Siku ya Choo Duniani: Je, wewe una choo bora?

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,799
Leo tarehe 19 Novemba 2019, ni Siku ya Choo Duniani

toilet.jpg

Siku ya Choo Duniani ilianzishwa mnamo mwaka 2001 na kufanywa kuwa siku rasmi na Umoja wa Mataifa mwaka 2013. Siku hii ilianzishwa ili kusaidia kupambana na changamoto za usafi wa mazingira na kufanikisha kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG), ikiwa lengo namba 6 linaahidi usafi wa mazingira kwa wote ifikapo 2030. Siku ya Choo Duniani inaadhimishwa Novemba 19 kila mwaka.

Usafi katika jamii ni muhimu kwa watu binafsi na familia. Usafi wa mazingira unamaanisha usafi wa umma - kutumia vyoo safi na salama, kuweka vyanzo vya maji safi na utupaji taka.

Kama taka za binadamu (kinyesi) hazitasimamiwa, zitachafua maji, chakula, na kusababisha maradhi na maafa yanayoepukika katika jamii. Kutumia vyoo huzuia vijidudu kuingia kwenye mazingira, na kulinda afya ya jamii nzima.

Afya sio sababu pekee ya kujenga na kutumia vyoo. Watu wanataka sana:

Faragha:
Choo kinaweza kuwa rahisi tu kama shimo lenye kina ardhini. Lakini hitaji la faragha hulazimu choo kuwa sehemu nzuri yenye mlango ambapo mtu anaweza kufanya shughuli zake husika kwa uhuru na amani.

Usalama: Choo kinapaswa kuwa mahali salama pa kutumia. Hakuna mtu anayetaka kutumia choo ikiwa kuna wasiwasi kuwa huenda kitaanguka. Na ikiwa choo kipo mbali na nyumba, au mahali palipojitenga sana, basi watumiaji wake wanaweza kutohisi usalama kukitumia.

Tulizo: Choo kinapaswa kuwa sehemu ambayo watu wanatafuta tulizo kwa kutimiza mahitaji ya msingi ya kibaiolojia aidha wakiwa wamekaa kwenye kiti au kuchuchumaa.

Usafi: Ikiwa choo ni kichafu na chenye harufu mbaya, hakuna yeyoye ambaye atataka kukitumia au kukitumia kwa raha. Choo lazima kiwe safi kuzuia kuenea kwa vijidudu. Kazi ya kusafisha ni kuhakikisha kuwa vyoo vinatumiwa vizuri na kutunzwa.

Heshima: choo kilichohifadhiwa vizuri huleta hadhi na heshima kwa mmiliki wake. Hii inaweza kuwa hamasa kwa watu kutumia pesa na juhudi za kujenga vyoo bora.

Hata hivyo, pamoja na juhudi kubwa zinazoendelea kufanyika ulimwenguni kote ili kutatua changamoto ya vyoo, inakadiriwa watu zaidi ya milioni 600 duniani kote bado wanajisaidia maeneo ya wazi (kwa ukosefu wa vyoo).

Ni lazima kusaidia jamii kupata vyoo salama na kuhakikisha yeyote haachwi nyuma. Kwakuwa haijalishi wewe ni nani na upo wapi, usafi wa mazingira ni haki yako ya msingi ya kibinadamu.

Je, wewe una choo bora unachojihisi fahari kuwa nacho?
Unakithamini vipi choo chako?
Unachukuwa hatua gani kuelimisha wengine kuhusu umuhimu wa vyoo bora?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom