Slaa: Nitajinyima watoto wasome | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Slaa: Nitajinyima watoto wasome

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Anaruditena, Oct 19, 2010.

 1. A

  Anaruditena Member

  #1
  Oct 19, 2010
  Joined: Apr 29, 2010
  Messages: 52
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Slaa: Nitajinyima watoto wasome Send to a friend Tuesday, 19 October 2010 07:47 0diggsdigg

  Mussa Mkama, Shinyanga
  MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa jana alibadili hali ya hewa mkoani Shinyanga baada ya kuutikisha mji kiasi cha kusababisha bendera za CCM zilizotundikwa kwenye maeneo mbalimbali kushushwa, huku akisema kuwa yuko tayari kunyimwa kura kwa kosa la kulazimisha watoto kwenda shule.

  Mabasi ya daladala, pikipiki na magari madogo ya abiria (taksi) zinazotoa huduma ya usafiri mjini hapa zilifungwa bendera za Chadema na kufanya usafiri uonekane kama mali ya chama hicho.

  Baadhi ya pikipiki ambazo ni maarufu kama bodaboda zilisitisha huduma kwa ajili ya kumsindikiza mgombea huyo wa urais wakati akielekea kuhutubia mkutano wa kampeni.

  Jina la Dk Slaa lilitawala mji mzima huku baadhi ya wananchi wakieleza kuwa ikitokea kura za mgombea urais wa Chadema zimezidiwa na mgombea urais wa CCM, wataandamana kwa madai kuwa wanaamini kuwa CCM haipendwi na wananchi wa mkoa huo.

  "Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini asiposhinda, basi CCM itakuwa imetenda hujuma kubwa kwa kuwa haina wafuasi na sisi tumeichoka. Chama ni Chadema peke yake ndicho chenye matumaini nasi, CCM imeshindwa kutukomboa," alisema mmoja wa waendesha pikipiki hizo.

  Mji wa Shinyanga ulianza kutawaliwa na shamrashamra kuanzia majira ya saa 4:32 asubuhi wakati wakazi walipokuwa wakijiandaa kwenda kumpokea huku mazungumzo ya watu kwenye vikundi mbalimbali yakimuhusu mbunge huyo wa Karatu ambaye ameamua kupambana katika vita ya kuelekea Ikulu.

  Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Joshoni, Dk Slaa aliendelea kuzungumzia matumizi ya mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete akidai kuwa ametumia mamilioni ya fedha za walipa kodi kusafiri kwenda Ulaya kunywa chai na kurudi.

  Alisema haiwezekani kwa rais anayependa wananchi wake kutumia fedha nyingi kwenda Marekani ambako alidai alipewe nyandarua na rais wa wakati huo, George Bush wakati vyandarua hivyo vinatengenezwa nchini.
  Dk Slaa alisema hana ubaya na mwanachama wa CCM bali yeye anapambana na Kikwete, Yusuf Makamba, Pius Msekwa na vigogo wa serikali, kwa sababu hao ndio chanzo cha Watanzania kuishi maisha mabovu yasiyo na mwelekeo.
  "Rais wa nchi unakwenda Ulaya kunywa chai kwa kodi za wananchi halafu unarudi kwa kujigamba kuwa umepewa neti za mbu... ni jambo la aibu kubwa. Ameishia kukaa kuzungumzia wawekezaji tu na kusahau kushughulikia masuala ya wananchi, utadhani alipigiwa kura na wawekezaji," alikejeli Dk Slaa.
  Alisema kitendo cha Kikwete kuendelea kugharimia uchapishaji wa picha za kampeni ni matumizi mengine mabaya ya fedha, akidai kuwa mgombea huyo wa CCM amekuwa rais kwa miaka mitano na kila mtu anamjua.
  "Kwa nini fedha hizo zisitumike kwenye huduma za afya kama kweli wao (CCM) wana uchungu na wananchi wao," alihoji Dk Slaa.
  Kwa mujibu wa Dk Slaa, serikali inayojali wananchi wake ipo radhi kujinyima ili wananchi waweze kunufaika na wawe na maisha mazuri.


  Alisema serikali ya CCM imetengeneza wakimbizi wa ndani kwa kuwafukuza wafugaji wa jamii ya Kisukuma ambao sasa wamelazimika kuendelea kulipa faini ya Sh5,000 kwa kila mfugo katika mikoa ya Rukwa, Mbeya na Morogoro
  .
  "Tukipata ridhaa ya wananchi kuongoza nchi, tutarejesha mabwawa yote tuliyoachiwa na wazungu, ili mifugo yetu iweze kupata huduma zote. Hatutaki supermarket (maduka makubwa ya rejareja) zetu ziwe na nyama kutoka nje, wakati uwezo tunao na Tanzania ni nchi ya tatu Afrika kwa ufugaji wa ng'ombe," alisema Dk Slaa.
  Dk Slaa alisema Baba wa Taifa, Marehemu Julius Nyerere alisema kuwa ufunguo wa maisha ni elimu, lakini elimu iliyopo sasa ni ya kuanzia darasa la kwanza hadi la saba ambayo haimsaidii mhitimu kupata ajira.

  Dk Slaa alisisitiza mpango wa chama chake wa kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.
  "Afadhali uninyime kura kwa sababu ya kumlazimisha mtoto wako kwenda shule. Lakini sipo tayari kuona watoto wakiendelea kuchunga na kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu," alisema Dk Slaa.

  Alisema Chadema inataka kutoa elimu hiyo bure ili kufuta matabaka yaliyopo kati ya walionacho na wasio nacho.
  "Dk Slaa alisema taifa halijengwi kwa maneno ya Kikwete majukwaani... kama Kikwete ana uwezo wa kutumia fedha... kusambaza picha bure nchi nzima, kwa nini elimu ishindikane kupatikana bure," alihoji.

  "Mwaka huu hadi kieleweke; hakuna wizi wa kura wala nini; sisi wenyewe tutakuwa walinzi wa kura kituo hadi kituo mpaka dakika ya mwisho kwa sababu tuna matumaini makubwa kwamba Dk Slaa Shinyanga anapata kura nyingi kuliko mikoa yote," alisema mmoja wa wananchi waliofurika kwenye mkutano huo alipoongea na Mwananchi.
   
