Simulizi:Risasi Ya Nani?

Simulizi:Risasi Ya Nani?

The Box

Member
Joined
Jun 6, 2021
Posts
60
Reaction score
143

Risasi ya Nani?


Na Kijana Wa Kizazi Kipya

Dodoma Tanzania.
Simulizi hii ni ya kubuni!




Utangulizi


Dodoma, jiji lililojengwa katikati ya nchi, liligeuka kuwa jukwaa la kizazi kilichochoshwa na ukimya. Ilikuwa usiku wa giza nene baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa — matokeo yaliyotikisa mioyo ya vijana waliokuwa na ndoto za kuona Tanzania mpya. Barabara zilikuwa tupu, lakini anga lilijaa sauti za mitandaoni, maneno ya hasira na matumaini.


Katikati ya joto la usiku huo, kundi la vijana lilijikusanya kimya kimya kwenye uwanja wa Jamhuri, wakipeana ishara za mapambano. Walikuwa wameamua — ikiwa sauti haitasikika kwa kalamu, basi italazimika kusikika kwa miguu yao mitaani.


Miongoni mwao alikuwepo Ndelamiko Makaka, kijana wa Kigogo mwenye umri wa miaka thelathini na moja hivi, uso uliojaa alama za mateso lakini macho yaliyowaka kama moto wa haki. Hakukuwa na cha kupoteza tena kwake — maisha tayari yalikuwa yameyeyuka mikononi mwa ahadi zisizo na mwisho.
Hapo ndipo safari ya damu na mabadiliko ilipoanza.




Sura ya Kwanza: Mwanzo wa Moto


Ndelamiko alizaliwa miaka ya 1990's katika kijiji kidogo kiitwacho Msembe, wilayani Bahi, mkoa wa Dodoma. Kijiji kilichokuwa na vumbi zaidi kuliko maji, na matumaini machache kuliko mvua za masika. Alilelewa na mama yake, Mariamu, mwanamke mjane aliyekuwa akihangaika kuuza maandazi sokoni ili angalau mtoto wake apate kalamu na daftari.


Utoto wake ulikuwa ni simulizi ya njaa na matumaini. Alipenda sana shule, si kwa sababu ilikuwa rahisi, bali kwa sababu ndiyo sehemu pekee alihisi dunia inaweza kumsikiliza. Alipata alama nzuri kila hatua, na mwaka 2017 alihitimu masomo ya Ualimu wa Shule ya Msingi katika Chuo cha Ualimu Butimba, akiwa na ndoto kubwa — kufundisha, kuhamasisha, na kubadilisha kizazi chake kupitia elimu.


Lakini dunia haikuwa na nafasi kwa ndoto hizo.
Miaka ikapita — 2018, 2019, 2020… kila mwaka akijaza fomu za ajira, akipita ofisi za elimu, akiahidiwa, akiahirishiwa. Hatimaye ndoto zikaanza kukauka kama mashamba ya mahindi ya Mautya yaliyosahaulika na mvua.


Wakati wengine wakienda mijini kutafuta vibarua, Ndelamiko alibaki kijijini akifundisha watoto bila malipo,huko alifahamika kama Mwalimu Wa Kujitolea ,akiamini siku moja serikali itakumbuka ahadi zake. Lakini siku hiyo haikuwahi kufika.


Kizazi kizima cha vijana kama yeye kilikuwa kimenyimwa ajira, kilichoshuhudia ufisadi wa waziwazi, na woga wa kuhoji ukikuzwa kama maadili mapya ya uraia. Kila kitu kilionekana kimya, mpaka pale uchaguzi mkuu wa 2025 ulipofika — na mchakato huu ukaleta zaidi ya mshangao; ulileta Hasira.Vifo.Majonzi.Vilema!


Usiku wa tarehe 28 Oktoba, Ndelamiko alipokea ujumbe kwenye simu yake ndogo:


“Kesho tunaanza Dodoma. Huu ni wakati wa kizazi kipya. Uko tayari?”

Alitazama simu kwa muda mrefu, akihisi moyo ukipiga kwa kasi. Hakuwa mwanasiasa, wala hakuwahi kushika bango la maandamano, lakini alikuwa na kitu ndani yake kilichovunjika muda mrefu. Akafunga shuka lake, akaangalia picha ya mama yake ukutani, kisha akasema kwa sauti ya chini:


“Kama mimi nisipoamka, nani ataamka kwa ajili yetu?”

Usiku huo wa manane, aliondoka kijijini Msembe kuelekea Dodoma mjini — akiwa na begi moja, daftari lake la ualimu, na ndoto ya kuona haki ikirudishwa.


Hakujua kwamba safari hiyo ndiyo ingekuwa mwanzo wa simulizi itayotikisa taifa zima — Risasi ya Mabadiliko.Ilikuwa Risasi ya Nani?

Sura ya Pili: Usiku wa Risasi.Ilikuwa Risasi ya Nani?


Usiku wa tarehe 29 Oktoba 2025, anga la Dodoma lilikuwa limejaa upepo wa vumbi na hofu. Miji ilionekana kimya, lakini mioyo ya vijana ilikuwa inapiga kelele. Walikuwa wamechoka — si kwa njaa pekee, bali kwa kudharauliwa, kuchezewa akili, na kuahidiwa kesho ambazo hazijawahi kufika.


Kwenye kona ya barabara ya Nyerere, Ndelamiko na wenzake zaidi ya mia mbili walikusanyika kimya kimya. Walivaa mavazi meusi, wengine wakiwa wamefunga vitambaa vya taifa shingoni, wengine wakibeba mabango yaliyotengenezwa kwa makaratasi ya katoni.
Moja ya mabango hayo liliandikwa:


“KIZAZI KIPYA HATUNUNUI UOGA.”

Walipiga magoti, wakanyoosha mikono juu, wakianza kuimba taratibu:


“Tunaomba haki, si vita! Tunaomba ajira, si ahadiTunaomba Katiba Mpya!”

Lakini kabla wimbo haujakamilika, magari makubwa ya polisi yalifika yakipiga honi nzito. Taa za tochi zikalipuka gizani kama radi za ghadhabu. Muda mfupi baadaye, milio ya risasi ikasikika — pap! pap! pap!


Watu wakaanza kukimbia ovyo, wengine wakianguka, wengine wakijaribu kubeba walioumia. Vumbi, machozi, na mayowe vilichanganyika. Ndelamiko alihisi moto ukipenya kwenye paja lake la kushoto — risasi moja, ndogo lakini yenye uzito wa historia. Akapiga hatua mbili mbele kisha akaanguka chini, damu ikitiririka taratibu juu ya lami baridi.


Alipoangalia juu, akaona bendera ya taifa ikining’inia kwenye shingo ya rafikiye katika upepo wa usiku. Machozi yakamtoka — si kwa maumivu ya risasi, bali kwa maumivu ya nchi aliyoiamini ikimgeukia.


Wenzake wawili, Sehewa na Amina, walimvuta pembeni, wakijaribu kumsaidia. Amina alilia kwa uchungu:


“Tunaandamana kwa amani, kwanini damu? Kwanini damu tena?”

Ndelamiko akashika mkono wake kwa nguvu ndogo, akasema kwa sauti dhaifu:


“Usilie… hii si mwisho, ni mwanzo. Risasi hii… ni alama ya mabadiliko yetu.”

Usiku huo, jiji lote lilikaa kimya. Wengine walikamatwa, wengine wakatoroka, lakini picha zilzopigwa hazikwenda popote,wakati huo mitandao na vyombo vya habari vilikuwa gizani,hofu ilitanda nchi nzima na dunia kwa jumla,sauti za risasi na mabomu ya machozi yalilindima kote mjini.Wakati miji yote mikubwa ilishaingia shakani,vijana wasio na hatia wakiendelea kupigwa risasi.


Asubuhi ilipofika, jua lilichomoza juu ya Dodoma likiangaza damu iliyokauka kwenye barabara. Watu wachache waliokuwa wakipita walikaa kimya, wengine wakasali.


Katika hospitali ya Dodoma General, Ndelamiko alilala kwenye kitanda chenye shuka jeupe. Alikuwa hajapoteza fahamu, lakini macho yake yalikuwa yamejaa picha ya usiku ule — milio ya risasi, kilio cha Amina, na harufu ya damu.


Akaapa moyoni:


“Nikisimama tena, sitarudi kijijini kufundisha pekee — nitasimama kufundisha taifa zima maana ya haki.”

Na hapo, risasi ya paja ikageuka kuwa risasi ya ufahamu — ikaanza kuamsha roho za vijana wengine kote nchini.

Wakati yeye akiuguza jeraha la paja,vijana wenziwe walishakata roho,wengine hawana miguu.Wakati yeye anauguza paja,wengine walipigwa risasi za makusudi matakoni,wengine walipigwa vichwa na kutolewa ubongo.Kumbe hawakuwa waandamanaji tu.Hadi waliokuwa majumbani mwao,watoto,wamama,wazee.Ni nani alofanya hivi?
Hapa swali analojiuliza Ndelamiko ni moja tu.

Risasi iliyopiga pajani ni ya nani?
Risasi iliyowaua wenzangu ni ya nani?
Risasi ninayoisikia huko nje ni ya nani?

SIMULIZI:RISASI YA NANI?

Itaendelea.......

Kijana.
Dodoma Tanzania



 

Sura ya Tatu: Damu ya Ndoto Zetu



Nilikuwa naota kila siku kwamba maisha yatabadilika.
Kwamba siku moja, tutatembea mitaani bila hofu, tutapata kazi bila kuomba, na tutasikilizwa bila kupiga kelele. Lakini nilikosea — kumbe dunia hii inasikia tu pale damu inapomwagika.


Jina langu ni Anna Mwampamba, natoka mkoani Iringa, kijiji cha Nduli. Nilikulia kwenye familia ya watoto watano, mimi na dada yangu mdogo Neema tukawa tumaini la nyumbani. Tulifika Dar es Salaam mwaka 2022 tukiwa na ndoto zile zile za vijana wengi wa vijijini — kutafuta kazi, kujenga maisha, na kusaidia wazazi wetu waliobaki kulima mihogo.


Tulipanga chumba kimoja huko Mbagala — chumba kilichojaa matumaini, harufu ya sabuni ya bei rahisi, na ndoto zisizokuwa na mwisho. Tulifanya kazi za mikono, tukauza maandazi, tukasafisha nyumba za watu, lakini kila mwisho wa mwezi tulibaki na kitu kimoja tu: uchovu na matumaini.




Kila usiku tulipokuwa tukilala, tulisoma habari kwenye simu za mkononi. Tulisoma kuhusu vijana wa Kenya,Nepal na Madagaskar waliopigwa risasi wakidai haki. Niliona picha za vijana, wakilazwa hospitalini wakiwa na jeraha mwilini. Nilihisi kitu moyoni — uchungu, lakini pia fahari.


Neema alinigeukia siku moja usiku akaniambia:


“Anna, hawa watu wanapigania sisi pia. Haki wanayodai ni yetu wote. Kwa nini tuendelee kukaa kimya?”

Nilijaribu kumzuia, nikamwambia dunia haijawahi kuwa rafiki wa wanyonge. Lakini macho yake yalikuwa yamejaa moto wa matumaini, ule moto ambao mimi nilikuwa nimeupoteza muda mrefu.


Siku tatu kabla ya Oktoba 29, tulianza kuona ujumbe ukienea mitandaoni:


“Vijana wote wa Dar — tunakutana Ubungo. Ni wakati wa kusema inatosha!”

Tulikaa kimya kwa muda mrefu tukiangalia simu, mpaka niliposikia sauti yangu nikisema:


“Tutaenda.”

Neema alitabasamu, machozi yakimtoka kidogo.


“Leo nitavaa tisheti yangu yenye maandishi ‘Mabadiliko ni Sasa’. Nitakufa nikijua nilijaribu.”



Asubuhi ya Oktoba 29, 2025, jua lilichomoza kama moto unaowasha matumaini. Barabara za Dar ziligeuka bahari ya vijana — wengine wakiwa wamebeba matumaini, wengine wakitembea kimya lakini kwa uthabiti wa mioyo. Tulitoka Mbagala mapema, tukapanda gari hadi Ubungo, tukiimba nyimbo tulizozibuni wenyewe njiani.


