Shule hizi na majina ya kina Mugabe, Mkapa…!

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,115
Shule hizi na majina ya kina Mugabe, Mkapa…!

Johnson Mbwambo Juni 11, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

MPENZI msomaji, je umepata kujiuliza ni kwa nini unaitwa unavyoitwa? Ni kwa nini wazazi walikuchagulia jina hilo? Je, unalipenda au hulipendi? Kwa nini unalipenda au kwa nini hulipendi? Kama hulipendi, ulipata kuwaza kulibadilisha?

Wanazuoni kadhaa wamepata kutafiti suala la majina (onomastics) na kuchambua maana na siri zinazojificha katika jina la mtu au asasi

fulani (what is in a name), na wote angalau wanakubaliana katika kitu kimoja.

Kitu hicho ni kwamba, utoaji jina, iwe ni kwa kitoto kichanga kilichozaliwa au iwe ni kwa shule mpya inayofunguliwa, soko jipya linalojengwa, bendi ya muziki inayoanzishwa au hoteli mpya inayofunguliwa, ni kitu nyeti na kinachohitaji fikra nzito na umakini mkubwa kabla ya kukata shauri.

Ni kitu nyeti na kinachohitaji fikra nzito na umakini, kwa sababu jina litolewalo, huko mbele ya safari, linaweza kuleta manufaa au balaa kwa aliyelipewa.

Wako wanaoamini kwamba ukikipa kichanga chako jina "Chuki", kuna uwezekano mkubwa mtoto huyo akakua huku akifanana na jina lake; yaani kuwa na tabia ya chuki, hasira na ghadhabu.

Vivyo hivyo wako wanaoamini kwamba ukimpa mtoto wako jina la "Masumbuko" au "Tabu", ataishi maisha yake yote kwa kuhangaika na kukosa amani; hata kama ni tajiri mkubwa.

Lakini wako pia wanaoamini kwamba jina ni jina tu. Wanasema lipe ua waridi jina jingine, lakini bado litabakia na sifa ile ile; yaani harufu nzuri na rangi ya kupendeza machoni.

Lakini msomi wa India, Rajender Krishna hakubaliani na hoja hiyo. Anaandika www.boloji.com: "Jina ni kila kitu. Hata leo ambapo nimeshakuwa mkubwa bado jina nililopewa ndilo linalonisukuma kukabiliana na changamoto za maisha. Mara zote najitahidi mno kuishi kulingana na sifa na maana ya jina langu."

Jina ambalo Krishna analizungumzia ni "Rajender" ambalo kwa lugha yake ya asili lina maana ya "Mfalme wa Wafalme."

Anachosema Rajender ni kwamba jina, iwe ni kwa binadamu au kwa asasi, laweza mbeleni likawa ni "silaha" inayosaidia kumwongoza mhusika katika mema au likawa asili ya mambo mabaya maishani, ama kwa mhusika au jamii.

Katika tovuti ya asasi inayoitwa Kabalarian Philosophy (Teaching the Principles of Mental Freedom) kuna maelezo haya yafuatayo kuhusu mwongozo wa kuchagua jina kwa mtoto au hata mtu mzima au asasi:

"Unapochagua jina la mtoto au la asasi, unaandaa maisha ya baadaye ya mtoto huyo au asasi hiyo (creating the future).Toa jina lenye uwiano sahihi (balanced name) kwa sababu kwa kufanya hivyo, unaanzisha mchakato wa ujenzi wa viwango bora, ubongo unaochapa kazi, kujiamini, kujituma heshima na uadilifu."

Kama hivyo ndivyo, ninaweza nikaelewa na kusamehe watu wachache wanaowapa watoto wao majina ambayo sio balanced; lakini siwezi kuelewa au kuwasamehe wenzetu wanaozipa taasisi zetu za elimu majina yenye walakin yanayoweza kuwaathiri wanetu huko mbeleni katika safari zao ndefu za maisha.

Chukua mfano wa shule kama ile iliyopo Barabara ya Shekilango mjini Dar es salaam inayoitwa Mugabe Primary School. Sielewi ni kwa nini shule hiyo bado imeling'ang'ania jina hilo wakati Rais Robert Mugabe, kwa sasa, ndiye pengine Rais hovyo kushinda wengine wote duniani.

Hapa tunamzungumzia rais dikteta ambaye nchi yake ndiyo inayoongoza duniani kwa kuwa na kiwango kikubwa cha mfumuko wa bei (asilimia 200,000!). Hapa tunamzungumzia rais ambaye nchi yake ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wasio na ajira (asilimia 80!)

Hapa tunamzungumzia rais pekee duniani ambaye amekimbiwa na nusu ya wananchi wake; kwani karibu watu milioni 4 wanaishi, hivi sasa, uhamishoni (wengi wakiwa Afrika Kusini) kwa sababu ya kukimbia maisha magumu ya Zimbabwe ya Robert Mugabe.

Hapa tunamzungumzia rais ambaye amekataa kuondoka madarakani hata baada ya kutawala kwa miaka 28, rais ambaye hata baada ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu wa majuzi, amegoma kuheshimu matokeo.

Hapa tunamzungumzia rais ambaye, pamoja na wananchi wake kukabiliwa na njaa kali kutokana na ukosefu wa vyakula, majuzi, amevipiga marufuku vikundi vyote vya kimataifa vinavyojishughulisha na kutoa misaada ya kibinadamu (ikiwa ni pamoja na chakula) kufanya kazi Zimbabwe!

Kwa kitendo chake hicho tu, maelfu ya Wazimbabwe waliokuwa wakitegemea chakula cha msaada kutoka nje; hususan watoto, watakufa kwa njaa.

Hivi mtoto anayesoma darasa la tano Shule ya Msingi ya Mugabe pale Sinza, Dar es Salaam, akimuuliza mwalimu wake kuhusu huyu Robert Mugabe kwamba ni nani hasa, atapewa maelezo gani? Mwalimu atalazimika kudanganya au atamweleza mwanafunzi ukweli wote? Na mwanafunzi akiujua ukweli wote atajisikiaje kusoma katika shule yenye jina la mtawala kama huyo?

Ukiondoa ukweli kwamba Mugabe ni Rais wa kwanza wa Zimbabwe na alishiriki katika vita ya ukombozi, ni hiba (legacy) gani hasa analiachia bara la Afrika; achilia mbali watoto wanaosoma katika shule hiyo iliyopewa jina lake? Hiba ya udikteta na kupenda madaraka kupindukia?

Ipo pia shule nyingine ya sekondari mjini Dar es Salaam inayoitwa Benjamin Mkapa. Hivi wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo wanajisikiaje wanaposoma magazetini habari za tuhuma mbalimbali nzito anazohusishwanazo Mkapa wakati wa utawala wake?

Hata kwa vigezo vya kawaida tu; mtu unashawishika kujiuliza: Walifikiria nini kuipa shule hii jina lake? Na kwa nini mpaka sasa hawajabadili jina la shule hiyo; hasa baada ya mwenye jina kuandamwa na tuhuma za skandali hizo nzito?

Wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo wanajisikiaje kusoma katika shule yenye jila la mtu ambaye ni rais wa kwanza nchini kufanya biashara akiwa Ikulu? Si hivyo tu, huyu ni mtu ambaye akiwa rais alisimamia mauzo ya nyumba za serikali kwa watu binafsi .

Huyu (Mkapa) ndiye aliyekuwa rais katika kipindi ambapo Sh. bilioni 133 za umma zilichotwa na mafisadi katika akaunti ya Benki Kuu (BOT) ya EPA ; huku baadhi zikitumbukizwa katika kampeni za uchaguzi za CCM. Kiwango hiki cha ufisadi hakijapata kuonekana katika tawala nyingine zote zilizotangulia. Wanafunzi na walimu wa shule hiyo wanajisikiaje wanapopigwa na ukweli huo?

Hata katika masuala ya ujenzi wa demokrasia nchini, historia imemwandika Mkapa kama Rais aliyesimamia kufanyika marekebisho kwenye Katiba ya nchi (mwaka 2000) kwa lengo binafsi la kushinda urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Kwa ufupi, urais wa Mkapa haujaacha hiba yoyote kubwa kwa Watanzania kiasi cha kuhalalisha shule, inayotarajiwa kuwepo hata baada ya miaka 200, kupewa jina lake. Siamini kuwa anastahili kuwa role model katika shule hiyo.

Ni dhahiri vizazi vijavyo vitakapokuja kufanya utafiti na kujua alikuwa ni rais wa namna gani kiasi cha shule hiyo kupewa jina lake, vitawacheka mababu zao kwa kugawa majina kama karanga!

Hoja yangu ni kwamba tunapaswa kuwa makini katika kuzipa shule au asasi majina ya viongozi, wanasiasa au wafanyabiashara. Kwa sababu kuipa shule jina la mtu kwa matarajio kuwa atakuja kuisaidia shule kipesa, ni hongo. Nao pia ni ufisadi.

Kuipa shule au asasi jina la mtu hovyo na ambaye heshima yake katika jamii imepungua au inapungua, ni dhahiri huko mbele ya safari kutaathiri (kisaikolojia) maendeleo ya shule au asasi hizo na wote waliopitia humo.

Binafsi naifahamu shule moja ya msingi mjini Dar es salaam ambayo walimu wake wanahaha kulinda heshima na viwango vyake vya taaluma kwa sababu tu inaitwa JK Nyerere School. Inataka ifananefanane na maisha ya kutukuka ya Mwalimu Nyerere.

Sina hakika kama katika Mugabe Primary School na katika Mkapa Secondary School, azma ya walimu ni hiyo hiyo ya kulinda maisha na uchapakazi wa ‘kutukuka' wa waheshimiwa hao!

Vyovyote vile, nimalizie kwa kusisitiza kwamba tusiwe na pupa katika kuzipa majina shule zetu. Sote tunajua hujafa hujaumbika. Tungoje basi mpaka Mungu akishawaita viongozi wetu mbele za haki ndipo tukae chini na kutathmini utumishi wao na maisha yao hapa duniani, na ndipo tuamue kama wanastahili kuenziwa kwa shule au asasi kupewa majina yao.

Vinginevyo, tutaishia kuzipa shule na asasi zetu majina ya mafisadi, wakwepa kodi au wafanyabiashara za madawa ya kulevya. Na hapo ndipo tutakapokuja kuchekwa na vizazi vijavyo. Tafakari.

Email: mbwambojohnson@yahoo.com
 
kama ndo hivyo then what about the following:
1. Lake Victoria ........ how can we still name this beautiful lake after a british colonialiser bytch..!
2. Statue of Hans Meyer @ Mt. Kilimanjaro w/ words "the first man to climb Mt. Kilimanjaro"..! ...... how can this nazi mzungu be the 1st man to climb the mountain wakati babu zetu walikuwa wanaupanda kila siku kabla la huyu mzungu. and who had shown him the route to the peak kama sio mtu mweusi- yohani kinyala lauwo? and the funny thing is that rite beside this status kuna kijiwe cha blue dedicated to 6 porters who helped him to get up there. wre these people monkeys/dogs and not men? i jus can't believe that thsi statue of hans meyer is till there til today with the same words on it.
 
Back
Top Bottom