Simulizi: Tone la mwisho la uvumilivu

Simulizi: Tone la mwisho la uvumilivu

VAN HEIST

JF-Expert Member
Joined
Aug 26, 2014
Posts
1,434
Reaction score
617
George Iron Mosenya

SEHEMU YA KWANZA
Naitwa Lusubilo Mwaipaja, marafiki zangu wengi walizoea kuniita kwa ufupi. Waliniita Lusu! Niliyafurahia maisha sana nikiwa mjini Mbeya na familia yangu kwa takribani miaka ishirini na nne, mama yangu alikuwa akinieleza mara kwa mara
kuwa watu wengi wananipenda kwasababu ya upole na ukarimu wangu!

Lusu, angalia upole wako usizidi kipimo inaweza kukugharimu siku moja Mama aliwahi kunipa onyo ambalo sikujua kabisa alikuwa anamaanisha nini.Hakika! Sikujua anachomaanisha kwa wakati ule kwa sababu kila mtu katika jamii alinipenda na kuniheshimu kwa sababu ya huohuo upole. Kivipi mama ananieleza kuwa ipo siku upole wangu
utanigharimu?? Sikutilia maanani.

Giza likachukua nafasi, mchana ukaipokea nafasi hiyo. Ikawa usiku ikawa mchana siku zikazidi kusonga mbele.

Hatimaye ukakuchwa ule usiku ambao uliuleta mchana wa kukutana na Neema. Msichana ambaye na yeye kama ilivyokuwa kwa mama alinisifia kwa upole wangu na ukarimu. Lakini yeye aliendelea kunijaza sifa kila siku hatimaye jicho langu likamtazama katika namna ya pekee.

Mke mtarajiwa!
Sikujiuliza mara mbilimbili siku ambayo niliamua kumtamkia kuwa nahitaji kuwa naye katika mahusiano ya kimapenzi. Mahusiano ambayo yalidumu kwa muda mfupi kabla sijayapeleka katika uchumba, mama alikuwa wa kwanza kumfahamu Neema kisha baba.

Hatimaye nami nikajitambulisha kwao.Nikapokelewa kwa mikono miwili!! Wazazi wake wakanipenda!! Safari ya mapenzi yetu ikaongezeka kasi na hatimaye tukaoana.

Siku ile ya harusi mama yangu alinikumbatia kwa muda mrefu kupita ndugu zangu wote.Alidondokwa na chozi ambalo nilidhani kuwa lilikuwa la furaha lakini la! Nayakumbuka maneno ambayo alinieleza kwa sauti ya kunongona.

Lusu mwanangu, hakuna mwanamke anayekupenda duniani zaidi ya mimi mama yako, kama ingekuwa ndani ya uwezo wangu ungeishi nyumbani daima. Nyumba yenye mapenzi ya dhati kwako, ila nenda mwanangu, nenda umekuwa mtu mzima sasa..

Nikauacha rasmi mji wa Mbeya, mji ambao ulinipenda sana. Nikaondoka mimi na Neema. Tukahamia Morogoro, ambapo nilikuwa nimepata uhamisho wa kuhamia kule kama mwalimu!

****
Awali Neema alikuwa akinionyesha mapenzi ya dhati sana. Jambo ambalo halikuwa geni, nililitegemea vilivyo. Niliamini kuwa kama kweli mama ananipenda kuliko wanawake wote basi Neema ni wa pili katika orodha ile. Miezi mitatu pekee ya ndoa niliishi kwa amani ya moyo.

Mwezi wa nne ukaanza kwa mauzauza. Mauzauza ambayo hadi leo hii akitokea mtu ananiomba ushauri juu ya mwanamke gani wa kuoa. Sitakuwa na la kumjibu, zaidi atakuwa amenipandisha jazba tu!

Neema alianza kulalamika kuwa amechoka kukaa nyumbani. Anataka nimtafutie naye kazi ya kufanya ilimradi tu asiwe mtu wa kushindia nyumbani.

Nilishangazwa na ombi hili, wakati awali tulipanga vinginevyo. Nikaamua kuuvunja ukimya.Neema mke wangu, kwani mimi na wewe tulipanga nini mwanzo? Si tumekubaliana tupate mtoto kwanza ndo hayo yatafuata. Nilimuhoji. Akanitazama kwa jicho kali, kisha akasimama kwa ghadhabu akatoa msonyo mdogo wa kuonyesha kukereka, akaingia chumbani akaubamiza mlango. Looh! Ama kweli upole wangu, upole wangu lakini mama alinikanya!!

Nikasimama na kuelekea chumbani, nikamkuta amejifunika shuka gubigubi huku akitupa miguu huku na kule. Nikajongea kitandani nikaanza kumbembeleza. Nadhani ule ndo ulikuwa mwanzo wa Yule binti kuanza kuiendesha akili yangu. Nilimweleza kuwa kama kweli ana nia ya kufanya kazi basi ageuke tuzungumze. Neema akageuka huku akipekecha macho yake, ili kulazimisha machozi.

Mapenzi bwana! Ndicho nilichowaza kwa wakati ule kumbe yale hayakuwa mapenzi nilijidanganya tu!

Haya unataka kazi gani mke wangu!Neema akaachia tabasamu pana akanikumbatia na kunibusu, kisha akanieleza kuwa anataka kuwa anaenda dar kununua vitenge na nguop za wanawake kisha atakuwa anakuja navyo Morogoro
kuwauzia na kuwakopesha wanawake wa mtaani akianza na waalimu ambao naishi nao pale nyumba za shule.

Nikalifikiria wazo lake kisha nikamruhusu huku nikimkumbusha kuwa asisahau kuwa huku Morogoro ameacha mume anayempenda sana. Furaha ya Neema ikarejea. Akapiga mahesabu yake, nikampatia kiasi cha pesa akajipanga kwa
safari baada ya siku mbili! Nafsi yangu ilikuwa imemruhusu lakini kiukweli ni kwa shingo upande!!

Siku ikafika na mke wangu kipenzi akaondoka akiniachia manunguniko nafsini!! Akaenda jijini Dar es salaam!

Siku moja baada ya Neema kuondoka, mwalimu Jackson ambaye alikuwa ni mwalimu mkuu na yeye akaaga kuwa anaenda baraza la mitihani Dar. Nikamweleza kuwa akipata muda wa kuonana na Neema basi kuna zawadi nahitaji kumpa ampatie.

Mwalimu akanieleza kuwa hatapata muda kwa sababu anafika na kuondoka!! Lakini pia siku moja kabla Neema hajaondoka Mwalimu mkuu msaidizi naye aliondoka shuleni na sikujua wapi alielekea.Sikuwa na mashaka yoyote. Niliamini Neema ni wangu peke yangu!!

**Naam! Hii ni sehemu ya kwanza ya simulizi hii ya TONE LA MWISHO LA UVUMILIVU! Usikose kuwa nasi kesho tena muda na waktikama huu. Hapahapa!! Je? Ndoa hii itafikia katika kilele ama itakomea njiani nini maana ya TONE LA MWISHO LA UVUMILIVU?
 
SEHEMU YA PILI

Mwalimu Lusu anashawishiwa na mkewe juu ya
suala la kufanya biashara, baada ya kupinga na
mkewe kununa anaamua kumkubalia..
Mkewe anasafiri kuelekea Dar es salaam……
anaposafiri huku nyuma mwalimu mkuu na
msaidizi wake na wao wanaondoka!!!
ENDELEA!!!
AWALI mke wangu alisema kuwa atatumia siku
zisizozidi tatu kumaliza kile kilichompeleka Dar.
Japokuwa hazikuwa siku nyingi sana lakini kwangu
mimi ilikuwa ni kama mwaka mzima, nilikuwa
nimemzoea sana Neema wangu. Nilimpenda sana
mke wangu!
Siku ya tatu ilipofika majira ya jioni nilitegemea
kupokea simu kutoka kwake. Na sikudhani
ingekuwa simu inayoleta ujumbe mwingine tofauti
na kunieleza kuwa yupo nijiandae kumpokea siku
inayofuata.
Lakini haikuwa kama nilivyodhani… Neema
akanieleza kuwa mama yake mdogo wa Dar es
salaam anaumwa hivyo ataenda kumsalimia kwa
siku mbili kisha ndipo atageuza kurudi Morogoro.
Nilitamani kutia neno la kipingamizi lakini
ningeonekana mwanadamu wa ajabu sana. Ndugu
wa mke wangu anaumwa halafu sitaki aende
kumsalimia.
Nikakubali japokuwa kishingo upande tena.
Baada ya kukata simu nilijilaza kitandani kwa
muda kidogo kisha nikaingia bafuni ili nijimwagie
maji.
Hii ilikuwa kawaida yangu tangu utotoni, mara
nyingi nikiwa najimwagia maji bafuni ni muda
huohuo najikuta anakumbuka vitu Fulani ambavyo
nilikuwa nimevisahau tayari.
Na siku hiyo nikakumbuka kuwa Neema wakati
tukiwa Mbeya alinieleza kuwa yeye na mama yake
mdogo hawapatani hata kidogo na hakuna ambaye
ana mawasiliano na mwenzake. Sikumuuliza sana
nini chanzo cha ugomvi wao nikalipokea kama
lilivyo.
Ya ndugu waachie ndugu!!
Sasa kivipi leo hii anasema anaenda kumuuguza
adui yake?
Dah! Nilitamani kupiga simu nimuulize lakini
nikapiga moyo konde nikalipuuzia hilo!
Pia Neema alisema akiwa Dar hataki kuwasiliana
na mtu yeyote Yule anachukua mzigo na
kuondoka. Imekuwaje sasa akawasiliana na mama
mdogo?
Moyo uliniuma sana ndugu msikilizaji, nikajua moja
kwa moja mwanamke niliyemkabidhi moyo wangu
wote kwa mara ya kwanza alikuwa
ananidanganya……
Kwa nini sasa ananidanganya? Lazima ana sababu
zake!!
Nikajikunyata kitandani kama kinda la ndege
lisokuwa na mama. Usingizi ukanipitia.
Nikalala bila kula chochote!!
Nilikuja kushtuka majira ya saa tano na nusu
usiku.
Nikaitazama simu yangu.
Neema alikuwa amenitumia ujumbe tatanishi.
“Umeme unasumbua sana hapa kwa mamdogo,
simu haina chaji na muda wowote ule itazima….
Usiku mwema mume wangu nakupenda na
nimekumiss sana”
Ujumbe ule ulinifanya nitetemeke, na kwa mara ya
kwanza katika maisha yangu ya ndoa nikajikuta
napatwa na hasira sana.
Neema alikuwa akinidanganya tena!!
Anazo simu mbili tena kwa pamoja tunakiri kuwa
zinaongoza kwa kutunza chaji, ina maana alikuwa
anazichezeaje hadi zikaishiwa chaji kwa pamoja.
Usingizi haukunipitia tena hadi kunapambazuka.
Nikapiga simu ofisini kuwa sitaenda kazini najisikia
vibaya.
Nikajibiwa kuwa nijikaze tu niende maana mimi
ndiye mwalimu wa taaluma na mwalimu pekee
ninayeweza kuisimamia shule kwani mkuu wa
shule na makamu wake bado walikuwa
hawajarejea.
Kusikia jibu hilo kuwa mkuu wa shule na makamu
wake hawajarejea, nikapata tumaini kiasi Fulani
kuwa naweza kujua iwapo Neema ananiongopea
ama la! Nikampigia simu mwalimu mkuu na
kumsihi anisaidie sana jambo moja.
“Tafadhali mkuu nahitaji uwasiliane na mke
wangu, nahitaji tu kujua yu wapi. Najua wewe ni
mtu mzima tena mshauri wangu wa karibu utajua
ni maneno gani utatumia kumtambua yu wapi na
kwa sababu gani, ukirejea Moro tutazungumnza
kwa kina…” nilimsihi akanikubalia.
Baada ya masaa mawili akanipigia na kunieleza
kuwa Neema alikuwa kwa mama yake mdogo
ambaye ni mgonjwa kwa bahati nzuri ni jirani tu na
pale alipokuwa yeye. Maeneo ya Mwenge!!
Majibu ya mkuu wa shule yakanifanya upesi
niende kwenye kioo na kujitazama jinsi
nilivyokuwa nimenuna, nikajipigapiga makofi na
kisha nikatabasamu. Nikaitazama picha ya Neema
ukutani siku ile ya ndoa yetu. Nikaamini kuwa
sijafanya makosa kumuoa.
Na hapo nikajiandaa na kwenda kazini!!
Baada ya siku mbili Neema akarejea Morogoro
akiwa na mzigo aliosema kuwa anaenda
kuuchukua Dar.
Siku moja baadaye mkuu wa shule na yeye
akarejea!
Sikuhitaji kumueleza tena wasiwasi wangu juu ya
Neema, nilijiona mjinga sana na nitaonekana nina
wivu wa kipuuzi.
Sikuzungumza naye, badala yake nilizungumza na
mke wangu juu ya hali ya mama mdogo.
Akanieleza amemuacha akiwa na nafuu sana tu!
Kisha akaelezea juu ya tatizo la umeme linalokabili
baadhi ya maeneo Dar es saalam. Na hapo
akatokwa na kauli ambayo ilinivuruga upya.
“Yaani kule Tandika anapokaa mama mdogo sio
sehemu ya kuishi kabisa.. umeme unakatika hadi
siku tatu…”
Akili ikafyatuka!!
Mkuu wa shule alisema kuwa ameenda kuonana
na mke wangu maeneo ya Mwenge ambapo mama
yake mdogo ambaye ni mgonjwa alikuwa anaishi.
Mke wangu anasema mama yake mdogo anakaa
Tandika!
Sikuwa mwenyeji sana Dar es salaam lakini sio
ugeni wa kutojua umbali kati ya Tandika na
Mwenge.
Neema mke wangu ananidanganya!!
Nilijiwazia kichwani mwangu…
Kisha nikajiuliza kama kweli ananidanganya ni
kwanini ananidanganya?
Niliumia sana, nililia sana ndugu msikilizaji…….
Mwanamke wa maisha yangu anachezea hisia
zangu!!
**Naam! Lusu katika sintofahamu…. Nini
kinaendelea?
 
Lusubilo Mwaipaja kwa mara ya kwanza katika
maisha yake ya ndoa anahisi mkewe
anamdanganya!!!
Nini kitaendelea!!!
TUENDELEE!!
USIKU Neema alilala fofofo sana. Safari ya kutoka
Dar es salaam kuja Morogoro ilikuwa safari ya
masaa matatu tu, sikutegemea safari fupi kama ile
ingeweza kumchosha kiasi kile mke wangu. Lakini
ule upole ambao mama yangu alinieleza ulikuwa
kikwazo nikawa mpole pia katika hili.
Lakini sikuweza kulala hadi niliponyanyuka na
kupekua mkoba wa mke wangu, mwanamke
bingwa wa kutunza tiketi hata kama ni safari
fupifupi za mjini.
Nilitaka kujua alisafiri na basi gani hadi achoke
kiasi kile.
Nilipekua kila kona!
Hapakuwa na tiketi.
Mke wangu kuna kitu alikuwa ananificha!
Nililala jirani naye lakini sikumgusa kabisa nilihisi
kuna utofauti baina yetu, lile joto lake mwanana la
kike sasa nililiona kama moto unaounguza.
Nikaelekea upande mwingine na yeye akiwa
anakoroma huku akiwa anatazama upande wake.
Asubuhi niliwahi sana kutoka nyumbani tofauti na
siku nyingine. Sikutaka kuonana na mke wangu
kwa sababu nilikuwa najisikia kukasirika.
Amakweli mwone mtu ameng’ara na kila muda
analo tabasamu usoni, usitamani kuwa kama yeye
hata kidogo. Hujui kama lile ni tabasamu kutoka
moyoni ama la kuzugia tu!!
Sikuingia darasani kufundisha bali nilikaa ofisini
nikitafakari ni kipi nifanye ili kuujua ukweli, ni kipi
kilikuwa kinaendelea katika ndoa yangu!
Nilitaka kumpigia mama simu lakini nilihisi ni
udhaifu wa hali ya juu, yaani miezi mine tu katika
ndoa naanza kuonyesha kuzidiwa?
Hapana! Nikapuuzia hilo.
Nikatafakari ni nani rafiki wa dhati ambaye
naweza kuzungumza naye jambo hili.
Hata huyo sikumpata…
Nikaitazama pete kidoleni mwangu nikakumbuka
jinsi mama alivyolia kwa hisia kali huku akiwa
amenikumbatia. Siku ile ambayo nilikuwa nafunga
ndoa na Neema.
Nikaanza kuipata mana ya chozi lake. Pia
nikakumbuka maneno yake juu ya upole wangu!
Naam! Nikapata jawabu juu ya namna ya
kukabiliana na jambo ambalo lilikuwa mbele
yangu.
Natakiwa kuuvua upole wangu mara moja, la sivyo
nitakufa huku nikiwa ninatembea barabarani.
Na pale nikafunga ofisi yangu, nikatoweka pasipo
kuomba ruhusa yoyote.
Kwa mara ya kwanza nikarejea nyumbani bila
kutoa taarifa yoyote.
Nilipoifikia nyumba niliyokuwa naishi, nilimsikia
mke wangu akiongea kwenmye simu katika namna
ya kusisitiza sana.
Tatizo alikuwa anaongea kwa kabila yao!
Kabila ambayo sikuwa naelewa zaidi ya salamu tu!
Ila kwa sababu kile ni kibantu walau neno
mojamoja ningeweza kukisia maana yake.
Kuna maneno mawili yalijirudiarudia sana.
“Ntumbo nuumile…. Ntumbo nuumile..”
Nilikisia kuwa anazungumzia juu ya maumivu ya
tumbo na si vinginevyo.
Nikatambua wazi kuwa nikiingia ndani atapagawa
sana kwa sababu hajanitegemea kabisa.
Nilichofanya nikarudi hatua nyuma kisha
nikaondoka zangu!
Nilipofika mbali nikampigia simu, kwa mara ya
kwanza simu yake ilikuwa inatumika. Nilipopiga
mara ya pili ikapokelewa.
“Shkamoo mume wangu… nd’o tabia gani
kuondoka bila kuniaga? Jamani Lusu” alizungumza
kwa sauti ya kitotototo iliyojaa maringo, kana
kwamba alikuwa hajaamka kabisa.
“Hujaamka hadi wakati huu mpenzi” nilimuuliza,
lakini kitendo cha kumuita mpenzi kikanisulubu
sana nafsi.
“Sijaamka hata, si unajua tena uchovu wa safari..”
aliendelea kuniongopea mwanamke niliyeapa naye
akaapa kunipenda kwa shida raha.
Nilidondosha chozi hadharani!
Bahati ilikuwa upande wangu hapakuwa na watu
wengi barabarani, nikawahi kujifuta.
Nikamweleza kuwa nilikuwa narejea nyumbani
kwani sikuwa najiskia vizuri pia….
Kisha nikakata simu!!
Nilifika nyumbani na kuingia ndani, nikamkuta mke
wangu amejifunika gubigubi, nilipomuita mara ya
kwanza na ya pili hakunijibu, kisha mara ya tatu
akajibu kama mtu anayetokea usingizini.
Ananidanganya kuwa alikuwa yu hoi kwa usingizi!
Nilijiwazia.
Nikaelekea sebuleni nikawasha runinga kisha
nikazama katika dimbwi la mawazo. Nikiwa katika
mawazo yale nikamkumbuka rafiki yangu ambaye
ni kabila moja na mke wangu. Nikampigia simu
alipopokea nikamuuliza kwa sauti ya chini nini
maana ya Ntumbo nuumile.
Akanieleza kuwa maana yake ni ‘Tumbo linakata’.
Nikapigia mstari zile hisia zangu!
Kwa sababu mke wangu alijifanya amelala, nami
nikajilaza lakini sikupata usingizi kabisa. Moyo
wangu ulikuwa unauma sana, mapenzi yalikuwa
yananitesa mimi.
Baada ya kuamka mke wangu alienda kuoga.
Alipoingia bafuni na mimi nikatumia fursa ile
kuichukua simu yake ya mkononi nikatazama
namba alizowasiliana nazo, nikazinukuu namba
mbili za mwanzo kisha nikarejea sebuleni.
Sikukaa sana nikaondoka.
Kwa kutumia huduma ya vibanda vya simu
nikawasiliana na zile namba walau niweze kujua ni
sauti za akina nani.
Simu ile ya kwanza ilinikata maini na kunifanya
nibadilike na kuwa kiumbe mwingine kabisa.
Simu ya kwanza ilikuwa ni sauti ya mkuu wangu
wa kazi, mkuu wa shule ambayo nilikuwa
nafundisha.
Nikajikaza na kupiga ile namba nyingine.
Naam! Ilikuwa sauti ya mwalimu mkuu msaidizi…
Watu ambao nafanya nao kazi sehemu moja,
wakuu wangu wa kazi, wakubwa wangu kiumri,
washauri wangu!
Ati! Wanahusika pia katika kunipondaponda moyo
wangu!
Ni kitu gani wanawasiliana na mke wangu… ni kitu
gani kinaendelea?
Nilishikwa na kizunguzungu sana lakini ilikuwa
bahati tu sikuanguka!
Nilichanganyikiwa!!
**Naam! Hiyo ni sehemu ya tatu ya simulizi hii ya
maisha iiitwayo TONE LA MWISHO LA
UVUMILIVU……
 
SEHEMU YA NNE
Mwalimu Lusu amegundua kuwa mkewe
anawasiliana na mkuu wa shule pamoja na
makamu wake!!!
Ni kitu gani wanawasiliana watu hawa.
Lusu amepagawa!!
ENDELEA!!
NILIONDOKA pale huku nikiwa naonekana kuwa
mtu na timamu zake lakini waendesha pikipiki
kadhaa nd’o waliweza kugundua kuwa sikuwa
katika hali ya kawaida kabisa.
Nilipigiwa honi sikusikia, pikipiki moja
ikanikosakosa. Niliyasikia matusi juu yangu!
Hapo nikagundua kuwa nilikuwa nimepagawa!
Ili kujiepusha na hatari zaidi nikauendea mti na
kuketi chini yake. Kichwa kilikuwa kinauma katika
kiwango cha juu sana.
Nilipumzika kwa dakika kadhaa huku nikiilazimisha
akili yangu ikae sawa ilimradi tu niweze kuwa
makini barabarani.
Nikiwa pale chini ya mti ule wazo la ghafla
lilinipitia, wazo la kuwavamia mkuu wa shule na
makamu wake na kuwauliza ni kitu gani haswa
walikuwa wanafanya na mke wangu mbali na upeo
wa macho yangu.
Nikayafumba macho yangu na kuzikumbuka zile
kauli tata kati ya mkuu wa shule na mke wangu,
pale mmoja aliposema kwa mama mdogo ni
Tandika huku mwingine akisema ni Mwenge.
Nikajikuta naufikiria ukweli ambao sikutaka uwe
ukweli.
Yawezekana Neema wangu alikuwa yu pamoja na
mkuu wa shule wakati nampigia simu na kumsihi
aonane naye, na iwapo walikuwa pamoja basi
baada ya kukata simu walicheka kwa pamoja
kisha wakagonga mikono yao, na huenda walifikia
hatua hata ya kunitukana!!
Mawazo haya yaliniumiza, na kisha wazo la
mwisho kabisa likanifanya nianze kutokwa damu
puani kama ilivyokuwa kawaida yangu nikighafirika
kupita kawaida!!
Wazo kwamba mke wangu kipenzi ameshindwa
kuwa mkweli katika ndoa na sasa yu katika
mahusiano ya kimapenzi aidha na mkuu wa shule
ama makamu wake!!
Mapigo ya moyo yalizidi kasi yake wakati
napambana na damu iliyokuwa inavuja kutoka
puani.
Bahati nzuri nilikuwa na kitambaa, nikafanikiwa
kukabiliana nayo.
Simu yangu ya mkononi iliita wakati huo damu
zikiwa zimekata tayari. Kutazama jina katika simu
lilisomeka ‘MKE WANGU KIPENZI’…..
Chozi lilinitoka msikilizaji!!
Mara ya kwanza sikupokea lakini ile mara ya pili
niliipokea huku nikilazimisha uchangamfu.
Neema mke wangu alikuwa na kisu kingine kikali
tu cha kunichoma.
Naam! Akanieleza eti ya kuwa ule mzigo aliouziwa
ni feki hivyo ni muhimu arudi upesi Dar maana
aliambiwa kuwa zikipita siku nne hajarudisha
mzigo kama una matatizo basi hautapokelewa
tena.
“Tutazungumza nikirejea nyumbani mke wangu”
nilimsihi kwa upole kama ilivyokuwa kawaida
yangu.
“Hapana mume wangu, naomba tu nikimbie sasa
hivi, sasa hivi saa sita natumia masaa matatu
kufika kule halafu kesho asubuhi narejea
tafadhali.”
Alisisitiza Neema. Akili yangu ilikuwa haipo sawa
bado nikajikuta tu namwambia aende! Akashukuru
huku nikiyasikia mabusu kedekede ambayo
alinitumia kisha akasema ananipenda sana kuliko
wanaume wote.
La haula! Neema alikuwa shetani anayeua
polepole!!
****
Baada ya kutoa ruhusa ile bila kujua ni kwa nini
naitoa, wazo la ziada likakikumba kichwa changu.
TONE LA MWISHO LA UVUMILIVU!!
Ni hiki nilikifikiria, na kisha nikasimama kiujasiri na
kusema kuwa liwalo sasa na liwe. Ama zangu ama
zao!
Nikanyanyua simu yangu na kumpigia mwanamke
anayenipenda kuliko wote duniani!
Mama Lusu mama yangu mzazi!
Ama kwa hakika mtoto kwa mama hakui… ile
natoa salamu tu, mama akaniuliza iwapo nilikuwa
naumwa.
Nikakataa!
Akasema yawezekana kweli siumwi lakini nina
hasira! Nani kanikasirisha? Lilikuwa swali jingine.
Ule upendo wa mama ukanifanya nizidi kujisikia
vibaya. Nikatamani kumweleza kila kitu lakini
niliona muda hautoshi kabisa kwa sababu kuna
jambo la haraka sana nilitakiwa kulifanya.
Nikatamani kumweleza kwa kifupi lakini
asingeweza kunielewa!!
Nikiwa sijajua nini cha kusema ghafla mama
akaniambia.
“Lusu kama ni mke wako amekuudhi, chunga
mkono wako usije ukapiga mtoto wa watu.
Jichunge kabisa, na kama hasira zako hauwezi
kuzizuia nakuomba upande gari urudi Mbeya!
Sikutaka kuendelea kuzungumza na mama,
nikamuaga na kukata simu.
Nilipokata simu ya mama, mara ikaingia simu ya
mkuu wangu wa kazi. Akanipa taarifa kuwa niende
shuleni kwa sababu amepata dharula anaondoka
mara moja!
Wakati nazungumza naye mara nikaliona gari lake,
jirani na maeneo ya Msamvu likiwa limeegeshwa!
Bahati mbaya iliyoje, gari lake lilikuwa na vioo
vinavyoonyesha hadi ndani.
Bora vingekuwa vyeusi nisiweze kushuhudia
nilichokishuhudia!!
Neema mke wangu wa ndoa katika gari ya mkuu
wa shule!!
Nikajikuta nashindwa kuzungumza, nikaikata simu,
nikajaribu kusimama miguu haikuwa na nguvu hata
kidogo.
Hasira ilikuwa pomoni!!
Yaani mke wangu tena huenda anayo pete ya
ndoa kidoleni ananifanyie ushenzi kama huu.
Miezi minne tu ya ndoa!!
Swali likawa moja, kuna nini kinaendelea kati yao!
Kama ni wapenzi mbona muda mwingi tu mimi
nipo ofisini, kwanini wasikutane hapahapa
Morogoro maana maeneo ya kukutania ni mengi
tu!!
Kwanini wasafiri!!
Na bila shaka hii si mara ya kwanza kusafiri
pamoja, kitendo kile cha kukuta mke wangu akiwa
hana tiketi aliporejea kutoka Dar ilikuwa ni ishara
tosha.
Na hapohapo nikaukumbuka uchovu mkali
aliokuwanao mke wangu usiku ule?
Sasa kama alisafiri katika gari nzuri kiasi hiki
ilikuwaje akachoka kiasi kile!
Loh! Mkuu wa shule kuna kitu alimfanyia mke
wangu??
Nikajaribu kusimama tena…. Sasa niliweza
kusimama kiujasiri nikiwa imara kabisa……
ITAENDELEA!!!
 
SEHEMU YA MWISHO
Nilichoamua kilihamasishwa na ule usemi maarufu
wa zama hizo.
Ngoja ngoja huumiza matumbo… na heri nusu
shari kuliko shari kamili.
Nikaongezea na ule usemi wa kitemi, LIWALO NA
LIWE!!
Nikaamua kwenda pale lilipokuwa gari la mkuu wa
shule, niliuona waziwazi mwili wangu ukitetemeka
maeneo ya mikononi na misuli ya shingoni
ilinikakamaa.
Nikajaribu kumeza mate lakini hayakupita.
Sikujua nikifika nitafanya nini lakini nilihisi
nitafanya kitu ambacho hakuna mtu ambaye
ananifahamu angeweza kufikiria kuwa naweza
kukifanya.
Macho yangu yalikuwa yameelekea sehemu moja
tu! Alipokuwa mkuu wa shule na mke wangu!!
Ama!! Mke anauma jama!! Mke anauma, mke si
sawa na hawara, mke si sawa na mpenzi tu
mnayeishi kimazoea. Mke ni kitu kingine!
Maumivu niliyoyapata, ewe msikiliza uliye katika
ndoa wayajua hasahasa ukihisi mwenza wako
anakufanyia jambo baya nyuma ya kisogo chako
na usijue kinachoendelea!!
Ikiwa tu unahisi kusalitiwa unaumia kiasi hicho, je
mimi niliyemuona mke wangu akiwa na mkuu
wangu wa ngazi!!
Nilitamani moyo utoe kifuani kwa muda uwe nje
ya mwili wangu niumwagie maji ya baridi huenda
ungepoa!!
Sasa haukuwepo ule upole tena, nilikuwa
nimechanganyikiwa kwa jazba.
Wakati navuka barabara huku macho yangu yakiwa
bado sehemu moja tu.
Hatimaye macho yangu yakagongana nay ale ya
mke wangu!!
Ile taharuki aliyoipata sina maneno ya kukuelezea
uelewe!
Na hapo akawa amenizidishia hasira!
Nilipopiga hatua mbili mbele, hasira zangu
zikaishia pale ndugu msikilizaji.
Nilijikuta hewani juu juu kisha nikatumbukia
mtaroni, kichwa kilijibamiza kwenye kuta za
mtaro. Uso wangu ulikuwa unaelekea juu na
niliona jinsi mke wangu alivyokuwa shetani.
Alizuiwa na mkuu wa shule asije kutazama nini
kimenisibu, nikamuona akirudishwa garini.
“Nakulaani Neema, nakulaani wewe na kizazi
chako… nakuombea utasa, nakuombea umasikini,
nakuombea msongo wa mawazo, uishi kama kivuli
uwe mtu wa kukimbia kila siku iendayo kwa
Mungu, nakuombea huzuni we mwanamke….”
Nilijikuta nikijikaza kuongea ili Neema anisikie
lakini mbavu zilikuwa zinauma sana.
Baada ya muda kidogo kiza kikatanda!!
Naam! Fahamu zangu zikakomea pale, mambo
yaliyoendelea nilikuja kuhadithiwa tu nikiwa
hospitali. Siku tatu baada ya kupata fahamu.
Majira ya saa nne usiku nd’o muda ambao fahamu
zilirejea baada ya siku tatu kupita. Nilijikuta na
bandeji gumu kichwani mwangu, mbavuni pia
nilikuwa nimefungwa bandeji.
Nilijhisi nipo peke yangu lakini nilipojitikisa kidogo
na kuguna kwa maumivu nikasikia mtu akiniita.
“Lusubilo mwanangu kipenzi!!”
Ilikuwa sauti ambayo kamwe nisingeweza
kuisahau, sauti ya mama yangu kipenzi..
mwanamke anayenipenda kupita wote duniani.
“Mama, mama… Neema wa kunifanyia vile mimi?
Eeh! Mama Neema kweli? Naomba unisaidie
kunivua hii pete mama siitaki tena na sitavaa tena
pete” nilimsihi mama.
Lakini mama hakuwa na papara katika kunijibu.
Alivuta pumzi kisha akanieleza kwa sauti ya
wastani.
“Lusu, pembeni yako yupo mwanamke
anayekupenda kupita wote maishani. Na hata
pasipo na maisha! Sahau yaliyopita sasa,
watakusaliti wote lakini sio mimi mama yako. Na
nd’o maana nilikwambia kama una hasira urudi
Mbeya”
“Mama uvumilivu ulinishinda, tone la mwisho la
uvumilivu lilidondoka nisingeweza kuvumilia zaidi
ya pale… kwanza yupo wapi?”
“Pumzika mwanangu, si wakati wake!!”
BAADA ya kupata nafuu, mguu wangu mmoja
ulikuwa umevunjika nilikuwa natembelea magongo,
mbavuni nilikuwa na bandeji na kichwani pia!!
Kadri nilivyoendelea kupata nafuu nikiwa mjini
Mbeya, hatimaye mama akanieleza juu ya ushenzi
wa yule mwanamke.
Kumbe alikuwa na mahusiano na mkuu wangu wa
kazi, na aliyemkuwadia alikuwa ni makamu wake.
Katika rukaruka zao mkuu wa shule akamjaza mke
wangu mimba.
Na wazo la biashara aliloleta mke wangu ni ili
apate upenyo wa kwenda Dar kutoa mimba.
Jaribio la kwanza kwa kutumia kidonge
likashindikana, nd’o akapatwa na maumivu ya
tumbo wakaamua kurejea tena Dar kujaribu njia
nyingine.
Kwa habari nyepesi nyepesi tu ni kwamba ile
haikuwa mimba ya kwanza kutoa.
Nilitabasamu huku machozi yakinitoka!
Nilichomwambia mama ni kitu kimoja tu.
Na tuache maisha yaendelee, lakini hata maisha
yaendelee vipi katu sitakuja kushiriki mchezo
uitwao NDOA.
Si mchezo mzuri hasahasa kwa mchezaji kama
mimi ambaye nilipenda kwa moyo wote.
Mama hakunipinga!!!
Nikajiuguza hatimaye nikapona!
Mama alihisi nitaubadili uamuzi wangu siku moja,
ila hadi naamua kuyasimulia haya ili nawe
ujifunze!!
Wadogo zangu wawili wameoa na nilishiriki
ipasavyo harusi zao, marafiki zangu wengi tu
wameoa na hawa walinitumia kadi za michango!
Jamaa zangu wengine wapo katika mipango ya
harusi. Hawa waache waoe tu!
Ndoa iliyotaka kunitoa roho!! Sitaki kuisikia.
Nilipata bahati ya kukutana na Neema jijini Dar es
salaam, walau nami nikapata kumshukuru Mungu
kwa kukisikia kilio changu. Alikuwa hajaolewa
tena, alinisihi tuwe pamoja tena nikamwomba
abadilishe mada ili amani iendelee kutawala!
Tangu hapo sikumuona tena na ni heri kwa sababu
sihitaji kuonana naye mwanamke yule mwenye
roho ya kishetani!!
JIFUNZE!
Mapenzi yana chungu na tamu, waweza penda
usipopendwa na mapenzi yana raha na karaha!!!
MWISHOOO!!
 
Dah story nzuri sanaa mpaka mwili unasisimka Kuna kitu nimejifunza
 
Duh jamaa yangu pole sana
ww km ni Hadithi
mimi YALINITOKEA KWELI kabisa

Kinauma sana kugongewa mali zako
Mimi nilichapiwa mtarajiwa wangu wa Ndoa niliyemvisha pete na Mimba kumbebesha
kumbe alikuwa anatoka kwenda Usandaweni na jamaa mchimba visima (Drill) ambaye alikuwa tayari ana mke
nilipogundua mchezo wao naye akaachwa na huyo jamaa kurdi kwangu sikumtaka asilani
akakimbilia Tabora nako hajazaa mpaka leo
mm nikaja OA na nina watoto
yote nimemuachia MUNGU
 
Pole sana kaka duh inaumiza sana sema nipale tu Mungu katufumba kujua mwanzako anawaza nini.
 
Back
Top Bottom