Siku jaribio la 'kumtega' Kikwete lilipogonga mwamba Arusha! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Siku jaribio la 'kumtega' Kikwete lilipogonga mwamba Arusha!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Ngongo, Nov 10, 2009.

 1. Ngongo

  Ngongo JF-Expert Member

  #1
  Nov 10, 2009
  Joined: Sep 20, 2008
  Messages: 12,155
  Likes Received: 3,634
  Trophy Points: 280
  RAIS Jakaya Kikwete, hivi karibuni, "alijianasua katika mtego" aliowekewa na baadhi ya viongozi wa jamii ya wafugaji wa Kimasai katika Bonde la Hifadhi ya Ngorongoro la kumtaka aruhusu shughuli za kilimo ndani ya hifadhi hiyo kama walivyofanya viongozi wa awamu zilizopita.
  Hoja ya kutaka Rais aruhusu shughuli za kilimo katika hifadhi inadaiwa kupenyezwa na mmoja wa wanasiasa mwenye nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Ngorongoro kupitia kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wa wilaya hiyo, Metui Ole Shaudo.
  Imedaiwa kuwa hotuba ya Mwenyekiti huyo wa CCM iliandaliwa na mwanasiasa huyo (jina linahifadhiwa) ili Rais Kikwete akiruhusu kilimo, basi, watumie hoja hiyo kama msingi wa kuomba kura kwa wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
  Shaudo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji katika Bonde la Ngorongoro, aliwasilisha hoja mbele ya Rais Kikwete katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Olbalbal wakati Rais alipotembelea hifadhi hiyo hivi karibuni kabla ya kwenda Mbeya.
  Shughuli za kilimo katika hifadhi hiyo zilizuiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii baada ya taarifa za kitaalamu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Utamaduni na Mazingira (UNESCO) kuhusu kuongezeka kwa shughuli za binadamu katika bonde hilo na kutishia kuiondolea sifa ya kuwa moja ya maeneo ya urithi wa dunia.
  Taarifa za UNESCO kutishia kuoindoa hifadhi hiyo kama Urithi wa Dunia (World Heritage) zilitolewa kwa mara ya kwanza mapema mwaka huu na Kaimu Mhifadhi Mkuu, Bernard Murunya mbele ya kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira akiwemo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige walipotembelea hifadhi hiyo.
  Baada ya kupata maelezo na taarifa ya kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na shughuli hizo za kilimo na ufugaji ndani ya hifadhi, kamati hiyo ya Bunge iliridhia kuchukuliwa kwa hatua za dharura ikiwemo ya kusitisha shughuli hizo za kilimo ili kuiokoa hifadhi hiyo.
  Awali, shughuli za kilimo ambazo, hata hivyo, hazikuwemo katika sheria inayounda hifadhi ya Ngorongoro zinaelezwa kuwa ziliruhusiwa na mawaziri wakuu wa Serikali ya awamu ya pili, John Malechela na Fredrick Sumaye wa awamu ya tatu, kwa nyakati tofauti kwa malengo ya kisiasa.
  Katika mkutano uliofanyika katika kijiji hicho cha Olbalbal kabla ya kumkaribisha Rais Kikwete jukwaani, Mwenyekiti huyo wa CCM alieleza kuwa kero kubwa inayowakabili wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo ni kitendo cha kuwazuia kuendesha kilimo cha kujikimu ndani ya hifadhi.
  “Mheshimiwa Rais wetu mpendwa tunaomba uruhusu kilimo cha kujikimu kwa wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi kwa sababu kwa sasa wananchi wamezuiwa kuendesha kilimo hicho”, alieleza Mwenyekiti huyo.
  Shaudo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji katika wilaya hiyo, alimwambia Rais kuwa iwapo kilimo hicho hakitaruhusiwa, kuna uwezekano CCM ikashindwa katika uchaguzi mkuu ujao na vyama vya upinzani.
  “Vyama vya upinzani vinaweza kutumia suala hilo kama ajenda yao na kuipa wakati mgumu CCM katika uchaguzi mkuu ujao, na tunaweza kupoteza jimbo la Ngorongoro”, alieleza Mwenyekiti huyo; huku akishangiliwa na baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.
  Baada ya kumaliza kuwasilisha maombi hayo, Shaudo alirudi jukwaa kuu walikokaa viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdori Shirima na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali.
  Hata hivyo katika hali isiyotarajiwa, Rais Kikwete, ambaye alionyesha wazi kukerwa na mtego wa kuruhusu kilimo ndani ya hifadhi hiyo, alimwita Shaudo na kuanza “kuzozana” naye akimtaka aeleze matatizo ya msingi ya wananchi na si suala ambalo lina maslahi ya watu wachache.
