Sitamani kuwa na Rais kama Mh JK …….Sitamani !

The Fixer

JF-Expert Member
Mar 3, 2008
1,365
583
Sitamani kuwa na Rais kama Mh JK …….Sitamani !

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) “kimefunga ndoa” na mafisadi kwa kukataa kupokea ushauri wa kuwafukuza kutoka chama hicho.
Taarifa iliyotolewa Jumapili, mwishoni mwa vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC), haikutoa msimamo wa chama katika kukabiliana na ufisadi.
Vikao vya CCM vilimalizika mwishoni mwa wiki katika kitongoji cha Mwitongo, kijiji cha Butiama, mkoani Mara ambako vilichukua siku tatu.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya CC, alikuwa Waziri Mkuu wa zamani, Cleopa David Msuya aliyetoa hoja kutaka chama kishughulikie mafisadi kwa kuwafukuza uanachama.
Hoja mbili kuu za sasa ni makampuni 22 yaliyoghushi nyaraka na kujichotea Sh. 133 bilioni kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu (BoT).
Nyingine inahusu mkataba wa kufua umeme wa dharura kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (LLC) ambayo imethibitika kuwa kampuni hewa.
Msuya alitoa hoja hiyo wakati wa kujadili ajenda iliyohusu tuhuma za utafunaji fedha za chama unaodaiwa kufanywa na mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Wazazi, Abiud Maregesi na aliyekuwa Katibu wa mkoa wa Singida, Mujuni Kataraia.
“Mwenyekiti, hivi tunaishia wapi. Kama kweli tunataka kusafisha chama kwanini watu wanaodhoofisha chama wasifukuzwe uanachama. Hapa kuna watu wanatuhumiwa kwa ufisadi, tena mkubwa sana lakini tumenyamaza,” mjumbe mmoja alisema akimnukuu Msuya.
Alisema nchi imekuwa na umasikini uliotokana na wizi. “Umasikini wa Tanzania unatokana na ufisadi, na waliohusika katika matukio ya ufisadi ya EPA na mkataba wa Richmond, lazima wachukuliwe hatua.”
Wakati wote akitoa maelezo yake, Msuya alionekana kujiamini; huku akimkazia macho Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete.
“Haiwezekani kuwa Msuya alikuwa anaongea kwa niaba yake peke yake. Bila shaka alikuwa anawakilisha wengine wa msimamo wake katika chama,” ameeleza mtoa habari.
Msuya alitaka kwa vile tayari watuhumiwa wa mkataba wa Richmond wanafahamika, kulikuwa na haja, kwa chama, kuanza kuwachukulia hatua wote waliobainika na watakaobainika ili kukisafisha chama na kujenga msingi wa kuadabisha kila “anayechafua chama.”
Watuhumiwa wakuu wa kashfa ya Richmond ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na waliokuwa mawaziri, Nazir Karamagi wa Nishati na Madini na Ibrahim Msabaha wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Watuhumiwa wengine ni pamoja na Rostam Aziz, mbunge wa Igunga ambaye anatajwa katika kashfa ya EPA kwa kuchota Sh. 40 bilioni kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.
Suala la kuwafukuza watuhumiwa wa ufisadi liliibuka tena kwenye NEC ambako Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere alirejea hoja ya Msuya.
“… Mwenyekiti, mbona mnawaachia hawa? Ni lazima chama kichukue hatua za kuhakikisha wote waliohusika wanafukuzwa katika chama,” alisema mjumbe mmoja wa NEC akimnukuu Makongoro.
Makongoro, ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kutoa hoja hiyo kwenye kikao cha NEC kilichofanyika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, kabla ya mkutano mkuu wa CCM wa mwishoni mwa mwaka jana.
Hakuna taarifa zozote zinazoonyesha Mwenyekiti Kikwete alichukua kauli hizo kwa uzito uliostahili na mjadala juu yake ulififia kadri vikao vilivyoendelea.
Madai yaliyokuwa yameenea ndani na nje ya ukumbi, ni kwamba chama kingechukua hatua ya kuwafukuza watuhumiwa, wao wangehamia chama cha upinzani au wangeanzisha chao.
Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema kama watuhumiwa wangefukuzwa, wangejichimbia katika jumuiya tatu kubwa za CCM ambazo zimo katika hatua ya uchaguzi na kuzimega.
Jumuiya za CCM ni Wazazi, Wanawake na Vijana.
Kuchukuliwa kwa uongozi wa jumuiya hizo na waliofukuzwa kwenye chama, wachunguzi wanaeleza, kungetoa mwelekeo wa maasi ndani ya CCM na hata kundi hilo kuweka mgombea urais wake ifikapo 2010.
Mategemeo ya wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kabla ya vikao hivyo, hasa vikiwa vinafanyikia nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, yalikuwa makubwa na walitarajia chama kingetoka na hatua ya kutokomeza watuhumiwa wote.
Hatua hiyo, ama ya kuwafukuza uanachama au ya kuwafikisha mahakamani haraka, ingeipa nguvu serikali katika kushughulikia ufisadi katika maeneo mbalimbali ya uchumi nchini.
Akiongea na MwanaHALISI juu ya “ukimwa” wa CCM kuhusu ufisadi, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amesema “hakushangazwa na kimya hicho.”
“Ningeshangaa sana kama wangechukua hatua tofauti na walivyofanya, kwani watuhumiwa wamo miongoni mwao. Hata fedha nyingi zilizochotwa zilitumiwa na chama chao ili kuwaweka madarakani,” alisema Dk. Slaa.
Aidha, wale ambao wangechukua hatua ni walewale walioshiriki au waliowezesha uporaji wa mabilioni ya shilingi, alisema Dk. Slaa na kuongeza “hakika sikutegemea hatua yoyote kutoka kwa watu walewale.”
Hata hivyo, kuna taarifa za kuaminika kwamba wafadhili ambao wanasubiriwa kuahidi misaada katika bajeti ya serikali, wametishia kusita kusaidia iwapo watuhumiwa katika kashfa ya EPA hawatafikishwa mbele ya sheria.
Hii ina maana kwamba asilimia 36 ya fedha za bajeti kwa matumizi ya kawaida, itakosekana na hivyo kukwamisha utekelezaji wa majukumu ya serikali.
Wafadhili ambao huitwa “washirika wa maendeleo,” wamekuwa wakisisitiza kwamba sharti serikali ipambane na wala rushwa wakubwa badala ya kutumia nguvu nyingi kwa watoa milungula midogo.
Kama unadhani unamjua vizuri JK kuwa anaependa sana Tanzania na Watanzani wake, Umekosea sana ……Now you see the very best of Kiwete !

Source; Mwanahalisi.
 
Back
Top Bottom