Tulipofika, nilihisi kama historia inajitengeneza mbele yangu.
Watu walikuwa wanapiga kelele:


“Tunataka haki! Tunataka ajira! Tunataka amani!”

Lakini dakika chache baadaye, anga likabadilika. Gafla nikasikia mlio wa kwanza wa risasi ukipita juu ya vichwa vyetu kama radi. Watu wakakimbia, wakajificha nyuma ya mabasi. Nilimshika Neema mkono, nikamvuta chini, lakini kabla sijamaliza kumgeukia, nikasikia pap! — risasi moja, ikavunja ndoto, ikazima sauti, ikanyamazisha dunia.


Neema alianguka mikononi mwangu, damu ikitiririka kutoka upande wa kichwa chake. Nilishika kichwa chake kwa hofu, nikamwita mara kadhaa:


“Neema! Simama… tumeahidi tutafika mwisho pamoja! Neema!!”

Lakini hakujibu. Midomo yake ilitikisika mara moja tu, ikasema kwa sauti dhaifu:


“Tafadhali… usiache…”

Kisha ikatulia.
Nilihisi ulimwengu umesimama. Nilihisi kila risasi nyingine ikipiga kwenye moyo wangu badala ya hewani. Nilijaribu kupiga kelele, lakini sauti yangu ilikatika.


Watu walikuwa wanakimbia, magari yakipiga honi, moshi ukipanda hewani. Nilibaki nimekumbatia mwili wa dada yangu mdogo, nikiwa katikati ya barabara ya Ubungo, macho yangu yakitazama anga lililogeuka jeusi.




Saa kadhaa baadaye, nilikamatwa na polisi. Walinivuta kwa nguvu, lakini sikupinga — nilikuwa sina nguvu, sina hofu, sina chochote tena cha kupoteza. Waliniweka kwenye gari la klao, nikatazama nyuma nikiwaona vijana wenzangu wakitawanyika kama vumbi lililopulizwa na upepo wa ukandamizaji.


Lakini ndani ya moyo wangu kulikuwa na sauti moja tu ikisema:

“Neema hajafa bure.”



Nilijua siku moja jina lake litasemwa, si kama jina la msichana aliyepigwa risasi, bali kama alama ya kizazi kilichokataa kunyamaza.

Na nilijiambia, hata nikifungwa, hata nikiumizwa, nitasimulia hadithi yake — hadithi yetu — hadithi ya damu ya ndoto zetu.

Kama siyo leo basi kesho.Maana Neema kama kijana wa kizazi kipya amekufa akijaribu.Sijui ulipo mwili wake.Ila naamani Roho Yake Imelazwa Mahali Pema Peponi.

Lakini bado najiuliza moyoni mwangu,Risasi iliyomuua Neema ni ya Nani?


Itaendelea......

Kijana
Dodoma Tanzania
 
Risasi Ni Ya Nani?

Sura ya Nne: Moto Wa Ziwa Victoria.

Sauti ya injini ya pikipiki yangu ilikuwa ndiyo pumzi yangu ya mwisho ya matumaini.
Niliipenda, si kwa sababu ilikuwa ya bei ghali, bali kwa sababu ndiyo iliyonipa heshima yangu, chakula changu, na sauti yangu katika jiji hili lenye kelele — Mwanza, mji unaocheka mchana na kulia usiku.

Jina langu ni Peter Mayalla, umri wangu ni miaka ishirini na nne. Nilizaliwa kwenye mitaa ya Nyakato, pale ambapo watoto wanajifunza kuendesha baiskeli kabla ya kusoma majina yao. Nilikuwa mtoto wa mama mjane, mama aliyekuwa akiuza samaki sokoni kwa maisha yote. Kila siku aliniambia,

“Peter, haki haiji kirahisi. Lakini ukikosa kuipigania, utabaki mtumwa wa kimya.”



Nilicheka nilipokuwa mdogo. Sasa naelewa alimaanisha nini.


