Kanungila Karim
JF-Expert Member
- Apr 29, 2016
- 20,741
- 25,681
Ni mara nyingi sana tumekuwa tukihitaji sana baraka kutoka kwa Mungu japokuwa tumekuwa tukikataa kufanya yale yanayoweza kumfanya Mungu atubariki katika maisha yetu. Muda mwingi sana tumekuwa wavivu sana na wabinafsi kuwasaidia watu wenye matatizo mbalimbali. Hebu niambie, ni mara ngapi umekuwa na fedha mfukoni halafu ukakutana na ombaomba barabarani na kumpita kama haujamuona na hata wakati mwingine kusema kwamba uwepo wao unachafua jiji?
Kusaidia watu mbalimbali katika maisha yetu ndicho kitu pekee ambacho kitamfanya Mungu wetu atubariki na kutuongezea vitu katika maisha yetu. Inakuwa ngumu sana kwa Mungu kunipa baraka na wakati mimi mwenyewe ni mchoyo wa kuwapa wengine.
Hebu naomba ujiulize swali hili, ni mara ngapi umekwishawahi kuamka asubuhi ukanywa chai na kuanza kufikiria kwamba kuna watu hata shilingi hamsini hawana mifukoni mwao?
Hivi umekwishawahi kutoa hata mswaki mmoja kumgawia mtoto yatima mmoja ambaye ameonekana kukosa mswaki? Hivi umekwishawahi kumuona mtoto yatima akiwa amevaa mavazi yaliyochakaa na wewe kuvua shati lako na kumgawia? Kwa nini haujafanya hivyo? Unajishtukia au? Katika kipindi ambacho tunataka Mungu atupe baraka katika maisha yetu hatuna budi kufanya yale ambayo yataonekana kuwa mema katika macho yake.
Majumbani kwetu tunakula mpaka wakati mwingine tunasaza Hatuwafikirii wale ambao wamekuwa wakilala usiku bila kula, tumeshindwa kuwafikiria wale ambao wamekuwa wakishinda na mavazi yaliyochakaa. Hali inaonekana kubadilika sana, ndani hasa chumbani kwako umekusanya nguo nyingi sana na mwisho wa siku nyingine unaamua kwenda kuzichoma moto kwa sababu zinaonekana kuchakaa katika macho yako.
Ndugu yangu! Amini kwamba nguo hiyo hiyo ambayo imechakaa, kuna mtu kwake inaonekana kuwa mpya sana, kwa nini usiende kumpa? Mara nyingi tumekuwa watu wa kujisifia sana kwamba tumekwenda sehemu fulani kula bata, tunajisikia fahari sana kila tunapowaambia watu wa Facebook kwamba tumetumia fedha nyingi sana katika sehemu za starehe. Hivi kweli tunakumbuka kuwasaidia watu ambao mpaka katika kipindi hicho hawajawahi kushika hata shilingi 1000 mikononi mwao tena ikiwa fedha yao ya uhalali?
Tumewasahau watoto yatima. Kila siku tumekuwa watu wa kusema kwamba Wazungu wanapata fedha sana na mafanikio bila kukumbuka kwamba wao wamekuwa mstari wa mbele kuwasaidia watu waliokuwa na matatizo. Najua kwamba inawezekana unaishi peke yako, umepanga nyumba au unaishi nyumbani kwako. Najua kwamba unapokea mshahara mkubwa sana au biashara zako zinakuingizia fedha nyingi sana. Hivi unakumbuka kwamba haujawahi kumgawia mtoto yatima hata shilingi elfu kumi ya kununulia nguo?
Wakati umefika, wakati ambao itatupasa kumlazimisha Mungu atubariki katika maisha yetu. Hatumlazimishi kwa kumwambia, bali hapa tutamlazimisha kwa vitendo. Mungu anatuona hapa tulipo, Mungu anayaona maisha yetu, tunapoamua kuwasaidia watu wenye matatizo mbalimbali, Mungu hawezi kutuacha hivihivi, naye atakusaidia tu kwani huwa anapenda kumuona mtu mmoja akimsaidia mwingine.
Huu ni wakati wako wa kuonyesha mabadiliko, huu ni wakati wa kuamua kukitoa kiasi fulani kwa ajili ya kuwasaidia watoto fulani. Kama unajiona unaingiza fedha nyingi na za kutosha, basi jaribu kumsomesha hata mtoto yatima mmoja kwani kwa kufanya hivyo Mungu ataweza kukubariki kila siku, kwa kufanya hivyo, Mungu atazilinda fedha zako katika matumizi yako, Mungu atakulinda kwa kukupa afya njema, pia atakuongezea kwa kila kitu kizuri unachokihitaji na hata kile ambacho haukuwa na uwezo wa kukipata. Fanya hivyo, saidia watu wenye matatizo mbalimbali, Mungu atakutangulia.