  ‘Mzozo’ kati ya Rais Kikwete na Mwenyekiti huyo ulichukua wastani wa dakika nne hivi na kufanya shughuli za mkutano huo kusimama ghafla; huku wananchi waliokuwa chini wakishindwa kufahamu kilichokuwa kikiendelea “meza kuu”.
  “Hivi Mwenyekiti, hakuna matatizo ya msingi na kero za wananchi wa Ngorongoro?.......rudi jukwaani ueleze kero za wananchi, na si haya mambo ya kilimo cha robo eka ambacho hakina tija kwa wananchi”, alisikika akihoji Rais Kikwete kwa sauti ya chini.
  “Mimi nilifikiri ungeleta hoja kuwa mpewe ruhusa ya kupanda majani ya mifugo yenu katika maeneo mnayoishi ili kukabiliana na uhaba wa malisho ..…lakini Mwenyekiti unakuja na hoja dhaifu kama hiyo”, alisikika akisema Rais Kikwete.
  Hali hiyo iliwaacha na mshangao viongozi na wananchi waliokuwa wamejaa katika mkutano huo. Mwenyekiti huyo alilazimika kurudi jukwaani kuzungumzia “kero za msingi”.
  Ilikuwa ni dhahiri kuwa Rais Kikwete aliukataa ‘mtego’ wa viongozi hao wa Wilaya ya Ngorongoro kwa kutambua kuwa hatua hiyo ingekuwa ni sawa na kuingilia maamuzi yaliyochukuliwa na watendaji wake wa chini na pia umuhimu wa kutunza mazingira ya hifadhi hiyo ambayo ndiyo inayoongoza kwa kuvutia watalii wengi ikishindana na Mlima Kilimanjaro.
  Akizungumza baada ya “hali ya hewa” kutulia, Rais Kikwete aliwataka wananchi wa jamii hiyo ya wafugaji kujifunza ufugaji bora ambao unaleta tija kwao na Taifa badala ya ufugaji wa asili ambao umeanza kupitwa na wakati.
  Rais Kikwete alisema ili kubadilisha mfumo huo wa ufugaji katika wilaya hiyo yenye idadi kubwa ya mifugo, ni lazima watu wa jamii hiyo wakubali mabadiliko na kujifunza kutoka jamii nyingine za wafugaji akitoa mfano wa Ankole nchini Uganda.
  Waankole ambao ni maarufu kwa mifugo yao yenye pembe ndefu, ni wafugaji kama walivyo Wamasai wa Tanzania, lakini ufugaji wao unaelezwa kuwa wa kisasa zaidi tofauti na jamii nyingine za hapa nchini.
  “Wafugaji wa Ki-banyankole wamepiga hatua kubwa sana katika ufugaji unaozingatia matumizi bora ya ardhi…..ni vyema tukajifunza kwao. Kwa hiyo nitatuma ujumbe wa viongozi wa kimila wa hapa Ngorongoro na wale wa serikali ili kwenda kujifunza aina hiyo ya ufugaji”, alieleza Rais Kikwete.
  “Nitazungumza na kiongozi mwenzangu wa Uganda (Rais Yoweri Museveni) ili ujumbe wa viongozi hao uweze kupokelewa na kupatiwa mafunzo elekezi kuhusu ufugaji wenye manufaa”, alieleza Kikwete.
  Rais aliitaka jamii hiyo ya wafugaji kupanda majani kwa ajili ya mifugo yao katika maeneo wanayoishi ambayo yatasaidia sana malisho kwa ng’ombe; hasa wakati kama huu ambao ukame umesababisha vifo vya maelfu ya mifugo badala ya kung’ang’ania kilimo ambacho hakina tija.
  Hifadhi ya Ngorongoro ni hifadhi ya aina yake duniani kwani huchukuliwa kuwa moja ya maeneo ya urithi wa dunia (world heritage site) kutokana na uasilia wake ambapo wanyama pori na wafugaji wa Kimasai huishi pamoja ndani ya hifadhi hiyo bila kudhuriana.
  Tofauti na hifadhi zingine duniani pia ndani ya hifadhi hiyo sheria imeruhusu kuwepo kwa makazi ya wafugaji ambao huishi na familia zao na kufanya mfumo wa maisha ambao huwa pia kivutio kwa watalii wanaotembelea Ngorongoro.
  Ni tabia hizo za asili ndizo ziliifanya hifadhi hiyo kujipatia umaarufu mkubwa duniani na kuifanya Tanzania kutamba katika sekta ya utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na kuvutia watalii wengi kutoka kila pembe ya dunia wanaokuja kutembelea hifadhi hiyo.
  Lakini, hata hivyo, hifadhi inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya watu na mifugo ndani ya hifadhi tofauti na wakati hifadhi hiyo inaanzishwa mwaka 1959 ambapo kulikuwa na watu 8000 tofauti na takwimu za leo zinazoonyesha kuwa ndani ya hifadhi kuna watu zaidi ya 64,842 wakati uwezo wake ni watu wasiozidi 25,000.
  Idadi hiyo ya watu imeongezeka kutokana na watu kuzaliana na wengine kuhamia baada ya shughuli za kilimo kuruhusiwa. Kingine ni ujenzi holela wa mahoteli ya kitalii ambapo vigogo wengi kutoka serikalini na wafanyabiashara wameingia ubia kujenga mahoteli hayo.
  Kwa sasa takwimu za wilaya hiyo zinaonyesha kuwa kuna jumla ya mifugo milioni 1,050,000 ambapo ng’ombe wanakadiriwa kufikia 350,000, mbuzi 400,000 na kondoo 300,000, idadi ambayo pia imechagia sana kuharibu mazingira ya asili ya hifadhi hiyo.  Source: Raia mwema.
   
Loading...