---

Mambo yalianza baada ya kusikia taarifa kutoka Dodoma — vijana kupigwa risasi, mmoja kujeruhiwa vibaya, na dada wawili kupoteza maisha kule Dar es Salaam.
Picha za mitandaoni zilikuwa hazikaiki. Kila mara nikipita kijiweni, watu walikuwa wakizungumza kwa sauti ya chini:

“Umesikia? Huyu Ndelamiko yuko hospitali, lakini watu wanazidi kuamka...”



Ndani yangu kitu kilianza kuwaka. Nilikuwa nimechoka — kila siku kubeba abiria wasio na matumaini, kusikiliza maneno ya kukatisha tamaa, na kuona viongozi wakipita kwenye msafara wa magari mapya huku sisi tukipambana na mafuta ya pikipiki.

Tulikuwa vijana watatu: mimi, Moris na Tito. Wote tulikuwa bodaboda, marafiki tuliounganishwa na njaa, na tumaini.
Siku ya tarehe 30 Oktoba 2025, tuliamua kwamba hatuwezi kubaki kimya. Tuliona ujumbe ukisambazwa:

“Mwanza nayo iinuke. Ni wakati wa kusema inatosha.”



Tulikutana saa kumi alfajiri, pale kwenye stand ya Nyakato. Moris alikuwa amefunga bendera ndogo ya taifa kwenye pikipiki yake, akasema kwa sauti tulivu:

“Leo tukianguka, tutaanguka upande sahihi wa historia.”



Tulianza safari kuelekea katikati ya jiji, tukiungana na vijana wengine waliokuwa wakipiga honi, wakiimba nyimbo za matumaini.
Barabara ya Kenyatta ilikuwa imejaa watu — wachuuzi, wanafunzi, wafanyabiashara wadogo, wote wakishangilia, wengine wakilia kwa hisia. Nilihisi kana kwamba hatimaye nchi inasikiliza kilio chake.


---

Lakini saa nne asubuhi, kila kitu kilibadilika.
Mlio wa kwanza wa risasi ulisikika karibu na stendi ya Buzuruga. Watu wakatawanyika kama moshi. Nilimwangalia Tito aliyekuwa karibu nami, akasema kwa hofu:

“Peter, wanapiga watu! Wanarusha risasi!”



Tuligeuka nyuma, lakini tuliona askari wakiwa wameshika bunduki, macho yao yakiwa baridi kama chuma. Nilijaribu kupiga kelele:

“Tunaandamana kwa amani! Hatuna silaha!”



Lakini risasi hazisikii maneno.
Risasi ya kwanza ilimpiga Tito kifuani. Akaporomoka chini, damu ikimwagika juu ya barabara ya vumbi. Nilimkimbilia, nikajaribu kumuinua, lakini macho yake yalikuwa yamelegea, yakinitazama kwa upole wa mwisho.

Kabla sijapata muda wa kutulia, Moris naye alipigwa risasi ya kichwani. Kichwa chake kiligeuka kimya, pikipiki yake ikadondoka pembeni. Nilihisi ulimwengu unazunguka — nilitaka kupiga kelele, lakini sauti ilikataa kutoka.

Nilipiga magoti katikati ya barabara, nikiwa nimevaa jaketi lililolowa damu za marafiki wangu. Nilihisi hewa inakuwa nzito, nikasikia ndani yangu sauti ya mama yangu ikisema:

“Usiogope, haki huanza pale damu inapomwagika kwa sababu ya wema.”




---

Jioni ile nilijificha karibu na ufukwe wa Ziwa Victoria. Nilikaa kimya nikitazama maji yakitulia, kama hayajui kilichotokea.
Niliona mwanga wa jua ukizama taratibu, ukigeuza ziwa kuwa damu nyekundu. Niliweka mikono yangu juu ya kifua changu nikasema kimoyomoyo:

“Mungu, kama kweli unatusikia, basi kumbuka majina yao — Tito na Moris. Wamekufa kwa imani, si kwa ujinga.”



Nilikaa hapo kwa saa nyingi, machozi yakitoka bila kizuizi. Nilihisi upepo ukipita usoni mwangu, na kwa sekunde moja, nilihisi kana kwamba marafiki zangu walikuwa hapo — wakiniambia nisikate tamaa.

