Shairi: Kutunga nitunge nini?

IsangulaKG

JF-Expert Member
Oct 14, 2010
706
386
KUTUNGA NITUNGE NINI?

Niseme ya Magogoni, "Hapa Kazi" mafisadi?
Njipendekeze Chamani, Tumbo langu kulinadi?
Nimsifu Gazetini, "Atenda aloahidi" ?
Kutunga nitunge nini, ya kutunga yakizidi...

Nitunge nini kutunga, zinapozidi topiki?
Nitunge Vita ya Unga, vilotanda nyingi chuki?
Vyeti vya kuungaunga,na matukio ya kiki?
Kutunga nitunge nini, ya kutunga yakizidi...

Nitunge Mkatoliki, waniteke "Saa Nane" ?
Nikemee mabunduki, wanangu tusionane?
Redioni nihamaki, kesho nisionekane?
Kutunga nitunge nini, ya kutunga yakizidi...

Niimbe Fulai-Ova, uzinduzi barabara?
Kukwapua Ranji Rova, kero dawa maabara?
Nitunge malavalava, "wasafi" kwa kujipara?
Kutunga nitunge nini, ya kutunga yakizidi...

Nisifu Mange Kimambi, porini mniokote?
Ti Dar si yangu Kambi, nisitamke Bashite?
Ama nifuge kitambi, wasinifwate fuate?
Kutunga nitunge nini, ya kutunga yakizidi...

Niyatunge ya Bungeni, Danadana za Eala?
Ama nihoji wa nini, Ukatibu wa Kitila?
Nitaitwa Kamatini, nikisema neno Fala?
Kutunga nitunge nini, ya kutunga yakizidi...

Ukimya unitawale, "mrija" wasinkatie?
Nile na wana nilale, wabongo nsiwasemee?
Niwe kakinjekitile, "ukoloni" nikemee?
Kutunga nitunge nini, ya kutunga yakizidi...

malenga wa Ngumbalu
Kisima Cha Mashairi
 
Back
Top Bottom