Si maslahi ya CCM ama UPINZANI | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Si maslahi ya CCM ama UPINZANI

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Petu Hapa, May 19, 2009.

 1. P

  Petu Hapa JF-Expert Member

  #1
  May 19, 2009
  Joined: Jan 2, 2008
  Messages: 714
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  Tunavyotujitayarisha na uchaguzi wa mwaka 2010 ni vyema watanzania tujikumbushe misingi ya utanzania wetu na maana yake nini. Tunapochagua viongozi matumaini yetu juu ya ungozi wao ni yapi? Tunawapa wajibu gani katika kutuongoza lakini cha msingi kabisa sisi wenyewe tunajipa majukumu gani kuhakikisha wanatuongoza, na pale wasipo tuongoza ipasavyo tutawanya nini?

  Inawezekana majibu ya maswali haya tunayo katika nafsi zetu lakini imefika wakati watanzania tuhitaji kuongea kama watanzania si kama wanachama wa siasa kwani utanzania wetu ndio unaoanza kabla ya vyama, na ndio ambao utatutoa katika umasikini wetu. Tunahitaji tuongee nje ya migawanyikao ama makundi yetu – ya kazi, mikoa, urafiki, ushabiki, matabaka, na kuanza kujenga muunganiko wa agenda za kitaifa.

  Kabla ya vyama vya siasa havijaanza kurusha propaganda zao juu ya chama kipi ni bora zaidi ya kingine, ni jukumu letu kutambua mahitaji yetu ni yapi – kama wananchi na kama nchi. Naimani mabadiliko ya Tanzania hayawezi kuja kwa kuamini chama kipi ni bora zaidi kingine. Kwani kati ya wanaccm tunajua kunamasikini wakutupwa, na hata kambi za upinzani wengi wanalia njaa. Bila kujali itikadi wananchi kwa machungu yao wamepiga kelele juu ya ufisadi. Hii ni dhahiri kwangu kwamba utanzania wetu ni juu ya siasa za vyama.

  Ni dhahiri kwangu wananchi wa Tanzania, wanachama wa siasa na wale wasio wanachama, kwanamna moja ama nyingine tunajua mapungufu ya ccm na wasiwasi wetu juu ya upinzani. Sihitaji kusema CCM imetutoa wapi na inatupeleka wapi kwani machungu yake tunayaona katika ufisadi na huduma za jamii. Ni wale walio na pesa ndio wanaweza kumudu matibabu, kusomesha watoto, kumiliki mali na hata kupata ajira – hali ambayo imeleta misemo mbalimbali kama vile walalahoi na walalahai, wananchi wa daraja la kwanza na wala wa daraja la tatu. Na hata wale walio na maisha ya kati wakiwa wa kweli na wawazi watatambua mishahara yao ni ya kujikimu wao na watoto wao tu – wakati ndugu zao ama majirani zao wapo katika ufukara.

  Hofu yetu juu ya upinzani nayo ipo bayana kwani hatujaona kupevuka kwao katika siasa zetu. Lakini ni dhahiri upinzani wameonyesha uwezo wa kujadili ufisadi wa nchi hii, ila wasiwasi wangu mimi upo kwenye namna gani upinzani utaongoza taifa hili kwa manufaa ya watanzania walio wengi. Kelele nyingi zenye mshiko zimepigwa kuhusiana na ufisadi lakini sijasikia kelele juu ya huduma za jamii, ajira, familia bora ama elimu. Hivi karibuni kelele kubwa imepigwa juu ya umeme wa nchi hii na ufisadi wake lakini ukiangalia kwa undani makelele yote hayo yanongelea umeme usiozidi asilimia 20 ya watanzania. Ingawaji wapinzani wanaonyesha mwendo mzuri bado tunahitaji watupe uhalisia wa sera na itikadi zao ili tuweze kuelewa ni wapi watatupeleka iwapo watashika uongozi kwa manufaa ya wananchi wa tanzania.

  Nachotaka kuwakumbusha ndugu zangu Tanzania yetu ni moja, ingawaji hivi karibuni kumekuwa na viashiri vya malumbano ya Zanzibar na Bara, mara CCM na upinzani mara maskini na matajiri ili mradi kutupa wazimu. Nachotaka kuwakumbusha ndugu zangu, Tanzania kabla ya siasa, vyama, na tofauti zetu mbalimbali sisi ni taifa moja, lenye historia ya mapambano ya ukombozi iliyopata hitimisho miaka ya mwanzo ya 60. Tukaitwa mataifa huru, na badaya kuunganika Zanzibar na Tanganyika kuwa Tanzania. Tunamapungufu yetu katika muungano hayo yanaongeleka – kwa wale wanaojua muungano – na wale ambao hawana habari kwamba Tanzania ni nchi ya muungano- na hao wapo wengi – mbeleni tuelimishane kwani hilo ni la msingi katika kuundeleza muungano.

  Nia yangu leo sio kuongelea muungano ama tofauti zetu, nia yangu ni sisi kujikumbusha maana ya utanzania wetu. Watu wa kale wa taifa letu hili, na wale ambao walikuja kuongoza harakati za uhuru, walikuwa na imani kwamba umoja wetu ndio nguvu yetu, na utengano wetu ni udhaifu.

  Msingi wa taifa la Tanzania upo katika neno umoja. Sizungumzia umoja wa ujamaa na kujitegemea, ingawaji itikadi hiyo nayo ilijijenga katika maendeleo ya kushirikiana. Umoja naoungolea leo ni utambuzi kwamba katika dhana ya umoja tunaongelea utu, utaifa, na tamaduni. Ni mila na desturi ya kitanzania kumjali mtoto wa mwenzio kama wa kwako. Sasa, leo wewe mtanzania uliyenacho kidogo unapata raha gani kuona mwana wa mwenzio haendi shule? Je tunapata faida gani kuona watanzania wenzetu wanakufa kwa kuwa hawana pesa za matibabu? Kunaraha gani kuona wamachinga barabarani na makuli wakitafuta ridhiki bila mafanikio.

  Naamini kwamba utu wa mtanzania ni kuelewa kwamba ni wajibu wetu kuhakikisha binadamu wote ni sawa na wanapata haki katika huduma za kijamii ili kujiendeleza na kujenga taifa letu. Ni jukumu la kila mtanzania kuondoa umasikini na sio kutengeneza umasikini. Ni jikumu la mtanzania kufanya kazi na sio kukaa bila ajira. Ni haki ya mtanzania anayefanya kazi kulipwa mshahara bora kuliko ule wa manamba. Ni haki ya mkulima kula jasho lake na sio awe kibarua. Ni haki ya kila mtoto wa Tanzania kusoma na kuwa na afya bora – hizi sio haki za vyama wala bara na Zanzibar ni haki za mtanzania kuanzia mwaka 1961.

  Mwaka 1961 na ule wa 1964 ni miaka muhimu sana kwa taifa letu kwani haki za utanzania ziliwekwa kwenye mamlaka ya serikali ya muungano – tukawa taifa. Ni katika mamlaka hayo serikali inapaswa kutumikia wananchi na kutupa haki zetu za msingi. Sio viongozi kujineemesha ila viongozi wa jamhuri kazi yao ni kuongoza taifa hili na kulinda maslahi ya wananchi na nchi hii. Viongozi wetu wote wa taifa hili hula kiapo cha kulinda nchi, wananchi na mali zake huo ni mkataba kati yao na sisi. Sasa imefika wakati wa sisi kuwakumbusha viongozi mkataba wetu na wao ni upi!

  Huu ni wakati wa kuikumbusha serikali kwamba imepoteza taifa hili kwa muda sasa! Imetufanya wananchi tumekuwa kama tumedandia basi, na hili halitaendelea kukubalika. Ni wakati wetu kuiambia serikali iwajibike na kuwekeza kwa wananchi wake – kwenye elimu, afya, kilimo na tamaduni zetu – hili sio ombi ni jukumu la serikali. Ni haki ya utaifa wetu! Kwanini tuitwe watanzania? Na sio mkenya wala mganda? Kwanini niitwe mtanzania kama hakuna maslahi yoyote ya kulinda haki na urai wangu? Wajibu wangu ni nguvu kazi, wajibu wa serikali ni nini? Kama imesahau nitaikumbusha – ni kujenga mazingira kwa kila mtanzania kukua katika mazingira bora kiafya na kielimu ili kuendeleza na kulitumikia taifa hili.