Ndani ya usiku ule, niliona ndoto.
Niliona Tito amevaa tisheti nyeupe, uso wake uking’aa kama mwezi, akiniambia:

“Peter, usiache moto huu uzimike. Risasi zinaua miili, lakini si ndoto.”



Nilipoamka, machozi yalikuwa yametengeneza njia mashavuni mwangu.
Nilijua, bila shaka, kwamba mimi sasa ni sauti ya wale waliokwisha kufa.


---

Siku hiyo nilirudi nyumbani kwa mama yangu, nikiwa nimebeba pikipiki yangu iliyovunjika na damu ya marafiki zangu. Mama alinipokea kimya, macho yake yakinitazama kama anayesoma majeraha ya dunia.
Akasema kwa sauti ya upole lakini ya uchungu:

“Mwanangu, hii nchi inalia, lakini macho yake yamepofuka. Msipoendelea kupigania wema, hakuna atakayebaki kuota ndoto.”



Nilimkumbatia, nikajua kwamba chochote kitatokea, damu ya Tito na Moris haitapotea bure.

Na hivyo, Mwanza — jiji la ziwa, jiji la machozi — likawa sehemu nyingine ambapo historia ya mabadiliko iliandikwa kwa damu.

Lakini,Risasi Iliyomuua Tito na Moris ni ya nani?

---

Itaendelea....
 
Ngoja nikuignore kabisa nisiwe naona huu ujinga hasa kipindi hiki
 
Wakuu kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu,nitalazimika kuhariri baadhi ya taarifa hasa kuanzia sehemu inayofuata
 
Sura ya Tano: Kiti cha Moto

Kiti cha rais ni kiti kinachowaka moto — moto wa maneno, moto wa hofu, na moto wa damu.
Kwa macho ya nje, kila kitu kilionekana kitulivu: bendera zikipaa, wimbo wa taifa ukipigwa, magari ya kifahari yakizunguka ikulu. Lakini ndani ya kuta hizo nene za marumaru, kulikuwa na giza ambalo halikuhitaji taa kuonekana.

Rais Dkt. Rehema Mshana alikuwa amekaa kimya kwenye ofisi yake iliyopo nje mji wa Dodoki eneo liitwalo Chamunyu, akitazama ripoti ya usalama mezani. Ilikuwa imejaa picha za maandamano kutoka Dodoki, Dala, na Mwanana.
Watu walikuwa wamejaa mitaani, vijana wakiwa wamebeba mabango yenye maneno makali kama “Tume Huru Sasa!”, “Ajira kwa Vijana”, na “Haki kwa Wote.”

Aliweka ripoti chini, akavuta pumzi ndefu. Kwenye kioo cha dirisha alichoangalia kila siku, hakuona tena uso wa mwanamke aliyewahi kuwa na matumaini — aliona kiongozi aliyezungukwa na woga wa kupoteza mamlaka.


---

Miaka minne iliyopita, mtangulizi wake, Rais Poka Mnyika, alikuwa amefariki ghafla akiwa madarakani. Rehema, aliyekuwa makamu wa rais wakati huo, aliapishwa kwa haraka — machozi yakiwa hayajakauka, mikono ikishika Biblia na Katiba kwa wakati mmoja.
Watu walimpa matumaini. Walidhani angekuwa mwanga wa kizazi kipya. Lakini muda ulipita, na mwanga huo ukageuka moshi wa hofu.

Mtoto wake pekee, Chris Mshana, alianza kuwa gumzo mjini. Makampuni yake yalikuwa yakishinda zabuni serikalini kwa kasi ya ajabu. Wapinzani waliokosoa hali hiyo walipotea ghafla; wengine walipatikana wakiwa kimya milele.
Vyombo vya habari vilivyothubutu kuandika viliitwa “vichochezi.”
Na sasa maandamano haya mapya yalimfanya rais huyo ahisi kama historia inamgeukia.


---

Usiku wa tarehe 30 Oktoba, saa tano usiku, kikao cha siri kilifanyika kwenye chumba cha mikutano cha ikulu. Walihudhuria mawaziri wachache wa usalama, wakuu wa vikosi maalum, na mshauri mmoja kutoka nchi jirani ya Zambeka, taifa lililokuwa na uhusiano wa kijeshi na Tanzika.

