Lakini Dkt. Ndalichako alisema hakukuwa na upungufu wowote wa bajeti kwa kuwa serikali iligharamia shughuli nzima ya kusahihisha mitihani kwa asilimia 100, na kwa kuzingatia ongezeko la watahiniwa mwaka 2010 ukizinganishwa na mwaka uliotangulia.
Alisema muda waliodai kuwa ni mfupi kusahihisha mitihani hiyo haukuwa na tofauti na uliotumika mwaka 2009, na kuwa NECTA ilipanga walimu wa wengi zaidi wa kusahihisha kwa kuzingatia idadi ya wanafunzi waliotahiniwa.
"Mwaka 2009 tulikuwa na makers (wasahihishaji) 3,054 na mwaka jana tuliongeza idadi hadi 4,546 ili kukidhi ongezeko la wanafunzi, hivyo hatukuwa na upungufu na uliotumika ulikuwa sawa sawa," alisema Dkt. Ndalichako.
Dkt. Ndalichako alitoa mfano wa somo la Kiswahili lililochukua muda mrefu kusahihishwa kuwa lilitumia siku 32, walimu 293 mwaka 2009; na mwaka jana likatumia siku 36, walimu 539.
"Kwa hiyo hapo utaona kuwa tulizingatia ongezeko la wanafunzi, tukaongeza wasahihishaji na siku zilikaongezeka. Kwa masomo mengine siku zinatofautiana kulingana na idadi ya watahiniwa na walimu tuliopanga," alisema.