figganigga
JF-Expert Member
- Oct 17, 2010
- 25,689
- 55,661
Katibu Mkuu wa KNUT Bw Wilson Sossion.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) sasa anataka wanafunzi wawe wakiruhusiwa kutumia simu za mkononi wakiwa shuleni.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) Bw Wilson Sossion sasa anataka wanafunzi wawe wakiruhusiwa kutumia simu za mkononi wakiwa shuleni. Pendekezo hilo limetolewa huku katibu huyo akizidi kumkosoa Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang’i kwa kutoa sheria mpya za kuzuia wizi wa mitihani ambazo kulingana na Bw Sossion ni za kuumiza wanafunzi.
Bw Sossion alisema si busara kuzuia wanafunzi kutumia simu za rununu shuleni ilhali Serikali ya Jubilee inashinikiza uimarishaji wa mbinu za kidijitali katika masomo na uendeshaji wa taifa. “Tusiendelee kuwafanya wanafunzi kama wafungwa ilhali tunaazimia kuleta mageuzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano nchini,” akasema Alhamisi kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.
Bw Sossion alitoa pendekezo hilo akisema linafaa liwe chini ya mpango wa serikali ya kuwezesha elimu kidijitali na kuongeza kwamba zitasaidia wanafunzi kusoma vyema zaidi. Mbunge wa Mathioya Bw Clement Wambugu alipinga pendekezo hilo na kusema litachangia kukithiri kwa udanganyifu katika mitihani ya kitaifa na fujo. Akizungumza Mathioya wakati wa siku ya kutoa ushauri kwa wanafunzi, alisema simu zimekuwa zikutumiwa kusambaza karatasi za mitihani katika miaka michache iliyopita kupitia kwa mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp.
Mbunge huyo aliongeza kuwa simu zitafanya wanafunzi wasiwe makini kwa masomo yao na akataka viongozi wajihadhari na matamshi wanayotoa. “Kama mzazi, siwezi kuruhusu watoto wangu waende shuleni na simu na ninomba viongozi wakome kutoa matamshi kiholela wakitafuta umaarufu kutokana na mambo ambayo yatadhuru watoto na sekta ya elimu,” akasema. Kuhusu mpango huo wa kushauri wanafunzi, Bw Wambugu alisema ulileta mafanikio bora katika shule za msingi na upili.
Kupunguza fujo
Alisema ushauri unaotolewa umechangia kupungua kwa uhalifu kwani wanafunzi wengi huhitimu kujiunga na shule za upili na vyuo vikuu. “Ushauri huu pia umesaidia kupunguza fujo na tunaomba wazazi na walimu kushirikiana kwa karibu na wanafunzi ili kama kuna tatizo lolote walitambue mapema na kurekebisha kabla mambo yaharibike zaidi,” akasema. Mkuu wa elimu katika kaunti ndogo ya Mathioya Bw Saru Dabaso alitoa wito walimu wawe wakihamishwa mara kwa mara kwa sababu wakikaa sana katika shule moja huwa inaathiri matokeo ya mitihani.
“Wakuu wa shule nyingi ni wenyeji na wamekuwa katika shule hizo kwa muda mrefu na hivyo kusababisha kukosekana kwa mabadiliko,” akasema. Alilaumu pia wazazi wanaoachia wazee jukumu la kulea watoto wao na kusema hiyo imechangia kwa utovu wa nidhamu kwa watoto.