Rehema aliingia taratibu, akakaa kitini bila kusema neno. Macho yake yalikuwa makavu, lakini ndani yake kulikuwa na wingu la maamuzi mazito.

“Je, wamekataa kuondoka mitaani?” aliuliza kwa sauti tulivu.

Mkuu wa jeshi akainua macho, akasema kwa tahadhari,

“Bi. Rais, maandamano yameenea. Mwanana, Dodoki, Dala… watu wanapiga kelele za mabadiliko. Tume ya uchaguzi huru wanadai. Na sasa wameanza kuimba nyimbo zinazokukashifu.”



Kimya kizito kikafuata.
Rais akaweka mkono wake kwenye kidevu, akasema taratibu,

“Wanasema nataka madaraka. Wanasahau mimi nilichukua kiapo cha kulinda amani. Wanasahau jinsi taifa lilivyokuwa karibu kugawanyika baada ya kifo cha Mnyika. Hawa vijana wanataka vurugu. Na vurugu haitamalizwa kwa maneno…”.Endeleeni kufunga mitandao,vyombo vya habari vya ndani na nje visionekane mitaani



Mshauri kutoka Zambeka akainama mbele, akasema,

“Mhesimiwa, jeshi letu linaweza kusaidia kidogo,tuna vijana maalum kwaajili ya mambo kama haya. Hatuhitaji vita — tunahitaji onyo. Onyesho la nguvu tu.”.

Ikumbukwe kuwa Zambeka ni sehemu ya Muungano wa Tanzika



Kisha kimya kikafuata.
Rais akageuka, macho yake yakimeta kama chuma kilichopigwa moto:

“Sawa. Fanyeni onyo. Hakikisheni wanajua nchi hii bado ina serikali.”




---

Saa chache baadaye, magari ya kijeshi yaliondoka kimya kimya kutoka kambini, yakielekea kwenye miji mikuu. Upepo wa usiku uliubeba harufu ya damu kabla hata ya risasi kupigwa.

Wakati milio ya bunduki ikianza Dodoki, Mwanana, na Dala, rais alikuwa amesimama dirishani, akitazama anga la usiku likipambwa na radi.
Akajiuliza kwa sauti ndogo:

“Je, hii ndiyo njia pekee ya kuilinda nchi? Au ni njia ya kuilinda nafsi yangu?”



Lakini majibu hayakuja.
Aliona tu mvua ikianza kunyesha — mvua nzito, kana kwamba anga lilikuwa linaosha damu ambazo yeye mwenyewe alikuwa ameamuru zimwagike.


---

Usiku huo, wakati akilala, aliota ndoto.
Alikuwa amesimama katikati ya uwanja mkubwa wa taifa, amevaa vazi jeupe. Watu elfu walikuwa wamelala chini, kimya, kama bahari ya miili isiyopumua. Alijaribu kupiga kelele, lakini sauti haikutoka.
Kutoka mbali, alimuona kijana mmoja akitembea taratibu — Ndelamiko, akiwa ameshika bango lililochanika lililosomeka:

“Risasi ya Mabadiliko.”



Alipokaribia, akauliza kwa sauti ya upole lakini kali:

“Mama, unalinda amani au unaua matumaini?”



Ndipo alipoamka kwa woga, jasho likimtoka usoni.
Alitazama kioo chake — hakukuwa tena na uso wa rais. Aliona sura ya mwanamke aliyechoka, aliyepoteza usingizi kwa maamuzi yake mwenyewe.


---

Asubuhi yake, taarifa zilienea kote nchini:

“Vijana kadhaa wauawa katika maandamano.”
“Serikali yazima vurugu kwa nguvu.”
“Amani yarejea nchini.”
"Rais Mteule aapishwe"



Lakini kwenye mioyo ya wananchi, amani haikurejea — ilizikwa na damu.
Na kwenye kiti cha rais, moto ule ule uliendelea kuwaka — kimya, lakini ukiwaka ndani ya dhamiri ya mwanamke aliyeanza kuona roho za wale waliokufa zikipita kila alipofumba macho.

Risasi Ni Ya Nani?

Itaendelea Kesho......
 
Back
Top Bottom