Taazia: Rafiki ya Paul Sozingwa anamzungumza Mzee Sozigwa rafiki yake wa zamani

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,796
31,809
Mohamed Said May 12, 2017 0

DcyYzhP2SOjbvl27G-ztlUaJNhdts58kCo6fTXSQwjsvAvVn9sG-e5O7oDY0Dq9s6izBiiibhik=w328-h257-no

Paul Sozigwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Leo asubuhi mapema kabisa rafiki yangu mmoja wa Kariakoo kanifikishia taarifa katika ‘’whatsapp,’’ kuhusu msiba uliotufika wa Mzee Paul Sozigwa. Nami nikasita kusamabaza kwa kuhofu isije habari si za kweli maana umezuka mtindo wa maskhara ya kijinga. Si kama simwamini mpashaji wangu la hasha, ila wakati mwingine inapendeza kwa mtu kuchukua tahadhari.

Mzee Sozigwa ni jirani yangu nyumba kwa nyumba na wanangu wangu wanamwita babu na mkewe bibi. Kwa ajili hii basi nikifahamu ugonjwa wa Mzee Sozigwa na kulazwa kwake hospitali. Lakini kubwa zaidi ni kuwa mke wangu na binti yake walikuwa mashoga wakati wanasoma pamoja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa hali hii basi mkewe Mzee Sozigwa kwetu sisi ni mama yetu.

Haraka sana baada ya kuthibitisha msiba nikampelekea taarifa ya msiba huu rafiki yangu ambae sitamtaja jina kwa kuwa sijamuomba ruhusa ya kutumia aliyoandikia kuhusu Mzee Sozigwa kwa hofu ya kunikatalia na hivyo kupoteza historia muhimu katika nchi yetu kwani hatoandika tena haya aliyoaniandikia.

Yeye Mzee Sozigwa alikuwa rafiki yake wa karibu sana katika miaka ya mwishoni 1970 wakikutana katika mapenzi ya club ya mpira ya Pan Africa ya Dar es Salaam. Siku zile tukikaa akinihadithia mengi katika ‘’massive intellect,’’ ya Mzee Sozigwa.

Lakini raha yenyewe iko hapa. Huyu sahib yangu Mashaallah ana kichwa si cha kawaida. Nitaweka hapa aliyoniandikia kuhusu Mzee Sozigwa nanyi mpate kufaidi. Sahib yangu anasema hayo hapo chini kuhusu Mzee Sozigwa:

‘’Nilipata kuwakaribu sana na Mzee Sozigwa na tukaelewana na kupatana sana zile enzi za mpira Pan African. Mimi tukaelewana sana katika siasa za mitaani zilizoingia katika vilabu vya Yanga na Simba. Tukijadili sana tukiwa na marehemu Sam Mdee. Nikagundua huyu ni mkali sana kichwani! Jumapili moja tuliangusha mjadala juu ya makala ikitoka katika Sunday News kila wiki katika miaka ya 1970. Ilikuwa ikiandikwa kutoka Uingereza. Ikiwa na, ‘’heading.’’ "What they Say about Us." Mdee alikwama katika ‘’analysis,’’ ya nini kilichojificha, ‘’between the lines,’’ ya ile makala ambayo siku ile ilikuwa ikionesha kumsifu Mwalimu. Nyerere. Mdee aliona sifa. Mzee Sozigwa hakuona hivyo. Mie nikawa mtu wa kuduwaa, tu. Wakati huo Mdee Mwandishi na Msaidizi wa Mwalimu Nyerere Ikulu.’’

Naomba tusimame hapa nieleze machache ya makala haya kwani rafiki yangu hakueleza muktadha yake lakini mimi na yeye tulipata mara kadhaa kuijadili na akanipa michapo ya Mzee Sozigwa jinsi alivyotembea katikati ya mistari ya huyu mwandishi Muingereza.

