Simulizi ya binti aliyepigania uhai JKCI

Simulizi ya binti aliyepigania uhai JKCI

Donatila

JF-Expert Member
Joined
Oct 23, 2014
Posts
8,274
Reaction score
25,322
pic+mtoto.jpg




Ni miaka miwili tangu Salome Ngoma (14) alipoondoka Itigi wilayani Manyoni kuelekea jijini Dar es Salaam kusaka tiba ya maradhi ya moyo.

“Nilipanda treni Desemba 26 mwaka 2015 nikiwa sijui ninakoelekea, nilijisemea moyoni sitakufa, nitafanya kila mbinu kuokoa uhai wangu,” anasimulia Salome ambaye sasa amepata hifadhi ya makazi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Taasisi hiyo ilimfanyia upasuaji wa kurekebisha valvu za moyo Septemba 11, mwaka huu baada ya Mahakama ya Watoto kutoa idhini kwa JKCI kumpa matibabu binti huyo kutokana na familia yake kumkatalia asitibiwe kabla ya kumtelekeza.

Binti huyo anasema hamjui mama yake kwani alimtelekeza tangu akiwa mdogo na baba yake hakuwahi kumpa matunzo, hivyo muda mwingi aliishi na babu yake.

Salome anasema baba yake alimwondoa shuleni akiwa darasa la kwanza kwa madai kuwa hawezi kusomesha mtoto wa kike.

Anasimulia kuwa mwaka 2012 aliugua maradhi ya kifua na hakupata matibabu kwa wakati.

“Babu alinipeleka hospitali ya misheni ya St Gasper, nilifanyiwa vipimo na matibabu bure baada ya kwenda Kanisa Katoliki kuomba msaada. Maradhi hayakupona na mwaka 2015 niligundulika kuwa na matatizo ya moyo,” anasema Salome, ambaye anamtaja babu yake kuwa anaitwa Sostenes Ngoma.

Binti huyo alipewa rufaa akitakiwa kupata matibabu JKCI.

“Niliambiwa natakiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo Muhimbili, nikapewa karatasi za kuja huku. Nilienda nyumbani nikamwambia shangazi na babu wakaenda kumwambia baba yangu lakini hakuwa tayari kushughulikia tatizo langu,” anasema.

Anasimulia kuwa aliondoka nyumbani kwao kwenda stesheni akiwa hana fedha ya nauli na akiwa hapo aliomba msaada wa kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.

Salome anasema alipofika Dar es Salaam alimuomba askari wa stesheni aliyemfikisha Hospitali ya Taifa Muhimbili alikomuacha eneo la wagonjwa wa dharura.

Anasimulia kuwa maofisa wa ustawi wa jamii walimsaidia na alilazwa JKCI kwa miezi miwili na baadaye aliruhusiwa akitakiwa kutafuta Sh2.9 milioni kwa ajili ya gharama za upasuaji.

Kwa msaada wa JKCI ambayo imekuwa ikimhudumia kwa mavazi, malazi na chakula alirudi kwao Itigi kutafuta fedha hizo, lakini baba yake hakuwa tayari kumpatia.

Anasema akiwa huko alizidiwa na alipopelekwa St Gasper alipewa rufaa ya kurudi tena JKCI.

Salome anasema Juni 5 mwaka huu alifika tena JKCI alikoanza kupatiwa matibabu upya baada ya wafadhili kujitokeza kumsaidia na aliambiwa awatafute ndugu zake ili watoe idhini ya kufanyiwa upasuaji.

Anasema walipotafutwa, wazazi walisema hawawezi kutia saini.

Kutokana na hilo, mkurugenzi mtendaji wa JKCI, Profesa Mohammed Janabi aliagiza atafutwe mwanasheria kwa ushauri.

“Nilikwenda Mahakama ya Watoto Kisutu na bahati nzuri hakimu akakubali na kusaini kwa ajili ya upasuaji. Sasa nimepona lakini ninahitaji sehemu ya kuishi na kwenda shule, sihitaji kurudi tena nyumbani kwa sababu ya matendo waliyokuwa wananifanyia ya kuniacha na kutonijali,” anasema Salome.

Daktari wa upasuaji wa moyo kwa watoto, Godwin Sharau anasema tatizo la Salome limetokana na ugonjwa kutopata matibabu kwa wakati.

Anasema uchunguzi wa madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto akiwemo Dk Naiz Majani na Sulender Kuboja waligundua valvu moja kati ya nne ndani ya moyo wake zilikuwa zinavuja na kwamba tatizo hilo hakuzaliwa nalo bali alipata bakteria akakosa matibabu kwa wakati.

Dk Sharau anasema bakteria hao kitaalamu wanajulikana kwa jina la streptococcus na hushambulia koo na kusababisha ugonjwa wa mafindofindo na kwamba kwa Salome walisafiri kwa njia ya damu na walishambulia valvu.

Anasema hali hiyo ilisababisha upande wa kushoto wa moyo kuharibika na kuanza kupanuka.

“Tuliona ni vyema valvu ikatengenezwa badala ya kuibadilisha kutokana na changamoto ya mazingira alikotoka. Tulimpanga kwa upasuaji Desemba 2016, lakini hakuwa na wazazi ambao wangeweza kutoa ruhusa ya upasuaji,” anasema.

Dk Sharau anasema akiwa na miaka 14, Salome asingeweza kuelewa kwa undani tatizo lake na kutoa ruhusa inayotambulika kisheria ya matibabu. “Tulifanya utaratibu wa kutafuta wazazi wake, baba yake alikataa. Ndugu wa karibu hatukuwapata, hivyo tukaona hatuwezi kumfanyia matibabu, tukamruhusu,” anasema.

Anasema Juni alirudi tena JKCI akiwa mwenyewe na aliomba apate matibabu baada ya vipimo kuonyesha moyo umezidi kupanuka.

“Ukipanuka sana inafika kipindi hauwezi kurudi katika hali ya kawaida na vile vyumba hasa kile cha kushoto ambacho ni muhimu katika kusukuma damu kupeleka mwilini, kikitanuka sana kinashindwa kufanya kazi na matibabu pekee inakuwa ni kubadilishiwa moyo,” anasema.

Kutokana na hilo anasema waliamua Salome apatiwe matibabu ya moyo kwa kutengeneza valvu.

Anasema kutokana na umri wake, watu wa ustawi wa jamii na mwanasheria wa hospitali walikwenda Mahakama ya Watoto kuomba kibali ili apatiwe matibabu.

Mwanasheria mwandamizi wa JKCI, Maulid Kikondo anasema Salome tangu alipolazwa hospitalini hapo alikuwa akipokea matibabu ya kawaida ambayo baadaye yalilazimu kufanyiwa upasuaji na ilitakiwa idhini ya mtu wa karibu yake.

“Alitakiwa kupata idhini ya mtu mzima, wazazi, walezi au watu wa karibu, bahati mbaya tangu amekuja hakuwa na wazazi hicho ikawa ni kikwazo, taasisi ikaanza kutafuta ni jinsi gani atafanyiwa upasuaji na hapo ndipo sheria ikaanza kuangaliwa,” anasema Kikondo.

Anasema baada ya kufanya mapitio ya sheria, walibaini ipo inayotoa nafasi kwa mahakama kutoa idhini kwa niaba ya wazazi au mtoto mwenyewe ili kufanyiwa upasuaji.

Kikondo anafafanua kuwa walituma maombi namba 191 ya mwaka 2017 kuomba ridhaa ya upasuaji kwa Salome kupitia Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.

Anasema kwa kushirikiana na Hamis Mndeme wa ustawi wa jamii, JKCI iliandaa nyaraka na kuziwasilisha Mahakama ya Watoto.

Anasema Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa alisikiliza maombi hayo na kutoa uamuzi uliowezesha Salome kufanyiwa upasuaji.

Mwanasheria huyo anasema wakati Salome akitibiwa hospitalini hapo hapakuwa na mawasiliano yoyote kutoka kwa ndugu na juhudi za kuwatafuta hazikuzaa matunda.

“Baada ya upasuaji wiki mbili zilizopita ameruhusiwa kwenda nyumbani, lakini hakuwa na sehemu ya kwenda, JKCI kama ilivyoelekezwa na Mahakama inabidi ifanye kazi ya ulezi, imemchukua na kumweka wodini lengo ni aweze kuishi kwa kipindi ambacho tunasubiri msamaria mwema wa kumsaidia,” anasema Kikondo.

Akizungumzia upasuaji huo, Dk Sharau anasema wameitengeneza valvu na kumwekea chuma.

“Sehemu zilizoharibika tulizitengeneza na zilizokuwa fupi tukazirefusha ili arudi katika hali yake. Hii itamsaidia kwa kuwa hatahitaji kutumia dawa za kuwezesha damu isigande. Ukiwa umebadilishiwa valvu na kuwekewa za chuma si rahisi kwenda kuishi tena kijijini hasa kwa mtoto kama huyu ambaye anaonekana hana wazazi wa kumwangalia kwa ukaribu,” anasema.

Dk Sharau anasema kwa kawaida mgonjwa akiwekewa valvu ya chuma anatakiwa atumie dawa kila siku na akiacha anaweza akaanguka na kufa kwa sababu damu itaganda kwenye valvu ya chuma.

Anasema kwa kuitengeneza iliyokuwepo awali, wamegundua valvu hiyo kwa sasa haivuji na wanaamini itakuwa ni ya maisha marefu. “Tunafikiri atakaa nayo kwa miaka kati ya 10 na 15 itamfikisha angalau miaka 30 bila kuharibika, hivyo anahitaji kuilinda valvu hii kwa sababu ikishambuliwa na bakteria itakuwa na maisha mafupi, baada ya mwaka mmoja au miwili itaharibika,” anasema Dk Sharau.

Anasema kutokana na hali yake kiafya, Salome anahitaji msaada. Anasema kuwa upasuaji huo wa Salome umefanyika kwa msaada wa mfuko wa bima ya afya wa Strategies ambao ulitoa Sh10 milioni na amepatiwa kadi ya bima ya afya ya matibabu. “Strategies walitoa fedha nyingi kwa ajili ya matibabu yake wakisaidiana na Serikali lakini Salome anahitaji kuchoma sindano moja kila mwezi ili kuilinda valvu na kuwafanya bakteria wasiishambulie,” anasema.


Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom