Kadiri siku zinavyopita ndivyo migogoro ya kati ya wananchi na wawezekezaji inavyozidi kuongezeka. Kwa maoni yangu, chanzo cha matatizo ni serikali ya CCM, ambayo imeshindwa kusimamia vizuri sheria za nchi na hivyo kusababisha wananchi kuendelea kukosa haki zao za msingi. Inapotokea wananchi wameingia mkataba na mwekezaji bila ya wao wenyewe kushirikishwa na kuridhia isipokuwa viongozi wachache wenye uchu wa kujilimbikizia mali kufanya hivyo, hatusikii kama viongozi hao wanawajibishwa ili liwe fundisho kwa viongozi wengine wenye tabia kama hiyo. Zoezi la kuwahamisha wananchi ili kupisha mwekezaji, ambaye amepewe eneo lao kuliendelea linafanyika kwa ubabe na kuacha machungu mengi kwa wananchi husika, kama vile uhalibifu wa mali na fidia ndogo isiyoendana na hali halisi ya maisha na isiyolipwa kwa wakati.Mwekezaji anapata kibali cha kumiliki ardhi na kuiendeleza kwa urahisi zaidi kuliko mwananchi anayeomba hicho kibali kwa madhumuni yaleyale.Kuendelea kuwaomba wawekezaji kuja kumiliki maeneo mkubwa ya ardhi kwa kisingizio kuwa hakuna maendeleo bila wawekezaji na wananchi kuendelea kukosa fursa hiyo kunasababisha wananchi waone wanafanywa wageni ndani ya nchi yao kwa kuendelea kukosa ardhi maana kwao masharti ya kuipata ni magumu na hata wakiipata wanaweza wakashindwa kuiendeleza kwa muda uliopangwa kwa vile bado wanakusanya nguvu kutokana na kipato kuwa kidogo. Lakini mwekezaji mwenye mtaji mkubwa yeye hili siyo tatizo hata kidogo kwa maana yeye alishajiandaa muda mrefu.Wananchi wengi wanapata ajira zisizo endelevu kwa maana kwamba ni ajira zenye kipato kidogo na zinawafanya waishi at or below the subsistence level. Kwa hali ya namna hii, ni dhambi kujivunia kuwa wananchi wameajiriwa kwa sababu mtu anayeishi at or below the subsistence level hawezi kufanya savings za aina yoyote zitakazoweza kumsaidia kuwa na miradi ya kujiendeleza na kuindeleza familia yake.Kwa hali kama hii, ni wazi wananchi wataendelea kuona wawekezaji si watu wa kuwaletea maendeleo bali wa kuwaongezea dhiki katika maisha yao. Ili kuondokana na hali hii serikali ya CCM isiwaaminishe tu wananchi kuwa wawekezaji watawaletea maendeleo bali pia isimamie sheria za nchi vizuri na iweke mazingira ambayo yanawanufaisha wananchi na wawekezaji na siyo kudhani tu kuwa wawekezaji ndio watakaoleta maendeleo ya wananchi maana hata wao wamekuja kuchuma kwa ajili ya mahitaji yao na ya familia zao.