Taazia: Buriani Arthur Mambeta mwana Sunderland na Simba

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,922
30,271

Sunderland 1966 - 1968
Kulia waliosimama: Adam Athman, Arthur Mambeta, Emmanuel Mbele,

Haji Lesso, Shida Stua, Hassan Mlapakolo, Yusuf Maleta, Mussa Libabu,
Mbaraka Salum, Hamisi Fikirini

Waliochuchumaa: Kimimbi, Njunde, Ali Kajo, Said Walala, Hamisi Kibunzi

Marehemu Athman Kilambo alikuwa mzungumzaji wangu sana na nilifahamiana na yeye mwaka wa 1972 nilipoanza kazi East African Cargo Handling Services (EACHS). Kilambo alinisomesha mambo mengi sana katika mpira wa hapa nyumbani na Afrika ya Mashariki. Katika moja ya kazi niliyopewa kufanya nilipoajiriwa bandarini ilikuwa kuitumikia Hydra Club.

Hii ilikuwa club ya mpira kwa wachezaji wa mpira wa timu ya bandari na kwa ajili hii nikafahamiana na wachezaji wengi sana wa mpira wa wakati ule kwa karibu sana na kwa hakika hawa ndiyo walikuwa, ‘’the cream,’’ katika mpira wa Tanzania. Katika wachezaji niliowafahamu ambae alikuwa hana tabasamu usoni kwake alikuwa marehemu Mustafa Mabuge wa Cosmo. Lakini wakati mimi naanza kazi Mustafa alikuwa amestaafu kucheza. Kinyume chake Arthur kila alipokuja ofisini kwangu yeye alikuwa mtu wa kutabasamu na akipenda sana kuvaa vizuri. Katika wavaaji wa sifa pale bandarini katika wachezaji mpira alikuwa Arthur Mambeta na Abdulrahman Lukongo.

Nakumbuka nilimshughulika Arthur Mambeta kumpatia mkopo wa pikipiki kupitia Hydra. Hii club ya Hydra ilikuwa na fedha nyingi sana ‘’revolving fund,’’ ambayo wanachama wake wakikopeshwa kufanyia mambo tofauti. Ingawa mimi nikipenda Sunderland ambayo mwaka 1971 ikawa Simba nilikuwa na marafiki wengi sana Yanga. Sunday Manara alikuwa mtoto mwenzangu nah ii ilitufanya tuwek karibu zaidi kuliko wale ‘’senior players.’’ Kilambo akifahamu kuwa nilikuwa ‘’hasimu,’’ wake lakini hili halikuathiri uhusiano wetu hata chembe, zaidi ilizidisha sana mapenzi kati yetu na yeye akipenda sana kunitisha vipi Yanga itakavyotuadhibu katika Nationa League na wao kuchukua kikombe.

Kilambo alikuwa na akili safi sana ya kujua mambo hasa ya mpira. Ninapoangalia picha za zamani za Yanga na Simba toka enzi ya Sunderland kumbukumbu nyingi zinanijia. Asubuhi leo na kwa kweli kutoka jana nimekuwa napokea picha za Arthur mtandaoni na kumbukumbu nyingi zimenijia kwani katika picha hizo wengi wametangulia mbele ya haki.

Nimemuona Arthur Mambeta akicheza mpira viwanja vya Mnazi Mmoja katika club ndogo katika miaka ya mwanzoni 1960 kama Kahe na Liverpool Arthur akicheza pamoja na vijana wenzake wa wakati ule kama Hamisi Kisiwa, Hussein Shariff maarufu kwa jina la Italo, mchezaji wa Ethiopia, Bruno, Abdallah Mzee aliyekuwa mzungumzji wangu sana, Hamisi Dracula kijana mtanashati sana, Yusuf Salum Maleta, Shida Stua, beki mstaarabu sana, Emmanuel Mbele kuwataja wachache. Hawa walikuwa kaka zangu kwa umri na wakati ule bado walikuwa hawajanyanyukia kucheza Yanga wala Sunderland. Miaka ikapita na hawa wakaja kuwa wenzangu tukikaa pamja na kuzungumza na wakati ule sasa walikuwa wanacheza katika club hizi kubwa na timu ya taifa.

Nathubutu kusema kuwa katika hawa wachezaji ambao nimewataja hapa Arthur Mambeta alikuwa ndiyo bingwa wao katika kila idara kuanzia, ‘’dribbling,’’ ‘’ball control’’ na ‘’art’’ yenyewe ya uchezaji mpira.

Kilambo Alipata siku moja kuniambia kuwa wao Yanga walikuwa wanawataka sana wachezaji wawili kutoka Sunderland waje Yanga kuongeza nguvu - Arthur Mambeta na Hamisi Kibunzi. Lakini alikuwa akinambia, ''Tuliwataka sana wale waje Yanga lakini wale watoto wakipenda sana Sunderland hata kama tungefanikiwa kuwachukua wasingeweza kucheza Yanga kama wanavyocheza Sunderland.''

