Shairi - kisima nimekiacha | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Shairi - kisima nimekiacha

Discussion in 'Jukwaa la Lugha' started by Yakuonea, Dec 25, 2011.

 1. Y

  Yakuonea JF-Expert Member

  #1
  Dec 25, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 601
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35
  Mwenzenu ninajongea, taratibu nawajia
  Kwa haya yalotokea, ya kisima nawaambia
  Hofu menisogelea, na nguvu zimeishia
  kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena

  Kisima nilitumia, na mtu sikuchangia
  Usafi lizingatia, kwa ndani nikiingia
  Nilionyesha na nia, kufuli kukifungia
  Kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena

  Nanikiwa kisimani, mwenzenu ninafurahia
  Mengine siyatamani, siwezi wahadithia
  Ni raha iso kifani, moyo unavyotulia
  Kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena

  Nilikunywa nikaoga, na mengi nikafanyia
  Sikuwa hata na woga, madhara sikudhania
  Na watu nikawakoga, raha zilivyozidia
  kisima nimekiacha, Maji hayanyweki tena

  Kwa kweli nilijitamba, ijapo si mmiliki
  Nikawaita washamba, hata ndugu marafiki
  Nikawa mimi ni mwamba, kejeli nyingi na chuki
  kisima nimekiacha, maji hanyweki tena

  udhuru ulinipata, kwa mbali kusafiria
  Nyuma yaliyofuata, machungu kusimulia
  Waovu walikamata, mabaya kukusudia
  Kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena

  Kisima liharibiwa, waovu watu wabaya
  Tope walivyochimbuwa, kweli walikosa haya
  Umbole kahujumiwa, 'saizi' sasa yapwaya
  Kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena

  Kwa sasa kimepoteza, umbole lile asili
  Waovu nao wabeza, wasema hakina 'dili'
  Usijaribu penyeza, utazama wako mwili
  Kisima nimekiacha, maji hanyweki tena

  Kisima sasa hatari, wadudu wamejibanza
  kutumia kwa hadhari, fikiri kabla kuanza
  Nimeacha jivinjari, tamaa sije niponza
  kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena

  Na nyinyi enyi malenga, tahadhari nawambia
  Hakuna sifa kulenga, chini tutawafukia
  Mimi nimeshajitenga, na kule sintarudia
  kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena


  Wenu
  Sindano Mwana wa Ganzi. (SMG)
   
 2. C

  Choveki JF-Expert Member

  #2
  Dec 26, 2011
  Joined: Apr 16, 2006
  Messages: 448
  Likes Received: 13
  Trophy Points: 35
  Pokea pole mtani:

  Pokea pole mtani, kupoteza lako dili
  Maji hayo kisimani, nataka tuyajadili
  Tena fikiri kichwani, utafahamu dalili
  Kupoteza lako dili, pokea pole mtani

  Nafikiria kichwani, nahisi u m bahili
  Ukateka kisimani, halafu huku kijali
  Vya watu ukitamani, tafuta yake asili
  Kupoteza lako dili, pokea pole mtani

  Najua ulitamani, vya bure bila kujali
  Vina ladha mdomoni, hakika kama asali
  Wenyewe ni kina nani? kichwani uliza swali
  Kupoteza lako dili, pokea pole mtani

  Kisima siyo mtoni, uliza kwa wenye mali
  Walochimba kisimani, iweje hukuwajali?
  Busara yako kichwani, ni vipi hukujadili?
  Kupoteza lako dili, pokea pole mtani

  Vieleavyo majini, nasema vina asili
  Mtoni pia ziwani, baharini kuna meli
  Asili yake ni nani, uliza bila kejeli
  Kupoteza lako dili, pokea pole mtani

  Pokea pole mtani, ingawa si yako mali
  Jifunze tena kichwani, kujua yake asili
  Vya watu ni mtihani, usivifanye ni dili
  Kupoteza lako dili, pokea pole mtani
   
 3. Y

  Yakuonea JF-Expert Member

  #3
  Dec 26, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 601
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35


  Hapana sim'bahili, choveki hapa nakana
  Mengi nilikifadhili, kuepuka ya vijana
  Nikaweka na kufuli, ni tendo la uungwana
  Asante ndugu choveki, waovu si wenye mema

  Ukweli nilikijali, na nyingi njema dhamira
  Nilikiona asali, naramba pasi papara
  Sasa ni kama ajali, hakina tena ubora
  Asante ndugu choveki, waovu si wenye mema

  Ni lipi la kwangu kosa, choveki naomba jibu
  kwa huu wote mkasa, nipe busara za babu
  kisima nilikinasa, waovu wakaharibu
  Asante ndugu choveki, waovu si wenye mema

  wabaya wangu waovu, chunguza utanambia
  Na sasa nina makovu, moyoni nimeumia
  Naomba ya uokovu, kisima nakihofia
  Asante ndugu choveki, waovu si wenye mema


  Wako
  SMG
   
 4. Y

  Yakuonea JF-Expert Member

  #4
  Dec 26, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 601
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35
  Kiu imenizidia, kisima nakitamani
  vipi nitadumbukia, iwe kama zamani
  Nipate kufurahia, nijifariji jamani
  kisima kuharibiwa, wapi nitakunywa maji ?

  mwilini ninazizima, kiu ilivyonishika
  Naomba zenu hekima, moyoni nimedhofika
  Pumzi zaweza zima, kiu isipo katika
  kisima kuharibiwa, maji nitakunywa wapi ?

  Maji ya kununua, sipendi yana utata
  waweza hata ugua, faida huto ipata
  viwango huwezi jua, na kiu hutoikata
  kisima kuharibiwa, maji nitakunywa wapi ?

  Ya kisima ni matamu, ladha iso kifani
  ukinywa hayeshi hamu, hili si laubishani
  uyanywe tena kwa zamu, utata hutobaini
  kisima kuharibiwa, wapi nitakunywa maji ?

  SMG
   
 5. C

  Choveki JF-Expert Member

  #5
  Dec 26, 2011
  Joined: Apr 16, 2006
  Messages: 448
  Likes Received: 13
  Trophy Points: 35

  Hati miliki muhimu;

  Hati miliki muhimu, na umma kutangazia

  Kufuli siyo muhimu, hati ukishikilia

  Watakwepa wadhalimu, mwenyewe wakihofia

  Sikia kaka sikia, hati miliki muhimu


  Kamwe hawata dhulumu, safari ukianzia

  Heshima pia nidhamu, kwa kina kuheshimia

  Utadhania mwalimu, nidhamu kitapatia

  Sikia kaka sikia, hati miliki muhimu


  Uianze kwa salamu, wakati wakizengea

  Wajuwe siyo dhalimu, mwanzoni ukianzia

  Washenga na mabinamu, watume kwa asilia

  Sikia kaka sikia, hati miliki muhimu


  Ni muungwana wa hamu, na wao watahisia

  Wenyewe kukuheshimu, mwanzo mzuri anzia

  Wakuone si mgumu, na posa kuwatumia
  Sikia kaka sikia, hati miliki muhimu

  Tano zilizo muhimu, ni mwisho ninaishia

  Nahisi umefahamu, kosa usije rudia

  Utaupata wazimu, wengine wafanyizia!

  Sikia kaka sikia, hati miliki muhimu

   
 6. Y

  Yakuonea JF-Expert Member

  #6
  Dec 26, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 601
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35


  Nduguyo bado nasita


  Mtani nimekupata, hati wasisitizia
  Ila ni tabu kupata, kisima kiso kadhia
  vingi kwa kweli matata, lengo hutolifikia
  Visima viwango duni, nduguyo bado nasita

  vingi viwango ni duni, hasa ukisha kipata
  vina wingi urubuni, nasita rusha karata
  Tageuzwa majinuni, mwishowe waja kudata
  Visima viwango duni, nduguyo bado nasita

  uma nitatangazia, kisima nikiridhia
  Najiepusha kadhia, kwa vile vilo fifia
  Nataka chenye vutia, ili nipate tulia
  Visima viwango duni, nduguyo bado nasita

  Sitaki bora kisima, na maji yamezidia
  waweza pata dhahama, kuta zilivyo achia
  Hata nikija lalama, nani atanisikia
  Visima viwango duni, nduguyo bado nasita

  Kipata chenye viwango, choveki nitakwambia
  Huu ndo wangu mpango, ubora kuzingatia
  Hapa sirushi madongo, mwenzio nasubiria
  Visima viwango duni, nduguyo bado nasita


  wako

  SMG
   
 7. c

  chama JF-Expert Member

  #7
  Dec 27, 2011
  Joined: Aug 6, 2010
  Messages: 8,006
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Nasema pole sindano; wahenga hukusikia
  Maisha ni mashindano, si ajabu kutindikia
  Wajinadi kwa maneno, mrembo wajipatia
  Kususa uhayawani; ya bahari huyawezi.

  Jirani kajihifadhi; maji shinda kajitekea
  Kisima hakina maradhi; janga limekutokea
  Wamlaumu mahadhi; maji amejinywea
  Kususa uhayawani; ya bahari huyawezi


  Tuliza akili yako, maji hayana makombo
  Jitwalie kata yako, kisimani rudi zako
  Kunywa maji yako; ikate kiu yako
  Kususa uhayawani, ya bahari huyawezi.

  Yakisima yamezidi, utamu hauna mfano
  Mahadhi kajirudi, hana shari ya maneno
  Sindano nyumbani rudi, jilie raha zako
  Kususa uhayawani, ya bahari huyawezi.


  Chama
  Gongo la Mboto DSM.
   
 8. Y

  Yakuonea JF-Expert Member

  #8
  Dec 27, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 601
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35

  Uamuzi nilochukua, hakika niwa busara
  Jaribu kudadavua, sindano sina papara
  Hili ukishalijua, huwezi pata madhara
  Tope lishavurugwa, maji hayo sinywi tena

  Tope zilichimbuliwa, maji sasa karaha
  Sipendi kushutumiwa, nasema hayana raha
  Kisima lifumiliwa, tena pasi na staha
  Tope lishavurugwa, maji hayo sinywi tena

  Kisima kimechafuka, na tope kila sehemu
  Nduguyo nimeshituka, kwa pale sinayo hamu
  Siwezi kuwa mzuka, kujitoa ufahamu
  Tope lishavurugwa, maji hayo sinywi tena

  Vipi nikitia kata, tope likang'ang'ania
  kipi kitakachofata, kama sio kujutia
  Na maradhi nikipata, nani tanihudumia?
  Tope lishavurugwa, maji hayo sinywi tena

  Kisima tadumbukia, cha maji yalo salama
  Humo nitafurahia, na wala sintolalama
  Mbizi nitazidishia, kwa ndani ninavyozama
  Tope lishavurugwa, maji hayanyweki tena

  wako

  SMG
   
 9. c

  chama JF-Expert Member

  #9
  Dec 27, 2011
  Joined: Aug 6, 2010
  Messages: 8,006
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Kususa si uunngwana, busara kufikiria
  kisima chako bayana, hakuna wa kubishia
  Hakuna kulaumiana, hilo nakazania
  Mso hili analile, kaa chini fikiria

  Makosa uliyatenda, mwenyewe hukusikia
  Kisima hazina linda, vingapi utasusia
  Nasema njia panda, sindano wajitakia
  Mso hili analile, kaa chini fikiria

  Kosa kutendeana, hilo mbona halina shida
  Waungwana kusamehana, jambo hilo kawaida
  Jitulize na rehana; hata wewe umeranda
  Mso hili analile, kaa chini fikiria

  Kisima chako maridhawa, hakina msimu wa maji
  Hakika nakuweka sawa, usiwe mropokaji
  Waugopa ugonjwa, hali wewe msakaji
  Mso hili analile, kaa chini fikiria

  Chama nipo safarini, nikija nitakuona
  Usionione hayawani, hilo nimeshaliona
  Umepata mtihani, jaribu kushauriana
  Mso hili analile, kaa chini fikiria.

  Chama
  Gongo la Mboto DSM.
   
 10. C

  Choveki JF-Expert Member

  #10
  Dec 28, 2011
  Joined: Apr 16, 2006
  Messages: 448
  Likes Received: 13
  Trophy Points: 35
  Ukiona vyaelea;

  Ukiona vyaelea, ujuwe vimeundiwa
  Nami nakukumbushia, si kwamba vimejaliwa
  Tafuata chako tunzia, mengine ni majaliwa
  Ujuwe vimeundiwa, uonavyo vyaelea

  Nimeanza na msemo, kukumbusha ya wahenga
  Tena kipate kisomo, twakujulisha malenga
  Ama waleta mgomo, kufuga wipiga chenga?
  Ujuwe vimeundiwa, uonavyo vyaelea

