Shairi langu.....toka kifungoni(BAN) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Shairi langu.....toka kifungoni(BAN)

Discussion in 'Jukwaa la Lugha' started by CAMARADERIE, Sep 27, 2011.

 1. CAMARADERIE

  CAMARADERIE JF-Expert Member

  #1
  Sep 27, 2011
  Joined: Mar 3, 2011
  Messages: 4,427
  Likes Received: 158
  Trophy Points: 160
  Namba nawe mlimwengu, pulikiza matamko
  Nikweleze neno langu, uzinduwe bongo lako
  Nayo nda M'ngu si yangu, na ayani haya yako
  Uwatapo haki yako, utaingiya motoni

  Simama uitete, usivikhofu vituko
  Aliyo nayo mwendee, akupe kilicho chako
  Akipinga mlemee, mwandame kulla endako
  Uwatapo haki yako, utaingiya motoni

  Amkani mulolala,na wenye sikio koko
  Isiwe mato kulola,natutizame twendako
  Tuwate na kuduwala,usingizi si mashiko
  Uwatapo haki yako,utaingiya motoni

  Teteya kwa kula hali, usiche misukosuko
  Siche wingi wala mali,sabilisha roho yako
  Unyonge usikubali, ukaonewa kwa chako
  Uwatapo haki yako, utaingiya motoni

  Siche kifaru na ndovu, wangazidi nguvu zako
  Wapempe kwa uwekevu, unusuru haki yako
  Siandame wapumbavu,kilicho chako ni chako
  Uwatapo haki yako, utaingiya motoni

  Cha mtu hakifitiki,kikafungiwa kiliko
  Huzuka kikawa hiki,kazana utwae chako
  Uwatapo yako haki,fahamu ni dhara kwako
  Leo na kwa Mola wako,utaingiya motoni

  Fumbuwa unyang'arize, uone duniya yako
  Bure sijiangamize,kuangalia wendako
  Utatupa upoteze,wende ambapo si pako
  Uwatapo haki yako,utaingiya motoni

  Kadhalika nako pia,huko ambako sikwako
  Huwezi kujitetea,wala huwi na mashiko
  Basi iwaze duniya,kwani ya kale hayako
  Uwatapo haki yako ,utaingiya motoni

  Kadi tamati shairi,sitii la ongezeko
  Mwanati iwa tayari, utete haki yako
  Unyonge usiukiri,Jifunge ufe kwa chako
  Uwatapo haki yako, utaingiya motoni
   
 2. Barubaru

  Barubaru JF-Expert Member

  #2
  Sep 27, 2011
  Joined: Apr 6, 2009
  Messages: 7,162
  Likes Received: 29
  Trophy Points: 0
  Hakika ni ushari mzuri sana uliotungwa na Ahmad Nassir ( Malenga wa Mvita)
   
 3. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #3
  Sep 27, 2011
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  UZURI
  Uzuri Wa uso mwema
  Unavuta vitu vyote
  vya macho ya kutazama
  Walakini kwa kupima uzuri wa,
  tabia bora unapopita po pote

  uzuri kupita kupita huu
  katika hii dunia
  nawapa msisahau,
  Ni nzuri Wa tabia
  Ni johari ya heshima duniani
  kila mara

  Huendeshwa na tabia
  kama tabia Si njema,
  si ajabu kupotea.
  Kitu kilicho adhama ni tabia
  na busara

  Kwa kutengeza tabia
  Rai yangu na fikira
  Vyuo katika dunia
  Vingekuwa na tijara
  kwa kuwa nayo daima sera na
  tabia bora.


  From Malenga wa Mvita by Ahmad Nassir
   
 4. CAMARADERIE

  CAMARADERIE JF-Expert Member

  #4
  Sep 28, 2011
  Joined: Mar 3, 2011
  Messages: 4,427
  Likes Received: 158
  Trophy Points: 160
  NYANI AONE KUNDULE

  Funguweni masikizi, mupate yangu sikiya
  Ninenayo mumaizi, kesho musije kuliya
  Naeleza waziwazi, musije kosa sikiya
  Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

  Ni wa kale wanenele, katu haiwezekani
  Bara hadi maji male, mbinguni na duniani
  Nyani haoni kundule, hata kwa Kudura ipi
  Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

  Ela itawezekana, japo shime akitiya
  Apate kuzindukana, kwa mizani kujitiya
  Uzito wake kuona, bila tu kwa kukisiya
  Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

  Leo sikizi funguwa, hilino suwala tata
  Fanya hima kwiyelewa, kesho usije kujuta
  Nafusiyo kuelewa, kabula mwiya kupita
  Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

  Hata uwe jamadari, na tiara bega zima
  Usipo jitahadhari, "cheni" usimame wima
  Uizidishe fahari, ja aloumbwa kwa chuma
  Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

  Chunga unaposimama, kaguwa wako msingi
  Chunga usije terema, ukabiringa "biringi!"
  Jigange panapouma, japo mganga hagangi
  Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

  Hata uwe profesa, wajuwa duniya nzima
  Ama ni mwenyi mapesa, manoti ni chungu nzima
  Au mrembo kipusa, popote twakutazama
  Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

  Usinite mnafiki, kunirushiya matusi
  Lau japo hutosheki, usijawe wasiwasi
  Mbona kalamu hushiki, pamoya na karatasi?
  Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.
   
Loading...