Serikali ya umoja wa kitaifa

Serikali ya umoja wa kitaifa

Kurunzi

Platinum Member
Joined
Jul 31, 2009
Posts
10,198
Reaction score
11,632
ZIPO kila dalili zinazoonyesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), sasa inaanza kwenda mrama, baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif Hamad, kulalamikia kususiwa serikalini na viongozi.

Wakati Maalim Seif akitoa madai hayo, Makamu wa Pili, Balozi Seif Ali Iddi, amelalamika kupewa majina ya kashfa na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), wanapokuwa kwenye mikutano ya kisiasa.

Malalamiko ya Maalim Seif yanahusu kutopewa ushirikiano wa kikazi na watendaji wakuu wa Serikali hiyo, wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya.

Habari za uhakika kutoka Zanzibar zinasema hali hiyo imesababisha viongozi wa CUF kuchukua hatua ya kuratibu ziara za kiongozi wao ndani na nje ya nchi, pamoja na kumpa hadhi na heshima zinazostahili kama kiongozi wa juu serikalini.

CUF hivi sasa pia inaratibu hata viongozi wanaoambatana na kiongozi huyo katika ziara za kikazi, pamoja kuhamasisha wanachama kujitokeza kwa wingi kumlaki awapo kwenye ziara za ndani au akitoka katika ziara za nje ya nchi.

Habari ambazo RAI imezipata kutoka vyanzo vyake vya uhakika zimebainisha kuwa, hatua ya Maalim Seif kutengwa na viongozi na watendaji serikalini hususani wanaotoka CCM, imetokana na msimamo wake wa kudai dola ya Zanzibar, wakidai msimamo wake huo lengo lake ni kutaka kuvunja Muungano.

Kinachojiri Serikalini:

Chanzo chetu cha uhakika kutoka serikalini kimesema kuwa, msimamo huo wa Maalim ni dhahiri umewakera viongozi wa serikali wakiwamo wakuu wa wilaya na mikoa wa Zanzibar, na hivyo wameamua kutompa ushirikiano.

Habari hizo zinasema mkakati huo wa viongozi serikalini ingawa unafanywa kwa siri, lakini tayari kiongozi huyo ameshtuka na tayari malalamiko hayo yamewasilishwa kwenye kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea.

Chanzo hicho kilibainisha tukio la wazi la kutengwa kwa Maalim ni lile lililotokea Mei 12, 2013 alipokuwa katika ziara ya kikazi katika kijiji cha Nungwi, kilichopo Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Chanzo kilisema kuwa, katika ziara hiyo Maalim Seif alikwenda kuzindua mradi wa majaribio wa kukabiliana na athari za tabianchi, unaotekelezwa na ofisi yake.

Ilielezwa pamoja na kuzindua mradi huo, kiongozi huyo alizindua visima vya maji vinavyofadhiliwa na Serikali ya Japan kwa kushirikiana na Shirika la African Adaptation Program (AAP).

Chanzo chetu kilibainisha kuwa, katika ziara hiyo hakujitokeza Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini (A), Pembe Juma Khamis, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini (A), Riziki Juma Simai, Ofisa Tawala pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini (B), Khamis Jabir Makame.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, mradi huo unatekelezwa kwenye mikoa na wilaya za viongozi hao na walipohojiwa ni kwanini hawakujitokeza kwenye ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais, hawakutoa majibu ya kuridhisha.

“Walipoulizwa wakajibu walikuwa kwenye ziara ya kukabidhi Mwenge wa Uhuru katika mkoa mwingine, lakini hii si sababu ya msingi wangeweza wakajipanga walau mmoja wao akajitokeza.

“Mradi huo ni muhimu kwa wananchi wa Nungwi kwani kwa kipindi kirefu eneo hilo lilikuwa na tatizo la maji salama, sasa wafadhili wamejitokeza, katika hili hata wananchi nao wamesikitishwa na hatua ya viongozi wao kutojitokeza,” kilisema chanzo chetu.

Safari za nje za Maalim Seif:

Habari kutoka ndani ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais zimesema mara baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hali ya maridhiano ilionekana wazi.

Chanzo chetu kutoka ofisi hiyo kilisema awali Makamu wa Pili wa Rais alipokuwa akitoka kwenye safari za kikazi ndani na nje ya Nchi, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdallah Mwinyi, alikuwa akijitokeza kumlaki kiongozi huyo kwenye Uwanja wa Ndege.

