Historia ya Suleiman Masudi Mnonji, Lawi Nangwanda Sijaona na Julius Nyerere

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,915
31,992
MAREHEMU JUMA MNONJI ALIVYONISOMESHA HISTORIA YA LAWI NANGWANDA SIJAONA NA UDUGU WAKE NA SULEIMAN MASUDI MNONJI

Utangulizi
Adam Sijali Sijaona jana ameweka kumbukumbu ya baba yetu marehemu Lawi Nangwanda Sijaona na leo ikasadifu pia Safari Channel wamerusha kipindi cha mzee wetu huyu.

Nimeshindwa kustahamili.

Nimeingia Maktaba kuangalia nini nimeandika kuhusu marehemu hawa wawili yaani kijana Juma Mnonji na Mzee Lawi Sijaona.

Maktaba ina mitaa mingi.

Hebu tufungue lango kuu la Mtaa wa Lawi Nangwanda Sijaona na Mtaa wa Suleiman Masudi Mnonji.

Leo asubuhi na mapema nimefikiwa na taarifa kuwa rafiki yangu na mzungumzaji wangu mkubwa Juma Mnonji amefariki alfajir hii. Lakini wengi walimjua Juma Mnonji kwa mapenzi yake ya mpira akiwa shabiki mkubwa kwanza wa Sunderland katika miaka ya 1960 hadi kuja kwa Simba katika miaka 1970.

Lakini nahisi katika miaka yake ya mwisho wa uhai wake Juma Mnonji naweza kuthubutu kusema kuwa mapenzi ya Simba na mpira yalipunguka na kipimo chake mapenzi yake kilikuwa chini sana.

Nasema hivi kwa sababu katika siku hizi za karibuni nilikutananae msikitini sala ya L’Asri Masjid Nuur Magomeni Mapipa wakati ambao ingekuwa zamani kama kusali sala ya L’Asr angeisalia msikiti wa Uwanja wa Taifa kwa sababu siku ile na kwa wakati ule Simba walikuwa wanajitupa uwanjani kuacheza na Yanga, mahasimu wao wakubwa katika mechi muhimu ya Ligi Kuu.

Enzi yake Juma Mnonji angekuwa katikati ya jukwaa anaitia nguvu Simba Sports Club iwafunge Yanga.

Basi baada ya sala tukawa tumesimama nje ya msikiti tunazungumza hili na lile na kwa kustaajabu kwangu kukubwa hakunigusia chochote kuhusu hii, ‘’Dar es Salaam Derby,’’ (nimesikia watangazaji wa michezo katika radio wakiita, ‘’Kariakoo Derby),’’ingawa pale tulipokuwa tumekaa radio ilikuwa inarusha matangazo yake na washabiki wamefungua radio zao kwa sauti ya juu kupita kiasi wanasikiliza mpira.

Wala Juma hakuonyesha shauku ya kutaka kusikiliza nini kilikuwa kinatokea Uwanja wa Taifa siku ile baina ya Simba na Yanga. Baada ya muda tukaagana na kila mtu akashika njia yake.

Siku chache baadae nilimuona Juma msikitini petu sala ya Alfajr na nilipomuuliza iweje muda ule yuko mtaani kwetu akaniambia kuwa alikuwa anehamia mitaa yetu. Nilifurahi sana kwani kwa hakika kila utakapokutana na Juma Mnonji atakufurahisha kwa mazungumzo yake.

Mji wa Dar es Salaam ulikuwa unajivuna na watu wawili ambao wamehifadhi katika vichwa vyao historia ya mpira wa baina ya Simba na Yanga, historia inayokwenda nyuma zaidi ya nusu karne na hawa ni Captain Malik na Juma Mnonji.

Kwa bahati nzuri mabingwa hawa wa historia mmoja Simba na mwengine Yanga. Tofauti kubwa kati ya watu hawa wawili ni kuwa Captain Malik alicheza Yanga mwishoni mwa mwaka wa 1950 hadi mwanzoni mwa 1960 wakati Juma Mnonji yeye hakupata kuivaa jezi ya Simba.

Kwa hakika kabisa na nakiri kwa dhati ya nafsi yangu hawa ni watu wangu na baina yetu yapo mapenzi makubwa sana na hawa wote kwa miaka nenda miaka rudi nimekuwa nikizungumza nao na kuokoteza mengi katika historia ya mechi za kusisimua zilizopata kuchezwa baina ya vilabu hivi viwili, katika miaka 50 iliyopita na sijaweza kuamua nani bingwa wa historia hii ya mpira, nani kamzidi mwenzake kwa kujua mengi.

Juma Mnonji ametangulia mbele ya haki amebaki Captain Malik na namuombea Allah ampe afya njema na umri mrefu.

Mara ya mwisho nilipozungumza na Juma Mnonji alinambia kuwa yuko katika mpango na TFF wa kuandika historia za wachezaji mashuhuri waliopita kuanzia enzi za Tanganyika wakati marehemu Kitwana Ibrahim alipokuwa kiongozi wa mpira.

Jambo hili lilinifurahisha sana nikajua kazi hiyo ikikamilika tutakuwa na historia nzuri sana.

Juma Mnonji si tu kuwa alikua mpenzi wa club bali aliingiliana sana na wachezaji takriban wote wa wakati wake waliopita Sunderland na Simba akawajua vilivyo.

Miaka hiyo club ya Sunderland ilikuwa Mtaa wa Congo na Mchikichi katika nyumba ya akina Shariff Pazi. Leo nyumba hii haipo imesimama gorofa refu na barabara haikuwa ya lami bali mchanga.

Congo hii ya leo ni tofauti sana na Congo ya Sunderland. Congo ile ilikuwa inapitika bila ya tabu yoyote na magari yakipishana. Leo Congo ni mtaa uliojaa maduka na biashara kubwa za kila aina.

Juma Mnonji aliwajua wachezaji kama Haji Lesso, Laasad, Shida Stua, Adam Juma, Emmanuel Mbele, Ali Kajo, Kimimbi, Hatibu Mtoto, Hamisi Kisiwa, Njunde, Chuli, Tayari Mussa, Mussa Libabu, Said Walala, Arthur Mambeta, Abdallah Kibadeni, Abbas Dilunga, Salum Ali kwa kuwataja wachache.

Si wachezaji tu aliwajua pia viongozi na washabiki wakubwa wa club, Saad Juma Mzee, Hassan Haji Abdallah, Omari Kirundu, Ayubu Kiguru, Jahazi Ali, Mzee Tamalau, Juma Liwali, Bamchawi, orodha ni ndefu na wengi katika hawa wameshatangulia mbele ya haki.

Juma Mnonji ameshuhudia Sunderand ikichukua Songambele Cup, Kikombe cha Ngo’mbe na vikombe vingi. Ameona migogoro mingi ya club mkubwa ni ule auliosababisha Simba kugawanyika na kuundwa kwa Red Star.

Lakini mimi uhusiano wangu na Juma Mnonji na kitu kilichotuleta karibu tukawa marafiki wakubwa, akawa mzungumzaji wangu haukuwa mpira ingawa sote ni wapenzi wa Simba toka enzi za Sunderland.

Tulijenga urafiki wa karibu kwa sababu ya historia ya baba yake.

Juma Mnonji ni mtoto wa Suleiman Masudi Mnonji, mmoja wa wazalendo kutoka Lindi aliyepigania uhuru wa Tanganyika bega kwa bega na Mwalimu Julius Nyerere.

Kwa ajili hii Juma Mnonji anaingia katika orodha ya watoto ambao baba zao walikuwa wapigania uhuru na watoto hawa wakabahatika kwa kiasi fulani kumjua baba wa taifa letu Mwalimu Nyerere kwa kumuona akija nyumbani kwao na akizugungumza na wazee wao.

Hili si jambo dogo kwani watoto hawa sasa watu wazima wanapofungua vinywa vyao kuhadithia historia hii hakuna ambae hatopenda kutega sikio lake kusikiliza.

Mimi na Juma Mnonji tulijuana kwa karibu miaka ya 1980 wakati nafanya utafiti wa historia ya uhuru wa Tanganyika.