Kilambo akimuusudu sana Arthur. Alikuwa akisema Arthur akiwa katikati Simba na Yanga wakicheza, mpira unapendeza sana. Halikadhaika Kilambo akiniuliza, ''Hivi nyinyi Simba kwa nini mnampanga yule Bobeya? Yeye ndiyo anaharibu mpira. Kilambo akiusudu sana mpira kutembea katika majani na Bobeya alikuwa, ''hard tackler,'' akitumia nguvu katika uchezaji wake.

Kila siku asubuhi mimi na Kilambo tukinywa chai kwenye mgawa mmoja na huo mgahawa ulikuwa mashuhuri kwa wachezaji wote wa Yanga na Simba wa zamani na waliokuwapo kwa wakati ule. Nakumbuka sana Kilambo alikuwa kipenda kunywa chai, chapatti na ngisi. Mimi toka udogo wangu ngisi hakuwa upepo wangu. Siku moja Kilambo akaniuliza kama nimepata hata kumuonja ngisi. Nikamjibu kuwa bado. Basi siku hiyo akanambia hebu muonje. Nikala kipande kutoka katika sahani yake. Kilambo alicheka sana maana yule ngisi tulimmaliza pamoja. Kutoka siku ile ngisi akaongezeka katika samaki ninaowapenda.

Mchezaji wa Cosmo ninaemkumbuka ukimtoa Mustafa Mabuge, aliyekuwa bandarini alikuwa Jamil Hizam maarufu kwa jina la ‘’Denis Law,’’ mchezaji wa Manchester United. EACHS ilikuwa ikiajiri wachezaji wengi sana wa mpira. Wakati ule Branch Meneja wa EACHS alikuwa Mzee Thabit Awadh na Principal Training Officer alikuwa Abdallah Lupatu wote hawa wametanguliwa mbele ya haki. Lupatu alikuwa Yanga lakini alikuwa habagui akitoa kazi kwa wote na khasa watoto wa mjini. Ilikuwa yeye ndiye akiwafanyia usaili pale Cargo Training School iliyokuwa Azania Front (sasa Sokoine Drive).

Arthur aliingia kazini miaka michache akitokea nadhani East African Airways wakati ule mimi tayari alinikuta mwenyeji siku nyingi. Baba yake Arthur Mzee Mambeta alikuwa akifanya kazi EACHS upande wa Medical.

Nakumbuka siku ya maziko ya Kilambo nilikuwa na Hamisi Kibunzi tukielekea Kisutu makaburini baada ya kutoka Msikiti wa Manyema tulikomswalia Kilambo, nikamweleza habari hii ya yeye na Arthur kutakiwa Yanga. Kibunzi akanambia hakuwa anajua habari hizi.

Ile mechi ya 1973 Arthur alinieleza kwa kinywa chake kuwa yeye aliamua atacheza na Kitwana. Kitwana alikuwa mchezaji ambae alikuwa na vurugu kubwa sana kwenye goli la adui na alihitaji mtu wa kukaanae kumtuliza.

Iko siku asubuhi tunakunywa chai mimi Arthur, Kitwana na jamaa wengine. Katika maongezi wakawa jamaa wanahadithia ile mechi ilivyokuwa. Kitwana akawa anacheka anamwambia Arthur kuwa alikuwa akimchezea rafu hampi nafasi. Arthur akajibu akasema,'' ''Kitwana lakini si nilikuomba radhi baada ya mechi?''

Nilikutana na Arthur kama mara mbili tatu hivi ofisini kwa Khalid Abeid na tukizungumza na kukumbushana mambo ya zamani.

Mtu wa kwanza kunifahamisha maradhi ya Arthur alikuwa Hamisi Kisiwa kiasi cha kama miaka miwili iliyopita na mahali tulipokutana ilikuwa Magomeni Mapipa karibu na ulipokuwa mgawa wa Shomvi ‘’Michuzi Mikali.’’ Michuzi Mikali ulikuwa mgahawa wa shabiki mkubwa wa Yanga pale Magomeni Mapipa akiitwa Shomvi na likuwa bingwa wa kuku wa kukaanga kwa ugali au wali. Ukitoa ile kuwa ukienda kula Michuzi Mikali utakutana na wachezaji nyota wa wakati ule, kilichofanya magahawa huu uwe maarufu ni ile pilipili aliyokuwa akitengeneza Shomvi kwa ajili ya kulia kuku. Pale niliposimama na Kisiwa niliweza kuiona nyumba aliyokuwa akiishi Arthur Mambeta na nakumbuka niliwahi kujanae pale kanipakia katika pikipiki yake.

Kipaji cha Arthur hakuna asiyekijua kwa wale waliopata kumuona akicheza katika miaka ya 1960 hadi 1970 mwishoni. Arthur akiwa tayari kapumzika, ''competitive footbal,'' alikuwa akija kufanya mazoezi Jangwani timu ya Hydra na mimi nikicheza kunyoosha maungo.

