Suala la mchanga tunahitajika kusimama pamoja

talentbrain

JF-Expert Member
Oct 5, 2009
1,187
759
Habari wadau,

Nimelazimika kuandika uzi huu baada ya kusoma nyuzi nyingi kuhusu suala la Mchanga linalotokana na report ya tume maalum iliyoundwa na Mh. Rais P. Magufuli.
Kumekuwa na mgawanyiko wa hali ya juu ambao kama taifa tungeweka maslahi ya nchi kwanza yasingekuwepo. Kwakuwa kumekuwa na hoja mbalimbali nitazitumia hoja hizo kujadili suala hili.

TUMETOKEA WAPI?
Sekta ya madini ni sekta ambayo haina muda mrefu hapa nchini. Baba wa taifa alizuia kuchimbwa madini kwakuwa nchi ilikuwa haijajiandaa vya kutosha kuendesha sekta hii. Ila kutokana na mahitaji ya nchi na kwenda na muda ilifikia muda tukashindwa kuepuka suala la uchimbaji mkubwa wa madini. Tukichunguza kwa kina, matatizo mengi katika sekta hii na nyingine kwa mfano gas na viwanda vinatokana na sheria na sera zetu hasa tunapowavutia wawekezaji. Ni muda huo ambapo tuliweka sheria mbovu kwa kujua au kutokujua ambapo kwa masikitiko makubwa tulikubali kupewa mrabaha kidogo sana katika mapato ya madini. Kama hiyo haitoshi tukalazimika kuruhusu mchanga usafirishwe nje ya nchi kwa sababu tu kama smelter ingejengwa hapa nchini uzalishaji usingekuwa na faida kwakuwa kiwango cha uzalishaji wa mchanga ni kiasi kidogo kama 60.000 tones per year. Katika michakato hii na udhaifu tuliouonesha ili kuvutia wawekezaji, Tanzania imekuwa ikiambulia kidogo sana kama rasilimali tulizopewa na Mungu na kinachosikitisha zaidi ni kwamba tutabaki na mashimo huku nchi ikisalia masikini.

NANI MWENYEMAKOSA?
Kumekuwa na hoja kadhaa mfano wa zile za Lisu, Zitto, Chenge n.k zikionesha wapi tulikosea. Nami napenda kusema wapi tulipokosea:-
1. Tulikosea katika kuanza kwa shughuli hizi ambapo hatukujifunza kwa wengine waliofanikiwa au waliokosea. Kuna mifano ya nchi kadhaa zimekosea katika suala la madini kama sisi kwa sasa ili hatukutumia studies hizo kuepuka yanayotokea sasa.
2. Sheria zetu kwa makusudi ziliwapendelea na kuwapa uga mpana wawekezaji kujichotea huku tukiambulia kidogo tukiamini kuwa huenda njia hiyo ndio kuvutia wawekezaji. Kuna baadhi ya viongozi wasomi sana walifaidika katika hili ambapo waliandaa mazingira ya yanayotokea sasa. Katika hili wanasiasa kwa kujua na au kwa mihemko walikuwa wakikomoana ili kufanikisha adhma ya wawekezaji.
Kwa mantiki hii, ni wazi kwamba kama nchi tulikosea. Kupita kwa musuada wowote bungeni hata kama mimi au wewe ulisema SIIIIIIIOOOOOO haimaanishi inakuondoa katika waliopitisha muswada huo. Hivyo kama taifa kila mtu alikosea.

KINACHOFANYIKA SASA NI SAHIHI?
Kwa miaka mingi sana tumekuwa tukilalamika kuwa tunapunjwa au kuibiwa sana katika sekta ya madini. Kupunjwa na kuibiwa kwenyewe kunatokana na makosa yetu tangu awali. Katika hali ya kushangaza tumekuwa tukipewa 4% ya faida ila hawa wawekezaji ni kama hata hicho wanakiona kikubwa. Kama nchi tukubali kuwa hiki kinachosemwa kama wizi kinafanywa kwa kufuata sheria na kanuni. Ni wataalamu wetu kupitia TMAA wamekuwa wakiidhinisha kusafirishwa kwa mchanga kwa kukubaliana na vipimo. Ni wataalamu wetu wamekuwepo tangu migodini kuhakikisha kama taifa tunapata hata hicho kidogo. Ni wazi kuwa kama kuna upunguzaji wa vipimo, wataalamu wetu wamekuwa wakihusika.

TAARIFA ZA UTAFITI WA TUME NI SAHIHI?
Kuna hoja juu ya taarifa ya tume ya Mh. Rais kuwa sahihi au sio sahihi. Tumeona nyuzi nyingi hapa zikikosoa au kuunga mkono taarifa ya tume. Usahihi au ukosefu wa report unaweza kuthibitishwa kwa report nyingine. NImeona ACACIA wakiipinga report ya tume kuwa viwango walivyotoa ni vya juu sana. Kwahiyo naona kumbe kuna pa kuanzia hasa pande mbili zilete wataalamu independent wapime chini ya pande mbili zikijiridhisha kuona nini kilichomo kwenye mchanga. Suala hili kwa kiasi kikubwa kwa ACACIA linaondoa uaminifu kwa nchi na wateja wake huko nje ndio maana imetangwazwa kushuka kwa bei ya hisa za ACACIA kwa kiasi kikubwa.

WATANZANIA TUSIMAMIE WAPI?
Kwa namna yeyote ile waathirika katika suala hili ni sisi. Na kama ACACIA watakwenda mahakamani na kuishinda serikali ni wazi tutakaolipa ni sisi. Na kama nchi itaweza kufanikiwa katika hili ni wazi nchi italipwa mapunjo yote na hivyo tutapata faida kama nchi.

Zaidi ya kupata au kokosa katika hili, sisi wananchi inatakiwa tuwe wazalendo kwa nchi yetu. Uzalendo ni pamoja na kusimama upande wa nchi katika masuala yanayoihusu nchi na kutoa ushauri kwa njia sahihi ili kuepuka matatizo. Natambua tupo watu wenye mawazo, misimamo na itikadi tofauti. Ila linapokuja suala la nchi ni vema sote tukaungana. Yanayoporwa ni madini ya nchi hii hivyo tusimame pamoja. Huu ni muda wa vita, tukianza kubishana wenyewe tunampa adui nafasi ya kuelewa udhaifu wetu.

Niwashauri watanzania wenzangu, hasa wale wenye nafasi ya kuishuri serikali wafanye hivyo. Hatuwezi kuvumilia kuona tunaibiwa kweupe. Na kuhusu makosa ya kisheria tuliyoyafanya toka mwanzo ni wasaa sasa kwa kila mzalendo na hasa watunga sheria kuhakikisha sheria za madini zinafanyiwa marekebisho.

Mungu Ibariki Tanzania
 
Back
Top Bottom