Siku moja tukiwa Saigon Club aliniita pembeni akaniambia, ‘’Mohamed unajua kuwa baba yangu Mzee Suleiman Masudi Mnonji ni mmoja wa waasisi wa TANU Lindi?’’

Nilimjibu kuwa sikuwa nafahamu. Kilichotokea kuanzia hapo ilikuwa kama vile niko katika ukumbi wa senema naangalia mchezo wa kusisimua.

Juma Mnonji alianza na historia ya baba yake mtu maarufu na kujiweza katika mji wa Lindi katika miaka ya 1950 mwanzoni wakati vuguvugu la kudai uhuru limeanza Dar es Salaam.

Juma akanieleza ya kunieleza.

Kwa mtu aliyekuwa anamjua Juma Mnonji atakuwa anafahamu jinsi alivyokuwa mtu fasaha wa kuzungumza.

Akanieleza habari za Nangwanda Lawi Sijaona jinsi baba yake alivyomshawishi Sijaona wakati ule kijana mdogo aje Lindi kutoka Nachingwea aje kama msomi asaidie katika kuijenga TANU.

Juma akanambia, ‘’Mimi nilikuwa mtoto mdogo lakini nakumbuka siku Lawi Sijaona alipofika nyumbani kwetu kwa baba Mtaa wa Makonde na mkewe alikuwa amebeba mtoto mchanga mgongoni anaitwa Sijali.’’

Nilimfahamisha Juma kuwa Sijali tunafahamiana alipokuwa anaishi Dar es Salaam.

Juma Mnonji akaendelea kunipa historia akaniambia, ‘’Nyerere alifika Lindi mwaka wa 1955 na mimi nakumbuka vilivyo, shamrashamra zile kwani ofisi ya TANU ilikuwa nyumbani kwetu.

Juma Mnonji akaniambia, ‘’Nitakupa majina ya watu ambao wako hai na unaweza kwenda kuzungumzanao Lindi na watakuonyesha nyumba yetu na nyumba ambayo Mwalimu Nyerere alifikia ambayo ilikuwa inatazamana na nyumba ya baba yangu, nyumba ya fundi seremala, Issa bin Ali Naliwanda.’’

Juma Mnonji akanieleza mengi akaniambia, ‘’Mohamed safari ya pili ya Nyerere alipokuja Lindi mapokezi yalikuwa makubwa sana kwa kuwa sasa TANU ilikuwa na nguvu na ilikuwa imeenea sehemu zote za kusini hata kule ambako kanisa lilikuwa likipinga TANU hali ilikuwa imebadilika.

Juma Mnonji akanieleza kuwa Mzee Mhaiki alipojiunga na TANU kwa ushawishi wa baba yake jamaa zake wengi walimfuata katika chama.

Sisi watoto wa chuo cha Sheikh Yusuf Badi tulitolewa kwenda kumpokea Nyerere kwa zafa huku tukipiga dufu.

Safari hii Sheikh Yusuf Badi alimfanyia dua kubwa Mwalimu Nyerere usiku nyumbani kwetu na waliokuwapo katika dua ile ni pamoja na Bi. Sharifa Bint Mzee mama yake rafiki yako Ramadhani. Hii dua ilikuwa kubwa sana na aliiongoza mwenyewe Sheikh Yusuf Badi.’’

Rafiki yangu na mwalimu wangu wa historia ya TANU Lindi, Juma Mnonji akanipa majina mawili, Salum Mpunga na Yusuf Chembera, akaniambia niende Lindi nikazungumze na wazee hawa nitaipata historia kamili ya TANU Southern Province.

Mwaka wa 1993 nilifika Lindi kwa mara ya kwanza kwenda kuwatafuta wazee hawa waasisi wa harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.

Nilipokuwa naingia mji wa Lindi na basi ilikuwa kama vile narudi nyuma nauona mji wa Dar es Salaam ya miaka ya 1950. Ujenzi wa nyumba ulikuwa kama ule wa Dar es Salaam ya miaka iliyopita, watu wake na mavazi yao ni kama vile niko Mtaa wa Swahili, Dar es Salaam miaka ya 1950.

Tofauti niliyoiona na namna wanavyozungumza Kiswahili chao.

Wanazungumza kwa lafidhi tofauti sana lakini utapenda kuwasikiliza wanapozungumza.

Nilimkuta Mzee Salum Mpunga msikiti mkuu wa Lindi karibu na stendi ya mabasi.

Tulikaa kwenye baraza ya msikiti baada ya L’Asr.

Kwa takriban saa mbili hadi kuingia Maghrib mimi nilikuwa kimya nasikiliza na kuandika na siku ya pili nikaenda kumuona Mzee Yusuf Chembera.

Hakika Juma Mnonji alikuwa amenipa msaada mkubwa sana kwa kunijulisha kwa wazalendo hawa. Historia ya wazee hawa sasa ni mswada unasubiriwa kuchapwa kuwa kitabu.

Kwa masikitiko Juma Mnonji akaniambia kuwa baada ya uhuru baba yake alikamatwa na kuwekwa kizuizini.

Juma akaniambia ilikuwa simanzi kubwa sana kwao wao kama familia na anakumbuka kitu kimoja.

Iko siku alikwenda kumuona baba yake jela na baba yake akamwambia, ‘’Juma nataka uniandikie barua na hii barua umfikishie Bwana Lawi Sijaona na mwambie nimekutuma amfikishie Mwalimu Nyerere barua hii.

Nilikaa na baba na akawa anazungumza na mimi naandika maneno yake.’’

Barua ile Juma aliniambia kuwa Mzee Masudi Mnonji baada ya salamu alimuomba Mwalimu Nyerere amfahamishe sababu ya yeye kufungwa.

Akaendelea kusema kuwa kama ana kosa yeye angeshukuru kufikishwa mahakamani ili ahukumiwe.

Juma alikuwa akinisomea barua hii ghibu ikitiririka kwa namna ambayo msikilizaji ilikuwa inahuzunisha na kutia simanzi.

Anasema Sijaona alipofika Lindi alimwendea na kumpa barua ile aifikishe kwa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.

Juma alinifahamisha kuwa hana hakika kama ile barua Sijaona aliifikisha kwa Mwalimu Nyerere lakini haukupita muda mrefu Mzee Masudi Suleiman Mnonji aliachiwa.

Allah amghufirie ndugu yetu Juma Masudi Suleiman Mnonji dhambi zake na amweke mahali pema peponi.
Amin

Mohamed Said
28 Julai 2018

1732567806098.jpeg

1732567859415.jpeg

1732567903620.jpeg

1732567935241.jpeg

Picha ya kwanza Lawi Nangwanda Sijaona na Adam Sijali Sijaona, Juma Mnonji, Bi. Sharifa bint Mzee na wajukuu zake na kibao cha Mtaa wa Sheikh Mohamed Yusuf Badi Lindi.​
 
Sheikh Mohamed Said,

..kila nikisoma historia unayotufundisha napata picha kwamba Wakoloni wa Kiingereza walikuwa na utu kuliko wana'CCM wanaotutawala leo.

..namuangalia Tundu Lissu Makamu Mwenyekiti wa Chadema na ulemavu aliopewa. Namlinganisha na Mzee John Rupia Makamu Mwenyekiti wa Tanu.

..linganisha kesi ya Mwalimu Nyerere, na kesi ya Freeman Mbowe, au Juma Duni na wenzake. Kesi za wapinzani dhidi Mbowe, na Duni, hukumu yake kama zingeendelea ilikuwa ni KIFO au MAISHA. Kesi ya Mwalimu Nyerere hukumu ni faini au jela muda mfupi.

..Watanganyika tunapitia hali mbaya sana kisiasa kuliko wakati wa wakoloni Waingereza. Hao wazee waliopigania tujitawale wangefufuka leo na kuona kinachofanywa na Tanu / CCM yao naamini wangefadhaika sana.
 
Sheikh Mohamed Said,

..kila nikisoma historia unayotufundisha Zapata picha kwamba Wakoloni wa Kiingereza walikuwa na utu kuliko wana'CCM wanaotutawala leo.

..namuangalia Tundu Lissu Makamu Mwenyekiti wa Chadema na ulemavu aliopewa. Namlinganisha na Mzee John Rupia Makamu Mwenyekiti wa Tanu.

..linganisha kesi ya Mwalimu Nyerere, na kesi ya Freeman Mbowe, au Juma Duni na wenzake. Kesi za wapinzani dhidi Mbowe, na Duni, hukumu yake kama zingeendelea ilikuwa ni KIFO au MAISHA. Kesi ya Mwalimu Nyerere hukumu ni faini au jela muda mfupi.

..Watanganyika tunapitia hali mbaya sana kisiasa kuliko wakati wa wakoloni Waingereza. Hao wazee waliopigania tujitawale wangefufuka leo na kuona kinachofanywa na Tanu / CCM yao naamini wangefadhaika sana.
Joka Kuu,
Kwa Waingereza mbona umekwenda mbali?

Nilifanya mahojiano na Sheikh Haidar Mwinyimvua.

Aliniambia kuwa yaliyotokea baada ya uhuru kupatikana wengi yaliwashangaza.

Walifadhaika sana.
 
Joka Kuu,
Kwa Waingereza mbona umekwenda mbali?

Nilifanya mahojiano na Sheikh Haidar Mwinyimvua.

Aliniambia kuwa yaliyotokea baada ya uhuru kupatikana wengi yaliwashangaza.

Walifadhaika sana.
TEWA SAID TEWA MEMBER WA ''WEDNESDAY TEA CLUB,'' TAA, MUASISI WA TANU, RAIS WA EAMWS, WAZIRI SERIKALI YA KWANZA, BALOZI, MBUNGE NA KIONGOZI WA WAISLAM WA TANGANYIKA

(Mohamed Said Historia, Siasa na Maendeleo Tanzania December 01, 2016 0)

Utangulizi
Picha hizi zinatoka katika Maktaba ya Said Tewa mtoto wa marehemu Tewa Said Tewa ambae kwa miaka mingi amekuwa akiishi Denmark.

Said ni rika langu na tumekua sote katika mitaa ya Dar es Salaam ya miaka ya 1960 hadi Said alipoondoka Tanzania na kwenda kuishi Ulaya.

Said kila akija Dar es Salaam atafika nyumbani kwangu kunisalimia.

Said anasema ameniletea picha hizi baada ya kuona juhudi zangu katika kuhifadhi historia ya Tanzania na viongozi wake baba yake akiwa mmoja wao iliyokuwa karibu ipotee.

Hayo maandishi, ‘’caption,’’ katika baadhi ya picha ni mwandiko wake mwenyewe Mzee Tewa.

Picha nilizopokea ni nyingi sana zikimwonyesha Tewa Said Tewa katika mengi lakini nimeona nichukue hizi chache ambazo zitamuunganisha yeye na matokeo muhimu zaidi katika historia ya Tanzania na katika nafasi yake kama kiongozi wa Waislam akiwa Rais wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) upande wa Tanzania.

Binafsi nimejifunza mengi kutoka kwa Mzee Tewa tukiwa tumekaa sisi wawili tu nyumbani kwake Magomeni Mikumi akinihadithia historia ya uhuru wa Tanganyika.

Msikilize Mzee Tewa:

Tewa Said anakumbuka siku kabla ya uchaguzi pale Ukumbi wa Arnatouglo, kati ya Abdul Sykes na Nyerere April, 1953.

Abdulwahid Sykes alikwenda nyumbani kwa Tewa jioni.

Wakati huo Tewa alikuwa akikaa mtaa wa Aggrey na Swahili, si mbali sana kutoka nyumbani kwa Abdulwahid Mtaa wa Aggrey na Sikukuu.

Abdulwahid alimwambia Tewa maneno haya kuhusu mabadiliko ya uongozi ambayo waliamua kuyafanya katika TAA ya kumpa Julius Nyerere urais wa chama hicho kisha kuunda TANU na Nyerere aongoze harakati za kudai uhuru:

‘’Tewa, kesho tunakwenda kumpa huyu mtu, Nyerere, mamlaka ya kuendesha nchi hii.

Kuanzia hapo, mara tu tutakapomchagua kutuongoza hakuna namna tena ya kumnyang'anya madaraka tuliyompa.

Hatumfahamu vizuri sana lakini natumaini kila kitu kitakwenda sawa.’’
 
Back
Top Bottom