SEHEMU YA KUMI NA MOJA:
Nilikuja kuamka siku tano mbele baada ya kuutambua mwili wa Lameck. Mazishi ilibidi yafanyike bila ya uwepo wangu wala wa mama angu mpenzi. Baba ,mume wangu, ndugu wengine jamaa na marafiki walishirikiana kumuhifadhi mwanangu mpenzi. Mamangu mkwe na mawifi zangu nao walikuja msibani, cha ajabu ma mkwe hakushughulika chochote, ni kama alikuja kutusanifu kua mnaendelea na vita au mtatii masharti.
Baada ya kupata nguvu ilibidi tusafiri kama familia kwenda mkoani Iringa ambako ndio chimbuko la asili ya mume wangu. Mume wangu ni mkinga , kwahiyo kwa mila za kwao yeye akiwa kama mkubwa alitakiwa kuendeleza matambiko yote kwa usalama wa familia yao. Dominic alikua akijitahidi kufanya kila anachoambiwa, ambacho kilimshinda ni kafara za kutoa uhai wa binadamu na ndio maana akaamua kua atatoa dume la ng'ombe mweusi kila inapofika siku ya kuzaliwa ya mwanafamilia wake, huo mwaka ambao ulitokea ajali ya mtoto, hakumudu kufanya na ndio mama mkwe alipopata nafasi ya kutupa kombora lake.
Dommy alinieleza hayo siku mbili kabla hatujasafiri kua inabidi tukawekewe kinga maalumu maana mambo yanamzidi nguvu, na kua anaelekea kushindwa. Akanambia sitakiwi kumwambia yeyote hasa mama angu mzazi maana mama haamini katika mizimu, na kua sio kama haamini kua Mungu yupo lakini vita tuliyonayo ni kubwa mnooo, lazima apambane kila Kona, akaapiza kutulinda hata kama atatakiwa kutoa uhai wake sisi tuishi.
Tukiwa njiani, nilipokea simu kupitia namba ngeni, kupokea sauti ilikua ya mama mkwe wangu, akanambia nawatakia safari njema...umemchukua mwanangu nami mechukua wako, utakua umeelewa sasa inavyouma kubebewa mtoto...Nilibaki na mshangao wa mwaka, kumbe tupo vitani eeeh ?mume wangu akaniuliza unaongea na nani? Sikutaka kumficha nikamwambia kua mama mkwe amepiga simu anatutakia safari njema . Tulikua nanenane , kilomita chache kabla hujafika Morogoro mjini, Dominic akashauri hatuwezi kuendelea na safari maana kauli ya mamake anajua ni kebehi, hatutofika tunapoenda, nilikua kwenye gari, mimi, Dommy na mwanangu wa pili Mathew.
Safari ikabidi iishie Morogoro mjini baada ya kukoswakoswa na fuso lililokua linatokea njia ya dodoma wakati tunakunja tuingie barabara hiyo , ni kama akili ilisimama ghafla, nilisali Sala zote ninazozifahamu na ambazo sizifahamu, sikuwahi jua kua nafahamu kunena kwa lugha, ile siku nilinena. Dominic alipambana kukwepesha gari tukajikuta tumeenda kugonga nguzo ya umeme.Nadhani siku zetu zilikua bado hazijafika maana hadi tunatoka ndani ya ile gari hakuna alieamini kua tumenusurika.
Dominic akafanikiwa kunituliza na kukusanya vitu vyetu muhimu, wakaja trafiki wakapima na gari ikachukuliwa kupelekwa sehemu husika, sisi ikabidi tutafute hotel kupumzika, ndipo nilipopata wasaa wa kumpigia mama mkwe na kumuuliza kwa nini yote haya mama...sisi ni wanao...kwa Nini unatuumiza? Kwanini umeniondolea Lameck wangu? Kwanini umekatili maisha ya vijana wadogo 40, dereva na mwalimu wao. Kwanini mama, kwanini?
Akanijibu jibu rahisi sana, nirudishie mwanangu nami nitakuachia huyo kifaranga wako aliebaki...akakata simu. Dominic alikua anaongea na simu nje , aliporudi akanambia tunaondoka jioni na lory, ila tutapitia njia ya dodoma hadi tutokee Iringa nimeambiwa nikipitia njia ya Mikumi hatutofika....jiandaeni
Nilimpigia simu mamangu kipenzi na kumwambia kua aingie kwenye maombi , kuanzia huo mda hadi tutakapofika iringa kijijini Lupembe. Mama akaniuliza upo safarini? Kumbuka dommy alinambia nisimuage yoyote hata dada wa kazi tulimpa likizo kabla hatujasafiri maana hatukutaka ajue tunapoelekea, nikamwambia mama sina muda wa kukuelezea lakini nakuhitaji kuliko wakati wowote ule.
Safari ilianza jioni yake kwa kupitia njia ya Dodoma ,tulivikata vijiji na vitongoji kwa shida maana mwendo wa lori yataka moyo...tulifika kibaigwa usiku wa saa saba, Lori lilikua linaingia vijijini mbali na hapo, ikabidi safari yetu iishie pale. Dereva wa lori alitushusha karibia na gesti iliyokua njiani , uchovu, baridi, njaa na maumivu ya msiba bado havikutuacha salama.
Ilikua ni mara ya kwanza kulala katika chumba chenye hali duni namna ile, sio kama hatukua na pesa ya kutafuta hotel, ila matatizo yasikie kwa mwenzio, hata hamu ya kutafuta sehemu nzuri ya kulala haikuwepo, tulichokua tunaomba ni pakuche tusonge mbele. Niliamua kuingia vitani rasmi na mama mkwe wangu maana niliona ukimya wangu unazidi kuniumiza. Acha iwe anavyotaka iwe, ila nitapambana kumlinda mwanangu kwa gharama yoyote ile, ikibidi kutoa uhai wangu ili Mathew aishi nilikua radhi.
Hatimaye palikucha, watoto ni malaika jamani, na madhira yote yale mwanangu anakoroma kama chura, nilijikuta nacheka tuuuu, dommy akashtuka na kuniuliza hujalala ma Lameck, bado ananiita ma Lameck , sijui kama jina litakuja kusahaulika walahi, nikamwambia sijalala nawalinda, akaniangalia kwa upendo akanambia ahsante kwa kua mke wangu...Nakupenda we mwanamke, ahsante kwa kua jasiri...
Kulikucha na safari ikaendelea ,tulifika Dodoma mjini mapema tu, maana tulidamka saa kumi na moja na kupata private car iliyotusogeza hadi mjini. Tulifanikiwa kupata usafiri baada ya kupata kifungua kinywa na safari ikaanza mapema tu kuelekea Iringa. Mungu alikua upande wetu kwani licha ya mvua kubwa iliyokua inanyesha tulifanikiwa kuingia salama kijijini Lupembe usiku wa hiyo siku...kijijini ni kijijini tuuu, huduma mbovu , barabara mbovu, chakula cha utofauti, lakini nilipata amani mara mia ya ninayoipata ninapokua dar, kua mbali na mama mkwe wangu ilikua inanipa amani sana.
Tulifanyiwa tiba mbalimbali pamoja na kupewa kinga , baada ya siku saba za kulala kaburini kwa marehemu baba mkwe ,kutambika na kusoma dua tuliruhusiwa kurudi dar...safari hii tukitumia njia ya kawaida ya iringa kupitia Mikumi hadi Morogoro ,tuliingia salama salimini dar, jioni ya siku ya safari, mume wangu alishafanya utaratibu kupitia connections zake gari ikarekebishwa, na kurudishwa dar.
Maisha baada ya hapo yalikua mazuri na kutufanya kusahau madhira ya mama mkwe kwa mda....miaka kadhaa ikapita, mama mkwe akatupigia simu kuomba kikao cha familia. Mume wangu alirudi akanipa taarifa hiyo na kuniambia moyo wake mzito ,lakini mwisho wa siku yule anabaki kua mama ake, kama ametambua kosa lake yeye binafsi anamshukuru Mungu kwa huo muujiza. Nilichagua kua Thomaso katika hili, kuwaamini watu kumeniletea maumivu sana, nikampigia babu wa Lupembe na kumueleza kila kitu, babu akanisikiliza akanambia siku ya kikao niwasiliane nae.
Hatimaye siku ya kikao ikafika, tukatoka Mimi na mume wangu, mtoto wangu nikampeleka kwa mama, bado sikua na imani nao. Nikampigia babu akanambia chukua chumvi ya mawe changanya na karafuu vifunge kwenye mfuko wa nailoni, weka kwenye mkoba wako...na pia ukifika getini kwa mama mkwe wako kabla hujaingia tazama magharibi mara nne, nuia maneno yafutayo kila unavyotazama magharibi...' Wakuu naomba mtulinde' Wakuu naomba mtulinde' ....Mungu awatangulie.
Tulifika kikaoni, nikamuomba mume wangu atangulie mimi naongea na simu na mama nakuja, alipoingia tu ndani nikaanza kufanya kama nilivyoelekezwa...Kisha nikaingia ndani nikasamilia na kukaa kusubiria kikao..Mama mkwe alitoka baada ya kama nusu saaa hivi, mda wote tulikua na wifi zangu , walifurahi kutuona na unaona kabisa yanayoendelea hawapendezwi nayo lakini hawana namna, mama mkwe alikuja akatusalimia kwa kutukumbatia, alipofikia kwangu akanambia najua ulichofanya.
Asikwambie mtu sikuelewa kilichoendelea pale kwenye kikao, nachokumbuka ni wifi angu alinishika akanambia wifi kunywa juice inazidi kupoa , ndipo nilipogundua kua kumbe nimewekewa juice...sikumudu kunywa nikawaambia kua sijisikii vizuri ,tumbo linanisumbua. Ma mkwe akanambia kunywa Grace ningetaka kukuua hata hapa usingefika, Sina shida na wewe....nataka damu yangu tuuuu.
Tumbo la uzazi liliunguruma, nikajikaza nikanywa juice, mme wangu akamwambia mama hayo sio maneno ya kumwambia mkweo, tumeshayapita hayo...kikao kiliisha ,tukaaga na kuondoka salama. Mume wangu akawa anaenda kwao mara kwa mara na mtoto Mimi sikuwahi kanyaga tena. Wifi zangu wakaanza kuja kwangu, kawifi kangu ka mwisho kakaomba kuja kuishi na sisi, sikuona shida tukamkaribisha .