BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,126
By Herieth Makwetta, Mwananchi
Dar es Salaam. Uhaba wa sukari umeendelea kushika kasi nchini baada ya wafanyabiashara wa maduka ya jumla kuanza kuuza kwa rejareja, huku ile nyeupe kutoka India ikipatikana kwa urahisi katika baadhi ya maduka.
Utafiti uliofanywa na waandishi wa gazeti hili jijini Dar es Salaam, Kahama mkoani Shinyanga na wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, bei ya sukari imeendelea kuwa juu huku upatikanaji wake nao ukiwa wa shida.
Baadhi ya wafanyabiashara walihojiwa walibainisha kuwa bei ya sukari kwa kilo, inaanzia kwa Sh2,500 hadi 3,900, na bei hiyo imetofautiana kulingana na aina ya sukari. Sukari nyeupe inauzwa kwa Sh120,000 kwa mfuko wa kilo 50 na Sh2,500 kwa kilo kwa bei ya rejareja.
Raymond Sanga, muuzaji wa duka la jumla alisema sukari inayopatikana kwa wingi hivi sasa ni nyeupe ambayo inauzwa kwa bei nafuu kidogo ikilinganishwa na iliyozoeleka ya rangi ya kahawia.
Wakazi wa Tabata Segerea walikutwa wakinunua kwa foleni katika duka moja lililokuwa likiuza sukari ya kahawia, huku maduka machache ya jumla yakiuza ile nyeupe.
Mfanyabiashara Imani Mkwama alisema kuwa: “Wateja wangu ninawauzia kwa Sh2,900 kwa kuwa nimeinunua bei ya juu, hii ni pungufu kulinganisha na bei zilizozoeleka za Sh3,000 mpaka Sh3,500 kwa kilo moja,” alisema Mkwama.
Mjini Moshi, bei ya sukari bado ipo juu na mkazi wa Majengo kwa Mtei, Paul William alisema sukari inauzwa kwa Sh3,900 katika maduka ya rejereja. “Huku mtaani kwetu bado ni tatizo, Serikali inatuambia inasambaza sukari, tunaihoji hiyo sukari wanaisambazia wapi hadi haitufikii?” alihoji.
Bertha Shayo alisema kuwa mfuko wa kilo 50 wa sukari wananunua kwa Sh130,000.
Kutoka Kahama, sukari iliyosambazwa na Serikali imejaa madukani ikiuzwa Sh85,000 kwa mfuko wa kilo 50 sawa na Sh1,700 kwa kilo na maduka ya rejareja Sh2, 600 kwa kilo. Akielezea tofauti ya sukari nyeupe na kahawia, Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudensia Simwanza alisema kuna sukari nyeupe ambayo hutumiwa majumbani na ipo inayoingia nchini kwa ajili ya viwandani.
Alisema ni vigumu TFDA kubaini sukari iliyopo sokoni kwa kuwa bado hawajapita kuangalia iwapo ni ile inayofaa kwa matumizi ya majumbani.
Alisema sukari ya kahawia ina madini kama magnesium, calcium, potasium, chuma ambayo yanakuwa na kazi maalumu mwilini, wakati ile nyeupe ya viwandani haina madini hayo.