Kilichotokea ni kuwa huyu Mwingereza alikwenda kufanya mahojiano na Mwalimu Nyerere nyumbani kwa Mwalimu Msasani. Sasa aliporudi kwao akaandika makala na katika makala hayo kwanza, akaanza kwa kumsifia Nyerere na ‘’simplicity,’’ yake akasema watumishi waliokuja kuwaletea vinywaji walikuwa hawakuvaa nguo nadhifu hivyo na ukiangalia kama vile hazikupigwa hata pasi. Akaendela na kusema na ‘’juice,’’ aliyopewa ilikuwa ya moto haikuwa baridi akigongea labda nyumbani kwa Mwalimu hakuna jokofu kiasi inabidi wageni wake wanywe vinywaji vya moto.

Lakini jinsi alivyokuwa akieleza anakupa picha kuwa anamsifia Mwalimu kwa kutopenda makuu tofauti na viongozi wenzake wa Afrika mfano wa Mobutu waliokuwa wakiishi katika maksri.’’ Makala yale yalikuwa yanapita katika hali kama hii. Ni miaka mingi sana imepita siwezi kukumbuka kila kitu. Makala hii na mfano wa hizi zikawa zinachapwa na Daily News chini ya ‘’What They Say About Us,’’ wakati ule mhariri alikuwa Frene Ginwalla mama aliyekuwa akiwajua vyema Waingereza na vitimbi vyao na kejeli zao.

Sasa Mzee Sozigwa akawa anamwambia Sam Mdee, ‘’Huyu Mzungu hasifii huyu, huyu anaponda. Msomeni vizuri mtaona.’’ Lakini kama alivyoeleza sahib yangu, Sam Mdee yeye aliona Mwalimu kasifiwa kwa kutopenda makuu. Enzi zile zilikuwa enzi za siasa ya Ujamaa. Mzee Sozigwa yeye kaona Mzungu alikuwa anamdhihaki Mwalimu Nyerere na alikuwa na sababu nzito za kukubalika.

Huyu ndiye Mzee Sozigwa. Bingwa wa vijembe na kucheza na maneno, pia mtu wa kusikia yale ambayo hayakutamkwa, mpita katikati ya mistari ya waandishi. Hakuishia hapo tu. Paul Sozigwa akikaa nyuma ya ‘’microphone,’’ katika studio anasoma alichokiandika mwenyewe utasema yuko kakaa katika jamvi anazungumza na wewe na wala haitakujia fikra kuwa anasoma utadhani anasema.

‘’Topic,’’ yoyote atakayoizungumza katika radio wewe utamsikiliza hata kama hutaki. Huwezi kubadilisha stesheni wakati Mzee Sozigwa yuko hewani. Huo ni muhali mkubwa.
Sasa hebu turudi tena kwa rafiki yangu tumsikilize anavyosema kuhusu rafiki yake Mzee Sozigwa:

‘’Sozigwa Mkurugenzi TBC. Sozigwa akipenda kunibishia kila nilipokuwa na hoja ya kutoa ‘’Public Statement,’’ redioni kuhusu, ‘’controversies,’’ baina ya club na, ‘’other authorities.’’ Kumbe sababu yake kubwa ilikuwa kuni "shape" katika, ‘’thinking approaches,’’ zangu na hoja zake. Alifika mahali akawa na, ‘’great confidence,’’ kwangu na akizipenda hoja nilizozijenga; kiasi kwamba siku moja nilikuwa na, ‘’statement,’’ nzito na nyeti.

Tulianza kubishana ofisini kwake TBC. Aliporidhika akatoa amri nii ‘’record,’’ yote na itolewe hivyo katika kipindi cha michezo. Na ili kuhakikisha inatoka vizuri, aliamrisha mtu wa zamu aende kunirekodi katika, studio za ‘’External Services,’’ kulikokuwa na vifaa vya kisasa. Akaniweka jikoni studio, na ‘’recorder,’’ akawa, ‘’next room,’’ tunaenda kwa, ‘’signal lights.’’

Mimi binafsi namkumbuka Mzee Sozigwa katika mkutano wa viongozi wa Jumuia ya Madola Singapore na TBC wakawa wanamrusha Paul Sozigwa mubashara kutoka Singapore mara baada ya taarifa ya habari ya saa mbili usiku. Utafurahi na nafsi yako. Paul Sozigwa mwenyewe hatajitambulisha kama ‘’Paul,’’ bali, ‘’Paulo,’’na ‘’Singapore,’' ataitaja kama, ‘’Singapura,’’ na si bure anafanya hivi, hicho ni moja ya vijembe vyake kwa Waingereza kulibadili jina lake likae Kiswahili. Paul Sozigwa ataeleza yaliyopitika katika mkutano kisha atachomeka kijembe kidogo. Wakiwa Singapore iko siku ilikuwa ya mapumziko hakuna kikao. Ungetegemea siku hiyo pasiwe na kipindi mubashara cha Paul Sozigwa kutoka, ‘’Singapura,’’ hata kidogo, Paul Sozigwa akaingia katika kueleza viongozi waliojimwaga kucheza, ‘’golf,’’ ile siku ya mapumziko na viongozi wenzao katika viwanja.

Ukweli ilikuwa Paul Sozigwa alikuwa anawananga viongozi wa nchi za Kiafrika kuwa wao na ‘’golf,’’ wapi na wapi hasa wakati Afrika ya Kusini imekaliwa na Makaburu na nchi nyingine za Afrika bado ziko mikononi mwa wakoloni. Sasa njoo hapo anapoaga, ‘’signing off,’’ kutoka Singapore yeye ataaga kwa kusema, ‘’Huyu ni Paulo Sozigwa kutoka Singapura.’’

Iko siku Mzee Sozigwa alikuja nyumbani kwetu baada ya kutembelewa na Prof. Emmanuel Bavu kisha akamleta Prof. Bavu kwetu. Prof. Bavu alikuwa mwalimu wetu mimi na mke wangu Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Siku zote Mzee Sozigwa tukisalimiana kijuujuu tu ninapomwona nje ya nyumba yake lakini siku ile nilikuwa karibu na yeye, kwangu mimi hii ilikuwa heshma kubwa na jambo la kihistoria. Nilimwomba tupige picha na alinikubalia.

Waandishi wa leo hasa watangazaji wana mengi ya kujifunza kwa Mzee Sozigwa.

Picha aliyoniachia Mzee Sozigwa ni kumuona kila Jumapili asubuhi bila kukosa akifuatana na mkewe kwenda kusali kwenye kanisa lao Kigamboni.


ua72xCDFYLJsD-h1uH5WhNO4dcHj8oH7ZFNXLenK9SlHt1Xq-yGOGPRGR9ur1TYgGz3nxLmGgwlqn9OXTn14aRX6a1xd3IS2m2b3NtU-VLAPxy1-ezGEF-xw1WoR7j6SiUw8UU-sYut1xQqBbp4bpXgcPQXKSadRTcsujpLTGlfJBaP6a4hduzy3hsSS3e_PQB9hgaVJ-B5iPDIDf9wb0yqlNhvQm8AW_5Fi6wZ_R2MF0zpqTg-Ov0kW8d4oU48Xl1-krfvlg9yVj-F9tPthdyfNwUkZMgLgsnIgDSljWHiCTWKGCou-JDP7jfUcMEM-iYUHrCIulzUMM9tV1ihahDuZ0uSExi2Es-QNAFBd7QDATGMSiHg0jLge-_OySEoh-xE_MLPF2fRfcU_TNalmisbg851CL2YMc7-zfnf-iG4Z4xpKihQgGDWV_A8c6kmmeVfLW6WoQPR1ZDtpTvA3xh2VrhSWsxCuX3FryMiOEJu02Cns08K1hxdr0pAihXQRzTq8-2YcOhUr_oZce1BkBygf2U8HyerQmc5wApY6PR3s3dSY8H6KH3qCZx1IrkVhijP0HmopQXsvZKh2QnEDeq56hNmnk-O_OF96uzh7SR2dAAsZ=w1038-h692-no

Kulia: Paul Sozigwa, Mwandishi na Prof. Emmanuel Bavu

Taazia
 
RiP Mzee Sozigwa! Kiboko ya JK.....alitaka kulikata jina la JK.....kilichotokea ni historia
 
Back
Top Bottom