Chanzo hicho kilibainisha kuwa hivi sasa hali haiko kama awali, kwani kiongozi huyo anaporudi kwenye safari za kikazi anajikuta kwenye Uwanja wa Ndege akiwa pekee na wasaidizi wake tu.

“Siku hizi mambo yamebadilika na hatujaambiwa sababu na sisi tumeliacha kama lilivyo, lakini hali hii sio ya kufurahisha, kiutaratibu kiongozi wa Serikali wa level kama ya Maalim anatakiwa ziara zake zi ziratibiwe na ofisi yake, ikiwa ni pamoja na kupanga viongozi wa Serikali atakaoambatana nao kwenye ziara husika.

“Kinachofanyika sasa pamoja na viongozi wa Serikali wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya kupangwa kwenye ziara hizo, lakini hawatokei na utakuta Maalim ameongozana na viongozi wenzake wa chama, ilhali ziara ni ya kiserikali,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa, hali hiyo ya kutengwa Maalim haitokei akiwa kwenye ziara za ndani ya nchi pekee, lakini pia imeelezwa akiwa anapotoka kwenye ziara za nje ya nchi, kiongozi huyo hapewi mapokezi ya kuridhisha na viongozi wa Serikali.

“Kuna ziara za nje kiongozi huyu anazifanya, lakini anaporudi anatakiwa apewe mapokezi yenye hadhi ya kiongozi wa juu serikalini. Lakini kinachofanyika sio hivyo, hakuna kiongozi wa ngazi ya Serikali wala Mkuu wa Mkoa anayejitokeza kumpokea, ukiondoa Msaidizi wake wa karibu, Ismail Jussa na Mwandishi wake wa habari.

“Hali hii imesabisha Maalim pamoja na uongozi wa CUF kukasirika na kuanzia sasa wameweka utaratibu wa kwenda kumpokea wenyewe kiongozi wao, na kumpa heshima za uongozi wa juu serikalini, kilisema chanzo hicho.

Baraza la Wawakilishi laelezwa:
Mgogoro huu umechukua sura mpya sasa, baada ya hivi karibuni Baraza la Wawakilishi kuelezwa juu ya kuwapo sintofahamu hiyo inayotishia uhai wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, Mbunge wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, amelalamikia hatua ya Maalim Seif kutengwa kwa kutopewa hadhi ya kiongozi kama wanazopewa viongozi wenzake wa juu serikalini akiwamo, Makamu wa Pili wa Rais.

“Nia ya serikiali ya Umoja wa Kitaifa inaanza kuondoka, Maalim haagwi wala kupokewa, hakuna kiongozi anayekwenda kumpa ushirikiano, ukipanda mbigiri utavuna mbigiri.

Jussa alitoa kauli hiyo alipokuwa akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi katika bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais:
Naye Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, amethibitha mgogoro uliopo unatishia uhai wa SUK, huku akilaumu baadhi ya viongozi wa CUF kutumia majukwaa ya kisiasa kutukana viongozi wa CCM.

Akihitimisha makadirio ya bajetiya Ofisi yake, Balozi Seif alisema ingawa viongozi wa juu serikalini wanaonyesha kuelewana, lakini tatizo lipo kwenye majukwaa ya kisiasa ambapo viongozi wa CUF huyatumia kutukana viongozi wa CCM.

“Ninatukanwa na viongozi wa CUF ninaitwa majina mabaya, sijui nimewakosa nini, Wazanzibar wasipokuwa makini watarudi walikotoka na ile dhana ya Umoja wa Kitaifa itaondoka,” alisema Balozi wakati akihitimisha mjadala wa mamadirio ya ofisi yake.

Mwanzoni mwa mwaka huu gazeti hili liliwahi kuripoti juu ya mgogoro wa chini chini unaofukuta katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), unaotishia kuwapo maridhiano ya kweli yaliyofikiwa baina ya vyama vya CCM na CUF, katika kuiongoza Serikali.

Gazeti hili liliripoti kuwapo kutoelewana kati ya Mawaziri, Naibu Mawaziri, Katibu Wakuu na hata wakurugenzi wanaotoka katika vyama tofauti katika kuunda Serikali hiyo.



 
Back
Top Bottom