Siku zile club zote Dar es Salaam zilikuwa na kiwanja cha kufanya mazoezi Jangwani. Hapa Jangwani nilikuwa namuona Arthur kwa karibu sana na kwa kweli kile kipaji chake kilikuwa hakina mpinzani wala mfanowe. Mpira akiwanao huwezi kumnyang'anya.

Arthur Mambeta atakumbukwa kwa miaka mingi katika soka la Tanzania.
 
Sheikh Mohamed, I really enjoy kusoma articles zako zinazohusu mambo ya Dar ya miaka hiyo, kwangu ni hazina kubwa.
Pumzika kwa amani Arthur Mwambeta.
 
RIP Arthur. Bro Said Mungu akupe maisha marefu ilimu hii unayotupatia inatujenga mno, kwani kuijua kweli humuweka mtu huru.
 
Asante sana Legendary Mohammed Said kwa taazia hii juu ya Mwana Simba Arthur Mambeta.

Lakini kubwa kabisa nje ya taazia hiyo ni kuniwezesha kufahamu jina la mtaa wa Sokoine Drive la Zamani kwamba ilikuwa ni Azania Front. Siku zote nilikuwa najiuliza kwa kuwa Sokone ni mtu aliyekuja karibuni je zamani mtaa ulikuwa ukiitwaje? Nafahamu Samora Avenue was Independence Street lakini sikuwa nafahamu jina la Sokoine Drive.

Ahsante sana Sheikh wetu na Allah azidi kukupa maisha marefu na kumbukumbu zaidi utulishe.
 
Asante sana Legendary Mohammed Said kwa taazia hii juu ya Mwana Simba Arthur Mambeta.

Lakini kubwa kabisa nje ya taazia hiyo ni kuniwezesha kufahamu jina la mtaa wa Sokoine Drive la Zamani kwamba ilikuwa ni Azania Front. Siku zote nilikuwa najiuliza kwa kuwa Sokone ni mtu aliyekuja karibuni je zamani mtaa ulikuwa ukiitwaje? Nafahamu Samora Avenue was Independence Street lakini sikuwa nafahamu jina la Sokoine Drive.

Ahsanta sana Sheikh wetu na Allah azidi kukupa maisha marefu na kumbukumbu zaidi utulishe.
Chamakh,
Amin na ahsante sana.
Independence Avenue kabla ya uhuru 1961 ilikuwa ikijulikana kama Acacia Avenue.
 
Sheikh Mohamed, I really enjoy kusoma articles zako zinazohusu mambo ya Dar ya miaka hiyo, kwangu ni hazina kubwa.
Pumzika kwa amani Arthur Mwambeta.
Copper,
Amin.
Ahsante sana kaka.
 
Ahsante kwa kumbu kumbu hii ya enzi hizo. Hii yanga unayosimulia ni ya enzi za Mzee Mangara Taabu!! Kilambo Athuman akijulikana kwa jina la "Baba Watoto". Centre half wao akiwa Abdulhaman Juma na defenders Kitenge na Omari Kapera. Goalkeeper wao Elias Michael. Baba watoto wakisaidiana pale nyuma na Hassan Gobos. R.I.P Arthur Mambeta wa Sunderland.
 
Sheikh Mohamed Said pale Morogoro kuna mtaa unaanzia MASIKA na kuelekea ndani kukutana na Madaraka Rd, ule unaitwa MLAPAKOLO!

Katika kikosi kilichotamba cha RELI Morogoro, kilichokuwa na Marehemu Duncan Butinini, Gaspa Lupindo, Peter Mjata, Juma Salum, Hamad Masenga, Fikiri Magoso na wengineo, alikuwako Mchezaji akiitwa RAMADHAN KILAMBO, je wana nasaba na Kilambo the legend?
 
Sheikh Mohamed, I really enjoy kusoma articles zako zinazohusu mambo ya Dar ya miaka hiyo, kwangu ni hazina kubwa.
Pumzika kwa amani Arthur Mwambeta.
Bw.mohamed hebu tupe historia za wachezaji wafuatao
1.Mohamed bakari Tall
2.Ezekiel Greyson Jujuman
 
Sheikh Mohamed Said pale Morogoro kuna mtaa unaanzia MASIKA na kuelekea ndani kukutana na Madaraka Rd, ule unaitwa MLAPAKOLO!

Katika kikosi kilichotamba cha RELI Morogoro, kilichokuwa na Marehemu Duncan Butinini, Gaspa Lupindo, Peter Mjata, Juma Salum, Hamad Masenga, Fikiri Magoso na wengineo, alikuwako Mchezaji akiitwa RAMADHAN KILAMBO, je wana nasaba na Kilambo the legend?
Slim,
Sijui.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom