Tafakuri

654

Senior Member
Feb 1, 2012
172
40
Wanajamvi ebu tuangalie hii hoga ambayo Johnson Mbwambo ameiandika kwenye Toleo la Wiki Hii la Raia Mwema juu ya mkono wa sheria na mafisadi:WIKI iliyopita ilikuwa ni wiki ya furaha kubwa kwa wapiganaji wote wa vita dhidi ya ufisadi barani Afrika. Ni wiki ambayo fisadi papa lililokubuhu barani Afrika na lililokuwa likikwepa mkono wa sheria kwa miaka saba, lilifikia mwisho wa safari yake.

Namzungumzia James Ibori; yule gavana wa zamani wa jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta lakini lenye masikini wengi la Niger Delta la huko Nigeria.Jizi hilo, lililokuwa gavana wa Niger Delta kati ya mwaka 1999 na 2007, lilikiri lenyewe kuiibia Nigeria mabilioni ya pesa wakati lilipofikishwa katika Mahakama ya Southwork Crown ya huko Uingereza.

Lililazimika kukiri baada ya kuwasilishwa ushahidi mzito dhidi yake na polisi wa London waliouchunguza ufisadi wake kwa miaka saba na kuibuka na ushahidi kemkem dhidi yake.Kwa maneno mengine, jizi hilo lililokuwa mfadhili mkubwa wa kampeni ya urais ya Rais wa zamani wa Nigeria, Omar* Musa Yar'adua (marehemu), lililazimika kukiri ufisadi wake ili lisipewe adhabu kali baada ya kuona halina "pa kutokea".

Nina hakika tunaofuatilia masuala ya ufisadi barani Afrika tunalijua vizuri jizi hili la Nigeria ambalo mwenendo wake kisiasa ulifanana na wa baadhi ya mafisadi tulionao hapa Tanzania; hasa yale yanayojifanya yanasaidia kampeni za urais kumbe yanachotaka ni kulindwa tu na watawala dhidi ya ufisadi wao.

Kama yalivyofanya baadhi ya mafisadi yetu hayo hapa Tanzania ambayo, mpaka sasa, yamefanikiwa kuukwepa mkono wa sheria, James Ibori naye alitumbukiza mapesa ya umma aliyokwiba kwenye kampeni iliyosaidia kumwingiza madarakani Rais Yar' adua.

Ni utawala huo wa Rais Yar'adua ambao ulimlinda James Ibori; licha kwamba kila mtu katika Nigeria alikuwa akijua kuwa ni fisadi papa.Makeke yake ya utajiri mkubwa aliokuwanao uliotokana na ufisadi mbalimbali alioufanya akiwa gavana wa Niger Delta, ni pamoja na kununua magari kadhaa ya kifahari aina ya Range Rover ambayo hayapenyi risasi.

Aliyatumia magari hayo kuranda sehemu mbalimbali Nigeria akiwa na mabaunsa wake.Pia alijitengenezea utaratibu wa kifisadi wa kujiingizia mapato ya dola 250,000 kila mwezi kutoka fedha za mikataba ya mafuta ya jimbo hilo, na alifungua akaunti binafsi katika benki kadhaa za Ughaibuni alikoweka mapesa hayo.

Nchini Uingereza pekee alinunua majumba kadhaa yenye thamani ya pauni milioni 17.Lakini hakuna ufisadi usio na mwisho. Baada ya kifo cha Rais Yar'adua, Mei 2010 kilichosababisha Nigeria ipate Rais mpya, Goodluck Jonathan, "kinga" aliyokuwanayo James Ibori iliyeyuka, na asasi ya kupambana na ufisadi ya Nigeria (Economic and Financial Crimes Commission – EFCC) ikaanza kumchunguza upya.

Alipoona EFCC inakaribia kumkamata, James Ibori akatorokea Ughaibuni. Alikuja kukamatiwa Dubai na polisi wa kimataifa (Interpol) wakati akijaribu kununua ndege binafsi (private plane) yenye thamani ya pauni milioni 20.James Ibori akarejeshwa Uingereza kujibu makosa ya ufisadi ikiwa ni pamoja na kushiriki biashara chafu ya fedha (money laundering) nchini Uingereza.

Alikiri makosa hayo wiki iliyopita na hukumu yake itasomwa Aprili 4, mwaka huu.Kwa ufupi, jizi hili lililokuwa likilindwa katika uhalifu wake na Rais wa zamani wa Nigeria, lilifanya ufisadi unaokaribia pauni milioni 250.

Mali na fedha zake katika akaunti za benki mbalimbali za Uingereza sasa zitakabidhiwa kwa Serikali ya Nigeria zilikokwibwa ili zirejeshwe kwa watu wa Niger Delta ambao, licha ya utajiri mkubwa wa mafuta wa jimbo lao, wanaishi maisha ya kimasikini kwa sababu ya watu kama James Ibori!

Je, kuna chochote ambacho Watanzania tunaweza kujifunza kutoka katika sakata hilo la James Ibori? Jibu langu ni "ndiyo". Yapo mambo kadhaa ambayo Watanzania tunaweza kujifunza au kujipa matumaini.

Moja ni kwamba "kinga" ambayo mafisadi hapa nchini wanaipata kutoka kwa watawala wetu au kutoka chama tawala (CCM), si ya kudumu. Kinga hiyo inaweza kutoweka mara tu watawala wanaowalinda watakapong'oka au CCM kitakapoondolewa madarakani.

Kwa hiyo, kama wezi wa EPA, ikiwemo kampuni ya Kagoda Agriculture, wanatamba hivi sasa kwa sababu wamefanikiwa kuukwepa mkono wa sheria, wajue kuwa mambo yanaweza yakabadilika akiingia mtawala mwingine au chama kingine cha siasa kikikamata dola.

Kumbuka; "kinga" ya James Ibori iliyeyuka mara baada ya kifo cha Rais Yar'Adua, na sasa fisadi huyo anasubiri hukumu ya kifungo!Lakini kitu kingine tunachoweza kujifunza ni kwamba, tunapaswa sisi wenyewe kuiendesha vita hii dhidi ya mafisadi kuliko kutegemea Wazungu waiendeshe kwa ajili yetu.

Kwa hakika, Afrika tunaonekana wehu mbele ya Wazungu tunapowaachia wenyewe jukumu la kuwachunguza mafisadi wetu waliotuibia - tena tunawaachia kuchunguza kwa gharama zao wenyewe za pesa za walipakodi wao!

Katika suala hilo la Nigeria, kwa mfano, Idara ya Uingereza ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID) ndiyo iliyokipa fedha kitengo cha Polisi wa London kinachoshughulikia masuala ya ufisadi (POCU) kumchunguza James Ibori kwa miaka saba.

Gharama zake ilikuwa ni pauni 750,000 kwa kila mwaka!Hebu fikiria: Fisadi lenyewe ni raia wa Nigeria, fedha lilizokwiba ni fedha za wananchi wa Nigeria, na fedha zenyewe liliziiba Nigeria lilikokuwa kiongozi, lakini gharama za kulichunguza fisadi hilo ili kulikamata ili fedha hizo zirejeshwe kwa Nigeria, ni za walipa kodi wa Uingereza!

Hiyo maana yake ni nini? Hiyo maana yake ni kwamba sisi Waafrika hatujiwezi; maana tungekuwa tunajiweza, tusingeachia walipakodi wa Uingereza ndio wagharimie upelelezi wa kulitia mbaroni fisadi lililotuibia ambalo ni raia mwenzetu!Na hii inanikumbusha suala lile la ufisadi wa rada ambalo Mbunge Andrew Chenge na wenzake kadhaa wanatuhumiwa kuhusika.

Ukweli ni kwamba tuliwaachia Waingereza (kina Claire Short, DFID, SFO na wengine) kutupigania juu ya ufisadi huo hadi tumerejeshewa hiyo tuliyoiita "chenji".

Waingereza walitupigania; huku wakipata ushirikiano mdogo mno kutoka kwa watawala wetu, na walipofanikiwa, wakaturejeshea ‘chenji' yetu!Kelele za watawala wetu zilisikika tu pale Serikali ya Uingereza ilipotaka kuzikabidhi fedha hizo kwa NGOs za Tanzania.

Kabla ya hapo, watawala wetu walikuwa kimya kabisa na hawakuonyesha dhamira yoyote ya dhati ya kumchunguza Chenge!Na ndiyo maana,* mpaka leo, kina Andrew Chenge bado hawajafikishwa mahakamani kujibu shitaka lolote linalohusiana na tuhuma hizo za ufisadi wa rada.

Ni kama vile tunawasubiri tena hao hao Waingereza wafanye upelelezi ili wawakamate kina Chenge na kuwafikisha mahakamani – kama walivyofanya kwa James Ibori!Ni mambo kama hayo ya kusubiri tufanyiwe kila kitu na Wazungu ndiyo yanayonifanya nianze kuamini kuwa kweli Waafrika hatujiwezi.

Na ndiyo sababu nilimuelewa vyema Ayub Rioba alipoandika, wiki iliyopita, kwenye safu yake (Raia Mwema Na. 228) hivi:"Lakini watambue kwamba hulka ile ya Waswahili kukaa kitako wakisubiri matatizo yao yatatuliwe na mgeni, mfadhili au mhisani ndiyo inayowaletea usasa badala ya maendeleo.

Ndiyo inayowaletea wawekezaji kutoka nje wa sekta ya kilimo eti ndo wawalimie (Watanzania) chakula wale!"Rioba analalamika kwamba u-sasa umetufanya tuwategemee Wazungu kwa kila kitu kutuletea maendeleo. Labda niongeze hapa kwamba ni u-sasa huo huo ambao umetufanya Waafrika tuonekane hatujiwezi.Ndugu zangu, ni lini tutawaathibitishia Wazungu kwamba nasi tunajiweza?

Kwa nini tuwategemee Wazungu hata katika kuwakamata wezi wetu wenyewe wanaotuibia fedha zetu za umma?Kwa nini tusubiri kuelekezwanao kila kitu cha kufanya kupambana na ufisadi, na hata tunapokifanya tunafanya kwa shingo upande tu* japo tunajua ni kitu chema na chenye manufaa kwa taifa letu?

Wazungu wakisema tungeni sheria kali kuipa meno Takukuru, tunafanya hivyo, na kisha hatujali tena kama Takukuru inatumia meno hayo kung'ata mafisadi!Wakisema tungeni sheria kali ya maadili kuhakikisha viongozi wanatangaza mali zao hadharani, tunafanya hivyo kwa haraka, na kisha hatujali tena kama viongozi wanatangaza mali zao hadharani au la!

Wazungu wakisema anzisheni kitengo cha money laundering katika jeshi lenu la polisi, tunafanya hivyo haraka, na kisha hatujali kama kitengo hicho kina watendaji wa kutosha, bajeti ya kutosha na vitendea kazi vya kutosha!

Kitengo chetu hicho sasa ni taaban, na kipo kama hakipo!Katika hali kama hiyo, kwa nini Wazungu wasiamini kwamba Waafrika hawajiwezi, na hivyo kuchukua uamuzi wa kututafunia kila kitu; hata kama ni kwa kutumia kodi za wananchi wao Ulaya kutukamatia mafisadi wetu?

Je, Waafrika tunapaswa kuikubali hali hii? Ni lini Waafrika tutajiweza?Ni lini Tanzania tutawatia mbaroni kina James Ibori wetu na kuwafikisha mahakamani?

Nauliza hivyo; maana sote tunajua kwamba tunao mafisadi papa hapa nchini wanaolindwa na watawala wetu. Baadhi yao ndio waliovuta na kutia mifukoni mabilioni ya pesa za EPA; achilia mbali ushiriki wao kwenye ufisadi mwingine ukiwemo wa money laundering.

Yawezekana kabisa baadhi yao wameyalundika mapesa waliyotuibia katika akaunti za mabenki ya Uingereza na* Dubai kama alivyofanya James Ibori.Vyovyote vile; nihitimishe tafakuri* yangu ya leo kwa kurudia kusema tena kwamba, wiki jana ilikuwa ni wiki ya furaha barani Afrika kwa wapambanaji wa vita dhidi ya ufisadi.

Ni wiki ambayo mbio za miaka saba za fisadi papa, James Ibori, zilifikia ukingoni. Waingereza wanasema: One down, several to go!Tafakari.My submission
 
Duuu, mkuu nilivyo mvivu wakusoma,
Hii habari ungeifanyia editing ili tupate hamu ya kuisoma yote
 
Back
Top Bottom