SURA YA PILI
SAA sita na nusu za usiku tuliingia jijini kila mtu alikuwa amechoka vibaya.
Baadhi ya watu walishukia Ubungo ila kwa kuwa mr Magembe alikuwa akiishi
Gongo la mboto na mimi nilikuwa nikiishi Buguruni Malapa alinisogeza hadi
Buguruni Sheli na kuniacha pale.
Pale nilichukua bajaji usiku ule na kumtaka dereva anipeleke Malapa.
Njaa ilikuwa inauma lakini sikuwa na hamu ya kula chakula chochote, nilikuwa
mnyonge mno.
Usiku ule nilikuta geti la nyumbni kwangu limefungwa nilizunguka katika dirisha
la mama mwenye nyumba na kumgongea anifungulie mlango.
“Eeh Zahara huyoo!”
“Ndiye mimi mama”
“Karibu mwanangu, za huko”
“Salama tu mama za hapa”
“Hapa kwema mwanangu sijui mnatunyima nini huko”
“Mvua, matope na baridi”
Nilisema kwa utani, na hapo mama akacheka huku mimi nikifungua komeo la
mlangoni kwangu na kuingia ndani.
“Halafu….we Zahara ”
“Abee mama”
“Kuna baba mmoja amekuja hapa leo kukuulizia mara kumi kumi” alisema mama
mwenye nyumba.
“Baba yupi huyo?”
“Hajaniambia jina lake ila anasema mlikuwa wote huko Usukumani huko uliko
kuwa na mlikuwa katika safari moja leo”
“Unasema!!” moyo wangu ulipiga mkumbo kama mdundo wa nyimbo za Marijani
Rajabu, taswira ya yule mtu kule katika mgahawa ikanirejea tena usoni mwangu.
10
“Unasema kweli mama?”
“Ndio..kwanini nikuongopee mama”
“Hakuacha chochote hapa”
“Ameacha”
“Kaacha nini?”
“Namba ya simu”
Kidogo nilipata nguvu nikaona tumaini jipya la maisha yangu. Kwani niliamini
nitavipata vifaa vyangu,na kwa mara ya kwanza nilijikuta naomba toba kwa
Mungu wangu kwa kumuhisi vibaya yule mtu. Kwa kweli hakuwa ni mtu mbaya
angekuwa mwizi kama ambavyo tulimuona kamwe asingefika pale nyumbani
kunitafuta ilihali akiwa ameiba vitu vyangu.
“Mungu wangu nisamehe kwa kumuhisi vibaya huyu kaka” nilisema kimoyomoyo
huku nafsi yangu ikiwa na furaha.
Jambo moja ambalo sikuwahi kujiuliza muda ule ni vipi mtu yule alinifahamu
mimi kuwa nilikuwa Geita na pia kujisema kuwa alikuwa na mimi pamoja huko
Geita, lakini kubwa kuliko yote ni vipi alipajua nyumbani kwangu ninapoishi.
Nikiwa bado ni mwenye faraja moyoni, mama mwenye nyumba alinipa kipande
cha karatasi kilichokuwa kimeandikwa namba ya simu.
Kwa mara nyingine nilishukuru mno, niliingia ndani mwangu na kuwasha taa
kisha nikaketi kitandani, kabla ya kufanya lolote nilitoa kadi yangu ya posta na
kutoka nje kutafuta vibanda vya simu.
Sikupata tabu kupata kibanda cha simu,.niliandika zile namba kisha nikazipiga
Simu ilita upande wa pili kwa muda kidogo kisha ikapokelewa na sauti nzito yenye
mkwaruzo.
“Halow”
“Habari yako kaka” nilisalimia
“Sijambo. Ooh Zahara, hujambo bibie” alijibu yule mtu, nilistuka kidogo, vipi
huyu mtu anijue namna hii amejua vipi jina langu?
“Safi tu, nafikiri ni wewe uliyekuja kunitafuta nyumbani kwangu?”
11
“Bila shaka”
“Na bila shaka ni wewe uliyeondoka na jaketi langu kule Dodoma?”
“Haswaaa” alijibu tena yule mtu, nilishusha pumzi ndefu nikahisi furaha
ikiongezeka moyoni kwa kulipata jaketi langu lililokuwa na vitu muhimu. Sikujali
wala sikuwa na habari tena na namna yule mtu alivyotumia utaratibu wa
kulichukua lile jaketi kule katika mgahawa, kilichokuwa katika akili yangu wakati
huo ni kuhakikisha naipata ile nguo yangu hususani vitu vilivyokuwa ndani ya lile
jaketi
“Sasa nalipata vipi hilo jaketi?” niliuliza.
“Njoo mtaa wa Aggrey, Kariakoo”
“Sasa hivi?” niliuliza kwa mshangao huku nikitizama saa na kuona ilikuwa yapata
saa saba na nusu usiku.
“Ndio lazima iwe sasa hivi vinginevyo unaweza kulikosa, mie kesho asubuhi
naondoka na basi la Chakito kuelekea Mlalo huko Lushoto.
Nilisimama wima nikapatwa na taharuki ya kulikosa jaketi, japo sikuwa tayari
kabisa kulikosa tena lile jaketi.
Niliagana na yule mtu na kumuhakikishia kuwa nitakuwa mtaa ule wa Aggrey
muda mchache ujao.
Nilikurupuka na kutoka mule ndani bila hata kumwaga mama mwenye nyumba
usiku ule na kutokomea mtaani.
Nilipanda daladala inayoenda mjini kwa miaka hiyo yalikuwa ni yale mabasi ya
kizamani kabisa yenye kuitwa “Chai Maharage” lililonipeleka hadi mtaa wa
Aggrey, Kariakoo.
Hapo nilisimama mbele ya stendi ya mabasi ya Tabata na Buguruni kisha nikaingia
katika kibanda cha kupiga simu na nikampigia simu tena yule mtu.
“Shuka mbele kidogo huku, kama unakuja Mnazi Mmoja, tizama upande wa
kushoto utaona mashine ya kutolea pesa ya NMB kisha ingia katika ghorofa
inayofuatia, panda juu hadi ghorofa ya nne, utanikuta katika korido ya milango ya
lifti nakungoja..”
Baada ya kupewa maelekezo hayo nilizipiga hatua kuelekea eneo lile
nililoelekezwa, bahati ni kuwa hapakuwa mbali.
12
Dakika chache nyingine nilikuwa katika lifti ya jengo lile ambalo sikujua ni jengo
linalojishughulisha na nini, kilichonistajabisha ni kuwa hapakuwa na mlinzi katika
jengo lile.
Lakini hata hivyo sikujali sana kwani kilichonipeleka pale ni vitu vyangu vya
ofisini na si vinginevyo.
Sekunde kumi nyingine milango ya lifti ilifunguka, tayari nilikuwa ghorofa ya nne,
Nilitoka ndani ya ile lifti.
Hapo nikakutana na yule mtu mwenye kupenda kunitizama. Aliponiona aliachia
tabasamu ambalo nililiona kule Dodoma, lile tabasamu liliongea kitu, nafikiri
lilisema “nimekutana na mwanamke mrembo”.
“Karibu Zahara” alinikarimu huku akinipa mkono tabasamu lake likizidi kustawi
usoni mwake.
“Nashukuru sana”.
Nilijibu huku na mimi nikimpa zawadi ya tabasamu, akanionyesha ishara nimfuate,
wakati naongozana nae, macho yangu yalikuwa yakisaili ile nyumba ilikuwa ni
kama hoteli ya kisasa kwani kila tulipopita katika korido, niliona vyumba
vilivyoandikwa namba mithili ya vyumba vya hoteli ya kisasa, sikuwa na uhakika
sana na hisia zangu kuwa huenda ile nyumba ikawa hoteli kwani nilivyoingia
katika ile nyumba sikuona mapokezi wala sikukutana na mtu yeyote mbali na yule
mbaba mwenyeji wangu.
