Source of law in Tanzania

Comred Mbwana Allyamtu

JF-Expert Member
Jun 28, 2016
348
847
SHERIA NA VYANZO VYAKE TANZANIA.

Na. Comred Mbwana Allyamtu (CMCA)
Friday-06/05/2022
Kalema Tanganyika Katavi

Sheria ni kanuni zinazoongoza shughuli na mahusiano ya watu waishio katika jamii fulani.

Sheria inaelezea haki na wajibu wa wanajamii hao, inaweka masharti juu ya mambo fulani, kuelezea makosa na adhabu iwapo makosa ama masharti yaliyotajwa na sheria yatakiukwa, kwa mfano Sheria inayoweka mashariti na kueleza makosa na adhabu zake kwa Tanzania ni Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 (Tanzania Penal Code Cap 16)

Kuna aina mbili za sheria Tanzania, ambazo ni...
1. Sheria za madai (Civil Law)
2. Sheria za jinai (Criminal Law)

Katika sayansi ya sheria (Jurisprudence) kuna kitu huitwa vyanzo vya sheria, au source of law, ili sheria iweze kuwepo kama nilivyoeleza hapo juu, lazima kuwepo na chanzo chake kinacho izalisha hiyo sheria yenyewe

Vyanzo vya Sheria Tanzania....

1. Katiba
Katiba ni chanzo kikuu cha sheria, kwa lugha nyingine huitwa Sheria Mama, ni wajibu wa haki za wananchi kubainishwa katika katiba husika.

Sheria zote za nchi hupata nguvu kutoka katika katiba ya nchi, hivyo basi kama kuna sheria ambayo haikubaliani na Katiba basi itakataliwa na Mahakama kuu kwani sheria zote ni lazima zifuate Katiba ya nchi.

2. Sheria zilizoandikwa (Statutes/Written Laws).

Hii ni sheria ambazo zimeandikwa na kupitishwa na bunge au chombo kingine cha kutunga sheria.

Sheria hizi huwa katika madaraja mawili, sheria kuu na sheria ndogo au sheria ya uwakilishi

I. Sheria Kuu
Kwa Tanzania, sheria hutungwa na bunge, Sheria ambazo hutungwa na bunge lenyewe huitwa sheria kuu, Mfano wa Sheria Kuu ni, Sheria ya Ardhi za Vijiji, 1999.

Hata hivyo, bunge laweza kutunga sheria inayoruhusu chombo kingine au mtu kutunga sheria (Delegate legislation).

Il. Sheria Ndogo au Sheria Ya Uwakilishi

Hii ni Sheria ndogo au sheria ya uwakilishi ni ile ambayo hutungwa na mtu, chombo au mamlaka yoyote yale ambayo yameruhusiwa kutunga sheria hiyo kwa mujibu wa Sheria kuu iliyopitishwa na Bunge.

Mfano mmoja wapo wa sheria ndogo ni ile inayotungwa na Halmashauri za Wilaya/Manispaa au Waziri.

3. Sheria Zinazotokana Na Maamuzi Ya Mahakama (precedence/Case law).

Vyanzo vingine vikuu vya sheria ni maamuzi ya Mahakama ya rufaa au Mahakama kuu ambazo hufuatwa na mahakama za chini (Subordinate Court) katika kuamua kesi za aina hiyo.

Kwa hiyo, maamuzi yanayotolewa katika Mahakama hizi ni chanzo kingine cha sheria kwa mahakama za chini haswa katika kesi au mashauri yanayofanana.

Hali kadhalika, Mahakama kuu haina budi kufuata maamuzi ya Mahakama ya Rufaa kwani majaji wa mahakama hizi huitafsiri na kuzifafanua zaidi sheria.

4. Sheria Za Kawaida (Common Law).

Hii huitwa Sheria ya Kawaida ni sheria ya kitamaduni ya Uingereza ambazo baadaye ziliingizwa katika mahakama kwa nchi nyingi zilizowahi kuwa makoloni ya Uingereza.

Sheria hizi zinafanana na sheria zetu za kimila kwa vile hata sheria hizi zimetokana na misingi iliyofuatwa na watu.

Asili ya sheria za kawaida katika mfumo wa kisheria wa Tanzania ni baada ya kutumiwa nchini India wakati wa utawala wa kikoloni wa mwingereza.

Kwa mfano kanuni za adhabu za India, kanuni za madai za India, Sheria ya ushahidi ya India n.k. Mahakama za kikoloni za Tanganyika (kama Tanzania ilivyojulikana zama hizo) zilitumia kanuni hizi ambazo zilitungwa Uingereza katika utoaji haki kwenye mahakama zetu.

5. Sheria Za Kimataifa (International Law).

Hizi ni Sheria za kimataifa huongoza mahusiano kati ya mataifa, zinaunda haki na majukumu ya mataifa kwa raia na inaweza pia kuunda haki za watu binafsi.

Sheria za Kimataifa pia zinaweka kiada na viwango ambavyo vinatakiwa kuheshimiwa na kufuatwa na wananchi, mfano sheria ya kimataifa za mazingira, sheria za Kimataifa za bahari n.k

HATA HIVYO, kwa Tanzania sheria za kimataifa haziwezi kutumika nchini Tanzania bila utaratibu maalumu wa kuziingiza na kuzitumia ufanyike, Lazima zipitishwe na Bunge na zijumuishwe kwenye sheria za ndani ya nchi, au Tanzania isaini makubaliano ya Kimataifa kuridhia sheria hiyo au mkataba, itifaki au azimio hilo.

6. Sheria Za Mila.

Hii ni Sheria za Mila za jamii zetu nchini, Sheria hizi zinaweza kutafsiriwa kama kanuni za kimila au jadi ambazo zinatumika katika mkondo wa kisheria.

Sheria hizi zinatambulika na kukubaliwa na jamii yoyote na kupata nguvu ya kisheria kupitia katika serikali na katiba ya nchi.

HATA HIVYO, Ili kutumiwa, ni lazima zithibitishwe na kuhalalishwa katika mahakama za kisheria pale ambapo kuna kesi zinazohitaji kutumika kwa kanuni hizo ili kuamuliwa.

7. Sheria Ya Kiislam.

Sheria hizi ni zile zinazotokana na dini ya kiislam, ambazo zipo katika muuongozo wa kitabu kitakatifu cha Quran na vitabu vya Sunna ya uislam.

Sheria hii utambuliwa na Tanzania kama moja ya kanuni na utaratibu wa usimamizi na utoaji haki katika jamii.

HATA HIVYO, Ili kutumiwa kwa Sheria ya kiislam ni lazima zithibitishwe na kuhalalishwa katika mahakama za kisheria pale ambapo kuna kesi zinazohitaji kutumika kwa kanuni hizo ili kuamuliwa. Moja ya kesi ambazo sheria hizo zinaweza kutumika ni katika Mirathi pekee yake.

Ndimi Comred Mbwana Allyamtu
 
Back
Top Bottom