 2. Mallaba

  Mallaba JF-Expert Member

  #2
  Oct 19, 2010
  Joined: Jan 30, 2008
  Messages: 2,560
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 133
  SLAA: ELIMU KIDATO CHA NNE ITAKUWA LAZIMA
  Akisaka kura mkoani Shinyanga jana, Dk. Slaa, amesema akiingia madarakani, elimu ya awali hadi darasa la 14, itakuwa ya lazima kwa mtoto wa Kitanzania na kwamba, mzazi yeyote atakayeacha kumpeleka mtoto wake shule atakamatwa.
  Dk. Slaa alisema hayo wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa mjini Shinyanga na vitongoji vyake waliofurika katika mkutano wa hadhara wa kampeni zake katika Uwanja wa Joshoni, jana jioni.
  Alisema Serikali ya Chadema itaweka utaratibu huo baada ya kubainika kuwapo kwa baadhi ya Watanzania, hususan wanaotoka jamii ya wafugaji katika mkoa wa Shinyanga na kwingineko, kuwa tayari kutoa ng'ombe dume kwa walimu ili watoto wao wasiende shule, badala yake wakachunge mifugo.
  "Nilipokuwa (kijiji cha Malampaka (iliyoko wilaya ya Maswa, mkoani Shinyanga) nimekuta kuna baadhi ya wafugaji Wasukuma wana tabia ya kupeleka dume kwa mwalimu ili mtoto wake asiende shule. Nimesema mzazi wa aina hiyo tutamkamata," alisema Dk. Slaa na kuongeza: "Ni afadhali ninyimwe kura, lakini mtoto wa Mtanzania aende shule." Wakati Dk. Slaa akiendelea kuhutubia mkutano huo, kundi la vijana waliohudhuria, lilipaza sauti na kusema: "Kila siku ni dagaa, tumechoka, tunataka mabadiliko."
  Hali hiyo ilimfanya Dk. Slaa kukatiza hotuba na kushirikiana na askari polisi pamoja na walinzi wa chama, kufanya kazi ya ziada kuwatuliza vijana hao walioonekana kupandwa na jazba.
  Kauli hiyo ilitolewa na vijana hao baada ya Dk. Slaa kuueleza mkutano huo kuwa alipokuwa katika kijiji cha Malampaka jana asubuhi, alitokwa na machozi baada ya kukumbuka jinsi mkoa wa Shinyanga, ulivyojaliwa utajiri wa kila kitu, yakiwamo madini, pamba na mifugo, lakini wananchi wake wananuka umaskini.
  Katika mkutano huo, Dk. Slaa alitoa pole kwa vijana watatu waliokimbizwa hospitali baada ya kuanguka kutoka juu ya mti na kujeruhiwa.
  Vijana hao walilazimika kupanda juu ya mti ili kufuatilia hotuba ya Dk. Slaa, baada ya uwanja wa mkutano kufurika watu na kukosekana nafasi.
  Dk. Slaa alisema pembeni mwa wilaya ya Maswa, kuna eneo la Mwadui, ambako kuna mashimo yanayoashiria kuchimbwa kwa almasi iliyotapakaa kila mahali.
  Alisema pia juzi akiwa ndani ya helikopta katika anga ya Wilaya ya Kahama, mkoani humo alishuhudia mgodi wa Buzwagi, akaona mashimo, huku matani kwa matani ya madini yakichimbwa na kupelekwa Marekani.
  Pia alisema alipita kwenye mgodi wa Kakola ikamkumbusha jinsi vijana walivyoshambuliwa kwa mabomu katika ardhi yao. Alisema katika mkoa huo pia kulikuwa na mabwawa yaliyojengwa na wakoloni kwa ajili ya matumizi ya maji kwa binadamu na mifugo, lakini hivi sasa hakuna hata moja. Vilevile, alisema kulikuwa na kiwanda cha kusindika nyama cha Tanganyika Packers na matawi yake, lakini kiwanda hicho kwa sasa hakipo.
  Alisema wafugaji wenyeji wa mkoa wa Shinyanga, wamegeuzwa wakimbizi katika nchi yao kwa ajili ya kwenda kutafuta eneo la kuhudumia mifugo yao.
  Dk. Slaa pia alisema kilichomuuma zaidi ni kwamba, alipoingia katika wilaya ya Meatu, mkoani hapa, alishuhudia nyumba za nyasi, wakati Tanzania ni nchi tajiri. "Shinyanga haina maji, majosho ya mifugo na wananchi wake ni maskini wa kupindukia. Hali niliyoiona Maswa, iko pia Dodoma, Singida na Arusha. Nikapata picha kuwa tangu kufariki Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Watanzania wametelekezwa," alisema Dk. Slaa.
  Alisema mapato ya mauzo ya wakia moja ya dhahabu, yanatosha kusomesha Watanzania, lakini madini hayo yanaishia kupelekwa nchini Marekani.
  Hata hivyo, Dk. Slaa alisema umaskini unaonuka mkoani Shinyanga, unachangiwa na wenyeji wa mkoa huo kuichagua CCM.
  "Wasukuma bahati mbaya kuna kitu kinawamaliza. Kitu chenyewe ‘ndo shida'. Msukuma akiumwa, akikamatwa na polisi ‘ndo shida," alisema Dk. Slaa.
  Hata hivyo, Dk. Slaa alipotamka hivyo, umati wa watu waliohudhuria mkutano huo walipaza sauti na kusema: "Tumeamkaaaa! Tumestukaaa!"
  Aliwataka kuhakikisha wanalinda kura katika uchaguzi na waache kutoa visingizio kwamba, wanaibiwa kura na kuhoji: "Kama shati unalovaa hauibiwi, kwanini kura unaibiwa? Karatu, Tarime, Kigoma na Mpanda Kati wanapiga kura, lakini hawaibiwi, nyinyi kwanini mnasema mnaibiwa kura?" Alisema baada ya vita ya Iddi Amin, Watanzania waliambia wafunge mikanda kwa miezi 18, lakini kwa bahati mbaya wameifunga kwa miaka 18 zaidi.
  "Tunaiambia Serikali fungeni mikanda Watanzania waneemeke," alisema.
  Alisema akiingia madarakani, atarudisha mabwawa yote yaliyotoweka ili wafugaji wenyeji wa mkoa wa Shinyanga walioko nje ya mkoa huo kutafuta maji ya kulisha mifugo yao warejee nyumbani.
  Pia, aliahidi kurejesha hadhi ya mkoa huo na kuufanya uwe kitovu cha kusindika nyama ili kuachana na utaratibu wa kuagiza kitoweo hicho kutoka Kenya.
  Imeandikwa na Beatrice Bandawe, Mkuranga na Muhibu Said, Shinyanga.
   
Loading...