  Ni vingi vyenye viwango, machoyo ukifungua
  Tumia wako ubongo, kwa dhati utajulia
  Wala huhitaji hongo, vinono kujipatia
  Ujuwe vimeundiwa, uonavyo vyaelea

  Tafuta chako utunze, utashangaa mavuno
  Tena kutunza jifunze, utafaidi vinono
  Kisima chako kitunze, kwa yako hiyo mikono
  Ujuwe vimeundiwa, uonavyo vyaelea

  Hapa nasema tamati, nahisi umenipata
  Mradi ujizatiti, nasema utakipata
  Na tena cha madhubuti, kisima na yake kata
  Ujuwe vimeundiwa, uonavyo vyaelea
   
 11. Y

  Yakuonea JF-Expert Member

  #11
  Dec 28, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 601
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35

  SI KAMA NIMESUSIA

  Mengi nilifikiria, wala sikukurupuka
  Busara nimetumia, ndo kisa cha kufunguka
  Na wala sitojutia, hili halina mashaka
  si kama nimesusia, lenye mwanzo lina mwisho

  Ni vipi wanishutumu, ukweli hutaki ona
  Hivi nikilamba sumu, wadhani naweza pona?
  Napingana na dhalimu, walojaa kila kona
  Si kama nimesusia, lenye mwanzo lina mwisho

  Mbona nimeshasamehe, madhila nilofanyiwa
  Kwao wao iwe sherehe, kila jambo majaliwa
  Nangoja yangu tarehe, kwa lile nilopangiwa
  Si kama nimesusia, lenye mwanzo lina mwisho

  siwezi jilazimisha, moyo wangu umzito
  kisima tabadilisha, nataka umotomoto
  Nianze yangu maisha, niachane na majuto
  si kama nimesusia, lenye mwanzo lina mwisho

  safari nakutakia, ufike huko salama
  Na tena ukirudia, sikose kunitazama
  Ndio mambo ya dunia, ngoja niache lalama
  si kama nimesusia, lenye mwanzo lina mwisho


  SMG
   
 12. Y

  Yakuonea JF-Expert Member

  #12
  Dec 28, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 601
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35

  KIPI ZAIDI YA KIPI?

  cha kwangu nitatafuta, hili nimedhamiria
  Tena nikisha kipata, walahi nitatulia
  Vya watu sitafuata, mola tanisaidia
  vya pwani na kule bara, kipi zaidi ya kipi?

  Kuna visima vya pwani, wengi wavisimulia
  vyajua mambo fulani, raha hazitaishia
  Hata kiwe cha zamani, mwenyewe utaridhia
  Vya bara na kule pwani, kipi zaidi ya kipi?

  Majiye kama nanasi, walonavyo meniambia
  Havipatikani nkasi, mombasa ndo asilia
  utatulia kwa nafsi, usijute na dunia
  vya bara na kule pwani, kipi zaidi ya kipi?

  Na kuna vya kule bara, sifaze sijazipata
  Labda navyo imara, Choveki unazo data?
  Vipi kikiri kakara, vyaweza kweli kunata?
  Vya bara na kule pwani, kipi zaidi ya kipi?

  Visima vya asilia, kwa sasa tabu kupata
  mchina kaingilia, soko amelikamata
  Na kama hujajulia, kundini waweza fata
  vya bara na kule pwani, kipi zaidi ya kipi?

  Mtani usinichoke, nduguyo nahangaika
  Naomba nihifadhike, niache kulalamika
  salama nisalimike, maisha yenye mashaka
  vya bara na kule pwani, kipi zaidi ya kipi?


  SMG
   
 13. C

  Choveki JF-Expert Member

  #13
  Dec 28, 2011
  Joined: Apr 16, 2006
  Messages: 448
  Likes Received: 13
  Trophy Points: 35
  Muhimu Kuridhika nacho tu;

