"Simba Wa Yuda" Azichapa Hadharani. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

"Simba Wa Yuda" Azichapa Hadharani.

Discussion in 'Sports' started by Junius, Aug 9, 2009.

 1. Junius

  Junius JF-Expert Member

  #1
  Aug 9, 2009
  Joined: Mar 11, 2009
  Messages: 3,183
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 133
  Amfuata mwanachama jukwaani

  na Wilbert Molandi  KATIBU Mkuu wa Simba, Mwina Kaduguda ‘Simba wa Yuda' , jana alishindwa kudhibiti hasira hadi kumchapa ngumi mwanachama mwenzake, Kessy Rajabu, baada ya kutokea tofauti baina yao kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
  Kisa hicho kilitokea ikiwa ni dakika kama tano tangu kuanza kwa mechi ya vijana wa chini ya miaka 20 wa Simba dhidi ya Lyon, iliyopigwa kwenye huo.
  Tukio hilo ambalo lilishuhudiwa na wengi hasa waliokuwa wamekaa kwenye jukwaa la Simba, litabaki kukumbukwa kila litakapofika tamasha hilo kila Agosti 8.
  Rajabu mwenye kadi namba 0027, alikumbana na ngumi ya Kaduguda baada ya kumtamkia maneno makali kwamba kwa aina ya uongozi wao wasubiri kutatoswa kwenye uchaguzi wa Desemba isipokuwa mwenyekiti wao Hassan Dalali.
  "Ninyi mwisho wenu ni Desemba, Simba haiwezi kuongozwa na viongozi kama ninyi (Kaduguda)… wote tutawang'oa isipokuwa Dalali," mwanachama huyo alisikika akimtamkia Kaduguda.
  Baada ya hapo, mwanachama huyo aliyejitambulisha kama mwangalizi wa gari ya Kocha Mkuu, Mzambia Patrick Phiri, alikwenda kuketi jukwaani.
  Hata hivyo, Kaduguda akionekana kukerwa na kauli za Rajab, alimwita na alipogoma, alimfuata na kumchapa ngumi.
  Baada ya mwanachama huyo kupigwa ngumi, naye akajibu mashambulizi kwa kurusha kibao, hivyo kuanza kushikana, lakini watu wakawaamulia na kuanza kurushiana maneno makali.
  Baada ya hapo, Kaduguda alishuka jukwaani na hakuonekana tena, ingawa kulikuwa na habari kuwa alikuwepo uwanjani hapo.
  Tanzania Daima ilipomtafuta Rajab kuelezea kisa hicho, alisema yeye amemwachia Mungu kama ambavyo alifanya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, alipopigwa kibao kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee.
  Rajab alisema kwa kitendo kile cha Diamond Jubilee, mhusika alishtakiwa na jamhuri na kuhukumiwa na mahakama, hivyo yeye amemsamehe Kaduguda, lakini anamshtakia kwa wanachama na hukumu yake ni Desemba.
  "Nimekuwa sipendezwi na staili ya uongozi wao…nilivyomuona nikamweleza mwisho wao ni Desemba, hivyo akachukia akanifuata na kunipiga ngumi, nimemsamehe na Rais Mstaafu Mwinyi… wanachama ndio watamhukumu Desemba," alisema Rajabu.
  Alipoulizwa haoni kama alikuwa mchokozi na utovu wa nidhamu kwa kiongozi wake, Rajab alisema haoni kosa kwani hata viongozi wenyewe wamekuwa wakizozana.
  Rajab alisema, viongozi wengi wa klabu yao, wamekuwa wakiendekeza malumbano, hivyo hawafai kurejea madarakani katika uchaguzi ujao na yeye Kaduguda angekiona cha moto Jumatano wakati wa kuteuliwa katibu mkuu wa kuajiriwa.
  Tanzania Daima ilipomtafuta Kaduguda kwa ufafanuzi zaidi, simu yake iliita muda mrefu pasipo kupokelewa.
  Kwa upande wa tamasha, lilifana kutokana na kuhudhuriwa na watu wengi wakiongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta.
  Sitta jana alikabidhi zawadi ya ngao kwa wanachama na wadau mbalimbali ambao wamekuwa msaada kwa klabu hiyo.
  Hao ni wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Kilimanjaro.
  Wengine ni kundi la Friends of Simba, Godfrey Nyange ‘Kaburu', Dioniz Malinzi, Prof Juma Kapuya ambaye ni Waziri wa Ulinzi na Kujenga Taifa na Sitta mwenyewe aliyekuwa mgeni rasmi.
  Aidha, Simba jana walitambulisha jezi zitakazokuwa zikitumiwa na timu hiyo ambapo ikiwa nje, itakuwa ikivaa jezi nyekundu na nyeupe nyumbani.
  Kwa upande wa mechi ya wakubwa yaani Simba na SC Villa ya Uganda, wenyeji walishinda bao 1-0, kwenye mechi iliyojaa kila aina ya ufundi na ushindani.
  Bao pekee lililoipa ushindi Simba, lilifungwa dakika ya nane na Hilaly Echesa.
  Echesa alifunga bao hilo baada ya kuuwahi mpira uliokuwa umetemwa na kipa wa Villa kutokana na shuti la Mussa Hassan Mgosi.
  Licha ya timu zote kushambuliana kwa nguvu na kuwepo kwa kosakosa nyingi kwa milango yote, hadi mapumziko, Simba walikuwa mbele.
  Katika kipindi cha pili, licha ya timu zote kufanya mabadiliko, hayakuweza kubadili matokeo. Akizungumzia kipigo hicho, Kocha wa Villa, Sule Katto, alisema vijana wake hawajaelewana vema kutokana na wengi kuwa wageni.
  SOURCE: TANZANIA DAIMA.
   
Loading...