  Natambua kwamba serikali haiwezi kufanya kila kitu, na wala watanzania hawategemei serikali ifanye kila kitu maana asili yetu sisi ni wachapakazi – hiyo ndio mila na desturi ya jadi zetu. Sio lengo la watanzania kusema serikali itoe kila kitu bure – kama ilivyokuwa kwenye siasa za ujamaa – ila tunasema serikali ni lazima ijenge mazingira ya kulinda haki za watanzania wote kwa usawa. Watanzania tunaelewa kwa mazingira ya uchumi wa leo serikali haiwezi kufanya kila kitu peke yake, na wala haijawahi kufanya kila kitu peke yake. Siku zote, wananchi tumelima bila kupata masoko, tumefanya kazi kwa mishahara duni, tumesoma bila kuthaminiwa, tumekua kwa kubahatisha bahatisha. Na sasa imefika wakati wa kusema imetosha. Tunahitaji serikali ijayo iweke mazingira ya sera na sheria ambazo zitatoa na kujenga mazingira ya haki sawa kwa wananchi wa Tanzania. Kwamba yule mtoto wa mkulima wa magu na mtoto wa upanga waweze kuwa na haki sawa ya elimu. Kijana wa manzese na yule na yule wa upanga wawe na haki sawa katika ajira. Mama mjamzito wa kiboloroni na yule wa geita wawe na nafasi ya kujifungua salama.

  Tunahitaji taifa hii lijenge imani ya wananchi kwamba tunaweza kujiongoza katika umasikini. Tunahitaji viongozi warudishe imani juu ya uwezo wa watanzania katika kuleta maendelo. Ni amani ya kwamba taifa hili halitaendelea kuwa maskini. Leo hii wananchi wanaamini Tanzania ni maskini, watanzania ni wazembe, wavivu. Na kunawale wanaoamini kiaongozi asiyechuma mali madarakani basi ni mjina, na wapo wananchi watakaomcheka kama ataendele kuwa fukara. Hii ni hatari kwani watanzania wengi hawana imani na taifa lao kwahiyo kila mtu anchukua chake mapema. Taifa linapokosa mipango dhabiti ya uzeeni ama huduma za jamii, wananchi wanaona ni bora wajilimbikizie mali. Ama wale wakulima wakilima wanakosa masoka wanajiuliza kunafaida gani kulima kama mazao yataozea shambani? Basi wanalima gunia mbili ama tatu za kula tu. Matokeao yake wananchi wanapoteza imani kwa taifa, na kila mtu anabaki kivyakevyake.

  Uchaguzi ujao, wananchi turudishe imani. Siongelei imani hewa, naongelea umefika wakati wananchi kuamini kwamba matendo yetu na juhudi zetu zinatija katika maisha yetu. Ni vyema taifa kurejesha imani juu ya nguvu kazi – kwamba hajalishi nimetoka wapi wala baba yangu anaitwa nani ama nimezaliwa kijijini ama mjini, ila iwapo nitafanya kazi kwa bidii nitafanikiwa katika maisha yangu. Serikali inapaswa kuweka wazi taratibu za mafanikio ya kila mmoja wetu ili kujenga matumaini kwa wananchi kwamba kunamahusiana kati ya nguvu kazi na maendelea, kunamahusiana kati ya ushuru na huduma za afya, kunauhusiana kati ya uraia na haki zake. Ni katika imani hizi wananchi wanaweza kuamini kwamba umasikini unaweza kuondoka Tanzania.

  Uchaguzi ujao tusipigie kura juu ya chama tu, bali tuwaulize wagombea wetu, agenda zao juu ya afya, elimu, maliasili ni zipi? Tuwaulize juu ya mabadiliko ya katiba na watupe vipengele watakavyovibadilisha! Watuambie mpango wa maendeleo ya vijijiji ni upi. Katika vikundi vyetu na majimbo yetu tujadili na tukubaliane agenda za msingi kwa maendeleo yetu kwani hiyo ndio njia pekee ya kuondoa taifa letu katika umasikini.

  Taifa hili litaondoka katika umasikini pale tu sisi kama wananchi tutaamua tunataka Tanzania ya namna gani. Bado naimani na Tanzania. Bado na imani na watanzania. Naimani na utashi wetu na nguvu ya machungu yetu kutuongoza katika kuchagua viongozi watakaojali maslahi ya taifa hili si kwa manufaa yetu sisi tu bali kwa vizazi vijao na hata yule mtoto wa jirani yako ama vijana wetu wamachinga.

  Mungu ibariki tanzania
   
Loading...