Shida ya Tanzania ni nini hasa? Na je tufanyeje

Mangole Valles Michael

JF-Expert Member
May 30, 2021
333
671
Anaandika Dr Christopher Cyrilo

Jana nilipata bahati ya kutembelea Malembo Farm na kukutana na rafiki yangu Lucas Malembo. Nimshukuru Malisa GJ kunileta kwenye darasa hili la kilimo na ufugaji.

Nimejifunza mambo mengi sana kuhusu kilimo na ufugaji. Kuna mambo ya kufurahisha, na mengine ya kufikirisha.

Nimejifunza, kumbe watu Malaysia walikuja kujifunza kilimo cha michikichi/mawese Kigoma. Leo ndio wanatuuzia mafuta bora wakati sisi bado tunazalisha mafuta ghafi ya mawese na hatuwezi kuuza nje. Mafuta tunayozalisha kutokana na mazao mengine kama ufuta na alizeti pia hayatoshi.

Nimejifunza, kumbe Vietnam walikuja kujifunza kilimo cha Mpunga na Korosho nchini Tanzania, wakachukua na mbegu, halafu leo wanatuuzia mchele na wanauza korosho nyingi na bora zaidi kwenye soko la dunia kuliko sisi.

Naambiwa, Kenya kuna utaalamu wa ufugaji wa ng'ombe ambao wanaweza kuzalisha hadi lita 40 za maziwa. Na utaalamu huo walijifunza Tanzania enzi za Nyerere, na sasa haupo Tanzania (au upo kwenye makaratasi).

Huko Botswana kuna kilimo na ufugaji mkubwa wa kisasa. Kiongozi mmoja wa Tanzania aliwahi kwenda huko, alipojionea huo ufugaji akaomba wataalamu waje Tanzania wasaidie utaalamu. Akaambiwa karibu wataalamu wote kwenye hiyo miradi ni watanzania.

Sasa hayo ni machache kati ya mengi yaliyonifikirisha sana. Lakini pia hayo ni madogo kwa muhimu. Yapo makubwa na muhimu zaidi;

1. Kilimo bila utafiti ni sawa na kuingia baharini bila kujua kuogelea. Tunahitaji tafiti ili kujua aina ya mbegu bora na imara. Lakini si hivyo tu, tunahitaji kujua mbegu zinazozalisha mazao kwa wingi kutegemea na mazingira ya kwetu.
Kwa wajasariamali wadogo wanahitaji kujitoa kufanya utafiti japo wa soko la bishaa au mazao yake badala ya kufuata upepo. Kutana na wataalamu, wakupe taarifa, wakupe michongo na hata ratiba ya kulima. Kuna mazao ukilima mwezi huu unapata hasara halafu unalaumu aliyekushauri. Kumbe hujawa na taarifa za kutosha kabla ya kwenda field.

2. Inawezekana kabisa kuondoa kuku chotara (broiler) nchini Tanzania kama tutawekeza kwenye ufugaji wa kuku wa kienyeji kwa njia za kisasa. Kumbe kuku wa kienyeji anaweza kuwa na kilo hadi 4, lakini kuku wetu wana wastani kilo 1 na nusu.

3. Sehemu kubwa ya mazao yetu hayakidhi masoko ya kimataifa, kwa kigezo cha ubora na hata kiasi. Kwa mfano, Zabibu ya Dodoma inayozalishwa leo 'imechoka' kwa sababu ni mbegu iliyokuwapo miaka na miaka. Kwahiyo ubora umepungua na uzalishaji umepungua. Mfano mwingine ni kwenye kilimo cha mihogo. Naambiwa, walikuja wawekezaji kwa ajili ya kujenga kiwanda ambacho kingeitaji tani milioni 2 za mihogo kwa Mwaka. Lakini wakashindwa kujenga kwa sababu wasingepata hicho kiasi.

4. Watu wakisikia mbegu bora na za kisasa wanafikiria ni mbegu zilizoboreshwa kijenetiki (GMO), hapana. Kilimo na Ufugaji wa kisasa si lazima vihusishe maboresho ya kijenetiki, bali matumizi ya elimu ya sayansi ya kilimo na ufugaji kwa njia salama kabisa. Mfano, mbolea inayotokana na mkojo wa Sungura! Hapo kuna maboresho gani ya kijenetiki?

5. Soko la chakula la ndani na nje lipo. Mazao mengi tunayozalisha hayana ubora, na kwahiyo baadhi ya mahoteli ya kitalii yanalazimika kiagiza nje. Serena Hotel (mfano)hawawezi kununua kuku wa kilo moja na nusu kwa ajili ya wateja wao, (hasa watalii), kwahiyo wanalazimika kuagiza kuku wa kienyeji wa kilo nne hadi tano kutoka nje. Na kuna hoteli za kitalii zaidi ya 400 kwa Zanzibar pekee.

Hayo ni machache sana kati ya mengi niliyojifunza. Fikiria tulikuwako hapo Malembo Farm kwa masaa matano, nikala supu ya kuku wa kienyeji hapo, nikazungushwa wee... aisee.

Bado najifunza.
 
Back
Top Bottom