Simon Sirro ni mfano wa bahati mbaya ya Polisi

bittersweet

Member
Jan 16, 2017
22
17
Hakika huyu mwandishi wa habari aliona mbali.

WIKI iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alipata ujasiri wa kuhoji hadharani uadilifu wa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro.

Kwa ambao tunamfahamu Kamanda Sirro, kauli ile ya Makonda, kwamba pengine wafanyabiashara wa shisha wamemhonga na ndiyo maana hapambani nao kwa nguvu, ilitushtua.

Kwa maoni yangu, wakati utakapofika wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, kustaafu wadhifa wake huo, kuna askari wachache sana wana sifa za kuchukua wadhifa huo kuliko Sirro.

Nimeandika hivyo si kwa kubabaisha. Mwezi mmoja kabla ya Mangu kuteuliwa kuwa IGP, niliandika kwenye gazeti hili kwamba yeye ana nafasi kubwa. Na akapata nafasi.

Hivyo ninaposema kwamba Sirro ana sifa zote za kuwa IGP; tena akiwa na uwezo mkubwa kuliko hata baadhi ya watangulizi wake, ninazungumza kama mtu mwenye uelewa wa jeshi hilo.

Ndiyo maana, kauli ile ya Makonda ilinitatiza kidogo. Maneno yale dhidi ya Sirro, tena mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, yalikuwa na lengo lipi?

Je, Makonda ana mtu wake anayemtaka awe IGP baada ya Sirro na kwa sababu hiyo ametumia fursa ile kutumia silaha ya kisaikolojia inayompa faida “mtu wake” na kummaliza kabisa Sirro?

Maana kuna wanaoamini kwenye msemo kuwa mke wa Kaisari hatakiwi hata kutuhumiwa. Kwa kumtuhumu kwake tu; hata kama baadaye itakuja kubainika kuwa zilikuwa tuhuma tu, tayari sifa za Sirro zitakuwa zimeingia doa.

Au pengine Makonda hamtaki Sirro hapa Dar es Salaam na akaamua kutumia mkutano ule kueleza hisia zake hizo?

Miezi michache iliyopita, Makonda alizungumza mbele ya Rais John Magufuli, wakati wa uzinduzi wa Daraja la Kigamboni, kwamba alikuwa hamtaki aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji, Wilson Kabwe (Mungu amrehemu).

Labda Makonda alishindwa kumwambia Majaliwa amwondoe Sirro kwa sababu Waziri Mkuu hana uwezo huo. Lakini, kama alitaka kutuma ujumbe mahali, ujumbe ule utakuwa umefika.

Swali kubwa ambalo nimekuwa nikijiuliza tangu wiki iliyopita ni kwamba; kwanini Makonda alifanya alivyofanya? Kama hamtaki Sirro Dar au kwenye nafasi za juu kabisa, kwanini?

Lakini nilijiuliza pia swali la pili. Je, Makonda ambaye baba yake alikuwa askari, angeweza kutamka tuhuma zake zile dhidi ya Sirro kama mhusika angekuwa mwanajeshi?

Kwamba labda tuseme Kanda ya Dar es Salaam ingekuwa inaongozwa na mwanajeshi mwenye cheo cha walau Brigedia Jenerali, je Makonda angethubutu kutuhumu?

Askari Polisi wana bahati mbaya. Kwa sababu ya kufanya kazi zao katika namna inayowakutanisha zaidi na raia, wao wamekuwa watu wa kuangushiwa tuhuma lukuki.

Kwa sababu tunakutana nao barabarani, tunasema trafiki ni wala rushwa. Kwa sababu wanasaidia ulinzi viwanjani, tunasema askari ni wala rushwa.

Kwa sababu tukifanya makosa tunapelekwa katika selo za Polisi, tunasema Polisi ni wala rushwa. Bahati nzuri kwa wanajeshi ni kwamba wenyewe wamelindwa kwa mujibu wa taratibu zao za kazi.

Nina uhakika kuwa kama wanajeshi ndiyo wangekuwa wanafanya kazi za Polisi, leo hii pengine wanajeshi ndiyo wangekuwa wanachukiwa zaidi. Lakini wanapendwa kwa sababu hawana mwingiliano na shughuli za kila siku za kiraia.

Polisi si wanajeshi. Ndiyo maana, katika historia ya dunia, hujawahi kusikia Polisi wamepindua nchi. Wanaopindua nchi ni wanajeshi. Yawezekana ukweli huu umewafanya waonekana kama “Majoka ya Kibisa”

Msomi mmoja alipata kutamka huko nyuma kuwa tofauti kubwa kati ya askari na raia ni kwamba Polisi anaruhusiwa kushika silaha. Vinginevyo wote wako sawa.

Kwa sababu hii, askari wamekuwa kama gunia la mazoezi. Nimeona mara kadhaa wanasiasa wa upinzani wakiwakashifu askari.

Cha ajabu, mambo yote mazuri ambayo raia tunayafanya na kuona ya kawaida, yanafanyika kwa sababu ya uwepo wa askari.

Kuna nchi zinaitwa nchi zilizoshindikana, mfano ni Somalia na Afghanistan. Nchi zina matatizo kwa sababu wanaoshika bunduki ni raia na askari hawana kitu.

Matokeo yake ni kwamba watu wanaogopa kutembea barabarani kwa sababu wanaporwa. Watu hawatembei usiku na wengine hata kazini hawaendi. Wanajeshi wapo lakini Polisi hamna.

Nadhani Makonda ameona fursa hii kwa askari Polisi. Unaweza ukasema unachotaka na maisha yakaendelea kama kawaida.

Hata hivyo, kwa wale wote ambao wanadhani kwamba Polisi ndiyo gunia la mazoezi; wafahamu kwamba ipo siku katika maisha yao ambayo wataamka na kuheshimu kazi ya wenzao hao.

Kwa bahati nzuri, askari wamejaaliwa subra. Na vitabu vya dini vina sentensi nzuri sana kwa watu wa namna hiyo; “ Wamejaaliwa wale wenye subra”.


Chanzo: Raia Mwema
 
kuna watu walijaaliwa kuamka mapema hali wenzao wangali usingizini. huyu mwandishi kwa hakika aliusoma upepo mapema.
 
Back
Top Bottom