kamati ya ulinzi ya bunge kumkaanga dk. Rashid
2009-03-10 11:03:26
na waandishi wetu
kauli ya mkurugenzi mtendaji wa shirika la umeme nchini (tanesco), dk. Idris rashid, kwamba nchi itagubikwa na kiza katika siku za usoni kutokana na kukosekana umeme, imeanza kumgeuka na sasa kamati ya bunge ya mambo ya nje, ulinzi na usalama imeeleza kwamba, itamwita ili kumhoji kuhusu kauli hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, wilson masilingi, alisema wamefikia hatua hiyo kwa vile umeme ni suala nyeti linalogusa moja kwa moja usalama wa nchi, hivyo hawawezi kuacha kauli nzito kama hiyo ya dk. Rashid ipite hivi hivi bila kufanyiwa kazi.
Masilingi ambaye pia ni mbunge wa muleba kusini (ccm), alisema hayo alipozungumza na nipashe jana.
``nitaita kamati yangu kujadili kauli yake (dk. Rashid) kisha baadaye tutamwita ili tumhoji, kwani umeme ni usalama wa nchi,`` alisema masilingi.
Alisema bosi huyo wa tanesco hana mamlaka ya kutoa kauli kama hiyo na kwa vile kamati yake inashughulika na masuala ya ulinzi na usalama wa nchi, wanachelea kuwajibika endapo hujuma yoyote inaweza kufanywa kutokana na kauli hiyo.
Ijumaa wiki iliyopita, dk. Rashid aliitisha mkutano na waandishi wa habari na katika jumla ya maelezo yake, alidiriki kutamka kwamba: ``wananchi wa tanzania watafanya maamuzi yao hapo ambapo nchi itakuwa imegubikwa na kiza, mahospitali hayatoi huduma, viwanda havizalishi, wanafunzi vyuoni wanashindwa kusoma kwa sababu tulishindwa kufanya maamuzi.``
kauli hiyo aliitoa alipokuwa akitangaza uamuzi wa tanesco kufuta nia yake ya kununua mitambo ya kufua umeme ya kampuni ya dowans na kueleza kwamba upotoshaji wa kisiasa kuwa chanzo cha kufikia uamuzi huo.
Dk. Rashid alisema hali ya ukuaji wa uchumi nchini inafanya ongezeko la mahitaji ya umeme kwa kiwango cha megawati 75 kila mwaka, kwa sasa kuna nakisi ya megawati 150 na kama hali hiyo ikiendelea bila kuwapo na uzalishaji wa ziada, nakisi itakuwa megawati 225 ifikapo desemba mwaka huu.
Wakati hayo yakijiri, mkurugenzi mtendaji wa kituo cha sheria na haki za binadamu (lhrc), francis kiwanga, alisema jana kuwa kama itafikia nchi kuingia kiza, basi menejimenti na bodi ya wakurugenzi wa tanesco watapaswa wote kuwajibika.
Kiwanga alisema watawajibika kwa vile tishio la ukosefu wa umeme lilijulikana muda mrefu na hakuna hatua za makusudi zilizochukuliwa kudhibiti hali hiyo.
Kuhusu menejimenti ya tanesco kupuuza maagizo ya bodi, kiwanga alisema wajumbe wa bodi walitakiwa wachukue hatua mapema na si kulalamika hivi sasa.
Alisema kinachosababisha hali hiyo, ni muingiliano wa kiutendaji kati ya ikulu na bodi ya wakurugenzi wa tanesco.
``kwani dk. Rashid si mara ya kwanza kwenda kinyume na bodi. Mara ya kwanza alishindwa kazi akataka kujiuzulu, ikulu ikaingilia kati na kujenga mazingira ya yeye kutowajibika,`` alisema kiwanga.
Naye rashid alipotafutwa na nipashe kuzunguzia hatua hizi mpya zinazolengwa kwake, alisema amefunga mjadala wa kuzungumzia sakata la ununuzi wa mitambo ya dowans.
Akizungumza na nipashe kwa njia ya simu jana, mkurugenzi huyo alisema hivi sasa hataki kabisa kuzungumza na waandishi wa habari.
``sitaki kuzungumza na waandishi wa habari sasa, nilishafunga mjadala huo,``alisema.
Dk. Rashidi alimtaka mwandishi, iwapo ana jambo lingine lisilohusiana na dowans awasiliana na idara ya mawasiliano ya tanesco ili apatiwe ufafanuzi.
Hata hivyo, alipoulizwa kwamba haoni kuwa madai ya yeye kukosa nidhamu yaliyotolewa na mwenyekiti wa kamati ya bunge ya nishati na madini, william shellukindo, yanamgusa yeye binafsi, mkurugenzi huyo alionekana kukasirirka.
``kama ni langu binafsi basi ni mimi binafsi, nimekataa kuzungumza, siongei na waandishi mimi, nenda idara ya mawasiliano,`` alisema na kukata simu.
Chimbuko la dowans ni mkataba wa mradi wa ufuaji wa umeme wa dharura wa megawati 100 kati ya serikali/tanesco na kampuni ya richmond uliofikiwa mwaka 2006. Richmond baada ya kushindwa kuutekeleza mradi huo iliuuza kwa dowans.
Mkataba wa richmond ulizua mvutano kiasi cha kusababisha bunge kuunda kamati teule kuchunguza ikiongozwa na mbunge wa kyela, dk. Harrison mwakyembe, ripoti yake ilimfanya waziri mkuu, edward lowassa, ajiuzulu.
Pia mawaziri nazir karamagi (nishati na madini) na dk. Ibrahim msabaha (ushirikiano wa afrika mashariki) nao walijiuzulu kwa kashfa hiyo.
Katika maazimio ya bunge yaliyofikiwa baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya kamati ni kuvunjwa kwa mkataba wa richmond ambao ulikuwa umeuzwa kwa dowans.
Dowans imefungua kesi mahakama ya ushuluhishi mjini paris na tanesco nayo imefungua kesi mahakama ya biashara kuomba dowans isihamishe mitambo yake kutokana na kesi iliyoko paris.
Mapema wiki iliyopita, spika wa bunge, samuel sitta, aliitaka serikali kuepuka na nia ya kutaka kununua mitambo ya dowans ambayo amesisitiza kuwa ni michakavu.
Sitta alisema kununua mitambo hiyo kutaibua upya sakata la kampuni ya kufua umeme wa dharura iliyoibua utata ya richmond development lcc ya marekani.
Alisema hakuna sababu ya kununua mitambo hiyo kwa sh. Bilioni 90 kwani fedha hizo zinatosha kabisa kununua mitambo mipya ambayo inapatikana kirahisi sehemu mbalimbali duniani.
Aidha, alisema haiingii akilini serikali kung`ang`ania kununua mitambo ya dowans ambayo tayari imelishitaki tanesco kwenye baraza la kimataifa la usuluhishi huko paris, ufaransa na kwamba mitambo hiyo ni sehemu ya kufunguliwa kwa kesi hiyo.
Source: Nipashe