Siri ya siasa na mwanasiasa nyuma ya pazia

Yericko Nyerere

JF-Expert Member
Dec 22, 2010
17,005
20,421
Mara kadhaa nimekutana na marafiki zangu katika makutano ya kawaida ya vijana kuzungumzia mambo ya siasa, kwa mfano nafasi ya vijana katika siasa. Kutokana na yale tuliyofunzwa shululeni kuhusu dhima ya ujadilianaji mambo ya siasa, nilijikuta siku moja nikiwa na rafiki zangu John Mnyika Ben Saanane na Henry Kilewo nikiingiza ainisho la neno siasa katika utangulizi wa majadiliano yetu.

Nakumbuka siku ile tulipotoka mahakama ya Rufaa na kwenye mgahawani pale Upanga Barabara ya Umoja wa Mataifa kujipongeza ushindi wa kesi ya Mnyika dhidi ya CCM jimbo la Ubungo 2013, niliiambia hadhira mbele yangu hivi; Siasa maana yake ni njia azitumiazo mtu au kundi la watu kupata nguvu na madaraka, na ikitokea mtu akapata nguvu hizo huendelea na hatua ya pili ya njia hizo ili kuhahihisha anabaki na nguvu zake au na madaraka yake kwa lengo la kuendelea kufanya kile alichokikusudia. Kinachogomba hapo ni nguvu azipatazo mwanasiasa anazitumia kwa maslahi ya nani. Nikakazia kwakusema, Siasa ni mambo mengi lakini sio SAYANSI, Siasa ni medani ya mapambano ya kimadaraka (power struggle)

Baada ya mawasilisho niliulizwa masawali kadhaa, mengi yakihusu msingi wa mada yaani vijana na nafasi yao katika huo utafutaji na utumiaji wa nguvu. Wakati wa vinywaji, nyama choma na ndizi vikiendelea kutuburudisha, alinifuata kijana mmoja aliyekuwa meza yetu akaniuliza hivi; ‘kumbe mwenzetu uko katika siasa, nini siri ya urembo?’ kwa kuwa aliuliza swali kiutani, niliishia kumjibu (pengine bila kutafakari sana); ‘sio siri, ni kuamua tu’. Tuliishia kucheka na hatimaye maakuli na makorokocho ikawa imeisha, kuashiria mwisho wa kujipongeza kwetu.

Leo hii ninapotizama nyuma, ninawiwa kutafakari, nini siri ya mtu kuwepo katika siasa, kwa maneno mafupi nini siri ya siasa. Majibu yanaweza kuwa mengi, lakini leo nataka kuwashirikisha jibu hili, ambalo naamini kwa hakika linadokeza siri hasa ya siasa.
Jamii nyingi duniani zimegawanyika kiuchumi katika makundi mawili makuu, yaani wenye uwezo kiuchumi na wasio na uwezo huo. Yawezekana kukawa na kundi la katikati, lile la wenye uwezo wa wastani. Misemo mingi imekuwa ikitumika kuyaeleza makundi haya, matharani; wenyenacho na wasionacho, au walalaheri na walalahoi.

Kila moja ya makundi haya lina maslahi yake katika uchumi ambayo hayana budi kulindwa au kutetewa. Wenyenacho wanatamani kisiwaondokee na ikiwezekana wapate zaidi. Wakati huo huo wasionacho wanataka wapate na jitihada zao zisiishie kufyonzwa na wenyenacho. Kwa ufupi hayo ndio maslahi ya makundi haya. Ni katika jitihada za kulinda maslahi, ndipo linapojitokeza kundi la watu (yamkini wajanja wajanja hivi) wakiuomba umma uwape nguvu za madaraja ya kiserikali ambayo kimsingi ni nguvu za kutetea maslahi yao.

Ukichukulia mfano wa mechi ya mpira wa miguu, timu ya walionacho dhidi ya timu ya wasionacho, marefa, makamisaa na chama cha mpira ndio hao waamuzi wa mechi. Mambo yanaweza kwenda vyema kama waamuzi hawa watahakikisha ‘fair play’ tu ndio inakuwa sheria-mama ya mchezo. Lakini imetokea mara nyingi kwamba marefa wameionea timu fulani na kuipendelea timu nyingine.
Ninachomaanisha hapa, mwanasiasa ni refa wa kiuchumi katika jamii. Siri yake ni maslahi anayoyapata kutokana na kazi yake hiyo, na ili apate maslahi yake inategemea analinda maslahi ya nani. Mwanasiasa anaweza kuamua kulinda maslahi ya walionacho, mwingine anaweza kuamua kuwa mlinzi wa maslahi ya wasionacho, na mwingine akatetea maslahi ya pande zote mbili (au tuseme pande tatu, maana na yeye ana maslahi yake)

Tukiziangalia siasa za Afrika (waweza kusema za Tanzania) za wakati huu, kwa mtazamo wangu, wanasiasa walioko madarakani ni watetezi na walinzi wa maslahi ya mwenyenacho. Kwa kufanya hivyo nao wananufaika. Katika utetezi wao huo wamekuwa wakiambatanisha unafiki kwa kujifanya wanatetea maslahi ya wasionacho kwa kuwagawia viperemende ndani ya karatasi za plastiki.
Wakati huo huo kuna wanasiasa waliopewa jina la wapinzani. Hawa nao kwa kauli zao (nasisitiza; kwa kauli) wanajitahidi kuonekana wanatetea maslahi ya wasionacho, ingawa wengi wa wasinacho wanaelekea kutoelewa bado ni nini hasa hawa watetezi ‘wapya’ wanakimaanisha.

