Serikali yaumbuka tena bungeni; Wabunge waikataa bajeti ya Uchukuzi

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797

• Wabunge waikataa bajeti ya Uchukuzi

na Salehe Mohamed, Dodoma


KWA mara nyingine, ndani ya wiki mbili wabunge wameikatalia serikali kupitisha bajeti yake.

Baada ya kuikataa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini wiki iliyopita, jana ilikuwa zamu ya Wizara ya Uchukuzi, ambayo wengi walisema ni ndogo isiyokidhi mahitaji ya kukarabati miundombinu ya reli inayotoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja.

Katika mjadala wa jana, wabunge wa upinzani na wa CCM waliungana kukataa kuunga mkono hoja, mara baada ya hotuba za Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Peter Serukamba (CCM), na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, Mhonga Ruhanywa (CHADEMA) kuonyesha kuwa serikali ilikosa umakini katika kuandaa bajeti hizo.

Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) alienda mbali kwa kupendekeza serikali iwanyonge mawaziri na watendaji wazembe na kuwafilisi vigogo wanaoiba mali za umma.

Bajeti hiyo iliwasilishwa na Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu.

Katika hoja yake, Waziri Nundu aliliomba Bunge limuidhinishie sh bilioni 237.563. Kati ya fedha hizo sh bilioni 69.585 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh bilioni 167.978 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Peter Serukamba, akiwasilisha maoni ya kamati yake, alisema kamati haikuridhishwa na bajeti hiyo finyu ambayo haikidhi mahitaji ya utekelezaji wa shughuli za msingi za wizara hiyo.

Alisema kamati hiyo inaitaka serikali kutafuta fedha za kutosha kwa ajili kuimarisha usafiri wa reli, usafiri wa majini na kukomboa ndege za Shirika la Ndege la Tanzania zilizoko kwenye matengenezo nje ya nchi.


Alibainisha kuwa tangu Februari 11 mwaka huu, ATC haina ndege inayoruka, shirika linadaiwa sh bilioni 75, na hivi sasa lina tishio la mali zake kukamatwa kwa amri ya mahakama baada ya kampuni ya ndege ya Afrika Kusini na Celtic Capital Corporation kulifikisha suala hilo mahakamani.


Alisema kuwa kampuni ya meli nayo inakabiliwa na matatizo ya uchakavu wa meli zake na madeni makubwa yanayofikia sh bilioni 1.6.


Alibainisha kuwa kamati hiyo ilitarajia serikali ingekuja na mipango kabambe ya kufufua ATC, na kuimarisha usafiri wa reli na meli, lakini haikufanya hivyo, kwani ilitenga sh bilioni 167.97 kwa ajili ya shughuli za maendeleo badala ya sh bilioni 492.02.

Baada ya Serukamba kutoa maoni hayo, alifuatia msemaji wa kambi ya upinzani kwa wizara hiyo, Mhonga Ruhanywa, ambaye alisema bajeti iliyotengwa kwa wizara hiyo ni ndogo mno kulinganisha na majukumu yake, ambapo imetengewa sh bilioni 167 kwa ajili ya maendeleo kati ya hizo sh bilioni 95 ni fedha za ndani na sh bilioni 72.98 ni za wadau wa maendeleo.



Ruhanywa alisema kimsingi bajeti hiyo haiwezi kuikwamua nchi kiuchumi wala kuwaletea maendeleo wananchi wake kwa kuwa sekta nyeti ya usafiri ambayo ingetengeneza ajira nyingi haijapewa kipaumbele.


Alisema sekta ya uchukuzi inakua kwa kasi, na mchango wake katika pato la taifa ni takriban asilimia 5.1 (sawa na trilioni 1.6) ambayo ni mara mbili ya mchango wa sekta ya madini na mara nne ya mchango wa sekta ya uvuvi.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alipinga bajeti hiyo na kuwataka wabunge bila kujali itikadi zao kutoipitisha bajeti hiyo kama walivyofanya kwenye ya Nishati na Madini.

Mbowe alisema bajeti hiyo haina masilahi kwa taifa na iwapo itapitishwa italiangamiza taifa kwani wizara iliomba sh bilioni 500 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, badala yake ikatenga sh bilioni 95.


Alisema inastaajabisha kwa rais, waziri mkuu, Baraza la Mawaziri na wataalamu kukubali bajeti hiyo ipelekwe bungeni ilhali wakifahamu fika haina faida kwa Watanzania.

Alisema serikali ya CCM inatumia muda mrefu katika harakati za kuvuana magamba wakati taifa liko hatarini, na uchumi ukidorora, hasa baada ya nchi kuingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwenye soko la pamoja.
Alisema ni vema wanasiasa wakawapa fursa wataalamu wa uchumi waisaidie nchi kujikwamua kiuchumi badala ya kuwaingilia kwa masilahi ya kisiasa kama inavyoonekana hivi sasa hasa kwa wizara nyeti kupangiwa bajeti ndogo.
“Jamani sasa nyie CCM mnaweza kufanya jambo gani? ATC mmeiua, UDA inawashinda, TRL, Reli ipo hoi, Bandari ndiyo usiseme, kila siku mnawaza kuvuana gamba, CHADEMA tukiandamana mnapiga kelele, sasa mnataka tufanyeje? Tunaiharibu nchi yetu jamani,” alisema Mbowe.

Akichangia mjadala huo, Filikunjombe aliyetaka mawaziri na watendaji wabovu wanyongwe, alisema China imekuwa na utaratibu wa kuwanyonga viongozi wabadhirifu na wazembe.

Alitoa mfano wa mkandarasi aliyejenga Uwanja wa Taifa, kwanba alinyongwa hivi karibuni nchini China kwa sababu ya kutofanya kazi yake kwa ufanisi, hivyo aliitaka serikali kuiga mfano wa kuwanyonga mawaziri na watendaji wazembe.
Alisema kuwa ni aibu kwa viongozi wa Tanzania kukubali kuwahujumu Watanzania walio wengi ambao wanazidi kuwa maskini wakati wachache wanajinufaisha.



Alisema serikali imebweteka na kubaki ikilalamikia maandamano yanayofanywa na wafuasi wa CHADEMA, ambao wamekuwa wakiyafanya kwa lengo la kuleta mabadiliko.

Alionya kuwa endapo serikali itashindwa kusikiliza maoni ya wapinzani pamoja na wabunge kupinga kupitishwa kwa bajeti hiyo, atawahamasisha wananchi wake wafanye maandamano kuipinga.

Mbunge wa Mbozi Mashariki Godfrey Zambi, (CCM) aliitaka serikali kuivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa madai kuwa viongozi wake wamekuwa wakihusika kwa ufisadi wa kuihujumu UDA.

Aliitaka serikali kuchukua hatua kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, Idd Simba, na kwa Mbunge wa Urambo Magharibi, Juma Kapuya, (CCM) kwa kuliuza shirika hilo kinyemela.



Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli (CHADEMA), alimtaka Waziri Mkuu, Pinda awawajibishe Kapuya na Simba kwa kuiingiza serikali kwenye hasara kubwa baada ya kushiriki kwenye ufisadi wa kuuza hisa za UDA.


Mbunge wa Buchosa, Charles Tizeba (CCM), alisema haungi mkono bajeti hiyo na kama wabunge wataamua kuipitisha Watanzania watawapuuza, kwa kuwa haitawasaidia kuwakwamua kiuchumi, hasa kwa kushindwa kuimarisha usafiri wa reli ambao ni nafuu zaidi.

Alisema wabunge wengi wamekuwa wakipigia kelele ujenzi wa barabara za lami kwa sababu zinapitia katika majimbo yao na zinawapatia umaarufu wa kisiasa, tofauti na reli ambayo ina mchango mkubwa kiuchumi, lakini haiwapatii sifa za kisiasa.



Alibainisha kuwa Wajerumani hawakuwa wajinga kuanzisha ujenzi wa reli kwani walitambua kuwa ni njia rahisi na yenye gharama nafuu ya kusafirisha mizigo na abiria.


Alisema wabunge wanapitisha fedha za ujenzi wa barabara za lami ambazo baada ya muda mfupi zinaharibika na kuwalaumu mawaziri na watendaji kwa kushindwa kusimamia ujenzi wake ambao wakati mwingine umekuwa chini ya kiwango.


Alibainisha kuwa ukarabati na ujenzi wa reli hauhitaji fedha nyingi lakini anashangawa na kasi ya serikali kujenga barabara za lami badala ya kuimarisha reli.

“Naomba wabunge wenzangu tuikatae bajeti hii ili ikaangaliwe upya, tumechoshwa na takwimu zinazotolewa tunataka treni, ndege na meli zitembee na si porojo,” alisema Tizeba.



Mbunge wa Viti Maalumu, Maria Hewa (CCM) alisema amechoshwa na kauli za serikali za michakato, mipango, utaratibu na nyinginezo katika mambo muhimu ya taifa ambayo hayatekelezwi kwa kiwango kinachotakiwa.


Alisema anaikataa bajeti hiyo kwa nia njema, ili waziri na watendaji wake wakaiboreshe hasa kwa kutafuta fedha kwenye maeneo ambayo si muhimu, ili waziingize katika kuimarisha usafiri wa reli na majini.


