Makamba, baba yake Januari, ndiye aliyezuia ccm kushiriki midahalo ktk ngazi zote.

..waandishi walitakiwa wamkumbushe Januari suala hilo, kabla ya kuanza kuzungumzia midahalo ya mwaka huu.

..mimi naunga mkono midahalo, lakini ifanyike kwa ngazi zote.
 
Back
Top Bottom