  Chongo kuita kengeza, msemo ushasikia?
  Si fundi wa kueleza, ni wapi kulobobea

  Uzushi sitoeneza, na hilo kaka julia

  Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima


  Nchini kote uliza, majibu siyo sawia

  Wa pwani wanidokeza, visima vyao hulea

  Sauti utaipaza, kwa ladha ya asilia

  Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima


  Bara ni kama baraza, visima hivyo sikia

  Na kiu utamaliza, na mazingira sawia

  Kwa macho utaangaza, wakati wakodelea

  Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima


  Wasema hutopoteza, na bara utarudia
  Visima vyao vyajaza, kwa maji yalo sawia

  Mchina hajakatiza, vya bara ni asilia

  Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima


  Vya pwani siyo vilaza, mtani hapo julia

  Kwa mengi vinashangaza, ufundi wa asilia

  Kwa ndugu utaapiza, kisima kutoachia

  Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima


  Ridhika nimeeleza, muhimu hiyo sikia
  Chongo kuita kengeza, ishara ilo timia

  Utabaki waapiza, na mali ukagawia

  Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima


  Mtani ninamaliza, mwishowe ninaishia

  Ni mengi nimeeleza, wajibu kwako kujua

  Muhimu maji kujaza, kisima kilo tulia

  Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima

   
 14. c

  chama JF-Expert Member

  #14
  Dec 29, 2011
  Joined: Aug 6, 2010
  Messages: 8,006
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  ZAFANANA

  Sikiliza kwa makini, hasira ziweke kando
  Lako jipe tumaini, kisima safi ni kondo
  Utajitia mtoni, utaumudu mkondo
  Watanga walinena, hizo zote zafanana

  Bara na visiwani, kote nimepitia
  Wamiliki visimani, hakuna asiyejutia
  Wamelala malindoni, wajuvi wamepitia
  Watanga walinena, hizo zote zafanana

  Usijitie jutoni, rudi zako kisimani
  Busara zako sioni, fikiri tena makini
  Mapenzi yapo moyoni, hayapotei gharikani
  Watanga walinena, hizo zote zafanana

  Visima vina maudhi, na kweli vina madhara
  Usiogope maradhi, vitamu vina madhara
  Hatima yetu faradhi, nalo si masikhara
  Watanga walinena, hizo zote zafanana

  Maji tamu kisimani, sote twakimbilia
  Kila mtu atamani, hakuna pakulilia
  Asipoyanywa Hassani, chura atakimbilia
  Watanga walinena, hizo zote zafanana

  Tamati namalizia, rudisha zako hisani
  Tanga nakaribia, nijiendee kisimani
  Tuliza zako hisia, waulize makuhani
  Watanga walinena, hizo zote zafanana

  Chama
  Gongo la Mboto DSM
   
 15. A

  AmaniGK JF-Expert Member

  #15
  Dec 29, 2011
  Joined: Jan 10, 2008
  Messages: 1,101
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 145
  Mwanangu Yakuonea, sikiza wangu usia
  Ni mengi umeongea, yaani karibu kulia
  Kobisi nilikulia, nimeshindwa kuvumilia
  Nyumba wakaa mwenyewe, Kisima gharama tupu

  Hujaona ya kununua, Maji yapo sikia
  Kubaki jishebedua, kisima kujichimbia
  Umekua ka Ngamia, Maji mengi kujinywea?
  Nyumba wakaa mwenyewe, Kisima gharama tupu

  Ungeweza jipatia, Kilimanjaro maji sawia
  Kwa bei ya kutupia, Uhai wajimwagia
  Na ladha ilo sawia, Sayona wajionjea
  Nyumba wakaa mwenyewe, Kisima gharama tupu
   
 16. Y

  Yakuonea JF-Expert Member

  #16
  Dec 29, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 601
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35

  WOSIA NIMEUPATA

  kweli nazidi shukuru, mengi wanisaidia
  wanipa mwanga na nuru, kwa yale nisojulia
  Nisingependa kufuru, na mola takujalia
  Wosia nimeupata, nasema tazingatia

  kuridhika ni lazima, kama ulivyosema
  Hivyo ni vyema kupima, tena kungali mapema
  singoji jua kuzama, ndio nije kulalama
  Wosia nimeupata, nasema tazingatia

  Mchina ajulikana, popote hakosekani
  Iweje twaambiana, vya bara hapatikani
  si kama twachunguzana, niondoe mashakani
  Wosia nimeupata, nasema tazingatia

  jibu ukinipatia, bara nitafikiria
  Naomba liwe sawia, unionyeshe na njia
  Na pwani nafatilia, malindi nitaanzia
  wosia nimeupata, nasema tazingatia

  Unguja na msambweni, nako pia nitafika
  Nimuone bwana Joni, anipe ya uhakika
  Mtani nihatarini, kisima nisipo shika
  Wosia nimeupata, nasema tazingatia