Pengine wanajiuliza kwamba, hawa wapinzani kinachowasukuma ni mapenzi yao kwa wasionacho au na wao wanatafuta nafasi ya kuwa karibu na mwenyenacho ili wafaidi? Wasionacho wanaendelea kujiuliza, vipi hao wachache toka upinzani ambao tumewasikiliza, wakapenya hadi kwenye viti vya madaraka na nguvu, wamekuwa watetezi wenye tabia gani?
Wanasiasa hupenda kuona ushaidi wa utetezi wao wa maslahi kwa alama ya mambo yaliyofanyika kwa jitihada zao, matharani miundombinu iliyojengwa, huduma za jamii na kadhalika.
Ndugu msomaji, halijengwi daraja la Kigamboni pasina kulengwa maslahi ya kundi. Daraja/barabara inaweza kujengwa ili mwenyenacho aufikie mzinga wa asali na kuirina kisawasawa. Lakini mwanasiasa kwa ulaghai wake atasimama na kuwambia wasionacho; jamani eehe, nimewajengea daraja au barabara ya lami. Wasionacho huenda wasione kwamba hiyo barabara badala ya kunufaika nayo, ndio kwanza inatumika kama mrija wa kufyonza kisima cha raslimali hadi kikauke. Mwigine atasimama na kusema; nipeni muhula wa pili nimejenga au nimepanua ‘intaneshono eapoti’ (uwanja wa ndege) na kununua ndege. Ni vyema umma ukaacha kushangilia tu ununuzi wa ndege na upanuzi bila kujiuliza na kutathmini kwa kina mambo hayo ni kwa maslahi ya nani. Yasije yakawa ni yale yale, ije midege isombe kila samaki na kutuachia mapanki, harafu ushuru wa mijidege uingizwe kwenye akaunti za wanasiasa Uswisi

Mara nyingi mimi huwa najiuliza ninaposikia hili neno miundombinu; hizi mbinu za nani? Huwa najiuliza pia, serikali bora ni ipi; inayojenga nyumba za wafanyakazi au inayojenga (inayosaidia kujenga) za wakazi? Mtawala ajengaye nyumba za wafanyakazi anataka wawe karibu na eneo la kunyonyewa nguvu kazi zao kwa maslahi ya mwajiri kisha wakistaafu ‘watajiju’, bali ajengaje za wakazi anaitakia jamii maisha bora ujanani na uzeeni.
Ndugu zangu, kwa siri hii niliyowashirikisha, natoa changamoto ya kuendelea kutafakari sera za kiuchumi za wanasiasa dhidi ya maslahi. Unaposikia sera kama; kuvutia wawekezaji, ubinafsishaji, uchangiaji huduma na nyinginezo, unaona ndaniye maslahi ya nani.

Siri ya siasa; ulinzi wa maslahi ya kundi ili mwanasiasa naye apate chake. Maslahi ya nani yanalindwa na mwanasiasa husika ndio yanayowatofautisha wanasiasa wetu. Kazi yetu kujua tunamchagua yupi.

Angalizo; miongoni mwa wanasiasa, wapo wachache sana ambao wanatoa kafara maslahi yao wenyewe kwa ajili ya kulinda tu maslahi ya kundi wanalolichagua kulitumikia, yamkini hao ndio walio bora kama wanasiasa.



Na Yericko Nyerere
 
hivi wewe Yericko Nyerere ni mwanasiasa au mwanaharakati?
mimi binafsi naona hujafika daraja la kuwa mwanasiasa bado unasafari ndefu sana kufikia huko,nakuweka kwenye kundi la wanaharakati.
jambo jema ni kwamba haupo kwenye kundi la wachumia tumbo kama vijana wengi wa leo walivyo.....
endeleza harakati huenda siku za mbele utakuwa mwanasiasa mzuri
 
hivi wewe Yericko Nyerere ni mwanasiasa au mwanaharakati?
mimi binafsi naona hujafika daraja la kuwa mwanasiasa bado unasafari ndefu sana kufikia huko,nakuweka kwenye kundi la wanaharakati.
jambo jema ni kwamba haupo kwenye kundi la wachumia tumbo kama vijana wengi wa leo walivyo.....
endeleza harakati huenda siku za mbele utakuwa mwanasiasa mzuri
Define your terms, then you can have a logical answer!
 
Kuna tatizo kubwa sana kwa watu wa Chadema kutofautisha (Siasa,harakati na kupigania haki)
 
Kuna tatizo kubwa sana kwa watu wa Chadema kutofautisha (Siasa,harakati na kupigania haki)

hujajibu swali la yeriko nyerere mambo ya msingi kazungumza tuache siasa ktk uchumi wetu.
 
Moja ya andiko bora sana kutoka kwako Yericko ...nimekusoma katikati ya mstari ....amini nakuambia miaka michache ijayo itazidi kukujenga na kukupa taswira halisi ya siasa zetu ....
 
Back
Top Bottom