Siku ya asteroidi - juni 30

njiwaji

JF-Expert Member
Jul 15, 2015
279
202
SIKU YA ASTEROIDI



Siku ya asteroidi inaadhimishwa kila mwaka tarehe 30 Juni. Siku hii ya kimataifa ilanzishwa mwaka 2014 na wataalamu na wanaharakati wa astronomia na kuidhinishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2016. Shabaha yake ni “kuongeza ufahamu kuhusu asteroidi na hatari ya kugongwa kwa Dunia”

AsteroidI KUBWA IKIGONGA DUNIA.jpg

Karibu karne moja iliyopita, siku ya tarehe 30 Juni 1908, tukio la ajabu lilitokea katika sehemu ya Siberia, Urusi. Katika eneo kubwa karibu na mto Tuguska watu walisika mlio mkubwa kama mfululizo wa milipuko au mapigo ya mabomu. Katika eneo kubwa la kilomita za mraba 2,000 miti yote ililazwa (kwa kulinganisha, ukubwa wa eneo lililoharibiwa ni kubwa kuliko mkoa wa Dar es Salaam au Kisiwa cha Unguja). Milango na madirisha ya nyumba zilivunjika katika kijiji cha Vanavara kilichokuwa umbali wa kilomita 65 kutoka eneo la mlipuko. Kwa umbali wa kilomita 500 abiria katika treni waliona mwako wa nuru na kutingishwa na mtetemeko. Hakuna uhakika ni watu wangapi waliopata madhara kwa sababu wakati ule watu pekee waliokuwa wakishi katika sehemu zilizoharibika walikuwa ni wawindaji wa kabila la Waevenki. Wataalamu waligundua baadaye kwamba tukio hili lilisababishwa na kuanguka kwa gimba kubwa kutoka anga la nje lililogonga angahewa ya Dunia na kupasuka hewani juu ya Tunguska. Gimba hili lilikuwa asteroidi yenye kipenyo cha mita 50 hivi.


Asteroidi ni vipande vikubwa vya miamba vinavyozunguka Jua letu sawa na sayari, katika eneo kati ya mizingo ya Mirihi na Mshtarii. Kama vipande hivi ni vidogo (chini ya mita chache) vinaitwa vimondo. Asteroidi huwa na ukubwa wa mita kadhaa hadi mamia ya kilomita. Hadi sasa, wataalamu wamegundua malaki ya asteroidi katika Mfumo wa Jua lakini idadi yake inakadirikwa kufika mamilioni. Nyingi kati ya hizo zinazunguka Jua kwa mizingo thabiti lakini nyingine zinaweza kukaribia sayari na kuvutwa na graviti na kutoka katika mizingo yao na kuzileta jirani na Dunia hadi kuweza kugongana.


Miaka minne iliyopita, dunia ilishuhudia anguko la kimondo kikubwa cha mita 20 hivi juu ya mji wa Chelyabinsk huko Urusi tarehe 15 Februari, 2013. Kimondo kilipasuka juu ya mji huo na kusababisha mshtuko uliovunja vioo vya madirisha na kuharibu majengo kiasi 7,200 na kujeruhi watu 1,500.


Kama asteroidi au vimondo vinaingia katika angahewa ya Dunia vinasuguana na hewa yenyewe na kupashwa joto kali na kulipuka juu ya ardhi jinsi ilivyotokea pale Urusi mwaka 1908 na mwaka 2013. Kama asteroidi ni kubwa sana au kama ina metali nyingi ndani yake inaweza kufika hadi uso wa ardhi na kugonga pale. Mfano ni Kimondo cha Mbozi chenye tani 16 za chuma tupu kilichoanguka labda miaka 1000 iliyopita. Katika nchi nyingi kuna mabaki ya kasoko (mashimo makubwa) yaliyosababishwa na anguko la asteroidi miaka milioni iliyopita. Yanaonekana kama pete ya vilima vinavyozunguka eneo tambarare. Umbo hili ni sawa na ule tunaouona kama matone ya mvua yanaanguka juu ya mchanga laini au majivu.


Mbozi KIMONDO.jpg


Kugongwa kwa Dunia na asteroidi kubwa kunaweza kuleta hatari nyingi. Athari yake ni tofauti kama inaanǵuka kwenye nchi kavu au kwenye bahari. Miaka milioni 65 iliyopita asteroidi kubwa yenye kipenyo cha kilomita 10 iligonga pwani la Meksiko. Mshtuko huu ulisababisha mawimbi ya tsunami, mitetemeko mikali ya ardhi na kutokea kwa volkeno katika nchi za mbali. Vumbi nyingi ilirushwa hewani na kusababisha giza Duniani kote. Inaaminiwa kwamba wakati ule, spishi nyingi za viumbehai zilitoweka, pamoja na dinosauri, kutokana na mabadiliko makali ya tabianchi iliyoletwa na mgongano huu.


Dunia inagongwa na violwa vidogo vingi kila siku. Vikikaribia Dunia yetu vya kutosha kutoka kwenye anga za nje vinashikwa na mvuto wa gravity ya Dunia. Ingawa hatutambui, kila siku karibu tani 100 ya vumbi zinaanguka Duniani kutoka kwenye anga ya nje. Wakati mwingine tunaweza kuiona wakati wa usiku tukiona ghafla mistari midogo ya nuru inayowaka kwa sekunde moja au mbili. Hii ni dalili ya kwamba kimondo kidogo kilianguka katika angahewa na kusuguana na molekuli za hewa hadi kushika joto na kuungua. WaSwahili wa Kale waliviita “Vinga vya shetani” kutokana na imani ya kwamba malaika walivirusha dhidi ya mashetani wanaopita angani.

Vitu vinavyoonekana hivi kama mstari wa nuru ni vidogo tu, mara nyingi kama vumbi au punje tu zenye ukubwa wa milimita chache.

Vimondo vya mistari ya nuru.png


Vipande vikubwa zaidi ambavyo haviungui kabisa, huanguka Duniani kama vimondo. Kawaida vipande hivi hupotea lakini vipande vilivyoanguka katika maeneo yaliyotengeka, kama vile katika majangwa nusu-kavu, na katika barafu za Aktiki na Antaktiki, vinabaki na vinakusanywa kwa ajili ya utafiti na kwa thamani yake.


Vipande vikiwa vikuwa vya kutosha kama mita kadhaa, hushuka angani kwa kasi kubwa sana kiasi cha kilomita 50 kwa saa. Hapo angahewa inakuwa kama ukuta ambao vimondo vinagonga na kulipuka juu kwa juu na kuangamia huku vikitoa mawimbi mshtuo yanayoharibu maeneo makubwa kama vile ilivyotokea Tunguska na Chelyabinsk. Vimondo vikubwa vilivyoundwa na metali ndani yake vinaweza kubaki na kuanguka ardhini kama vile kimondo cha Mbozi.


Chanzo kikuu cha asteroidi ni Ukanda Kuu wa Asteroidi ambao ni mkusanyiko wa malaki ya vipande vya mawe vya muundo na ukubwa mbali mbali. Vinazunguka Jua vikiwa vimesambaa katika nafasi kati ya obiti ya sayari za Mirihi (Mars) na Mshtarii (Jupiter) ambazo ni sayari ya nne na ya tano kutoka kwenye Jua. Asteroidi nne kati ya hizo ni kubwa sana, kiasi cha zaidi ya kilomita 500.

UKANDA KUU WA ASTEROIDI.jpg


Kama asteroidi zinavutwa na graviti na kuelekea karibu na obiti ya Dunia zinaitwa “Violwa vya kukaribia Dunia” (kifupi VKD). Kwa bahati nzuri kugongwa kwa Dunia na “VKD” kubwa haitokei mara kwa mara na uwezekano ni mkubwa kwamba hatutashuhudia kuanguka kwa asteroidi katika maisha yetu. Lakini maendeleo ya sayansi imeboresha elimu yetu juu ya violwa hivi kwenye anga la nje. Tunajua sasa kwamba VKD ni vingi sana. Tunajua pia kwamba hadi sasa tumegundua sehemu tu ya VKD hizo na tunajua pia kwamba kuanguka kwa asteroidi kubwa kunaweza kuleta uharibifu mkubwa. Tukio kama lile la Meksiko miaka milioni 65 iliyopita lingekuwa hatari kwa maisha ya watu wote Duniani. Maendeleo ya kiteknolojia yametuletea uwezo wa kutafuta magimba haya vizuri zaidi kwenye anga la nje.


Wataalamu wanakadiria sasa kwamba kugongwa na asteroidi kubwa (zaidi ya kilomita 1) hutokea takriban kila baada ya miaka milioni 100. Lakini asteroidi za mita chache kama ile ya Tunguska inaweza kugonga Dunia kila miaka 500 hivi. Kwa vile Dunia ina maeneo makubwa ya bahari, jangwa au pori baridi, hadi sasa, asteroidi zote kubwa zilizorekodiwa na watu zimepiga maeneo ambako hakuna watu wengi. Ila wataalamu wana uhakika kwamba siku moja tukio kubwa litaathiri pia maeneo yanayokaliwa na watu.


Hadi sasa haiwezekani kuzitambua asteroidi mapema kiasi cha kutosha na kuweza kutoa taarifa ya tahadhari kama kuna asteroidi ya ukubwa wa mita kadhaa ipo njiani kugonga Dunia moja kwa moja. Pia haiwezekani kwa sasa kueleweka kwa usahihi wa kutosha mahali kamili ambapo asteroidi itapiga ardhi.


Elimu ya kisasa inawezesha binadamu kuongeza mitambo ya kutambua mapema asteroidi zinazokaribia Dunia na hata kubuni mitambo inayoweza kubadilisha miendo yao katika anga la nje ili zisigonge Dunia. Kuna mipango kubuni roketi na vyomboanga vinavyoleta mabomu au mitambo mengine hadi asteroidi inayoelekea Duniani na kuipasua huko huko, au kubadilisha njia yake ili isigonge tena Dunia. Ila tu mipango hii inahitaji ushirikiano wa nchi nyingi. Hiyo ndiyo sababu ya Umoja wa Mataifa kutambua kuadhimishwa kwa Siku ya Asteroidi ulimwenguni kote ili elimu ya asterodi isambazwe Duniani, na watu watafakari pamoja na viongozi wao, namna ya kuchukua hatua za kujihami iwapo itatokea dharura.


Filamu kadhaa zilizotokea katika miaka ya nyuma zilijaribu kuwaza hadithi za mgongano wa asteroidi kubwa Duniani kama vile When Worlds Collide (1951), Meteor (1979), Deep Impact (1998), Armageddon (1998). Filamu ya 51º North (2015) ilihamasisha wataalamu kuanzisha Siku ya Asteroidi na filamu hii inaweza kutazamwa bure kupitia tovuti ya https://asteroidday.org.

Habari na taarifa mbali mbali kuhusu asteroidi zinapatikana katika tovuti ya https://asteroidday.org za kukusaidia kuleta taarifa hizi kwa wengine kwa kutumia video, uwasilishaji kwa PowerPoint, mazoezi na mengine mengi.


Unaweza kuangalia matangazo ya Siku ya Asteroidi tarehe 30 Juni 2017, moja kwa moja kutoka Luxemborg City kupitia mtandao https://asteroidday.org/live/. Tumia nafasi hii kuongeza ufahamu wa msuala ya asteroidi katika jamii yako, kazini kwako, au mashuleni na katika vyuo.

==MWISHO==​
 
Sasa inakuaje kwamfano mwezi june ukawa na siku 28??
Au ndio watasubiri mpaka mwezi mwengine wenye siku 30?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom