SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imetishia kumchukulia hatua za kisheria mwanasiasa au yeyote anayejiita Rais wa Zanzibar wakati Rais Dk Ali Mohamed Shein, tayari amechaguliwa na wananchi kwa mujibu wa katiba na anaongoza serikali.
Msimamo wa serikali umetangazwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Haji Omar Kher, alipokuwa akijibu hoja za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kabla ya kufungwa mjadala wa kujadili Ripoti ya Kamati ya kudumu ya katiba, Sheria utumishi wa Umma na Idara Maalumu ya Vikosi vya SMZ Zanzibar.
Alisema kwa mujibu wa katiba, uchaguzi umemalizika na Dk Shein ndiye Rais wa Zanzibar na ataendelea kubakia madarakani kwa muda wa miaka mitano hadi 2020, muda wa kufanya uchaguzi mkuu mwingine.
“Anayeamini kwamba Rais Shein si Rais aende mahakamani lakini serikali haitavumilia upotoshaji na viashiria vya uvunjifu wa amani.”alionya Waziri Kheir.
Aliwapongeza Wazanzibari kwa kuendelea kuimarisha amani na umoja wa kitaifa lakini alisisitiza kuwa baada ya kukamilika uchaguzi wa marudio uliyofanyika Machi mwaka jana hakuna uchaguzi mwingine mpaka mwaka 2020.
Tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015 , aliyekuwa mgombea wa urais wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, amekuwa akidai yeye ndiyo mshindi wa urais wa Zanzibar akinukuu matokeo ya uchaguzi yaliyofutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jecha Salim Jecha.
Hata hivyo, Maalim Seif na CUF walisusia uchaguzi wa marudio na kupoteza viti vyote vya wawakilishi na madiwani na kusababisha kukwama kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar baada ya wapinzani kushindwa kufikia mashariti ya katiba ya kupata asilimia 10 ya matokeo urais wa Zanzibar.
Kuhusu tuhuma za kuwapo askari wanaoshirikisha biashara ya dawa za kulevya na magendo , Waziri Kher ,alisema hakuna askari ambaye yupo juu ya sheria na kwamba watashughulikiwa.
Aliwataka wajumbe wenye ushahidi kuwaripoti katika vyombo vya sheria lakini askari na raia wote wanapaswa kukaguliwa na vyombo vya usalama katika maeneo ya kuingia na kutoka uwe uwanja wa ndege au bandarini.
Waziri Kheir alisema Wizara yake imeandaa mpango kazi wa kuimarisha doria na kuzitambua bandari bubu Unguja na Pemba katika kupambana na magendo na dawa za kulevya Zanzibar