Serikali yabadili mfumo vocha za ruzuku

BabuK

JF-Expert Member
Jul 30, 2008
1,845
329
WIZARA ya Kilimo, Chakula na Ushirika na wadau wa sekta hiyo kwa pamoja wameridhia mapendekezo ya Kamati maalumu iliyoundwa kuangalia utaratibu mbadala wa kumfikishia mkulima pembejeo za ruzuku.

Mabadiliko hayo ya usambazaji wa pembejeo za vocha za ruzuku utaanza kutumiwa mwakani msimu wa mwaka 2013/2014.

Katika mfumo huo mpya, Serikali itatoa Sh bilioni 100 na kuingiza kwenye mfuko wa thamani ya pembejeo na kuzipatia benki zitakazoteuliwa ambapo benki hizo pia zitaweka kiasi cha Sh bilioni 200 zitakazowakopesha wakulima watakaojiunga kwenye vikundi vidogo vilivyosajiwa na kununua pembejeo moja kwa moja kutoka kampuni za uzalishaji wa pembejeo.

Uamuzi huyo umeridhiwa na wajumbe wa Kamati iliyoundwa na Serikali hivi karibuni ya kuangalia utaratibu mbadala wa kumfikishia mkulima pembejeo za ruzuku iliyokutana awali mkoani Dodoma kuandaa mapendekezo hayo ambayo yaliafikiwa kwenye mkutano wa pamoja uliofanyika juzi mjini hapa.

Mkutano huo uliowashirikisha baadhi ya wakuu wa mikoa ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ikiwemo ya Ruvuma, Iringa, Mbeya, Rukwa, Katavi, Njombe, Singida, Mtwara, Manyara Tabora na Morogoro pamoja na wataalamu mbalimbali wa Serikali na taasisi za umma, kampuni za uzalishaji wa mbolea na usambazaji wa pembejeo na mawakala wa pembejeo nchini.

Mkurugenzi Msaidizi wa Pembejeo za Kilimo wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Dk Mshindo Msola, alisema hayo mbele ya waandishi wa habari juzi mjini hapa baada ya kumalizika kwa mkutano huo na wajumbe wa Kamati hiyo kufikia maamuzi ya pamoja ya kutaka mfumo huo uanze kutumika mwaka mmoja baadaye ili kutoa nafasi ya wadau kujipanga katika utekelezaji wake.

“Utaratibu wa awali wa matumizi ya vocha uliodumu takribani miaka minne, pamoja na mafanikio yaliyopatikana ya kuongeza tija na wananchi kuelewa matumizi ya pembejeo na kuzipata eneo lao, kumekuwepo na changamoto kubwa ya kuhusu udanganyifu wa mawalaka wa pembejeo kudanyanya wakulima kwa kutotoa pembejeo ama kununua vocha za ruzuku,” alisema Dk Msola.

Dk Msola alisema, kampuni za pembejeo sasa zitahusika moja kwa moja kupeleka pembejeo vijijini na kuwateua mawakala wao ambao watawajibika kwenye kampuni hizo .

Pia alisema, mkulima aliye katika kikundi atalipa asilimia 20 ya bei ya pembejeo aliyokopa na asilimia 80 ya deni lake atalipa wakati wa kuuza mazao yake.

Alisema, katika mpango huo wa mabadiliko, wakulima waliojiunga kwenye vikundi watajisajili ili watambuliwe rasmi na benki ambazo , halmashauri za wilaya zao ndizo zitakazoingia mikataba na benki .

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Mohammed Muya, ambaye alishiriki kwenye mkutano huo alisema mpango huo utawawezesha wakulima wengi zaidi kufikiwa na pembejeo za ruzuku za kilimo na pia kutaka elimu itolewe zaidi kwa wakulima na watendaji wa Serikali kuanzia ngazi ya juu hadi chini.

Chanzo: HabariLeo
 
Back
Top Bottom