Safari yetu ilishia mbele ya mlango mmoja ulioandikwa Room No 104. Alisukuma
mlango wa chumba kile na kujitoma ndani.
“Karibu Zahara, pita ndani”
“Asante”, niliingia ndani ya chumba kile, kilikuwa ni chumba nadhifu ndani
kukiwa na kila kitu cha thamani kinachotakiwa kuwapo chumbani.
Niliketi katika kochi huku macho yangu yakizidi kusaili mule ndani,.sikuwa na
wasiwasi na lolote.
Kitu kimoja ambacho sikuwahi kukijua wasaa ule ni kuwa uwepo wangu eneo lile
ungeweza kunisababishia madhila makubwa mno ambayo nisingeweza kuyasahau
kwa milongo mingi juu ya mgongo wa ardhi.
13
Yule mtu alisogea katika kabati la nguo na kufungua, kisha alitoa jaketi langu na
kunikabidhi, nilifurahi, muda huo huo nilianza kulipekua ili kuona kama vifaa
vyangu vipo salama.
Naam vitu vyangu vyote vilikuwa salama, nilishusha pumzi ndefu na kuhisi furaha
nyingi moyoni.
“Asante sana kaka yangu, sina cha kukulipa kwa kweli, ila nashukuru mno kwa
wema wako vitu hivi ni muhimu mno”
Yule mtu alitabasamu, lakini hakufumbua mdomo, alitizama pembeni bila kujibu
shukrani zangu kwa sekunde sita au saba kisha akasema,
“Usijali Zahara ilikuwa ni lazima hili litokee ili upate kunifahamu”
“Ndiyo, ni kweli, hakika Mungu ndio mpangaji wa kila kitu ulimwenguni”
“No, no,no hili halihusiani na mipango ya Mungu Zahara, huu ni mpango wa sisi
wanadamu”
“What!!”
Niliuliza kwa mshangao, maneno ya yule mtu yalinichanganya.
Yule mtu alinisogelea pale sofani na kuketi mkabala na mimi.
“Huu ni mpango wangu mahsusi” alisema tena kwa utulivu huku akinitumbulia
macho yake makali pasina kupepesa kando.
Nilifikiri kwa muda, nikaona kwa dakika nyingine tena nashindwa kabisa
kumuelewa yule mtu yale maneno yake.
“Any way, acha niseme tu nashukuru na sasa wacha mie niondoke maana usiku
ushakuwa mkubwa”
Hatimaye niliona ni kheri niage na kuondoka maana sikuwa na sababu nyingine ya
kuumiza kichwa kwa maneno ya yule mtu ambayo nilihisi alitamka pasina kufikiri,
aidha hisia zingine zikaniambia pengine alikuwa amekunywa pombe kidogo na
kuvuruga kidogo ubongo wake.
Nilisimama na kuzipiga hatua kuelekea mlangoni,
“Sawa kila kheri mrembo” yule mtu alisema.
Sikumjibu zaidi ya kuachia tabasamu lililosema,
14
“Tuko pamoja”
Nilipita katika ile korido na kukata kulia kuelekea katika lifti. Pale katika korido ya
lifti nilikuta lifti zote tatu zikiwa zinatumika, hivyo nilisisima na kusubiri kwa
muda kidogo.
Dakika moja badae mlango wa lifti moja katika zile tatu ukafunguka, bila
kuchelewa nikajitoma ndani.
Nilibonyeza kitufe kilicho andikwa G1, lifti ilishuka chini na sekunde tano tayari
taa ya kijani ikaonyesha nimeshafika G1, nilitoka ndani ya lifti ile nikiamini sasa
naweza kutoka nje ya jengo lile na hatimae kurejea nyumbani usiku ule.