“Ndugu zangu wabunge, tuwahurumie wenzetu masikini ambao sasa hawana uwezo wa kusafirisha mizigo, kufanya biashara au kutumia usafiri wa reli, tuikatae bajeti hii ili waipange upya,” alisema.


Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Zitto Kabwe, alisema bajeti hiyo ikipitishwa Watanzania wasitarajie jambo lolote jipya kwani hakuna fedha zilizotengwa kwa ajili ya reli ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi.

Alisema hata Waziri Nundu anajua hili kwani alishamwandikia barua waziri mkuu kulalamikia bajeti ndogo iliyotengewa wizara yake.

Zitto alisoma sehemu ya barua hiyo na akasisitiza kwamba Waziri Mkuu Mizengo Pinda hakutoa majibu.

Aliongeza kuwa Kamati ya Miundombinu iliikataa bajeti hiyo lakini wizara ikawarubuni kwa madai kuwa itapata mkopo kutoka Benki ya Dunia, fedha ambazo watazitumia kwenye reli.
“Jamani tuna uzoefu wa miradi ya Benki ya Dunia inavyochukua muda mrefu mpaka fedha zitolewe, leo hii tunataka kupitisha bajeti kwa kuwategemea hawa jamaa, ninawaomba tusiipitishe bajeti hii,” alisema.


Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah (CCM), alisema ni aibu kwa serikali kila kukicha ingoje isemwe ndipo irekebishe mambo, hasa katika kipindi nchi inapoelekea kuangamia kiuchumi.

“Waziri, msikubali kuwa mbuzi wa kafara, haiwezekani kila siku kazi yenu kusemwa tu ndiyo mbadilishe mambo, kama mnaona watendaji wenu wanawaangusha wafukuzeni kazi kuliko kungojea kudhalilishwa humu ndani,” alisema.

Shah alisema si vema kwa UDA kuuzwa kwa bei ya kutupwa katika mazingira tatanishi ambayo fedha zake ziliingizwa katika akaunti ya Mwenyekiti wa bodi hiyo, Idd Simba.
Alisema ni vema serikali ikawakamata Meya wa Jiji la Dar es Salaam (Didas Masaburi), Mkurugenzi wa Jiji (Bakari Kingobi), Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, Idd Simba na watendaji wengine waliohusika na kuuza hisa za UDA.
Alisema haiwezekani UDA yenye rasilimali za sh bilioni 12 ziuzwe kwa sh bilioni 1.2 kwa Kampuni ya Simon Group ambayo ununuzi wake wa hisa umegubikwa na mizengwe.
“Nawaomba polisi wawakamate viongozi wote waliohusika na kuuza hisa za UDA bila kujali nyadhifa zao, Takukuru ifanye kazi yake na aliyenunua hisa hizo ajue ametapeliwa,” alisema Shah.
Pamoja na idadi kubwa ya wabunge kuikataa bajeti ya Wizara ya Uchukuzi bado inaendelea kujadiliwa na hatima yake itajulikana leo. Hii si mara ya kwanza kwa wabunge kuikataa bajeti ya serikali kwani wiki mbili zilizopita waliikataa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo walidai hiendani na matakwa ya mahitaji ya kutatua mgawo wa umeme.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kampuni ya Simon Group iliyonunua hisa za Shirika la UDA, Robert Kisena, ameeleza kuwa kampuni hiyo ilifuata utaratibu katika ununuzi wa hisa zilizokuwa chini ya bodi ya shirika hilo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Kisena alisema kampuni yake ilinunua hisa zinazojulikana kama ‘unallocated’, hivyo iwapo kuna tatizo lolote basi wahusika wanapaswa kulipeleka suala hilo mahakamani.
Alisema kampuni hiyo ilinunua hisa za asilimia 52.553 zilizomilikiwa na bodi kwa utaratibu wa kisheria pasipo kuingilia hisa zinazomilikiwa na serikali ambazo ni 49 wala zile 51 za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Alisema iwapo Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) imebaini matatizo wanapaswa kulifikisha suala hilo mahakamani kuliko kuendelea kulipotosha.

Kisena alieleza kuwa mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kuutafsiri mkataba huo na kama ikibainika hawakufuata taratibu, basi chombo hicho ndicho chenye nguvu ya
kuuvunja mkataba huo.
Juzi Zitto alieleza kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa ununuzi wa shirika hilo, kwani hata fedha zilizolipwa na kampuni hiyo ziliingia kwenye akaunti ya Idd Simba, ambaye alikuwa mwenyekiti wa bodi ya UDA.

 
Back
Top Bottom