  Mwaka nao wakatika, umri pia waniaga
  Yaani nipatashika, hili ni bonge la 'saga'
  Naomba kusitirika, mola nipe msaada
  wosia nimeupata, nasema tazingatia

  SMG
   
 17. Y

  Yakuonea JF-Expert Member

  #17
  Dec 29, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 601
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35

  SIO ZOTE ZAFANANA

  Mgosi nafurahika, kwa wewe kurudi tena
  Mwenzio nahangaika, maisha hayajafana
  Hujafa hujaumbika, angalizo la rabana
  Sio zote zafanana, chunguza utanambia

  wembamba sio upana, jaribu kupambanua
  Na usiku si mchana, hivi kweli hujajua?
  Kikongwe hawi kijana, naomba kufafanua
  sio zote zafanana, chunguza utanambia

  Na fupi kamwe si ndefu, vipimo vi tofauti
  Hata uwe umpofu, gogo huliiti jiti
  Mfupa sio mnofu, tuulize watafiti
  Sio zote zafanana, chunguza utanambia

  Vya mombasa si vya bara, kimaisha na fikira
  Na pwani haiwi ngara, mwembe hauwi mpera
  Tafiti acha papara, uone kilicho bora
  sio zote zafanana, chunguza utanambia

  kuna zile za minato, nyingine zimeachia
  Na hata kwa manukato, huwezi badilishia
  utapatwa machafuko, na mengi yenye kadhia
  sio zote zafanana, chunguza utanambia

  SMG
   
 18. Y

  Yakuonea JF-Expert Member

  #18
  Dec 29, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 601
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35

  YA CHUPA SIJAZOEA

  Ya chupa nilijaribu, ila kweli yana kifu
  Nilikosa na jawabu, sikuona unadhifu
  kwa kero na zake tabu, hunywi kwa uadilifu
  Ya chupa sijazoea, hayakati kiu yangu

  Ijapo wamewekea, kwa ladha za mbalimbali
  kuyanywa nayagomea, kwa kuwa ninajijali
  sina nayo mazoea, nisije pata ajali
  Ya chupa sijazoea, hayakati kiu yangu

  Ya chupa yana karaha, na raha hutoipata
  utaishia kuhaha, huwezi kunywa kwa kata
  Hizi ni zangu nasaha, si kama eti nanata
  Ya chupa sijazoea, hayakati kiu yangu

  Chunguza haya chupa, ukinywa hautosheki
  unywe lita na mapipa, 'kiuyo' haikwepeki
  chupa nyingine zi bapa, kwa kweli sishawishiki
  Ya chupa sijazoea, hayakati kiu yangu

  SMG
   
 19. c

  chama JF-Expert Member

  #19
  Dec 30, 2011
  Joined: Aug 6, 2010
  Messages: 8,006
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  ZAFANANA


  Mimi mchimba mahiri, kazi yangu naijua
  Nimetafiti dhahiri, yote nimeyajua
  Nimekula vya hariri, hakuna asiyejua
  Zimefanana kwa hila, tabia na maumbile

  Visima si tofauti, maumbile nagusia
  Utakunywa kwa nyakati, hilo nakumbia
  Fanya zako harakati, kiasi utajutia
  Zimefanana kwa hila, tabia na maumbile

  Kisima wakiingia, mbizi wajipigia
  Hazina wakimwagia, maradhi cha kupatia
  Kauli yakuishia, vilinge wavikimbia
  Zimefanana kwa hila, tabia na maumbile

  Sadiki yangu maneno, visima vyote ni sawa
  usije jitoa meno, utamu wako maridhawa
  Umejikunya kiuno, akili za kupagawa
  Zimefanana kwa hila, tabia na maumbile


  Usijitie kisoi , utamu wako mwenyewe
  Kamuulize mtoi, mrukaji kama mwewe
  Hata lile goigoi, lawa tamu kama wewe
  Zimefanana kwa hila, tabia na maumbile

  Chama
  Gongo la Mboto DSM
   
 20. Elli

  Elli JF-Expert Member

  #20
  Dec 30, 2011
  Joined: Mar 17, 2008
  Messages: 26,827
  Likes Received: 10,122
  Trophy Points: 280
  Nawashukuru wote kwa tungo hizi kali sana! Thanks you have brightened my day!!!!
   
Loading...