TaESA yaonya wafanyao kazi nje ya nchi

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,903
WAKALA wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) imewataka Watanzania kutokubali kusafirishwa pia kuajiriwa nje ya nchi pasipo kufuata taratibu za kisheria, anaandika Happiness Lidwino.

Pia, Watanzania wametakiwa kuwa makini na mawakala binafsi ambao huwatafutia kazi bila kufuata utaratibu ambapo hufanya hivyo kwa kujinufaisha wenyewe.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar ers Salaam na Jamila Mbarouk Afisa habari wa TaESA ambapo amesema, Watanzania wengi wamekuwa wakikimbilia kuajiriwa nje ya nchi baada ya kupata nafasi kutoka kwa mawakala binafsi bila kupitia TaESA kwa ushauri wa kisheria hali inayowafanya kutotambua haki zao za msingi wawapo huko.

Amesema, Watanzania wengi hawaelewi wapi pakuanzia pindi wanapopata ajira nje ya nchi hivyo kusaini mkataba ambao unawakandamiza wanapokuwa katika sehemu za kazi.

Mbarouk amesema, ili kuepuka adha hiyo ni vyema mawakala wa ajira na wanaotafutiwa ajira kuwaona TaESA kwa ushauri wa kisheria na mambo mengine muhimu ambayo wanapaswa kufahamu kabla ya kwenda nje ikiwa ni pamoja na maslahi yao.

Pia amesema, hadi sasa wamewasaidia watu zaidi ya 20,000 kupata ajira ndani na nje nchi na kuongeza kuwa , wameandaa semina kwaajili ya wanavyuo ili kuwaandaa kukabiliana na changamoto ya soko la ajira nchini.

Pamoja na kuwasaidia watu hao TaESA inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kuwatafutia watu ajira ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya watu kuliko mahitaji, waomba kazi kuwa na matarajio makubwa zaidi ya uhalisia hivyo kushindwa kupata nafasi.

“Mtu anaomba kazi anatarajia ajenge nyumba na kununua gari ndani ya miezi sita kitu ambacho hakipo na haiwezekani kwahiyo linapokuja suala la malipo inakuwa ngumu kukubaliana”amesema Mbarouk.

Mbarouk amesema, changamoto nyingine kuwa ni waajiri wengi kuhitaji watu wenye uzoefu wa miaka mingi katika nafasi wanazoomba, kutokujiamini na wengine kukosa sifa wakati wa usahili.
 
Ili kupunguza au kuondoa kabisa mikataba inayowaumiza hawa wananchi wenzetu wanaokimbilia kufanya kazi nje ya nchi kwa kupitia mawakala binafsi, kwa nini TaESA au wizara ya kazi kwa ujumla isiandae standard template ya mkataba ambao utapaswa kutumiwa na waajiriwa, waajiri pamoja na mawakala binafsi?

Ikishakuwepo hiyo template pia kuwepo na sheria kwamba ndiyo hiyo pekee itakayotumika kwenye mikataba ya ajira nje ya nchi na kama ikigundulika kwamba wakala, mwajiri au mwajiriwa yeyote amesaini mkataba tofauti na huo uliokubalika kisheria, basi wote watatu wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Kuna taarifa nyingi za wananchi wanaookotwa na kuajiriwa kiholela na kupelekwa ughaibuni hususani nchi za kiarabu ambako wananyanyaswa sana huku wakiwa hawana namna ya kukatisha na kujinasua na mikataba hiyo kandamizi.

Pia ni muda muafaka sasa kwa TaESA kutumia media kikamilifu ili kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi kuhusu taratibu za kisheria zinazotakiwa kufuatwa katika hizi ajira zinazohusisha mawakala ambao nao uchangia kwa kiasi kikubwa kwenye kuandaa hiyo mikataba iliyojaa ulaghai.
 
Serikali imefanikiwa kuwaunganisha Watanzania wanaotafuta kazi wapatao 20,000 ikiwa ni moja ya hatua ya kupunguza tatizo la ajira nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Msemai wa Wakala wa Huduma za Ajira nchini (TaESA) Bi Jamila Mbarouk wakati wa mkutano na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam.

Akizungumzia watafuta kazi waliongushwa tangu kuanzishwa kwa wakala huo Jamila alisema kuwa wengi waliounganishwa walikuwa wahasibu, Makatibu muhtasi, wataalamu wa huduma za jamii.

“Jukumu letu letu ni kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri ndani na nje ya nchi ili waweze kupata huduma hii kwa urahisi kwa kuzingatia sheria na kanuni za Ajira hapa nchini” alisisitiza Jamila.

Katika kupanua huduma ili kuwafikia watanzania walio wengi Jamila amebainisha kuwa (TaESA) imefungua ofisi za Kanda katika Mikoa ya Dodoma,Mwanza, na Arusha .

Mafanikio Mengine ni wakala kuendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo watafuta kazi 3185 ili kuweza kuhimili ushindani na changamoto za soko la ajira.

Mafunzo hayo yametolewa mbalimbali ikiwemo chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Taasisi ya Uhasibu (TIA), Chuo cha Ardhi na Taasisi ya Teknplojia Dar es salaam (DIT).

Akieleza Umuhimu wa mafunzo hayo Jamila amesema kuwa yanalenga kuwajengea uwezo watafuta kazi ili waweze kuandika barua za maombi ya ajira kwa ufasaha, kuandaa wasifu binafsi (CV) na kuwajengea uwezo wa namna ya kufanya mahojiano kwa ufanisi kwa kuzingatia mbinu za kisasa.

Kwa upande wake Afisa Kazi wa TaEsa Bw. Amani Kasale amesema kuwa baadhi ya watafuta kazi wamekuwa na kasumba ya kuchagua maeneo ya kufanyia kazi hasa yale yaliyopo katika miji mikuu hali inayozorotesha juhudi za Serikali kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri katika maeneo mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi.

Akifafanua Kasale alisema kuwa huduma ya kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri inatolewa bure kwa watanzania wote wanaotafuta ajira kwa kuzingatia sheria na Kanuni za ajira hapa nchini.

Pia Kasale alitoa wito kwa vijana wote wanaotafuta ajira kuachana na kasumba ya kuchagua maeneo ya kufanya kazi hasa yale yaliyo katika miji mikuu na kutumia fursa zilizopo maeneo ya pembezoni.

Wakala wa huduma za Ajira Tanzania TaESA Ulianzishwa kwa sheria ya wakala Na. 30 ya mwaka 1997 ikiwa na lengo la kuunganisha watafuta kazi na waajiri wenye fursa za ajira ndani na nje ya nchi.
 
Back
Top Bottom