Ajabu ni kuwa, pale lifti ilipo simama na mimi kutoka nje, nilikutana na mazingira
mageni machoni mwangu. Halikuwa eneo la nje ila nilipochunguza vizuri
niligundua nilikuwa ghorofa ya kwanza, hapo nikagundua nilifanya makosa wakati
nilipokuwa mule ndani ya lifti ile, sikutakiwa kubonyeza ‘G1’ badala yake
nilitakiwa kubonyeza ‘G’ pekee, hiyo ingenipeleka hadi chini kabisa ya ghorofa
lile.
Lakini hata hivyo sikuona tabu kwani chini hapakuwa mbali ni kiasi cha kushuka
ngazi kama nne na kuweza kuwa nje ya jengo lile.
Nilizifuata ngazi na kuanza kushuka chini. Eneo lile lilikuwa kimya, kulikuwa na
taa za bulbu kubwa zilizotoa mwanga hafifu wa rangi ya njano, nilishuka ngazi ya
kwanza na sasa nikashika ngazi ya pili. Chini ya ile ngazi ya pili, nilipata kuona
kitu.
Eneo lilikuwa kimya kama nilivyopata kusema. Mwendo wangu wa kasi wa
kushuka ngazi ukabadilika na sasa nilishuka taratibu nikitupia macho kitu
nilichoweza kuona, na hapo nika jua alikuwa ni mtu.
Alikuwa amejikunyata pembezoni mwa zile ngazi, alikuwa amejifunika shuka
nzito la rangi nyekundu mwili wote kasoro kichwani.
Jambo moja lilipita kichwani mwangu, kwa vyovyote vile yule mtu atakuwa ni
mlinzi, wazo hilo lilizidi kustawi katika akili yangu baada ya kutizama saa na
kuona ilikuwa yapata saa nane kasoro dakika kumi za usiku, “hawezi kuwa mtu wa
kawaida eneo hili, tena muda huu pasina kuwa ni mlinzi”.
15
Hatua zangu zikiwa za kawaida kabisa nilifika eneo lile ambapo mtu yule alikuwa
amejikunyata, nilimpita pasina kumsemesha lolote na kukuta kushoto kwa ajili ya
kuanza kushuka ngazi zinazo fuatia.
Ila ghafla.
Sauti ilitoka kwa yule mtu ilinifanya nitishike vibaya mno,yule mtu alisema,
“Usiku mwema Zahara”
Niligeuza shingo na kutupa macho yangu na kumwangalia yule mtu, hapo
nikakutana na kitu ambacho kilinifanya hali ya mshangao, niliduwaa, macho
yamenitoka, midomo imefumbuka kama lango la daladala aina ya UDA la
Mbagala, nikaanza kutokwa na jasho, kitu kisicho cha kawaida nikaona
kinanyemelea maisha yangu.
Alikuwa ni yule mtu aliyekuwa na jaketi langu lililokuwa na vitu muhimu vya
ofisi.
Nilijikuta nataka kutimua mbio ila miguu ilikuwa mizito nikabaki nimeganda
namtizama yule baba.
“Hivi Zahara pamoja na kusaidia kibarua chako hujataka kunifahamu hata jina
langu bibie?” Yule mtu aliuliza huku akisimama kwa tabu eneo lile.
“We umefikajefikaje hapa?” badala ya kujibu nilijikuta namtupia swali huku
nikiendelea kumshangaa na sasa haukuwa mshangao tu bali ulikuwa ni hofu kubwa
iliyochanganyikana na mshangao.
Yule mtu alisimama wima akiwa bado amejifunika lile shuka jekundu, miguuni
akiwa peku.
“Katika maisha yangu ya kichawi sijawahi kuona mwanamke msomi lakini wakati
huo huo ni zumbukuku wa mwisho kama wewe!” Yule mtu alisema, kauli ile
ilinifanya mwili wote uingiwe na baridi na kuwa kama mithili ya mtu
aliyemwagiwa maji ya baridi.
Pumzi zilinitoka kwa kasi sasa nikaona kumbe nimekutana na kiumbe kisicho cha
kawaida, sikutaka zaidi kuyatafakari maneno mengine ya yule mtu, neno
“mchawi” lilitosha kabisa akili yangu kuiamrisha miguu yangu ikimbie kwa kasi
eneo lile.
16
Nilitoka mbio nikiwa nimekumbatia jaketi langu kifuani nikitoa yowe dogo la
msaada, nilizishuka ngazi upesi upesi upesi huku nikiyumba hovyo.
Nikamaliza zile ngazi sasa nikashika ngazi za mwisho na kuwa chini ya jengo lile,
wakati nashuka ngazi ya kwanza, ngazi ya pili ile nashuka ngazi ya tatu tu.
Nilijikuta nikifunga breki ghafla na kubaki nimesimama huku nikiweweseka.
Yule mtu alijitokeza kutokea kona ya mwisho ya ile ngazi, alitembea kikakamavu
kunisogelea huku mwendo wake ukifanana kabisa na viumbe aina ya Saibogi,
alikuwa akinijia kwa mwendo wa kunyata lakini akijiamini, macho yake yakiwa
makali, huku sura yake kwa ujumla akiifinya na kufanya awe na mwenekano wa
kutisha, alichanua vidole vya mikono yake na kutanua mikono yake huku akitoa
ngurumo ndogo mithili ya mtu aliyepandisha mashetani na akawa ananisogelea.
Kwa kweli niliogopa mno.
Kwa muda wa sekunde zisizozidi tatu, nilibaki nimebung’aa nikishangaa yale
mambo yaliyo kuwa yanajiri mbele yangu katika jumba lile kabla ya kujikuta
nikipiga kelele kwa nguvu.
“Mamaaaa, mamamaaa nakufaaaa uwiiiiii nisaidieniii” nilipiga kelele nyingi huku
nikitoka mbio kupandisha ngazi kurudi juu.
Nilikuwa nahema kwa kasi, nikizidi kupiga kelele huku nikijitahidi kuzipanda
ngazi za jengo lile kujitenga na yule mtu wa ajabu, mashaka makubwa yalikuwa
kifuani kwangu.
Sikumbuki vizuri nilipanda ngazi hadi ghorofa ya ngapi, ila ninachokumbuka ni
kuwa ilifikia hatua mapafu yangu yalichoka, nilichoka kupiga mayowe kwa nguvu
huku nikizipanda ngazi tena nikiwa nakimbia.
Niliangaza nyuma yangu na kuona niko peke yangu, hapakuwa na mtu yeyote aliye
kuwa akinifuata lakini pia hakujitokeza mtu kunisaidia, pamoja na kwamba
nilikuwa nikipiga makelele ya hali ya juu, lakini hata hivyo sikumwona tena yule
mtu wa ajabu.
Sasa nikiwa najisukuma kwa mbele kwa mwendo wa kutembea nikiendelea
kuzipanda zile ngazi, nilikuwa nahema kwa kasi, machozi na kamasi vilikuwa
vikinitoka kwa pamoja, woga wa kuingia katika mikono ya mchawi ulikuwa
mkubwa.
17
“Mungu wangu wa mbinguni uko wapi sasa muda huu! Huoni ninavyoingia katika
madhila haya? Sasa unangoja nini kunisaidia yarabii” nilijikuta nikitamka yale
maneno huku nikiwa nimepagawa katika kiwango cha mwisho.
Nilizidi kuzipanda ngazi bila kuona dalili yoyote ya kufatwa ama uwepo wa mtu
katika jengo lile, eneo lote lilikuwa kimya, ilikuwa ni sauti ya vishindo vya hatua
zangu kupanda zile ngazi ndio zilizosikika. Yaani ilikuwa ni kama kwamba kile
kilichotokea muda mchache kilikuwa hakijatokea.
Ni hapo nilipo ingiwa na fikra hizi, kuwa huenda ndani ya ghorofa hili kulikuwa na
mtu mmoja tu yanii yule mtu mchawi.