KITABU kinachozungumzia kashfa ya kihistoria ya ununuzi wa rada, uliowahusisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) Dk. Idriss Rashidi, kimechapishwa.
Ndani ya kitabu hicho, kilichokuwa kikusubiriwa kwa hamu na wengi wa watanzania kiko katika soko, kinachoitwa
The Shadow World Inside The Global Armrs Trade, mtunzi Andrew Feinstein ameeleza kwa kina mchakato ulivyoendeshwa, ukiwahusisha watu wa madaraka na kada mbalimbali ambao ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.
Blair anatajwa katika kitabu hicho kuwa ndiye aliyemshawishi aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Benjamin Mkapa, kununua rada hiyo kutoka kampuni ya kutengeneza silaha ya Uingereza BAE-Systems.
Anasema mwandishi wa kitabu hicho katika sehemu moja ya maandishi yake: "Wakati akipigia chapuo, Tume yake ya Afrika (Commission for Africa) juu malengo ya kuwa na utawala bora katika Afrika, Tony Blair alimshawishi Rais wa Tanzania, moja ya nchi masikini kabisa duniani kununua rada ya kijeshi kwa bei ya zaidi ya dola za Marekani milioni 40.
Wakati huo Tanzania ilikuwa na ndege nane tu za kivita, nyingi zikiwa katika hali mbovu kiasi cha kuzifanya zisitengenezeke. Rushwa ya karibu dola za Marekani milioni 10 inadaiwa ililipwa kwenye mpango huo."
Kwa mujibu Andrew Feinstein, akiba ya dhahabu iliyohifadhiwa katika BoT ambayo, hata hivyo, thamani yake halisi haijafahamika, ndiyo iliyotumika kufadhili upatikanaji wa mabilioni ya fedha kwa njia ya mkopo kutoka Benki ya Barclays, ili kufanikisha ununuzi wenye utata wa rada ya kijeshi.
Katika taratibu za benki kuu mbalimbali duniani, dhahabu imekuwa ikihifadhiwa kama moja ya njia za nchi husika kujimudu dhidi ya mitikisiko ya kiuchumi. Tanzania ni kati ya nchi inayotumia mfumo huo wa kuhifadhi dhahabu.
Source :
The Shadow World: Inside the Global Arms Trade: Amazon.co.uk: Andrew Feinstein: Books