Hercule Poirot
JF-Expert Member
- Mar 14, 2011
- 1,789
- 1,606
Rai ya Jenerali
Tutaendelea na maafa, zahma, misiba
Jenerali Ulimwengu
Toleo la 288
3 Apr 2013
- Lengo ni kukidhi maslahi ya wachache?
KAMA ilivyo ada, nami nalazimika kujumuika na wote walioguswa na zahma ya kuporomoka kwa jengo kubwa katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kuua binadamu kadhaa. Nami natoa rambirambi kwa wote waliopotelewa na ndugu na wana wao, na pia pole kwa wale wote waliopoteza mali zao katika mkasa huo.
Wakati tukipeana rambirambi na pole, ni vyema kuchukua fursa iliyotokana na msiba huu kufanya tafakuri juu ya yale ambayo nimekuwa nikiyajadili kwa muda sasa, hususan kuhusu ujenzi wetu na majengo yetu.
Kuporomoka kwa jengo hili majuzi ni uthibitisho mwingine wa saikolojia ya kufanya mambo yetu kwa mtindo wa mpito, fasta fasta katika haraka ya kupata faida ya sasa hivi, bila kuchelewa, kwa sababu tumo njiani kwenda kwingine. Ni nini hasa kinachotupeleka kwa kasi hiyo?
Kuna haraka ya kutengeneza fedha na kulimbikiza mali. Wenye mitaji haramu wana haraka ya kuificha katika majengo makubwa kabla hawajabainika na wale wanaowatafuta. Hili limekuwa muhimu hususan hivi sasa kwa sababu majasusi wa Marekani wanafuatilia kwa karibu mno kila fedha inayovuka mpaka kutokana na kuhofia fedha hizo kutumika katia ugaidi.
Wenye fedha moto zinazoweza kuwaingiza matatani na Serikali ya Marekani wanatafuta kila aina ya fursa ya kuziwekeza katika shughuli yoyote ambayo, juu juu, inaonekana kama halali, Kutokana na haraka hiyo ya kuficha fedha mahali ambako hazitatiliwa shaka, watu kama hawa hawana wasaa wala muda wa kufanya tafakuri ya kina wala ya muda mrefu kuhusu hicho wanachotaka kukijenga; jengo, alimradi lionekane ni kubwa, ni uficho wa kutosha.
Hivi sasa, pwani ya mashariki ya Afrika imeandamwa na matukio ya uharamia wa baharini, ambako maharamia wa Kisomali wanavamia, kuteka meli na kuzitumia kudai fedha nyingi kabla ya kuziachia meli hizo na mabaharia wake. Fedha zinazotokana na uharamia huu pia ni fedha moto ambazo zinahitaji hifadhi ambayo inapatikana katika majengo ya aina hii.
Aidha, wako watu waliofanikiwa kukwapua mapesa mengi kutokana na ufisadi unaofanyika katika idara za serikali, hapa hapa nyumbani na kwingineko. Watumishi wa serkali wamekuwa ndiyo wezi wakuu katika nchi zetu, na imekuwa kawaida sasa kwamba kila anayepata ofisi ya serikali anajipangia kuwa jukumu lake la kwanza kabisa ni kuiba kiasi anachoweza kuiba kabla ama hajastaafu ama hajakamatwa (kama kweli kuna kukamatwa siku hizi).
Wezi wa aina hii pia huhitaji uficho wa majengo ya fasta fasta kama njia ya kuosha fedha zao chafu.
Wote hawa, na wengine wengi, wanayo maslahi mazito katika majengo yanayofumuka kama uyoga katika miji kama Dar es Salaam na Nairobi, na pia wanachochea mfumuko wa bei za viwanja katika miji yetu. Kwa mfano hivi sasa, bei ya kiwanja kisichozidi nusu eka jijini Dar es Salaam kinauzwa kwa bei kubwa zaidi kuliko nyumba nzuri iliyokamilika jijini Johannesburg au Cape Town.
Kwamba wakuu wa serikali hawashitushwi na hali hii inayoonyesha uwazi uliofunguka katika soko la kuosha fedha miongoni mwetu. Soko hilo linazidi kushamiri kutokana na fedha za aina hiyo kuingizwa katika mikondo ya kisiasa kwa maana ya wenye mitaji hiyo kutumia fedha zao kununua ofisi za kisiasa.
Ununuzi wa ofisi za kisiasa nao umejenga himaya kamili ya fedha chafu katika kila ofisi ya umma, ikiwa ni pamoja na idara za usimamizi na ukaguzi, ambazo zilikwisha kuacha kazi zake muda mrefu uliopita. Nimemsikia ofisa mmoja akisema kwamba alilikagua jengo lililoporomoka mara tano kabla halijabomoka. Bila shaka maana yake ni kwamba alikwenda kukusanya malipo yake haramu mara tano.
Kwa hiyo tumejifunga katika minyororo ya kudumu ya kuwa watu wa kuomboleza siku zote kutokana na ajali ambazo si ajali, bali ni matukio yaliyosanifiwa na waroho miongoni mwetu, nasi tumeshindwa kuwashughulikia. Wachina wanawapiga risasi; sisi tunawachagua kama viongozi wetu.
Kutoka majengo ya mijini hadi barabara zetu, hali ni ile ile. Kila ninapomsikia waziri wa ujenzi akijisifu kwa kazi aliyoifanya katika ujenzi wa barabara napata kichefuchefu kwa sababu, kimsingi, hajui barabara ni kitu gani. Angejua barabara ni kitu gani, angekuwa amekwenda kuangalia wenzake wanavyojenga barabara asingesifia mizaha inayojengwa kwa mabilioni ya shilingi halafu inasombwa na mvua za kwanza baada ya kukabidhiwa kwa serikali.
Yumkin, ajali nyingi zinazotokea katika barabara zetu ambazo zimegeuka kuwa machinjio, zinatokana na uhafifu wa barabara zetu. Hapa napo tunaona ishara kwamba tunajenga kwa ajili ya muda mfupi na hatuna uwezo wa kuangalia masafa marefu.
Tujiulize kidogo, tangu ijengwe reli ya TAZARA ni wapi tumeona miundombinu iliyojengwa ili idumu kwa muda wa miaka mia moja ijayo? Ni kwa nini tunadhani kwamba tukiondoka sisi tuliopo leo, na nchi nayo itaondoka?
Hali hii ya mpito-mpito, utamaduni huu wa fasta-fasta, ujenzi huu wa haraka-haraka, ni hali inayowanufaisha wezi, matapeli na mafisadi, ambao kimsingi hawana maslahi ya kuwekeza katika masafa marefu kwani wanachotaka ni maslahi ya leo-leo.
Tutaendelea kuumizwa na vifo visivyo vya lazima kwa sababu tunatumikia maslahi ya watu wachache, kama vile tumetekwa na majangili na hatujui ni vipi tutajinasua. Majangili wametapakaa kila mahali na wana mawakala wao kila kona, na wanafanya kila jitihada tusitambue kwamba tu mateka wao.
Mfano mmoja umejitokeza tena juzi. Mkuu wa serikali katika sehemu moja ya nchi kulikotokea vifo katika machimbo yaliyokatazwa huko nyuma aliulizwa ni kwa nini watu waliachwa kuendelea kuchimba katika sehemu hiyo iliyokwisha kukatazwa.
Jibu lake lilikuwa, (najaribu kukumbuka): Ah, bwana, ninachoweza kusema ni kwamba kilichotokea kimekwisha kutokea, na kila kikitokea tunapata nafasi ya kujifunza upya ..
Si kweli. Jamii ya fasta-fasta haijifunzi lolote kwa muda mrefu. Tutalalama kwa muda, tutapiga mayowe kwa sasa, lakini kesho tutakuwa tumesahau, na tayari kupokea maiti nyingine, upya.